2020
Urejesho Unaoendelea
Aprili 2020


UrejeshoUnaoendelea

Urejesho ulianza katika Msitu Mtakatifu miaka 200 iliyopita na unaendelea leo—na mimi na wewe tunaweza kuwa sehemu yake.

Picha
Joseph Smith kneeling

The Desires of My Heart (First Vision), na Walter Rane

Huu ni wakati wa kupendeza na kusisimua kuwa ulimwenguni. Tumebarikiwa kushiriki katika matukio makuu yanayofanyika katika kipindi cha utimilifu wa nyakati, kama matayarisho kabla ya Ujio wa Pili wa Bwana.1 Tuna nafasi si tu ya kushuhudia matukio haya ya ajabu yakijitokeza lakini pia kuwa sehemu yake.2

Wakati mwingine tunazungumzia Urejesho wa injili kana kwamba ulifanyika kwa wakati mmoja. Miaka mia mbili iliyopita, Ono la Kwanza lilianzisha mchakato, lakini Urejesho kamwe, bila shaka, haukuishia hapo. Kazi ya Bwana kupitia Joseph Smith na washiriki wake iliendelea kwa kutafsiri Kitabu cha Mormoni, kurejesha ukuhani, kuanzisha Kanisa, kuwatuma wamisionari, kujenga mahekalu, kuanzisha Muungano wa Usaidizi wa Akina Mama, na kadhalika. Matukio haya ya Urejesho yalianza mnamo mwaka 1820 na kuendelea maisha yote ya Joseph Smith.

Ajabu ilivyo vitu ambavyo Mungu alifunua kupitia kwa Joseph Smith, Urejesho haukukamilika katika maisha ya Joseph. Kupitia manabii waliomfuata tumepokea vitu kama ukuaji unaoendelea wa kazi ya hekaluni; maandiko ya ziada; kutafsiriwa kwa maandiko katika lugha mbalimbali; kuenezwa kwa injili kote ulimwenguni; kuanzishwa kwa Shule ya Jumapili, Wasichana, Msingi, na akidi za ukuhani; na marekebisho mengi ya mpangilio na utaratibu wa Kanisa.

“Sisi ni mashahidi wa mchakato wa urejesho,” Rais Russell M. Nelson amesema. “Kama unadhani Kanisa limerejeshwa kikamilifu, unashuhudia mwanzo tu. Kuna mengi zaidi yanakuja. … Subiri hadi mwaka ujao. Na kisha mwaka utakaofuata. Kunyweni vidonge vyenu vya vitamini. Pumzikeni. Itakuwa ya kufurahisha.”3

Kwa kukubaliana na tangazo la Rais Nelson kwamba Urejesho unaendelea, tumeona mabadiliko mengi muhimu katika Kanisa kuanzia wakati alipokuwa Rais wake. Miongoni mwa hayo ni kupangwa upya kwa akidi za ukuhani, kuhudumu kuchukua nafasi ya ufundishaji wa nyumbani na wa kutembelea, na kuanzishwa kwa kujifunza injili kunakolenga nyumbani, na kusaidiwa na Kanisa.4 Mabadiliko zaidi yamefanyika tangu wakati huo, na zaidi yanakuja.

Mfano kutoka Afrika Magharibi

Ushuhuda wangu wa asili ya Urejesho unaoendelea uliathiriwa na miaka mitano ambayo nilihudumu katika Urais wa Eneo la Afrika Magharibi. Kuanzia wakati nilipokuwa mvulana, nimekuwa na ushuhuda wa injili. Lakini wakati nilipoishi Afrika, nilishirikiana na baadhi ya Waafrika wa Magharibi wa kwanza kukubali injili. Pia niliona Kanisa likienea kwa haraka kote barani, pamoja na mamia ya kata na vigingi vikiundwa, mahekalu na majumba ya mikutano yakifurika kwa waumini waaminifu, na wanawake na wanaume wema wakiikumbatia, kwa mioyo yao yote, injili ya urejesho. Mbele ya macho yangu niliona kutimizwa kwa unabii wa Joseph Smith kwamba Kanisa “litajaza ulimwengu.”5

