Liahona
Kuwa Wafuasi, Kuujenga Ufalme
Machi 2024


Ujumbe wa Urais wa Eneo

Kuwa Wafuasi, Kuujenga Ufalme

Ulimwengu unakabiliwa na changamoto nyingi. Lakini, ufalme wa Bwana haujawahi kuwa imara kuliko ulivyo katika siku yetu. Mnamo Aprili 2018, katika hotuba yake ya kwanza kwenye Mkutano Mkuu kwa uumini wa Kanisa, Rais Russell M. Nelson alitangaza, “Mwokozi na Mkombozi wetu, Yesu Kristo, atafanya baadhi ya kazi Zake kuu zaidi kati ya sasa na wakati atakaporudi tena. Tutaona madhihirisho ya kimiujiza kwamba Mungu Baba na Mwana Wake Yesu Kristo, wanasimamia Kanisa hili katika ukuu na utukufu.”1

Na, ndivyo ilivyo. Katika Mkutano Mkuu wa Oktoba 2023, Kanisa lilitangaza ujenzi wa mahekalu mapya 20. Hayo ni mahekalu mengi zaidi kutangazwa katika siku moja kuliko ilivyowahi kutangazwa na kujengwa katika miaka 150 ya mwanzo ya historia ya Kanisa! Wiki chache baadaye, mnamo Novemba 1, Kanisa lilitangaza uundwaji wa misheni 36. Hizo ni misheni nyingi zaidi zilizowahi kuwepo katika Kanisa baada ya miaka 100 ya uwepo wake. Idadi ya mahekalu yaliyotangazwa, yaliyo kwenye ujenzi na yanayofanya kazi sasa ni 335. Idadi ya misheni ulimwenguni kote sasa ni 450. Hizi ni baadhi ya kazi kuu ambazo Bwana anazifanya katika ufalme Wake kwenye siku yetu.

Eneo la Kati la Afrika ni kiini cha yote, changamoto za ulimwengu na miujiza inayotendeka katika ufalme wa Bwana. Misheni zinaundwa na marafiki wengi wanajiunga na Kanisa. Mahekalu mapya yametangazwa na baadhi yapo kwenye ujenzi.

Waumini katika Afrika wanauliza, “Ninawezaje kushinda changamoto zangu binafsi?” au “Ninawezaje kulisaidia Kanisa likue na liimarike?” Tunapokaribia 2024, Urais wa Eneo la Kati la Afrika umezingatia kile tunachoweza kufanya ili kuwasaidia waumini wenye maswali hayo. Tumekusudia kutengeneza Fokasi na Vipaumbele vya Eneo ili vituongoze sisi kama waumini na viongozi kadiri tunavyokabiliana na changamoto katika maisha yetu na kufanya kazi ili kuimarisha Ufalme wa Mungu katika Afrika ya Kati.

Ningependa kushiriki Fokasi na Vipaumbele vya Eneo na kujadili jinsi kila mmoja wetu anavyoweza kuongeza imani yetu na kupokea baraka tunazozitafuta kwa kujumuisha fokasi kwenye maisha yetu binafsi na huduma ya Kanisa katika kipindi cha mwaka 2024.

Fokasi ya Eneo

Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ni Kanisa la Yesu Kristo lililorejeshwa hapa duniani. Yesu Kristo ndiye kiongozi wa Kanisa. Baada ya ufufuko Wake, Yesu aliwauliza viongozi Wanefi, “Je, hamjasoma maandiko, ambayo yanasema, lazima mjivike juu yenu jina la Kristo, ambalo ni jina langu?” Aliwafundisha, “chochote mtakachofanya, mfanye katika jina langu . . . kwa hivyo, mtaliita kanisa katika jina langu; na mtamlingana Baba katika jina langu ili aweze kubariki Kanisa kwa ajili yangu (3 Ne. 27:5, 7).”

Yote tunayoyafanya Kanisani yanafanywa katika jina la Yesu, kwa utukufu Wake na kwa uwezo Wake. Rais Nelson alihitimisha mazungumzo yake ya Mkutano Mkuu wa Aprili 2023 akishuhudia, “Maswali au matatizo yoyote uliyo nayo, jibu daima linapatikana kwenye maisha na mafundisho ya Yesu Kristo. Jifunze zaidi kuhusu Upatanisho Wake, upendo Wake, rehema Yake, mafundisho Yake, na injili Yake iliyorejeshwa ya uponyaji na uendelevu. Mgeukie Yeye! Mfuate Yeye!”2

Maneno ya Rais Nelson ni wito wa kuongeza kina cha ufuasi wetu. Fokasi ya Mpango wa Eneo letu ni kuongeza kina cha imani yetu na ufuasi wetu katika Mwana wa Mungu. Kama vile Mormoni wa zamani kila mmoja wetu anaweza kutangaza, “Tazama, mimi ni mfuasi wa Yesu Kristo, Mwana wa Mungu. . . (3 Ne. 5:13)” na tufanye kazi kudhihirisha hilo katika maisha yetu kila siku. Hiyo ndiyo fokasi ya Eneo la Kati la Afrika.

Vipaumbele

Kadiri kila mmoja wetu anavyofanya kazi ili kuwa mfuasi bora zaidi, kuna maeneo ya maisha yetu ambayo yanahitaji kuboreshwa. Kadiri Urais wa Eneo ulivyozingatia baadhi ya maeneo ambayo yanahitaji maboresho binafsi na ya pamoja katika Eneo letu tumebainisha mambo matatu.

