Mkutano Mkuu
“Ndipo Nitafanya Mambo Dhaifu Yawe Yenye Nguvu”
Mkutano mkuu wa Aprili 2022


“Ndipo Nitafanya Mambo Dhaifu Yawe Yenye Nguvu”

Tunapojinyenyekeza na kufanya imani katika Yesu Kristo, neema ya Kristo na dhabihu Yake isiyo na mwisho ya upatanisho hufanya iwezekane kubadilika.

Rais Thomas S. Monson aliwahi kushiriki hadithi ya msimamizi wa gereza Clinton Duffy. “Katika miaka ya 1940 na 1950, [Msimamizi Duffy] alijulikana sana kwa juhudi zake za kuwarekebisha wanaume katika gereza lake. Alisema mkosoaji mmoja, ‘Unapaswa kujua kwamba chui hawabadili madoa yao!’

“Msimamizi Duffy akajibu, ‘Unapaswa kujua sifanyi kazi na chui. Ninafanya kazi na wanaume, na wanaume hubadilika kila siku.’”1

Mojawapo ya uwongo mkubwa zaidi wa Shetani ni kwamba wanaume na wanawake hawawezi kubadilika. Uongo huu husemwa na kusemwa tena kwa njia nyingi tofauti kama ulimwengu unavyosema kwamba hatuwezi kubadilika—au kibaya zaidi, kwamba hatupaswi kubadilika. Tunafundishwa kwamba hali zetu hutufafanua. Tunapaswa “kukumbatia utambulisho wetu,” ulimwengu unasema, “na tuwe wakweli kwa nafsi zetu wenyewe.”

Tunaweza Kubadilika

Ingawa kwa hakika ni vizuri kuwa wakweli, tunapaswa kuwa wakweli kwa nafsi zetu halisi, kama wana na mabinti za Mungu wenye asili ya kiungu na hatima ya kuwa kama Yeye. Ikiwa lengo letu ni kuwa wakweli kwa asili hii ya kiungu na hatima, basi sisi sote tutahitaji kubadilika. Neno la kimaandiko la mabadiliko ni toba. “Watu wengi sana,” Rais Russell M. Nelson anafundisha, “huchukulia toba kama adhabu—jambo la kuepukwa isipokuwa katika jambo la muhimu zaidi. … Wakati Yesu anapokuomba wewe na mimi ‘kutubu,’ anatualika tubadilike.”3

Masharti ya Mungu

Watengenezaji wa programu za kompyuta hutumia kauli za masharti kuiambia kompyuta nini cha kufanya. Kauli hizi wakati mwingine hujulikana kama kauli ikiwa. Mfano, ikiwa x ni kweli, basi fanya y.

Bwana pia hufanya kazi kupitia hali: hali ya imani, hali ya wema, hali ya toba. Kuna mifano mingi ya kauli zenye masharti kutoka kwa Mungu kama vile:

Kama ukitii amri zangu na kuvumilia hadi mwisho [ndipo] utakuwa na uzima wa milele, zawadi ambayo ni kubwa zaidi ya zawadi zote za Mungu.”4

Au “kama mtauliza kwa moyo mnyofu, kwa nia ya kweli, mkiwa na imani katika Kristo, [ndipo] atadhihirisha ukweli wake kwako, kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.”5

Hata upendo wa Mungu, ingawa hauna mwisho na mkamilifu, pia hufuata masharti.6 Kwa mfano:

Kama mkizishika amri zangu, [ndipo] mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake.”7

Mzee D. Todd Christofferson alifafanua zaidi juu ya ukweli huu wa injili alipofundisha: “Wengine wamezoea kusema, ‘Mwokozi ananipenda jinsi nilivyo,’ na hiyo ni kweli. Lakini hawezi kumpeleka mmoja wetu katika ufalme Wake kama tulivyo, “kwani hakuna kitu kichafu kinaweza kuishi kule, au kuishi katika uwepo wake.” [Musa 6:57]. Dhambi zetu kwanza lazima zisafishwe.”8

Mambo Dhaifu Yanaweza Kuwa Yenye Nguvu

Baraka ya kupokea nguvu za Mungu ya kutusaidia kubadilika pia ina masharti. Mwokozi, akizungumza kupitia kwa nabii Moroni katika Kitabu cha Mormoni, alifundisha: “Ikiwa watu watakuja kwangu nitawaonyesha udhaifu wao. Ninawapa wanadamu udhaifu ili wawe wanyenyekevu; na neema yangu inatosha kwa watu wote wanaojinyenyekeza mbele yangu; kwani wakijinyenyekeza mbele yangu, na kuwa na imani kwangu, basi nitafanya vitu dhaifu kuwa na nguvu kwao.”9

Tukitazama kwa ukaribu zaidi kile Bwana anachotufundisha hapa, tutaona kwamba Yeye kwanza anasema kwamba anawapa wanaume na wanawake udhaifu, umoja, ambao ni sehemu ya uzoefu wetu wa maisha haya kama viumbe walioanguka au wa kimwili. Tumekuwa wanaume na wanawake wa asili kwa sababu ya Anguko la Adamu. Lakini kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo, tunaweza kushinda udhaifu wetu au asili yetu ya kuanguka.