Waumini wawili waaminifu kama hao, James Ewudzie na Frederick Antwi, walinisaidia siku moja Acrra Ghana katika Hekalu. Miaka michache kabla ya wamisionari Watakatifu wa Siku za Mwisho kuwasili Ghana, James alikuwa sehemu ya kikundi cha watu 1,000 ambao walitumia Kitabu cha Mormoni na nyenzo zingine za Kanisa katika mikutano yao ya kanisani. Walisali kwa ajili ya siku ambayo Kanisa lingeenda Ghana. Alijiunga na vijana wengine ambao walizunguka nchini Ghana na kufundisha injili jinsi ilivyopatikana katika nyenzo zetu. Mara tu wamisionari walipowasili mwaka 1978, alibatizwa siku ya kwanza wakati ubatizo wa Watakatifu wa Siku za Mwisho ulipofanyika Ghana.

Picha
Frederick Antwi

Fred Antwi, muumini mwanzilishi wa Kanisa kule Ghana

Mapema katika wakati wa Fred kama muumini, alihudhuria mazishi ya jamaa ambaye alikuwa chifu wa kikabila. Hapo aligundua kwamba mpango wa familia ulikuwa kumtawaza awe chifu mpya. Akifahamu kuwa wadhifa kama huo ungemsababisha yeye kufanya vitu ambavyo havikubaliani na imani yake ya injili, alikimbia baada ya maziko na kukataa wadhifa ambao ungemletea umaarufu na mali.

Wakati Hekalu la Accra lilipowekwa wakfu, wote wawili James na Fred walisafiri zaidi ya masaa manne, kwenda tu, kila wiki ili waweze kuwa wahudumu wa hekaluni. Nilipotekeleza ibada pamoja nao, nilijawa na hisia za historia ambazo zilinizunguka. Nikitambua historia ya Kanisa katika Afrika ambayo wawili hao waliiwakilisha, nilihisi ilifanana na kuwa na John Taylor au Wilford Woodruff au waumini wengine wa Kanisa wa mwanzo wakiwa pamoja nami tukizifanya ibada hizo.

Nilichoshuhudia, kupata uzoefu, na kuhisi katika Afrika Magharibi ilikuwa ni sehemu ya kile Bwana alichomwambia Henoko kitafanyika: “Na haki nitaishusha kutoka mbinguni; na ukweli nitaueneza kutoka duniani, ili kutoa ushuhuda wa Mwanangu wa Pekee; … na haki na ukweli nitavifanya viifagie dunia kama vile kwa gharika, ili kuwakusanya wateule wangu kutoka pande nne za dunia.” (Musa 7:62).

Niliona haki na ukweli vikifagia kote katika bara la Afrika na wateule wakikusanywa kutoka upande huo wa ulimwengu. Ushuhuda wangu wa Urejesho uliongezeka kwa sababu nilishuhudia sehemu hiyo muhimu ya Urejesho ikifanyika mbele ya macho yangu.

Pia niliona kitu kingine kuhusu Urejesho unaoendelea: imani changamfu na nguvu za kiroho miongoni mwa waumini Waafrika. Nimemsikia Mzee David A. Bednar wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili akisema, “Kirtland [Ambapo Watakatifu wa Siku za Mwisho waliishi katika miaka ya 1830] haipo tu Ohio. Pia ipo katika Afrika.” Watu wengi wanajiunga na Kanisa katika Afrika kutokana na uzoefu wao binafsi wenye nguvu wa kiroho. Hao waumini wapya huleta nguvu ya kiroho na uhitaji wa kujifunza injili zaidi. Kwao Urejesho unaendelea katika hali ya binafsi. Wanapojifunza zaidi na zaidi kuhusu Kanisa, kweli za injili zinazidi kujitokeza kwenye mtazamo wao. Hilo pia ni kweli kwetu sisi wote tunapozidi kupanua uelewa wetu wa injili.

