2023
Maafisa Wakuu Wanajiingiza kwenye Huduma kwa Nchi Nne za Afrika ya Kati
Machi 2023


Habari za Eneo

Maafisa Wakuu Wanajiingiza kwenye Huduma kwa Nchi Nne za Afrika ya Kati

Viongozi wakuu wa Wavulana na Shule ya Jumapili walitoa mafunzo na huduma nchini Kenya, Ethiopia, Uganda na Tanzania.

Brad Wilcox, wa Urais Mkuu wa Wavulana na Milton Camargo, wa Urais Mkuu wa Shule ya Jumapili, waliendesha huduma kwa nchi nne za Afrika ya Kati mnamo mwezi Septemba.

Viongozi wawili wa imani wa ulimwenguni wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho wanatoa mafunzo ya uongozi, kuwaimarisha wamisionari na kutoa usaidizi kwa waumini na familia zao.

“Lengo letu la kuja Afrika kwanza ni kumwakilisha Mwokozi na kushiriki upendo Wake kwa waumini wote na viongozi hapa,” Kaka Camargo alikiambia chumba cha habari cha Afrika. “Pili, ni kuwasaidia waumini waone jinsi hasa walivyobarikiwa kuwa waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Tatu, kuwasaidia wajifunze kumhusu Yesu Kristo na waishi injili Yake katika nyumba zao na familia zao.

Viongozi walianza matembezi yao kwa kikao cha mafunzo ya uongozi huko Nairobi, Kenya.

Wakati alipoombwa kuhitimisha ujumbe wake kama kiongozi wa Shule ya Jumapili, Kaka Camargo alisema, “Ujumbe wangu unabebwa vyema na [ahadi] ya . . . Rais Russell M. Nelson: tunapofanya kadiri tuwezavyo kuzibadili nyumba zetu kuwa kimbilio la imani na kuwa kiini cha kujifunza injili, waumini watapokea baraka tele. Baraka hizi ni kwamba, baada ya muda, sabato zao zitakuwa hakika zenye furaha, watoto wao watafurahia kujifunza na kuishi injili na ushawishi wa adui utapungua katika maisha yao na yale ya familia zao.”

Kama kiongozi wa Wavulana, Kaka Wilcox alisisitiza umuhimu wa programu ya Watoto na Vijana. Programu, alisema, “inahusu akina kaka na akina dada viongozi wakifanya kazi pamoja na kupanga pamoja ili kuwasaidia vijana [wafanikiwe]. Ni baraka halisi.”

Kutembelea Ethiopia kuna umuhimu wa kipekee kwa Kaka Wilcox, ambaye aliishi nchini humo akiwa mtoto mdogo. “Kuja kwenye eneo hili ni kama kuja nyumbani,” alisema baada ya kuwasili. “Asili yangu ni Afrika, sionekani hivyo, lakini nimekulia hapa, Ethiopia. Niliondoka nilipokuwa na miaka saba na hivyo ninasema, ‘Jambo!’”

Viongozi wanasindikizwa katika huduma yao na washiriki wa Urais wa Eneo la Kati la Afrika.

Matthew L. Carpenter, Rais wa Eneo la Kati la Afrika, alitoa wazo kwamba matembezi ya akina kaka yanaweza kuwasaidia waumini kuishi injili vyema zaidi katika nyumba zao. “Pamoja na uzoefu wao, wanatoa mwongozo wa kufanyia kazi vyema ujifunzaji wa Njoo, Unifuate na programu za Vijana katika eneo la kati la Afrika, ili kwamba wengi wa watoto wa Mungu waweze kunufaika kutokana na dhabihu yake ya upatanisho,” alisema.

“Tunawapenda, tunapata msukumo kutoka kwao na tunatumaini kufanyia kazi kile wanachotufunza ili kwamba tuweze kuwa wafuasi bora zaidi wa Yesu Kristo.”