2023
Ushauri wa Kukabiliana na Siku za Baadaye zenye Kuogofya na Zisizo na Uhakika
Machi 2023


Vijana Wakubwa

Ushauri wa Kukabiliana na Siku za Baadaye zenye Kuogofya na Zisizo na Uhakika

Kwenye maisha yangu binafsi na yale ya kazini, nimepata uzoefu wa kutokuwa na uhakika na nimejifunza jinsi Baba wa Mbinguni anavyoweza kutusaidia kupita yote hayo.

Picha
glavu za ndondi

Nilipokuwa mdogo, familia yangu ilihama kutoka Tonga kwenda Marekani. Baba yangu alikuwa mwanandondi wakati tukiishi Tonga na alianza kunifunza ndondi baada ya kuwa tumewasili Marekani. Mpango kazi wake ulikuwa kwamba siku moja ningekuwa bingwa wa ulimwengu wa uzito wa juu. Alinifunza kutokuogopa. Huwezi kuwa mwoga kwenye uwanja wa ndondi ikiwa unataka kufanikiwa. Baba yangu hakuwa mshiriki kikamilifu Kanisani wakati huo, lakini alinifunza mengi kuhusu kukabiliana na ugumu na kuwa na ujasiri mbele ya hofu.

Kujifunza ndondi kuliniandaa kwa namna ya kipekee kwa ajili ya kazi yangu. Nilikwenda Chuo Kikuu cha Brigham Young kwa ufadhili wa mchezo wa mpira. Na hata kufanya kile ambacho watu wengi hudhani pengine ni jambo la kuogopesha sana kwenye uwanja wa mpira—kumkamata na kumwangusha mpinzani aliyedaka mpira—mara zote nilikifanya kwa utulivu. Sikuwahi kamwe kuwa na hofu. Hakika, nilipenda changamoto ya mpira.

Baba yangu alitarajia kwamba ningekuwa na taaluma ya kazi kwenye maswala ya michezo—ilikuja kuwa kwenye mpira, si ndondi. Lakini nafikiri mafunzo yangu yalinisaidia kwenye vyote kuwa na imani na kutazama mbele kwa imani na kuwa na tumaini kwenye hali ya kukosa uhakika.

Picha
baba wa Vai Sikahema akisherehekea manjonjo ya Vai uwanjani

baba wa Vai akisherehekea manjonjo ya mwanaye uwanjani.

Picha imepigwa na Mark Philbrick / BYU © BYU Photo

Kama vijana wakubwa, mnakabiliana na mambo mengi magumu na ya kutia hofu—maswala binafsi kama vile maamuzi kuhusu elimu, kazi, ndoa na familia. Na mnakabiliana na maswala mengi yenye uwanda mpana, kama vile mdororo wa kiuchumi, majaribu ya kijamii, mageuzi ya kisiasa na hata vita. Lakini kutokana na maisha yangu mwenyewe, ninajua kwamba tunapochagua kumweka Mungu kwanza katika maisha yetu, daima Yeye atakuwepo pale kutuongoza tushinde yote.

Ushawishi wa Marafiki Wema na Watu Wema

Nilikuwa na urithi mzuri wa kuwa na marafiki wema wakati niliporejea nyumbani kutoka kwenye misheni yangu. Rafiki niliyekutana naye kwenye kituo cha mafunzo ya umisionari alinitambulisha kwa mwanamke ambaye baadaye alikuja kuwa mke wangu. Sipingi kamwe ukweli kwamba rafiki zako mara nyingi huamua mafanikio yako au kushindwa kwako kwenye maisha. Marafiki na washauri wako wanaweza kukusaidia ufanye maamuzi ambayo yatakuongoza aidha karibu au mbali na Mungu.

Nilipokuwa katika Ligi ya Mpira ya Taifa (NFL), nilivutiwa na Gifford Nielsen, ambaye pia aliwahi kuichezea BYU kabla ya kwenda NFL, hatimaye akawa mchambuzi wa michezo na baadaye Sabini Mkuu mwenye Mamlaka. Nilikutana naye siku moja kwenye uwanja wa golfu na alinipa ushauri ambao ulibadili mwenendo wangu wa kazi yangu niliyosomea.