Njia Tatu za Kusaidia katika Urejesho Unaoendelea

Mungu ametupatia nafasi nzuri kabisa ya kutekeleza wajibu muhimu katika hii kazi. Bwana alisema kwamba “mwili [wa Kanisa] unahitaji kila kiungo” (Mafundisho na Maagano 84:110). Waumini wote wa Kanisa wana baraka ya kushiriki katika Urejesho huu unaoendelea. Tunawawezaje kufanya hivyo?

Njia moja ya kushiriki ni kufanya na kushika maagano matakatifu. Ibada, ikijumuisha ibada za hekaluni, hazina maana mpaka watu hasa wanapofanya na kuyashika maagano yanayohusika na ibada hizo. Dada Bonnie Parkin, aliyekuwa Rais Mkuu wa Muungano wa Usaidizi wa Akina Mama, amefundisha, “Kufanya maagano ni ishara ya moyo wenye kukubali; kushika maagano, ishara ya moyo wa uaminifu.”6

Kwa kufanya na kushika maagano, hatujitayarishi tu kwa ajili ya uzima wa milele, lakini pia tunasaidia kutayarisha na kuimarisha kile ambacho Bwana anakiita “watu wangu wa agano” (Mafundisho na Maagano 42:36). Tunafanya maagano na Mungu na kuwa sehemu ya watu Wake wa agano kupitia ubatizo, uthibitisho, sakramenti, ukuhani wa Melkizedeki, na ibada za hekaluni.

Njia ya pili ambayo tunaweza kushiriki katika Urejesho unaoendelea ni kwa kutimiza wito na majukumu tunayopokea. Hivyo ndivyo Kanisa linavyosonga mbele. Walimu waliojitolea hufundisha injili kwa watoto, vijana, na watu wazima. Akina dada na akina kaka wahudumiaji huwajali waumini binafsi wa Kanisa. Urais na uaskofu hutoa mwongozo kwa vigingi, wilaya, kata, matawi, akidi, mashirika, madarasa, na vikundi. Viongozi wa vijana wanawajali wasichana na wavulana. Makarani na makatibu huhifadhi taarifa muhimu ambayo inarekodiwa mbinguni, na wengine wengi hutekeleza majukumu muhimu katika kuwatayarisha watu kwa ajili ya uzima wa milele na Ujio wa Pili wa Mwokozi.

Picha
members in Ghana

Vijana wakipanga foleni kuingia katika Hekalu la Accra Ghana

Njia ya tatu ambayo tunaweza kushiriki katika Urejesho ni kusaidia kukusanya Israeli. Kutoka siku za mapema za Urejesho, hii imekuwa sehemu muhimu ya kazi hii. Kama ilivyofundishwa na Rais Nelson, tunayo nafasi na jukumu la kusaidia katika kukusanyika ambako kunafanyika pande zote za pazia. Katika ujumbe wake wa kuhitimisha katika mkutano wake mkuu wa kwanza kama Rais wa Kanisa, Rais Nelson kwa maneno mafupi dhahiri alisema, “Ujumbe wetu kwa ulimwengu ni rahisi na wa kweli: tunawaalika watoto wa Mungu wote kutoka pande zote mbili za pazia waje kwa Mwokozi wao, wapokee baraka za hekalu takatifu, wawe na furaha ya kudumu, na kustahili uzima wa milele.”7

Kukusanya Israeli kutoka upande huu wa pazia inamaanisha kazi ya umisionari. Kila mmoja wetu ambaye anaweza kutumikia misheni anapaswa kufikiria juu ya nafasi hiyo kwa umakini. Ninaichukulia kama baraka kubwa kwamba niliweza kutumikia misheni Italia wakati ambapo Kanisa lilikuwa changa mno huko. Matawi yetu yalikutana katika kumbi za kupanga, na tulitumaini ya kwamba siku moja vigingi na kata vingepatikana huko. Nilishuhudia waanzilishi jasiri wakija Kanisani na kuunda msingi wa kukusanya Israeli katika nchi hiyo kuu.