Kisha anasema kwamba neema Yake inatosha na kwamba kama tutajinyenyekeza na kuwa na imani katika Yeye, ndipo Atafanya “vitu vidhaifu [wingi] kuwa imara kwetu [sisi].” Kwa maneno mengine, tunapobadilisha kwanza asili yetu iliyoanguka, udhaifu wetu, ndipo tutaweza kubadilisha tabia zetu, udhaifu wetu.

Mahitaji ya Mabadiliko

Hebu turejee mahitaji ya kubadilika kulingana na muundo wa Bwana:

Kwanza, ni lazima tujinyenyekeze. Sharti la Bwana la kubadilika ni unyenyekevu. “Kama wanajinyenyekeza mbele yangu,”10 Alisema. Kinyume cha unyenyekevu ni kiburi. Kiburi huwepo wakati tunafikiria tunajua zaidi—wakati kile ambacho sisi tunachowaza au kuhisi kinakuwa na kipaumbele kuliko kile ambacho Mungu anafikiri au anahisi.

Mfalme Benyamini alifundisha kwamba “mwanadamu wa kawaida ni adui kwa Mungu, … na amekuwa tangu kuanguka kwa Adamu, na atakuwa, milele na milele, asipokubali … kumvua mtu wa kawaida na kuwa mtakatifu kupitia upatanisho wa Kristo aliye Bwana, na kuwa kama mtoto, mtiifu, mpole, [na] mnyenyekevu.”11

Ili kubadilika, tunahitaji kumvua mtu wa asili na kuwa wanyenyekevu na watiifu. Ni lazima tuwe wanyenyekevu vya kutosha ili kumfuata nabii aliye hai. Mnyenyekevu vya kutosha ili kufanya na kushika maagano ya hekaluni. Mnyenyekevu kiasi cha kutubu kila siku. Ni lazima tuwe wanyenyekevu kiasi cha kutaka kubadilika, “kutoa mioyo [yetu] kwa Mungu.”12

Pili, ni lazima tuwe na imani katika Yesu Kristo. Tena, maneno ya Mwokozi: “Ikiwa watajinyenyekeza mbele yangu, na kuwa na imani ndani yangu,”13 Atatupa nguvu za kushinda udhaifu wetu. Unyenyekevu, ukiambatana na imani katika Yesu Kristo, utaturuhusu kufikia nguvu wezeshi ya neema Yake na utimilifu wa baraka zinazopatikana kwa sababu ya Upatanisho Wake.

Rais Nelson amefundisha kwamba “toba ya kweli huanza na imani kwamba Yesu Kristo ana uwezo wa kutusafisha, kuponya, na kututia nguvu. … Ni imani yetu inayofungua nguvu za Mungu katika maisha yetu.”14

Tatu, kwa neema Yake anaweza kufanya vitu dhaifu kuwa vyenye nguvu. Kama tunajinyenyekeza na kuwa na imani katika Yesu Kristo, ndipo neema Yake itatuwezesha kubadilika. Kwa maneno mengine, atatuwezesha kubadilika. Hili linawezekana kwa sababu, kama asemavyo, “Na neema yangu inatosha watu wote.”15 Neema yake ya kutia nguvu na ya kuwezesha inatupa nguvu ya kushinda vipingamizi vyote, changamoto zote na udhaifu wote tunapotafuta kubadilika.

Udhaifu wetu mkubwa zaidi unaweza kuwa nguvu zetu kuu. Tunaweza kubadilishwa na “kuwa viumbe vipya.”16 Mambo dhaifu kiuhalisia yanaweza “kuwa na nguvu [kwetu].”17

Mwokozi alifanya Upatanisho Wake usio na mwisho na wa milele ili kwamba kwa kweli tuweze kubadilika, kutubu na kuwa bora zaidi. Tunaweza kweli kuzaliwa mara ya pili. Tunaweza kushinda mazoea, uraibu na hata “hamu ya kufanya maovu.”18 Kama wana na mabinti wa Baba wa Mbinguni mwenye upendo, tuna uwezo ndani yetu wa kubadilika.

Mifano ya Mabadiliko

Maandiko yamejaa mifano ya wanaume na wanawake waliobadilika.

