2023
Daima Umekuwa Ukijua
Machi 2023


“Daima Umekuwa Ukijua,” Liahona, Feb. 2023.

Taswira za Imani

Daima Umekuwa Ukijua

Nilikuwa nimepokea ushuhuda wa injili iliyorejeshwa, lakini nilikuwa bado nimebakiwa na miezi kumi kwenye mkataba wangu kama mchungaji wa kanisa jingine.

Picha
mwalimu pamoja na wanafunzi wa seminari

Picha imepigwa na Leslie Nilsson

Nilipokuwa na takriban miaka tisa, nilipata maumivu makali ya jino. Maumivu yalikuwa makali kupita kiasi, lakini hatukuwa na pesa ya kwenda kwa daktari wa meno. Wakati huo, niliishi na malaika bibi yangu nchini Mexico.

Kwa machozi katika macho yake, aliniuliza, “Je, unaamini katika Yesu na kwamba Yeye anaweza kukusaidia?”

Nilimwambia ndiyo. Aliniomba niende chumba cha pili, nipige magoti na niombe kwa ajili ya muujiza. Niliumimina moyo wangu katika sala, lakini hakuna kilichotokea. Nikiwa mwenye hasira, niliweka nguvu kubwa kadiri nilivyoweza kwenye taya langu na kutoa sala ya pili. Punde maumivu yaliondoka! Nilipokimbia kumwambia bibi yangu, nilimkuta akiwa amepiga magoti, akimsihi Mungu amsaidie mjukuuu wake mdogo. Kamwe sijasahau tukio lile na ninamshukuru bibi yangu.

Uzoefu mwingine wa kiroho ulifuatia.

Nilipofikisha miaka 14, nilihamia Texas, Marekani, kujiunga na wazazi na ndugu zangu. Nilipata kanisa katika eneo lile na nilianza kuhudhuria mara kwa mara. Kwa sababu ya uzoefu wangu kwa Mungu, nilitaka kushiriki jina Lake na injili Yake kwa kila mtu ambaye angeweza kunisikia. Katika umri wa miaka 15, nilijiunga na shule wa uchungaji ili niwe mchungaji. Kwa miaka miwili, nilihudhuria madarasa ya Biblia kabla ya shule, baada ya shule na wikiendi.

Asubuhi moja katika shule ya sekondari ya juu, nilisikia kelele kwenye chumba cha wavulana cha kuhifadhia vitu. “Wewe Mmormoni!” mtu alipayuka. Sikuwa nimewahi kusikia neno hilo kabla, lakini lilisikika kama tusi.

Baadaye niligundua kwamba mtu aliyekuwa akipayukiwa alikuwa rafiki yangu mwema Derek.

“Pole kwa kuitwa Mmormoni,” nilisema.

Derek alitabasamu na kuuliza, “Hujui Mmormoni ni mtu gani, sivyo?”

Aliniambia lilikuwa jina la utani kwa waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.

“Kwa hivyo, ninyi ni Wakristo?” Niliuliza.

Aliposema ndiyo, nilifurahi kujua kwamba tulikuwa na imani moja katika Yesu Kristo.

“Je, Ulimuuliza Mungu?”

“Hawa Wamormoni ni akina nani,” nilijiuliza “na wanaamini nini?”

Nilienda mtandaoni kutafuta majibu. Baada ya dakika chache, nilihitimisha kwamba rafiki yangu hakuwa Mkristo kabisa na kwamba alikuwa anakwenda motoni. Kwa hivyo, nilijiingiza kwenye misheni ya kumwokoa.

Kwa miaka miwili iliyofuatia, nilisoma kila kitabu nilichoweza kupata kilichohusu Kanisa, ikiwa ni pamoja na Kitabu cha Mormoni chote—mara mbili. Pia nilikutana na Derek pamoja na wamisionari ili nijaribu kuwasaidia.

Nilipofikisha miaka 17, nilihitimu shule ya uchungaji, nikatawazwa kuwa mchungaji na nikawa pasta wa kusanyiko dogo la Texas. Miezi miwili baada ya utawazo wangu, nilikuwa na mjadala mwingine na wamisionari.

Mmoja wao aliuliza, “Umesoma Kitabu cha Mormoni na umepata masomo yote tunayoweza kufundisha, lakini je, umemuuliza Mungu ikiwa ujumbe wetu ni wa kweli? Ungeweza kutambua jibu kutoka Kwake, sivyo?”

“Bila shaka,” nilijibu kwa majivuno.

“Kwa jinsi ninavyoona, pande zote zina manufaa kwako,” mmisionari alijibu. “Ikiwa utamuuliza Mungu kama kile ambacho rafiki yako anakiamini ni cha kweli na Mungu akasema hapana, basi utakuwa umefanikisha misheni ambayo kwayo uliianza safari hii. Lakini ikiwa atasema ujumbe wetu ni wa kweli, basi fikiria ni mengi kiasi gani ungeweza kunufaika nayo.”

Sikuwahi kabisa kulifikiria kwa namna ile. Usiku ule nilipiga magoti ndani ya chumba changu baada ya kusoma Moroni 10:3–5. Jibu langu kutoka kwa Mungu lilikuwa rahisi lakini lenye nguvu. Katika sauti ndogo, tulivu, Yeye alinijibu: “Daima umekuwa ukijua.”

Ukurasa Mpya katika Ufuasi Wangu

Sasa nikiwa nimepata ushuhuda wa injili iliyorejeshwa, vipi kuhusu uchungaji wangu? Nilikuwa bado nimebakiwa na miezi kumi kwenye mkataba wangu kama mchungaji. Baada ya sala nyingi na kushauriana na Mungu, niliamua kukamilisha huduma yangu. Kwa miezi kumi iliyofuatia, niliendelea kushiriki kweli za kawaida za Biblia, lakini pale ilipowezekana niliongeza mtazamo wa injili iliyorejeshwa. Watu walikubali na kuzipenda kweli zile na kundi langu dogo lilikua kutoka watu 20 hadi takriban watu 150.

Baada ya kumaliza mkataba wangu, nilipewa nafasi ya kudumu, lakini nilijua kwamba ulikuwa wakati wa kubatizwa ndani ya Kanisa. Ulikuwa wakati wa kuanza ukurasa mpya katika safari yangu ya ufuasi.

Nilipowaambia wanafamilia yangu, hawakuwa na furaha—mwanzoni. Lakini miezi mitatu baadaye nilijiunga na Kanisa, nilimbatiza mama yangu na wawili kati ya ndugu zangu. Baada ya kuhudumu huko Oklahoma misheni ya Oklahoma City, nilimbatiza mdogo wangu wa kike.

Ikiwa mtu anauliza kwa nini nilibadilisha dini yangu, mara zote ninajibu, “mimi sikubadili dini yangu—mimi bado ni Mkristo mcha Mungu. Badala yake, nimeimarisha tu uhusiano wangu na Mwokozi kwa kuwa muumini aliyebatizwa wa Kanisa Lake—Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Ninamjua binafsi zaidi sasa na kwa undani zaidi kuliko hapo kabla kwa sababu ya Urejesho wa injili, Kitabu cha Mormoni, manabii wa siku za leo na ibada takatifu za wokovu na kuinuliwa zinazopatikana ndani ya hekalu.”

Leo ninayo fursa ya kufanya kazi kama mwalimu wa muda wote wa seminari. Bado nimeyatoa maisha yangu kwa Yesu Kristo na injili Yake. Na bado ninaendelea kumwambia kila mtu ambaye atasikiliza kuhusu “habari njema ya furaha kuu” (Luka 2:10).