Mmoja wao alikuwa Agnese Galdiolo. Sisi wote tulihisi Roho kwa nguvu wakati alipofundishwa masomo ya umisonari. Lakini, hata kuhisi Roho huyo, alijua kwamba familia yake wangepinga vikali kubatizwa kwake. Wakati fulani, hata hivyo, akiwa amejawa na Roho, alikubali kubatizwa. Lakini akabadili uamuzi wake asubuhi ya ubatizo wake uliokuwa umeratibiwa. Alikuja mapema kwenye ukumbi wa kupanga ambapo angebatizwa kutuelezea kwamba kwa sababu ya upinzani kutoka kwa familia, hangeweza kubatizwa.

Kabla ya kuondoka, alikubali kwamba tungeweza kuzungumza kwa dakika chache. Tulienda katika darasa ambapo tulipendekeza tusali pamoja. Baada ya kupiga magoti, tulimuomba asali. Baada ya sala alisimama akitokwa na machozi na kusema, “Ni sawa, nitabatizwa.” Na dakika chache baadaye alibatizwa. Mwaka uliofuata alifunga ndoa na Sebastiano Caruso, na waliwalea watoto wanne, wote ambao walitumikia misheni na wanaendelea tangu wakati huo kuhudumu Kanisani.

Picha
Caruso family

Mzee na Dada Curtis pamoja na baadhi ya wanafamilia wa familia ya Caruso

Agnese na Sebastiano pia walitumikia misheni, Sebastiano kama rais wa misheni. Wakati nilipotumikia misheni ya pili Italia, miaka 25 baada ya ile ya kwanza, niliweza kuona kile ambacho familia ya Caruso na waanzilishi wengine walikuwa wamefanya ili kupanua ufalme wa Mungu huko. Mimi na wamisionari wangu tulifanya kazi kujenga Kanisa, tukiwa na ndoto kuwa siku moja hekalu lingejengwa Italia. Fikiria furaha yangu kwamba sasa tuna Hekalu la Roma Italia.

Kuna furaha chache ambazo zinaweza kulinganishwa na furaha ya umisionari. Ni baraka kuu iliyoje kuzaliwa wakati ambapo tunaweza kushiriki kwa furaha katika Urejesho unaoendelea kwa kusaidia kukusanya Israeli!

Furaha ya umisionari, bila shaka, haipatikani tu kwa wamisionari pekee. Kila mmoja wetu anaweza kusaidia katika uongofu na kuwarejesha katika uhudhuriaji kamili dada zetu na kaka zetu kwa kufanya kazi pamoja na wamisionari. Tunayo nafasi ya kukusanya Israeli kupitia kuwaalika wengine waje na waone na kwa kushirikiana na wale wanaofundishwa.

Ni kupitia kazi ya hekaluni na historia ya familia ambapo tunasaidia kukusanya Israeli upande mwingine wa pazia. Kwa miaka mingi imekuwa jukumu letu takatifu kuifanya kazi hii. Kabla ya kifo cha Joseph Smith, Watakatifu walifanya ubatizo kwa niaba ya wafu, na wachache walipokea endaumenti zao na kuunganishwa. Baada ya kukamilika kwa Hekalu la Nauvoo, endaumenti kwa ajili ya wanaoishi zilianza kwa bidii. Endaumenti na kuunganishwa kwa ajili ya mababu pia zilianza katika mahekalu ya Utah.