Tulikuwa tumeketi ndani ya gari dogo la golfu, mimi na yeye peke yetu na baada ya kumwelezea kuhusu mpango wangu wa kuonekana kwenye televisheni kama yeye baada ya kuwa nimemaliza kucheza mpira, alinipa ushauri wa kutoendelea kufanyia kazi lengo la kazi ambayo itanihitaji niwe kwenye michezo siku za Jumapili. Kwa kufanya hivyo, ningeweza siku zote kuwa na wito Jumapili na kutumikia Kanisani.

Ulikuwa rahisi hivyo, lakini ulikuwa ni ushauri ambao sikuwahi kuuwaza. Na hilo lilibadili mwenendo wa maisha yangu.

Simamia Kile Unachokiamini

Muda mwingi wa kazi yangu nikiwa NFL ulikuwa wa kutia hofu na kukosa uhakika. Ni asilimia 2 pekee ya wachezaji wa mpira hufika NFL, na hata wakati nilipopangwa kwenye timu, ningeweza kutolewa muda wowote. Kuweza kudumu kwa muda mrefu kama nilivyodumu ilikuwa baraka kubwa, lakini kuishi bila mpango wa dharura ilikuwa ngumu. Ilihitaji imani kubwa.

Ukiwa NFL, unahamishwa kutoka timu moja hadi nyingine, mwaka hadi mwaka, ukizunguka nchini kote. Ilionekana ya kuvutia, lakini watu wengi hawaoni kipengele kisichovutia sana. Ni njia ngumu sana ya kuishi. Na ni njia ngumu ya watu kuishi pia; hiyo ndiyo sababu kuna kiwango kikubwa cha talaka kwa wanariadha wenye taaluma.

Kilichosaidia ni kwamba nilifahamu mahali niliposimama. Nilikuwa na msingi imara katika Kristo na mara nyingi nilifanya mambo yale ambayo yaliniweka karibu Naye na Baba wa Mbinguni.

Unaweza usipitie njia ya kazi ambayo imejawa mashinikizo na majaribu, lakini katika suala langu, kuwa mwanariadha mwenye taaluma kuliniweka katika mitindo tofauti tofauti ya maisha kuliko nilivyozoea. Kwa mfano, tulipokuwa tukifika kwenye miji mikubwa na kusafiri mwanzoni, wanatimu wenzangu bila kupoteza muda walitaka kutoka ili wakashiriki kwenye shughuli mbalimbali ambazo hazikuendana na viwango vya injili na nilifahamu wakati uleule kwamba nisingeweza kusimama mguu mmoja Sayuni na mwingine Babeli. Nisingeweza kujibu “acha nifikirie” ili niwaridhishe. Badala yake, nilihitaji kuwa imara katika imani yangu na kufafanua kwa nini sikuweza kuungana nao.

Picha
Akina Sikahema kwenye siku ya harusi yao.

Vai akiwa na mkewe, Keala, katika siku ya harusi yao

Picha za familia kwa fadhila ya mwandishi

Nilikuwa mwenye bahati kwamba nilioa wakati nikiwa chuoni. Nilipokwenda NFL, mke wangu na mtoto wetu wa miezi sita walikuwa pamoja nami. Tulikuwa tumefunga ndoa hekaluni na nilijua kile ambacho maagano yalimaanisha kwangu na kile ambacho yalihitaji kutoka kwangu. Kwa hivyo, ningewaambia wanatimu wenzangu, “hapana, sifanyi hilo.” Na wakati walipong’ang’aniza, ningesema, “Mimi na mke wangu tulifunga ndoa katika nyumba ya Bwana ambapo tulifanya maagano matakatifu. Maagano hayo ni muhimu zaidi kwangu kuliko kitu kingine chochote.”

Na cha kushangaza ni kwamba wakati waliponiuliza maswali yale na walipopata uhakika kuhusu mimi nilikuwa mtu wa aina gani, wanatimu walewale walianza kunilinda na kuheshimu viwango vyangu na maagano yangu. Inahitaji ujasiri kusimamia kile unachokiamini na kukithamini.