La kwanza ni Kufanya na Kutunza Maagano Matakatifu. Agano ni makubaliano kati ya Mungu na mwanadamu yaliyofanywa rasmi kwa kushiriki katika ibada. Kwa mfano, tunafanya rasmi uamuzi wetu na msimamo wetu wa kumfuata Yesu Kristo na kutii amri Zake kwa kushiriki katika ibada ya ubatizo. Maagano ni njia ya kuimarisha uhusiano wetu na Mungu na Mwana Wake.

Ulimwenguni, tunatumia makubaliano rasmi kutengeneza na kuimarisha uhusiano. Kusaini mkataba na mtu wa kununua au kuuza bidhaa hutengeneza uhusiano halali ulio imara zaidi ya mabadilishano rahisi ya maneno. Kufunga ndoa kulingana na sheria hutengeneza msimamo imara na uwajibikaji kuliko kuishi tu na mtu.

Mungu amesanifu njia ya maagano na ibada kwa ajili ya watoto Wake. Kila agano tunalolifanya na Mungu limekusudiwa kuimarisha uhusiano wetu na Yeye na kupiga hatua kuelekea kuingia kwenye uwepo Wake katika siku za baadaye. Njia hii ya agano huanza na ubatizo. Ubatizo huongoza kwenye uthibitisho. Maagano mengine zaidi matakatifu- endaumenti na kuunganishwa-hufanywa kwenye Nyumba ya Bwana. Wanaume wanatakiwa kufanya agano la ukuhani ili wapokee maagano ndani ya hekalu.

Dhumuni la haya yote ni kumpatia kila mmoja wetu uwezo na nguvu ya kustahimili majaribu na changamoto zetu katika maisha haya. Tunafanya upya uwezo wa maagano yetu kila wiki kwa kujitayarisha na kupokea ishara za kifo cha Kristo kupitia ibada ya sakramenti. Sakramenti hufanya iwezekane kuwa safi na kuwa na wenzi wa daima wa Roho Mtakatifu ili atuongoze karibu na Mungu.

Mwaka huu tunawaalika waumini wote na viongozi wa Kanisa kuingia kwenye maagano ambayo bado hatujayaingia na Mungu na kwa uaminifu zaidi tutimize ahadi tulizozifanya kama sehemu ya maagano. Lengo la kustahili lingeweza kujumuisha lengo la kupokea ibada za hekaluni au kuwa mwenye bidii zaidi katika kushiriki sakramenti kila wiki.

Kujitegemea

Baba wa Mbinguni anamtaka kila mtoto Wake kuwa mwenye kujitegemea. “Kujitegemea ni uwezo, msimamo na juhudi ya kukidhi mahitaji ya kiroho na kimwili ya maisha ya mtu binafsi na familia”3

Tunakuwa wenye kujitegemea kwa kujifunza na kuishi kanuni za kujitegemea katika maisha yetu ya kila siku. Tunapata kuwa wenye kujitegemea kiroho wakati tunaposali, kusoma maandiko, kufunga, kutii amri na kuwatumikia wengine. Tunakuwa wenye kujitegemea kimwili kwa kupata elimu, kufanyia kazi kile tunachopokea, kuweka bajeti ya rasilimali zetu, kulipa zaka na matoleo na kuwasaidia wengine. Fikiria lengo unaloweza kuliweka ili kuwa zaidi mwenye kujitegemea mwaka huu. Tengeneza mpango wa kukusaidia ufanikishe lengo hilo.

Penda, Shiriki na Alika

Kuna maelfu wanaotuzunguka wakitafuta baraka zinazokuja kupitia injili ya Yesu Kristo. Jirani zetu, rafiki zetu, wafanyakazi wenza na wengine tunaokutana nao kila siku ni mabinti na wana wa thamani wa Mungu ambao wanatafuta na wanahitaji baraka za Mungu. Bwana anawaomba wale ambao wamepokea baraka hizi wawasaidie wengine wajifunze upendo Wake kwa ajili yao. Tunaweza kufanya hili kadiri tunavyofikiria njia za kawaida na za asili za kuwaalika wengine kujiunga kwenye shughuli za familia na Kanisa pamoja nasi, kuhudhuria Kanisani au kuwaruhusu wamisionari wawafundishe. Ikiwa tutaomba usaidizi wa Mungu kila siku, atatupatia fursa za kupenda, kushiriki na kuwaalika wengine waingie kwenye zizi la Mungu kupitia ubatizo.

Hitimisho

Ninashuhudia kwamba kwa kuimarisha imani yetu katika Kristo na kufanyia kazi vipaumbele hivi vitatu tutabarikiwa na kuimarishwa katika maisha yetu binafsi na ufalme utaendelea kukua. Na, tutaona miujiza mingi katika siku za mbeleni.

Tanbihi

  1. Rais Russell M. Nelson, ”Ufunuo kwa ajili ya Kanisa, Ufunuo kwa ajili ya Maisha Yetu”, Liahona, Mei 2018.

  2. Rais Russell M. Nelson, “The Answer is Always Jesus Christ”. Liahona, Mei 2023.

  3. General Handbook: Serving in The Church of Jesus Christ of Latter-day Saints, 22.0, Gospel Library.