Eliza R. Snow, mshiriki mkuu katika mchakato huo wa urejesho, alielewa umuhimu wa sehemu hiyo ya Urejesho. Alitumia muda mwingi katika nyumba ya endaumenti, akisaidia katika ibada huko.8 Wakati wa utembeleaji mmoja wa Muungano wa Usaidizi wa Akina Mama mnamo mwaka 1869, aliwafundisha dada zake, “Nimekuwa nikitafakari juu ya kazi kuu tunayohitajika kuifanya, hata kusaidia katika wokovu wa wanaoishi na wafu. Tunataka kuwa … wenza wastahiki wa Mungu na Walio Watakatifu.”9

Na, bila shaka, kupatikana kwa ibada za hekaluni kumepanuliwa pakubwa sana na ujenzi wa mahekalu mengi kote ulimwenguni, na mengi yanakuja.

Pamoja na vifaa ambavyo tunavyo kwa matumizi yetu, kazi ya hekalu na historia ya familia inaweza kuwa sehemu ya kawaida ya kushiriki kwetu katika Urejesho unaoendelea. Nimevutiwa na kushiriki katika kazi ya historia ya familia kwa miaka mingi, lakini vifaa vya mtandaoni vimeimarisha pakubwa mafanikio yangu katika kutuma majina hekaluni. Nina kumbukumbu takatifu za kuketi kando ya meza nyumbani kwetu kule Ghana na kutafuta majina ya mababu zangu wa kutoka Uropa ambayo mimi na mke wangu tungeweza kupeleka katika Hekalu la Ghana Accra. Nafasi hiyo ya furaha imetufuata katika sehemu zingine ambazo tumetumwa.

Kupitia kwa Nabii Joseph Smith, Mungu alianza mchakatio wa “kukamilisha urejesho wa mambo yote yaliyonenwa kwa vinywa vya manabii watakatifu tangu mwanzo wa ulimwengu” (Mafundisho na Maagano 27:6). Urejesho huo umeendelea hadi leo pale Mungu “ambapo sasa anayafunua” na “atayafunua mambo mengi makuu na muhimu yahusuyo Ufalme wa Mungu” (Makala ya Imani 1:9). Ninashukuru sana kwamba tuna nafasi ya kushiriki katika Urejesho huu unaoendelea.

Muhtasari

  1. Ona Waefeso 1:10; Mafundisho na Maagano 27:13.

  2. Ona Danieli 2:35–45; Mafundisho na Maagano 65.

  3. Russell M. Nelson, katika “Latter-day Saint Prophet, Wife and Apostle Share Insights of Global Ministry,” Okt. 30, 2018, newsroom.ChurchofJesusChrist.org.

  4. Ona “Mwelekeo wenye Uvuvio,” Liahona, Mei 2019, 121.

  5. Mafundisho ya Marais wa Kanisa: Joseph Smith (2007), 137.

  6. Bonnie D. Parkin, “Kwa Utakatifu wa Moyo,” Liahona, Nov. 2002, 103.

  7. Russell M. Nelson, “Acha Tusonge Mbele,” Liahona, Mei 2018, 118–19. Kwa kurudia wazo hilo, Rais Nelson alisema katika mkutano mkuu mwaka mmoja baadaye: “Na acha tuweke wakfu na kuweka wakfu upya maisha yetu ili kumtumikia Mungu na watoto Wake—pande zote za pazia” (“Maneno ya Kutamatisha,” Liahona, Mei 2019, 112).

  8. Nyumba ya endaumenti ilijengwa katika Temple Square wakati Hekalu la Salt Lake lilipokuwa likijengwa. Ilipowekwa wakfu mwaka 1855, nyumba ya endaumenti ilitumika kwa ajili ya ibada za hekaluni hadi kufikia 1889.

  9. Eliza R. Snow, address to Lehi Ward Relief Society, Okt. 27, 1869, Relief Society Minute Book, 1868–79, Church History Library, 26–27.