Sauli, Mfarisayo na mtesaji wa kanisa la kwanza la Kikristo,19 akawa Paulo, Mtume wa Bwana Yesu Kristo.

Alma alikuwa kuhani katika nyumba ya Mfalme muovu Nuhu. Alisikia maneno ya Abinadi, akatubu kikamilifu na akawa mmoja wa wamisionari wakuu wa Kitabu cha Mormoni.

Mwanawe Alma alitumia ujana wake kutafuta kuharibu Kanisa. Alikuwa miongoni mwa “watenda dhambi wabaya sana”20 mpaka akawa na badiliko la moyo na akawa mmisionari mwenye nguvu kwa wakati wake mwenyewe.

Musa alilelewa katika familia ya Farao na akalelewa katika maisha ya anasa akiwa mwana mfalme wa Misri. Lakini alipokuja kuelewa yeye alikuwa nani hasa na kujifunza juu ya hatima yake takatifu, alibadilika na kuwa nabii mtoa sheria mkuu wa Agano la Kale.21

Babu wa mke wangu, James B. Keysor, amekuwa akinivutia kila mara kwa mabadiliko makubwa ya moyo wake.22 Akiwa amezaliwa na waasisi waaminifu wa Watakatifu wa Siku za Mwisho katika bonde la Salt Lake mnamo 1906, alimpoteza mama yake katika umri mdogo na alihangaika katika ujana wake wote. Miaka yake ya uvulana na ujana ilitumika mbali na Kanisa; wakati ambapo alikuwa na tabia nyingi mbaya. Hata hivyo, alikutana na kuoa mwanamke mwaminifu na walizaa watoto watano pamoja.

Mnamo 1943, kufuatia miaka migumu ya Mporomoko wa Kiuchumi wa Dunia na wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, Bud, kama alivyoitwa na marafiki na familia, aliondoka Utah na kuhamia Los Angeles, California, kutafuta ajira. Wakati huu akiwa mbali na nyumbani, aliishi na dada yake na mume wake, ambaye alikuwa akihudumu kama askofu wa kata yao.

Kwa upendo na ushawishi wa dada yake na shemeji yake, alianza kufufua shauku yake katika Kanisa na akaanza kusoma Kitabu cha Mormoni kila usiku kabla ya kwenda kulala.

Usiku mmoja, wakati yeye alipokuwa anasoma katika Alma sura ya 34, moyo wake uliguswa wakati alisoma maneno yafuatayo:

“Ndiyo, ningependa kwamba mje mbele na msishupaze mioyo yenu mara nyingine. …

“Kwani tazama, maisha haya ndiyo wakati wa watu kujitayarisha kukutana na Mungu; ndiyo, tazama, wakati wa maisha haya ndiyo siku ya watu kufanya kazi yao wanayohitaji.”23

Wakati yeye alipokuwa akisoma mistari hii, hisia yenye nguvu ilimjia na alijua kwamba alipaswa kubadilika, kutubu na alijua alichopaswa kufanya. Aliinuka kitandani kwake na kupiga magoti na kuanza kuomba, akimsihi Bwana amsamehe na kumpa nguvu alizohitaji kufanya mabadiliko katika maisha yake. Ombi lake lilijibiwa, na tangu wakati huo na kuendelea, hakutazama nyuma kamwe. Bud aliendelea kuhudumu katika Kanisa na alibaki kuwa Mtakatifu wa Siku za Mwisho mwaminifu hadi mwisho wa maisha yake. Alibadilishwa katika kila njia. Akili yake, moyo wake, matendo yake, utu wake vilibadilishwa.

Akina kaka na akina dada, hatima na kusudi letu takatifu hatimaye ni kuwa kama Baba yetu wa Mbinguni na Mwokozi, Yesu Kristo. Tunafanya hivi tunapobadilika, au kutubu. “Tunapokea sura [ya Mwokozi] katika nyuso [zetu].”24 Tunakuwa wapya, safi, tofauti na tunaendelea kufanyia kazi kila siku. Wakati mwingine unaweza kuhisi kama hatua mbili mbele na hatua moja nyuma, lakini tunaendelea kwa unyenyekevu kusonga mbele kwa imani.

Tunapojinyenyekeza na kuonyesha imani katika Yesu Kristo, neema ya Kristo na dhabihu Yake isiyo na mwisho ya upatanisho hufanya iwezekane kubadilika.

Mimi ninatoa ushahidi na kushuhudia kwamba Yesu Kristo kwa kweli ni Mwokozi na Mkombozi wetu. Neema Yake kweli inatosha. Ninatangaza kwamba Yeye ndiye “njia, kweli na uzima.”25 Katika jina la Yesu Kristo, amina.