2020
Kupata Imani Yangu Hatua Baada ya Hatua
Aprili 2020


Kupata Imani Yangu Hatua Baada ya Hatua

Kupata ushuhuda inachukua muda. Kawaida inachukua matukio madogo yanayokuja pamoja.

Picha
1. Legs with bare feet, 200 liter barrel being pushed along dirt road. Scene of Zimbabwe in background. 2. Legs walking off page. Pants and shoes suitable for church. African scene in bkgrd. _Spot: Elder Dube approx 22 yrs old bearing testimony from church benches.

Mojawapo ya nyakati muhimu sana katika maisha yangu ilikuwa wakati nikiwa na umri wa miaka 10 wakati nilipotumia wiki mbili kujifunza mafundisho ya Wakatoliki katika misheni ya Loreto Roman Catholic, takriban maili 20 (32 km) mbali na nyumbani kwetu kijijini Silobela, Zimbabwe. Nimekuja kumjua na kumpenda Mwokozi Yesu Kristo na kumtegemea Bwana kupitia masomo na misukumo hii ya awali.

Wakati nilipokuwa katika kanisa la Katoliki, niliona michoro yenye mandhari kutoka Maisha ya Mwokozi ikining’inia kwenye ukuta: mandhari ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo, kufundisha hekaluni, kusali katika Bustani ya Gethsemane, akibeba msalaba kuelekea Kalvari, akisulubiwa Golgotha, na Kufufuka Kwake. Nilihuzunishwa sana kuona misumari na miiba hiyo. Wakati nilipofikia mchoro wa Kusulubiwa, macho yangu yalikuwa yamejawa na machozi. Na kila wakati ningelia na kusema, “Ala, kwa kweli alivumilia mengi, kwa ajili yangu.”

Wakati wa sherehe ya uthibitisho, mmoja wa makasisi alinitazama machoni na kusema, “Wewe ni nuru ya ulimwengu” (ona Mathayo 5:14). Kisha, akionesha mshumaa uliokuwa ukiwaka, alidondoa maneno ya Mwokozi: “Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele za watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.” (Mathayo 5:16).

Nilipojifunza zaidi kuhusu Yesu, nilianza kutaka kuwa mwenye huduma kwa wengine. Kwa mfano, tulihitajika kuteka maji yetu zaidi ya maili tano (8 km) kutoka kijijini kwetu. Kwa kawaida, wanawake katika kijiji, ikijumuisha mama yangu, wangebeba mtungi wa lita 20 uliojaa maji juu ya vichwa vyao. Baada ya uzoefu wangu katika seminari ya Katoliki, mara nyingi nilisukuma mtungi wa lita 200 za maji ili kumsaidia mama yangu, na pia niliwasaidia wajane wengine wawili ambao walikuwa jirani zetu. Ninakumbuka hisia nzuri niliyohisi kila wakati nikiwasaidia wengine.

Uzoefu huu ulisaidia kujenga imani yangu katika Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo na kwa namna isiyo ya moja kwa moja kunitayarisha kukubali injili ya Yesu Kristo wakati nilipokuwa na miaka 22.

Kupokea Kitabu cha Mormoni

Nilikua katika wakati wa mabadiliko nchini mwangu. Wazungu walio wachache wakiongozwa na Ian Smith walitangaza uhuru kutoka kwa Uingereza mwaka 1965. Hilo lilichochea vikwazo kutoka kwa Umoja wa Mataifa na kuanzisha miaka ya vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo viliendelea hadi 1980, ambavyo vilipelekea uhuru wa Zimbabwe. Wakati nilipomaliza masomo yangu, nilihamia jijini kufanya kazi na sikuhudhuria kanisa lolote kwa miaka kadhaa.

Siku moja nilikuwa nikicheza na wana wa bosi wangu. Walikuwa na umri wa miaka tisa na saba. Walisema, “Unajua baba yetu ni rais wa tawi katika Kanisa letu.” Walifafanua maana ya rais wa tawi na, bila kufikiria, nilisema, “Baba yenu hataenda mbinguni.” Niligundua nilikuwa nimefanya kosa kubwa, na nikafikiria bila tumaini kuhusu kile ambacho ningeweza kusema kwao kuwafanya wasahau matamshi yangu. Mwishoni mwa siku, wakati walipomwona baba yao, walimkimbilia na kurudia kile ambacho nilikuwa nimesema. Nilidhani ningepoteza kazi yangu.

Bosi wangu alikuwa amenionesha kabla koti kutoka wakati alipokuwa katika jeshi na ambalo lilionesha alikuwa ameua. Hiyo ndiyo sababu nilisema kile nilichosema. Kwa upole sana, aliniuliza kwa nini nilisema hivyo. Nilisema, “Bosi, kumbuka, uliniambia kwamba uliua vitani. Katika Biblia inasema, ‘Usiue.’”

Aliniuliza kanisa nililokuwa nikihudhuria. Nilimwambia kwamba niliwahi kushiriki katika Kanisa la Kikatoliki lakini sikuwa nimehudhuria kwa miaka saba. Alishiriki matukio kutoka Agano la Kale kuhusu vita na uhasama, na kisha akanipa nakala ya Kitabu cha Mormoni. Nilifurahia sana kwamba sikuwa nimepoteza kazi yangu.

