Liahona
Je, ni Jinsi Gani Maisha Yangu huendana na Mpango wa Milele wa Wokovu wa Baba wa Mbinguni?
Machi 2024


Makala

Je, ni Jinsi Gani Maisha Yangu huendana na Mpango wa Milele wa Wokovu wa Baba wa Mbinguni?

Kama mama mwenye msichana wa miaka minne mwenye usonji, nimehangaika kutafuta majibu ya jinsi ya kumsaidia binti yangu kwenye njia ya agano. Kwa kawaida vitu rahisi kama kukaa kimya, kuwa mnyenyekevu au kuweka umakini kwa wazungumzaji ni ngumu kwake kufanya. Mbali na haya, nimejaribu kumfundisha kanuni nyingi muhimu zenye msingi wa kumjua na kumpenda Mwokozi na lengo la Mungu kwetu katika maisha haya.

Mara kwa mara nilijiuliza jinsi ya kutii amri za Bwana ili kuweza kuwafundisha watoto wetu injili. Mengi ya maandiko yangu pendwa yahusianayo na kufundisha injili wakati mwingine yalikuwa ukumbusho wa huzuni wa kile nisichoweza kufanya.

Kadiri muda ulivyosonga, nilijilaumu mwenyewe na kujiuliza wapi nilikosea, na kama Baba wa Mbinguni alikuwa amenikasirikia.

Kwa sababu ya udhaifu wa binti yangu wa kutokuwa mnyenyekevu au kukaa darasani kwa muda mrefu, mahudhurio ya kanisani yakawa changamoto kwangu. Mwanzoni, nilidhani kwamba siku za kuhudhuria sakramenti si zangu tena. Nilijua nisingeweza kumwacha mtoto wangu nyuma kwa sababu mahudhurio yangu hayakukamilika bila yeye; nilimhitaji karibu nami.

Nimejaribu kupambana, kila wiki nikihudhuria kwa kiasi kikubwa kwenye mkutano wa sakramenti. Nimesali nikiwa njiani kwenda kanisani kwamba walau ningeweza kushiriki sakramenti kabla binti yangu hajaanza vurugu zake.

Nina shukrani kwa himizo la Askofu na imani yake kwenye uwezo wa binti yangu wa kuweza kutulia katika mkutano wa sakramenti. Hakunihukumu kwa kushindwa kumfanya binti yangu awe mnyenyekevu muda wote. Sitasahau siku aliyonipangia kutoa hubiri lihusianalo na jukumu la mama. Nilihisi ni jukumu nililolishindwa lakini haikuwa hivyo kwa askofu wangu. Kwenye Siku ya Akina Mama, Askofu akiwa anajua mara zote huwa naondoka kanisani mapema, alinikimbilia kuhakikisha kwamba yeye mwenyewe ananipatia kadi ya Siku ya Akina Mama na zawadi na hilo lilinigusa sana.

Nimekuja kuhisi hakikisho kutoka kwa Roho Mtakatifu kwamba binti yangu pia, ni wa kipekee na binti anayependwa wa kiroho wa Mungu. Nimejifunza mengi kutoka kwenye upekee wake. Nimejifunza kuweka tumaini langu lote kwa Mungu, nimenyenyekezwa kwa kutokuwa kwake na hatia na hamu yake ya kuendelea kujifunza na kujaribu kufanya vitu rahisi ambavyo wengi hawavijali. Amenifundisha kuwa na shukrani kwa vitu vingi vidogo na rahisi na kuonyesha imani kwa Mungu na muhimu zaidi kuwa na mtazamo wa Milele. Katika njia nyingi zaidi ya moja, yeye ni mfano mkubwa wa mpango wa wokovu wa Mungu wa Milele.

Nina shukrani kwa msaada usio na kikomo na ushawishi chanya ambao baba yake amekuwa nao kwenye maisha yake, akimsaidia kutembea njia hii ya mpango wa wokovu.

Nina ushuhuda kwamba Yesu Kristo ni nguvu ya wazazi, na Yeye alivumilia vitu vyote, ili kwamba Yeye aweze kujua jinsi ya kutufariji. Ombi langu ni kwamba sote tujifunze wakati fulani kutembea njia ya upweke ili kurejea kwa Baba yetu wa Mbinguni wakati tukiendelea kushikilia fimbo ya chuma katikati ya mzaha na vicheko kutoka jengo kubwa na pana.

Katika jina la Yesu Kristo, Amina.