2020
Badiliko Kuu la Moyo
Aprili 2020


Masomo kutoka Kitabu cha Mormoni

Badiliko Kuu la Moyo

Kwa sababu ya Upatanisho wa Yesu Kristo, hatusafishwi tu kutokana na dhambi; tunaweza pia kuponywa kutokana na utendaji dhambi.

Picha
rusted metal heart

Kufuatia Anguko la Adamu, magonjwa na dhambi viliingizwa duniani. Vyote viwili vinaweza kusababisha mauti katika falme zao husika. Kati ya magonjwa yote, labda hakuna ulioenea au unaodhuru kama saratani. Katika baadhi ya mataifa, zaidi ya theluthi moja ya idadi ya watu watapata aina fulani ya saratani, na inachangia karibu robo ya vifo vyote.1 Saratani kawaida huanza na seli moja, ndogo sana inaweza tu kuonekana kwa kutumia hadubini. Lakini ina uwezo wa kukua na kuenea haraka sana.

Wagonjwa wa saratani hufanyiwa matibabu ili kupunguza makali ya saratani. Kupungua kikamilifu kuna maana kwamba hakuna ushahidi wowote wa ugonjwa huo ambao unaonekana. Hata hivyo, wataalamu ni wepesi kusema kwamba ingawaje mgonjwa anaweza kuwa anaonekana kupata nafuu, haimaanishi kwamba amepona.2 Hivyo basi, ingawa kupata nafuu kunaleta faraja na matumaini, wagonjwa wa saratani daima hutumainia kitu ambacho ni zaidi ya kupata nafuu—wanatumaini kupona. Kulingana na chanzo kimoja, “Kuthibitisha mtu amepona kutokana na saratani, mtu anapaswa kusubiri kuona ikiwa saratani itarudi, kwa hivyo, wakati ndicho kipengele muhimu. Kama mgonjwa atabakia katika kupata nafuu kwa miaka kadhaa, saratani inaweza kuwa imepona. Aina fulani ya saratani zinaweza kutokea tena baada ya miaka mingi ya kupata nafuu.”3

Ugonjwa na Dhambi

Kama jinsi saratani ilivyo na madhara makubwa kwenye mwili, dhambi ina madhara zaidi kwa nafsi. Dhambi kawaida huanza kidogo kidogo—wakati mwingine udogo usioweza kutambulika—lakini ina uwezo wa kukua kwa haraka. Inaharibu, kisha kulemaza, na kisha kuangamiza nafsi. Ni chanzo kikuu—kwa kweli, chanzo cha pekee—cha kifo cha kiroho katika uumbaji wote. Matibabu ya dhambi ni toba. Toba ya kweli inafaa kwa asilimia 100 katika kumpatia mtenda dhambi nafuu, au kusababisha msamaha wa dhambi. Msamaha huu huleta faraja na furaha kwa nafsi. Hata hivyo, kupokea msamaha wa dhambi na kuwa huru kutokana na dalili na athari zake haimaanishi kwamba mtenda dhambi ameponywa kikamilifu. Kuna kitu fulani kuhusu moyo wa mwanadamu aliyeanguka ambacho kinawezesha au kinafanya iwe rahisi kutenda dhambi. Hivyo basi, dhambi inaweza kutokea tena, hata baada ya miaka mingi ya kupata nafuu. Kusalia ukiwa na nafuu, au kwa namna nyingine, kudumisha msamaha wa dhambi, ni muhimu kwa ajili ya kupona kikamilifu.

Kusafishwa na Kuponywa

Analojia hii inatusaidia kuelewa kwamba kiroho, hatusafishwi tu kutokana na dhambi lakini pia tunaponywa kutokana na utendaji wa dhambi. Vita ambavyo vinapiganisha nia yetu ya kutenda mema dhidi ya asili yetu ya kutenda maovu inaweza kuchosha. Tukiwa waaminifu, tutakuwa washindi si tu kwa sababu tumeilazimisha nia yetu juu ya asili yetu, lakini kwa sababu tumesalimisha nia yetu kwa Mungu na Amebadili asili yetu.