Alinipa Kitabu cha Mormoni mwaka 1981, lakini sikukisoma au hata kukifungua kwa muda wa miaka miwili. Jumapili moja nilikuwa nimechoshwa wakati rafiki zangu walipokuwa wametoka nje ya mji, kwa hivyo nilikichukua kitabu na kwenda katika kituo cha reli kilichokuwa karibu na kukisoma. Niliposoma siku hiyo, niliweza kuhisi motisha ya kufanya mema, lakini kile kilichonigusa sana baadaye katika usomaji wangu ilikuwa 3 Nefi 11. Nilisoma kuhusu Wanefi walionusurika ambao walishuhudia vita na ghasia, na kisha Mwokozi Yesu Kristo akawatokea.

Taifa langu lilikuwa limepitia vita vyetu wenyewe kwa miaka 15. Baadhi ya watu niliokuwa nimekua nao katika kijiji changu walikuwa wameenda vitani na hawakurudi. Wengine walikuwa wamelemazwa maisha yao yote.

Kwa hivyo, nilipokuwa nikisoma kuhusu Wanefi, nilihisi kana kwamba Mwokozi Yesu Kristo alikuwa ananijia wakati Aliposema, “Inukeni na mje kwangu, ili … mguse alama za misumari katika mikono yangu na katika miguu yangu, ili mjue mimi ni Mungu wa Israeli, na Mungu wa ulimwengu wote, na nimeuawa kwa ajili ya dhambi za ulimwengu, (3 Nefi 11:14).

Nilihisi kana kwamba Alikuwa ananitafuta mimi binafsi, na kunialika niende Kwake. Ilinijia kwamba ningeweza kufanya hivi. Ilibadilisha kila kitu.

Kupata Ushuhuda Wangu

Ilichukua miezi kadhaa kupata ujasiri wa kwenda kanisani. Nilijua mahali kanisa lilipokuwa, lakini hapakuwa na wamisionari katika tawi letu dogo. Mnamo Februari 1984, niliingia katika kanisa la Kwekwe. Nilitaka kurudi nje. Sikuwa na hakika kama nilistahili na niliketi upande wa nyuma, tayari kukimbia. Baada ya mazoezi ya ufunguzi, rais wa tawi, Mike Allen, alitoa ushuhuda wake kuhusu Mwokozi Yesu Kristo na Kitabu cha Mormoni. Nilihisi kuhusika. Mtu aliyefuatia pia alitoa ushuhuda wake juu ya Mwokozi na Kitabu cha Mormoni, na hivyo ndivyo wa tatu alivyofanya pia. Nilifurahia sana. Sikuwa na ujasiri wa kwenda kwenye mimbari kwa hivyo, nilisimama pale nilipokuwa na kusema, “Nampenda Yesu. Nasoma Kitabu cha Mormoni.” Na nikaketi chini. Huo ulikuwa mwanzo wa ushuhuda wangu.

Picha
1. Legs with bare feet, 200 liter barrel being pushed along dirt road. Scene of Zimbabwe in background. 2. Legs walking off page. Pants and shoes suitable for church. African scene in bkgrd. _Spot: Elder Dube approx 22 yrs old bearing testimony from church benches.

Shuhuda hizo zilikuwa njia ya Bwana kunifikia kwa sababu ilinisaidia kuhisi kwamba nilikuwa sehemu ya mahali pale. Nilihisi kwamba hawa walikuwa kaka na dada zangu. Katika siku zilizofuata nilisali kwa niaba yao na kwa ajili ya kukubalika. Nilikutana na waumini huko ambao walikuwa wakarimu mno na ambao walinisaidia.

Mengi yalifanyika siku hiyo wakati nilipoingia kanisani. Nawaza ni nini kingetokea kama waumini hao hawangeshiriki shuhuda zao? Huwezi kujua kama kuna mtu fulani anapitia changamoto. Unaposimama na kusema kile unachohisi, inaweza kuwa hasa kile ambacho mtu fulani anahitaji kusikia.

Toa ushuhuda wako kila mara. Mnapofanya hivyo, mnajiimarisha nyinyi wenyewe na wengine walio karibu yenu. Tetea kile unachojua. Unapofuata ushauri kutoka kwenye Kitabu cha Mormoni, utamkaribia Mwokozi.

Mkaribie Mwokozi

Muda niliotumia katika Misheni ya Loreto Roman Catholic uliniweka katika njia ya kuwa mwanafunzi wa Mwokozi Yesu Kristo. Tangu wakati huo nimejifunza kwamba kuwa mwanafunzi ni mchakato na tunahitaji kusonga mbele licha ya udhaifu na mapungufu yetu. Wakati tunapokubali mwaliko: “Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu” (Mathayo 5:48), tutaendelea kuelekea uzima wa milele “amri juu ya amri, kanuni juu ya kanuni” (ona Mafundisho na Maagano 98:12).

Tunajua njia daima haitakuwa rahisi, na tutakumbana na changamoto kadhaa na kuvunjika moyo katika mchakato, lakini kumtegemea Bwana ni njia ya pekee ya kupata amani katika maisha yetu.

Upatanisho wa Mwokozi Yesu Kristo ni kila kitu kwangu. Najua kwamba Mwokozi anatufikia. Tunahitaji kutazama juu, kumfuata Yeye, na kwenda kuwainua wengine jinsi Anavyokuja kutuinua sisi.

Nimejifunza kwamba kuwa mwanafunzi ni mchakato na tunahitaji kuendelea kusonga mbele.

Vielelezo na Greg Newbold