2021
Mpende Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo kwa Moyo Wako Wote
Julai 2021


UJUMBE WA URAIS WA ENEO

Mpende Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo kwa Moyo Wako Wote

“Tunawabariki wale wanaotuzunguka vyema zaidi tunapoifanya amri ya kwanza kuwa ya kwanza. Upendo unapaswa kuwa motisha yetu.”

Upendo wetu kwa Baba wa Mbinguni na Mwokozi wetu Yesu Kristo unadhihirishwa kwa kujitoa kwetu na utiifu wetu kama wafuasi wa Yesu Kristo.

Alipoulizwa na mfarisayo ambaye alikuwa mwanasheria: “Mwalimu, katika torati ni amri ipi iliyo kuu?”

Yesu alijibu bila kusita, “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote.

“Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza”1.

Ninajua kwamba wengi wanajiuliza kwa nini Baba yetu wa Mbinguni aliweka amri hii ya kwanza kuwa ya kwanza, kama ilivyofundishwa na Mwokozi Yesu Kristo.

Jibu ni jepesi na kama tukitafuta kuelewa “kwa nini”, ukweli utadhihirishwa kwetu na Roho Mtakatifu kwamba sisi sote ni wana na mabinti wa Baba wa Mbinguni mwenye upendo. Yeye anatujua na anatupenda: kama Yohana alivyofundisha, Mungu ni upendo2. Anatamani shangwe na furaha yetu. Ameweka mpango wa wokovu na kuinuliwa ili kuturuhusu sisi kufikia baraka za kuinuliwa kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo, ili kwamba tuweze kuwa kama Yeye. Upendo kwa Baba Yetu wa Mbinguni na Mwanawe Yesu Kristo unapaswa kuwa ni motisha inayoongoza maisha yetu kila siku. Kama tunampenda Mungu na Mwanawe Yesu Kristo, tutataka kushika amri zote na watakuwa ushawishi muhimu zaidi katika maisha yetu.

Ngoja tujifunze kutoka kwenye uzoefu wa Yosefu huko Misri, ambaye alipaswa kufanya uchaguzi kati ya Mungu, ajira yake na mke wa Potifa. Yosefu alijiuliza swali yeye mwenyewe alipokabiliana na jaribu “Nifanyeje ubaya huu mkubwa nikamkose Mungu?”3

Alipokuwa njia panda na kutakiwa kufanya uchaguzi, Yosefu alikumbuka yeye ni nani, na ufahamu huu wa utambulisho wa kiungu ulimsaidia kumchagua Mungu kwanza kuliko kuchagua ulimwengu. Alikuwa na shauku ya kumfurahisha Mungu kuliko kitu kingine chochote, bila kujali gharama ambayo angelipia. Yosefu alimpenda Baba Yetu wa Mbinguni na Mwanawe Yesu Kristo kwa moyo wake wote.

Mzee Dieter F. Uchtdorf alifundisha: “Tunapoelewa vyema kile inachomaanisha kumpenda . . . Baba yetu wa Mbinguni na Mwanawe Yesu Kristo kwa moyo wetu wote, mkanganyiko hutoweka na vipaumbele vyetu hufungamana. Safari yetu kama wafuasi wa Kristo huwa yenye shangwe zaidi. Maisha yetu hupata maana mpya. Uhusiano wetu na Baba yetu wa Mbinguni huongezeka maradufu. Utiifu unakuwa shangwe badala ya kuwa mzigo”4.

Tunadhihirisha upendo kwa Baba yetu wa Mbinguni na Mwanawe Yesu Kristo tunaposhika amri na maagano yetu. Hii ndiyo njia ya kupima imani yetu, utiifu wetu, na kuashiria ukomo wa kweli wa ufuasi wetu. “Yeye asemaye, Nimemjua, wala hazishiki amri zake, ni mwongo, wala kweli haimo ndani yake”5.