Mfalme Benyamini alifundisha “Kwani mwanadamu wa kawaida ni adui kwa Mungu, na amekuwa tangu kuanguka kwa Adamu, na atakuwa, milele na milele, asipokubali ushawishi wa Roho Mtakatifu, na kumvua mtu wa kawaida … kupitia upatanisho wa Kristo aliye Bwana” (Mosia 3:19). Katika kujibu haya na mafunzo mengine, watu wa Benyamini walisali, “Ewe tuhurumie, na utumie damu ya upatanisho wa Kristo kwamba tupokee msamaha wa dhambi zetu, na mioyo yetu isafishwe” (Mosia 4:2; msisitizo umeongezwa). Baada ya wao kusali, Bwana alijibu ombi lao lililokuwa na sehemu mbili. Kwanza, “Roho wa Bwana aliwashukia, na wakajazwa na shangwe, wakiwa wamepokea msamaha wa dhambi zao, na kupata amani katika dhamira zao” (Mosia 4:3).

Alipoona kwamba watu wake walikuwa “wamepokea msamaha,” Mfalme Benyamini aliwahimiza kupata tiba kamili kwa kuwafundisha jinsi ya kuhifadhi msamaha (ona Mosia 4:11–30). “Kama mtafanya haya,” aliahidi, “mtapokea furaha daima, na kujazwa na upendo wa Mungu, na daima kuhifadhi msamaha wa dhambi zenu” (Mosia 4:12).

Watu waliamini na kujifunga wenyewe kwa maneno ya Mfalme Benyamini, ambapo Bwana alijibu sehemu ya pili ya sala yao—kwamba “mioyo [yao] isafishwe.” Kwa shukrani na kusifu, watu walilia kwa sauti, “Roho wa Bwana Mwenyezi … ameleta mabadiliko makuu ndani yetu, au mioyoni mwetu, kwamba hatuna tamaa ya kutenda maovu tena, lakini kutenda mema daima” (Mosia 5:2). Mfalme Benyamini alieleza kwamba badiliko hili kuu lilimaanisha kwamba walikuwa wamezaliwa na Mungu (ona Mosia 5:7).

“Je, Inafanywa Vipi?”

Nabii Alma alifundisha kwamba ni sharti tutubu na tuzaliwe tena—tuzaliwe na Mungu, tubadilike katika mioyo yetu (ona Alma 5:49). Tunapoendelea kutubu, Bwana ataondoa dhambi zetu zote na Ataondoa kile ambacho kiasili kinasababisha au kuleta dhambi ndani yetu. Lakini, kwa maneno ya Enoshi, “Bwana, je, inafanywa vipi?” (Enoshi 1:7). Jibu ni rahisi, tena la kina na la milele. Kwa wale ambao wameponywa kutokana na hali yoyote, ya kimwili au kiroho, Bwana alisema, “Imani yako imekufanya mkamilifu” (ona Marko 5:34; Enoshi 1:8).

Badiliko kuu la moyo alilokuwa nalo Alma lilifanyika “kulingana na imani yake,” na mioyo ya wafuasi wake ilibadilika wakati “walipoweka tumaini lao katika Mungu wa kweli na anayeishi” (Alma 5:12, 13). Mioyo ya watu wa Mfalme Benyamini “ilibadilishwa kwa imani katika jina [la Mwokozi]” (Mosia 5:7).

Kama tutakuwa na imani kama hii, ili tuweze kumwamini Bwana kwa moyo wetu wote, ni sharti tufanye kile kinacholeta imani na kisha tufanye kile ambacho imani inaleta. Miongoni mwa vitu vingi ambavyo huleta imani, katika muktadha wa badiliko hili la moyo, Bwana amesisitiza mfungo, sala, na neno la Mungu. Na ingawaje imani huleta vitu vingi, toba ni tunda lake la kwanza.

