2021
Kuwanyooshea Mkono wa Upendo Waongofu Wapya na Waumini Wasioshiriki Kikamilifu
Julai 2021


MAFUNDISHO YA MARAIS WA KANISA

Kuwanyooshea Mkono wa Upendo Waongofu Wapya na Waumini Wasioshiriki Kikamilifu

Kila mwongofu anahitaji urafiki, jukumu, na kulishwa kwa neno la Mungu, alifundisha Rais Gordon B. Hinckley (1910–2008).

Kukiwa na ongezeko la idadi ya waongofu, ni sharti tufanye ongezeko la juhudi kuu ili kuwasaidia wao wanapojaribu kutambua mambo. Kila mmoja wao anahitaji vitu vitatu: rafiki, jukumu, na kulishwa na “neno zuri la Mungu” (Moroni 6:4). Ni wajibu wetu na nafasi yetu kutoa vitu hivi.

Urafiki

[Waongofu] wanajiunga na Kanisa kwa shauku kwa ajili ya kile walichokiona. Sisi ni sharti mara moja tujenge juu ya hiyo shauku. . . . Kuwasikiliza, kuwaongoza, kujibu maswali yao, na kuwapo ili kuwasaidia katika hali zote na katika mazingira yote. . . . Namwalika kila muumini kunyoosha mkono wa urafiki na upendo kwa wale ambao wanajiunga na Kanisa kama waongofu.

Tunao wajibu mkuu kwa wale wanaobatizwa katika Kanisa. Hatuwezi kuwatelekeza. Hatuwezi kuwaacha wasimame pekee yao. Wanahitaji msaada wanapojifahamisha mienendo na desturi za Kanisa hili. Ni baraka kuu na fursa kwetu kutoa msaada huo. . . . Tabasamu angavu, salamu za mkono wa urafiki, neno la kutia moyo linaweza kufanya maajabu.

Acha tuwanyoshee mikono watu hawa! Acha tuwafanye marafiki zetu! Acha tuwe wakarimu kwao! Acha tuwatie moyo! Acha tuongeze kwenye imani yao na elimu yao hii, kazi ya Bwana.

Ninakusihini . . . kwamba muwakumbatie wale wanaojiunga na Kanisa na kuweni marafiki zao na kuwafanya wajisikie kukaribishwa na kuwapa faraja basi tutaona matokeo ya ajabu. Mungu atawabariki ili mtoe msaada katika mchakato huu mkuu wa kuwabakiza waongofu kanisani.

Jukumu

Kanisa hili linatarajia kitu kutoka kwa watu. Lina viwango vya juu. Lina mafundisho mazito. Linatarajia huduma kuu kutoka kwa watu. Hawatakaa bila kazi. Tunawatarajia wafanye mambo. Watu huitikia hilo. Wanakaribisha fursa za kutumikia, na wanapofanya hivyo, watakua katika uwezo wao, katika uelewa wao, na katika tabia zao na kufanya vyema.

Wapeni [waumini wapya] kitu cha kufanya. Hawatakuwa na nguvu katika imani bila mazoezi. Imani na ushuhuda ni kama misuli ya mkono. Kama ukiutumia na kuurutubisha, utakuwa na nguvu zaidi. Kama ukiuweka mkono wako kwenye kitanzi na kuuacha hapo, utadhoofika na kuwa hafifu, na vivyo hivyo shuhuda.

Sasa, baadhi yenu husema hawapo tayari kukubali majukumu. Lakini hamna kati yetu aliyekuwa tayari wakati wito ulipokuja. Ninaweza kusema hivyo juu yangu. Je, Mnafikiri mimi nilikuwa tayari kwa wito huu mkuu na mtakatifu? Nilihisi kushindwa. Nilihisi kupungukiwa. Bado nahisi kushindwa. Bado nahisi kupungukiwa Lakini najaribu kusonga mbele, nikitafuta baraka za Bwana, na kujaribu kufanya mapenzi Yake na nikitumaini na kuomba kwamba huduma yangu ikubalike Kwake. Jukumu la kwanza nililokuwa nalo katika Kanisa hili ilikuwa ni mshauri wa rais wa akidi ya mashemasi nilipokuwa na umri wa miaka kumi na miwili. Sikuhisi kupungukiwa. Nilihisi kushindwa. Lakini nilijaribu tu kama mnavyofanya, na baada ya hapo yakaja majukumu mengine. Katu hapakuwa na hisia za kupungukiwa, bali daima hisia za shukrani na utayari wa kujaribu.

Kila mwongofu anayejiunga na Kanisa anapaswa kuwa na jukumu mara moja. Linaweza kuwa dogo, lakini litaleta tofauti kubwa katika maisha yake.

Ndiyo mwongofu mpya hatajua kila kitu. Kuna uwezekano akafanya makosa fulani. Kwani si sisi sote tunafanya makosa? Kitu cha muhimu ni ukuaji ambao utakuja kutokana na shughuli.

Kulishwa na neno zuri la Mungu

Naamini . . . kwamba waongofu hawa wana ushuhuda wa injili. Naamini wana imani katika Bwana Yesu Kristo na wanajua uhalisia wa uungu Wake. Naamini ni kweli wametubu dhambi zao na wana azimio la kumtumikia Bwana.

Moroni [anasema] kuhusu wao baada ya kuwa wamebatizwa: “Na baada ya hao kupokelewa kwenye ubatizo, na kupokelewa na kusafishwa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, walihesabiwa miongoni mwa watu wa kanisa la Kristo; na majina yao yalichukuliwa ili wakumbukwe na kulishwa na neno zuri la Mungu, kuwaweka kwa njia nzuri, kuwaweka waangalifu siku zote kwenye sala, wakitegemea tu katika nguvu ya wokovu wa Kristo, ambaye alikuwa mwanzilishi na mtimizaji wa imani yao” (Moroni 6:4).

Katika siku hizi kama ilivyokuwa katika siku hizo, waongofu ”wanahesabiwa kuwa miongoni mwa watu wa kanisa . . . ili wakumbukwe na kulishwa na neno zuri la Mungu, kuwaweka kwenye njia nzuri, kuwaweka waangalifu siku zote kwenye sala.” . . . Acha tuwasaidie wanapochukua hatua za kwanza kama waumini.

Ni muhimu sana kwamba [kila mwongofu mpya] ajihusishe na akidi ya ukuhani, Muungano wa Usaidizi wa Akina Mama, Wasichana, Wavulana, Shule ya Jumapili au Msingi. Sharti ahimizwe kuja kwenye mkutano wa sakramenti kupokea sakramenti, na kufanya upya maagano aliyofanya wakati wa ubatizo.

Gordon B. Hinckley alikuwa Rais wa Kanisa wa15, akitumikia kutoka Machi 12, 1995 hadi Januari 27, 2008.