Waumini wa kwanza wa Kanisa huko Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo walifanya ibada zao za Jumapili nyumbani kwa Kaka Dieudonne Mbuyi Nkitabungi huko Kinshasa. Makazi haya yalikuwa mbali sana kwa waumini wapya wa Kanisa waliokuwa wamebatizwa. Nakumbuka kwamba wazazi wangu walimwamsha kila mmoja katika familia mapema asubuhi, ili kwamba tujiandae kwa safari ndefu ya kuhudhuria ibada ya Kanisa kila Jumapili. Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa familia yangu na Watakatifu wengine wengi ambao waliikumbatia injili ya urejesho ya Yesu Kristo. Kama mvulana mdogo, nilijiuliza ni ipi sababu ya dhabihu hiyo kila wiki. Leo, naelewa kwamba huu ulikuwa uchaguzi uliofanywa na wazazi wangu wa kumpenda Baba yetu wa Mbinguni na Mwanawe Yesu Kristo kwa kuonyesha imani kwao. Walichagua kuwa watiifu kwa amri za Mungu na waaminifu kwa maagano tuliyoyafanya wakati tulipobatizwa. Upendo ndio ulikuwa motisha ya matendo yao.

Kujitoa kwao kwa Bwana kumetubariki wengi wetu na mifano yao imehamasisha wengi wa kizazi kinachoinukia kubakia kwenye njia ya agano. Tunawabariki wale wanaotuzunguka vyema zaidi tunapoifanya amri ya kwanza kuwa ya kwanza.

Tunaonyesha kwamba tunampenda Baba yetu wa Mbinguni na Mwanawe Yesu Kristo kwa Mioyo yetu yote, tunapowahudumia wengine kwa shangwe na katika “njia iliyo bora”6. Kama kuhudumu kwetu kutatakiwa kuwa kwenye mafanikio makubwa zaidi, kunapaswa kutekelezwa kwa upendo kwa Baba yetu wa Mbinguni na Mwanawe Yesu Kristo. Tunapaswa kuendelea kutafuta fursa za kuwahudumia wengine. Mwokozi Yesu Kristo alifundisha: “Kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi”7.

Katika Mkutano Mkuu wa Aprili 2018, nabii wetu mpendwa Rais Nelson alishiriki uzoefu binafsi alioupata miaka 63 iliyopita kuhusu jinsi alivyomhudumia Kaka Wilbur Cox. Huu ni mfano halisi na wa kweli wa jinsi tunavyoweza kuwabariki watu binafsi na familia kwa kuwahudumia. Kila tendo la wema kwa wengine hukuza hali zetu wenyewe za kiroho. Kuwahudumia wengine ndiyo hasa kile injili na maisha ya kuinuliwa humaanisha.

Rais Nelson alifundisha: “Kuna milango tunayoweza kufungua, baraka za ukuhani tunazoweza kutoa, mioyo tunayoweza kuponya, mizigo tunayoweza kusaidia, shuhuda tunazoweza kuimarisha, maisha tunayoweza kuokoa, na shangwe tunayoweza kuileta katika nyumba za Watakatifu wa Siku za Mwisho . . . kupitia kuhudumu kama Mwokozi alivyofanya na ambavyo angefanya.”8 Ninashuhudia hili katika jina la Yesu Kristo, Amina.

Thierry Kasuangi Mutombo aliidhinishwa kama Sabini Mkuu Mwenye Mamlaka mnamo Aprili 2020. Amemuoa Tshayi Nathalie Sinda. Wao ni wazazi wa watoto sita.

Muhtasari

  1. Mathayo 22:36–38.

  2. Ona 1 Yohana 4:8.

  3. Mwanzo 39:9.

  4. Dieter F. Uchtdorf, “Upendo wa Mungu”, Mkutano Mkuu Oktoba 2009.

  5. 1 Yohana 2:4.

  6. Ona 1 Wakorintho 12:31.

  7. Mathayo 25:40.

  8. Russell M. Nelson, “Kuhudumu kwa Uwezo na Mamlaka ya Mungu”, Mkutano Mkuu Aprili 2018.