Fikiria mistari miwili ifuatayo kutoka kitabu cha Helamani ambayo inaonesha kanuni hizi. Kwanza, tunasoma kuhusu watu ambao “walifunga na kuomba kila wakati, na wakapokea nguvu … wakawa imara zaidi na imara katika imani yao ya Kristo … hata kwenye kusafishwa na utakaso wa mioyo yao, utakaso ambao huja kwa sababu ya wao kumtolea Mungu mioyo yao” (Helamani 3:35). Kisha, kutoka kwa Samueli Mlamani, tunajifunza, “Maandiko matakatifu, ndio, utabiri wa manabiii watakatifu, … unawaongoza … kuwa na imani kwa Bwana, na kwenye toba, imani na toba ambavyo, huwaletea mabadiliko katika mioyo” (Helamani 15:7).

Picha
diamond heart

Kumtegemea Mungu

Hapa ni sharti tupumzike na kukiri kwamba badiliko hili kuu tunalolizungumzia linafanyika ndani yetu; halifanywi na sisi. Tuna uwezo wa kutubu, kubadili mienendo yetu, tabia zetu, hata tamaa na imani yetu, lakini hatuna nguvu na uwezo wa kubadili asili yetu. Kwa ajili ya badiliko hili kuu, tunamtegemea kikamilifu Mwenyezi Mungu. Ni Yeye ambaye kwa neema anasafisha mioyo yetu na kubadili asili yetu “baada ya kutenda yote tunayoweza” (2Nefi 25:23). Mwaliko Wake ni imara na wa kweli: “Tubuni, na mje kwangu na moyo wa lengo moja, na nitawaponya [ninyi]” (3 Nefi 18:32; msisitizo umeongezwa).

Athari ya kuponywa kutoka kuwa mwenye dhambi ni kwamba “tubadilishwe kutoka hali [yetu] ya kimwili na kuanguka, hadi hali ya utakatifu … kuwa wana na mabinti zake; Na hivyo [sisi] tunakuwa viumbe vipya” (Mosia 27:25, 26). Nyuso zetu zinanururisha Nuru ya Kristo. Aidha, maandiko yanatuambia kwamba “kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi” (1 Yohana 5:18). Hii si kwa sababu hatuwezi kutenda dhambi, lakini kwa sababu sasa ni asili yetu kutotenda dhambi. Hayo ni mabadiliko makuu, kwa kweli.

Inapaswa kukumbukwa kwamba kupata mabadiliko makuu ya moyo ni mchakato ambao hufanyika baada ya muda, sio wakati mmoja. Kawaida mabadiliko hufanyika polepole, wakati mwingine yanayoongezeka bila kutambulika, lakini ni ya kweli, ni yenye nguvu mno, na yanahitajika.

Kama hujapata uzoefu wa mabadiliko makuu kama hayo, ningekuuliza: Je, umetubu na kupokea msamaha wa dhambi zako? Je, wewe husoma maandiko matakatifu? Je, wewe hufunga na kusali mara kwa mara, kwamba uweze kuwa imara zaidi na zaidi katika imani ya Kristo? Una imani ya kutosha kumwamini Bwana kwa moyo wako wote? Unasimama imara katika hiyo imani? Je, wewe unachunga mawazo, maneno, na vitendo vyako na kushika amri za Mungu? Kama mtafanya vitu hivi, daima mtafurahia na kujazwa na upendo wa Mungu na daima kuhifadhi msamaha wa dhambi zenu. Na ukiendelea kuwa na nafuu, utaponywa, kupata tiba, na kubadilishwa!

Yesu Kristo ana uwezo wa kutusafisha kutokana na dhambi zetu na pia kutuponya kutokana na utendaji dhambi. Ana uwezo wa kuokoa, na kwa sababu hiyo, Ana uwezo wa kubadili. Kama tutampa mioyo yetu, kuwa na imani kwa kufanya mabadiliko yote ambayo tuna uwezo wa kuyafanya, Atatumia uwezo Wake ndani yetu kufanya mabadiliko haya makuu ya moyo (ona Alma 5:14).

Muhtasari

  1. Ona Stacy Simon, “Facts & Figures 2019: US Cancer Death Rate Has Dropped 27% in 25 Years,” American Cancer Society, Jan. 8, 2019, cancer.org.

  2. Ona “Remission: What Does It Mean?” webMD.com.

  3. Cathy Sweat, The Gates to Recovery (2019).