Kukabiliana na majaribu mengi ilikuwa ya kutia hofu mwanzoni, lakini kumtegemea Baba wa Mbinguni na kukumbuka utakatifu na maana ya maagano yangu mbele ya mashinikizo daima kulinisaidia kusimama imara kwenye njia ya agano katika kazi yangu. Unaweza kufanya vivyo hivyo katika hali yoyote unayokabiliana nayo kote katika safari yako.

Mfuate Nabii

Ninafahamu kwamba kama vijana wakubwa leo mnakabiliana na kutokuwa na uhakika kwingi na hofu kuhusu siku zijazo. Na mnaweza kujiuliza ni kipi mfanye na jinsi gani ya kukishinda. Jibu rahisi ni kufuata mwongozo wa nabii, Rais Russell M. Nelson. Nabii wa Mungu anapozungumza na kukupa jambo mahususi, ni rahisi tu kama vile kufuata tu ushauri huo.

Nimegundua kwamba Rais Nelson anapenda kutoa orodha rahisi ya mambo tunayoweza kufanya ili tuweze kusimama imara katika imani yetu. Kwa zaidi ya miaka michache iliyopita, amewapa waumini wa Kanisa mambo matano ya kufanya ili tukuze imani yetu, njia tano za kukuza kasi ya kiroho, mambo matatu ambayo unapaswa kufanya pale unapoanza mwaka mpya na mengi zaidi.

Hatoi orodha ya jozi za mambo. Ni mambo rahisi tu. Na ikiwa utafanya mambo hayo rahisi na kuwa thabiti, maisha yako yatabadilishwa kwa kufanya mambo rahisi kabisa. Msingi wako wa imani utasimama imara, hata wakati kunapokuwa na hali za kutia hofu ulimwenguni. Fanya mambo hayo na utakuwa SAWA. Utalindwa.

Inanikumbusha hadithi katika Agano la Kale Ya Naamani, jemedari wa jeshi ambaye alikuwa na ukoma. Alikwenda kwa Elisha, nabii, ambaye alimwambia aende akajioshe ndani ya Mto Yordani mara saba. Jemedari wa jeshi alidhani ni upuuzi, lakini watu aliokuwa nao walimhimiza yeye kama jemedari aende tu. Na alikuwa na imani ya kwenda na kutenda—jambo rahisi sana. Naye alifanywa safi. (Ona 2 Wafalme 5:1–15.)

Picha
Familia ya Sikahema

Familia ya Mzee Sikahema

Iweke Kesho Yako katika Mikono ya Baba wa Mbinguni

Sasa, sikuweza kuwa mwenye weledi kwenye ndondi, lakini nilijifunza baadhi ya mambo kuhusu kukabiliana na hofu. Kwa maamuzi na changamoto zote zinazokukabili sasa kama kijana mkubwa, ninakusihi ufanye yote uwezayo ili kuutafuta na kuutunza ushawishi wa Roho pamoja nawe daima. Hicho ndicho kiini. Kama vile Rais Nelson alivyofundisha hivi karibuni: “Msukumo chanya wa kiroho utatufanya tusonge mbele licha ya kuwako kwa hofu na kutokuwa na uhakika kunakosababishwa na majanga ya ulimwengu, sunami, milipuko ya volkeno na uhasama wa kutumia silaha. Msukumo wa kiroho unaweza kutusaidia tustahimili mashambulio maovu yasiyokoma ya adui na kuzuia jitihada zake za kuharibu msingi wetu binafsi wa kiroho.”1

Nilipokuwa mdogo na nikikabiliana na uhalisia wa kuhamia nchi mpya kama mhamiaji, sikuwahi kuwaza maisha yasiyokuwa na kukosa uhakika. Kadiri nilivyoendelea kukabiliana na kutokuwa na uhakika kote katika maisha yangu na kazi yangu, nimejifunza kwamba kama wafuasi wa Kristo, tunaweza kukabiliana na hofu zozote au vikwazo vyovyote katika njia yetu.

Unapojihusisha na watu wema, unapoweka viwango na kusimamia yale unayoyaamini na kumfuata nabii, kesho yako haitakuwa yenye kutia hofu. Na utaweza kusonga mbele kwa imani licha ya hofu na kutokuwa na uhakika. Unapoiweka kesho yako kwenye mikono ya Baba yetu wa Mbinguni mwenye upendo, unaweza kuwa na tumaini kwamba daima atakuwepo kwa ajili yako.