Mkutano Mkuu
Njoo kwenye Zizi la Mungu
Mkutano mkuu wa Aprili 2022


Njoo kwenye Zizi la Mungu

Ndani ya zizi la Mungu, tunapata uzoefu wa uangalizi wa Mchungaji Mwema, malezi Yake na tunabarikiwa kuhisi upendo Wake wenye kukomboa.

Kama wazazi vijana, Kaka na Dada Samad walijifunza injili ya Yesu Kristo katika nyumba ndogo ya vyumba viwili huko Semarang, Indonesia.1 Wakiwa wameketi kuzunguka meza ndogo, na taa isiyo angavu ambayo ilionekana kuleta mbu wengi kuliko mwanga, wamisionari wawili vijana waliwafundisha kweli za milele. Kupitia maombi ya dhati na mwongozo wa Roho Mtakatifu, walikuja kuamini kile walichofundishwa na kuchagua kubatizwa na kuwa waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Maamuzi hayo, na mpangilio wao wa kuishi tangu wakati huo, umewabariki Kaka na Dada Samad na familia yao katika kila kipengele cha maisha yao.2

Wao ni miongoni mwa Watakatifu waanzilishi wa awali katika Indonesia. Baadaye walipokea ibada za hekaluni, Kaka Samad alitumikia kama rais wa tawi na kisha kama rais wa wilaya, akiendesha gari kote katika Java ya Kati ili kutimiza majukumu yake. Kwa muongo uliopita, yeye ametumikia kama patriaki wa kwanza wa Kigingi cha Surakarta Indonesia.

Picha
Mzee Funk pamoja na Dada na Kaka Samad

Kama mmoja wa wamisionari katika nyumba hiyo ndogo, iliyojawa na imani miaka 49 iliyopita, nilishuhudia kile Mfalme Benyamini alichofudisha katika Kitabu cha Mormoni: “Ningetamani mtafakari juu ya hali ya baraka na yenye furaha ya wale wanaotii amri za Mungu. Kwani tazama, wanabarikiwa katika vitu vyote, vya kimwili na vya kiroho.”3 Baraka ambazo hutiririka katika maisha ya wale ambao wanafuata mfano na mafundisho ya Yesu Kristo, wale wanaochagua kuhesabiwa miongoni mwa wanafunzi Wake, ni nyingi sana, za furaha na za milele.4

Zizi la Mungu

Mwaliko wa Alma wa agano la ubatizo kwa wale walikusanyika katika Maji ya Mormoni huanza na kifungu hiki cha maneno: “kwa vile mnatamani kujiunga na zizi la Mungu.”5

Picha
Flock of sheep in the country side standing next to a rock fence.

Zizi au zizi la kondoo ni boma kubwa, mara nyingi lililojengwa kwa kuta za mawe, ambapo kondoo wanalindwa usiku. Lina mlango mmoja tu. Mwisho wa siku, mchungaji huwaita kondoo. Wanaijua sauti yake, na kupitia katika lango wanaingia katika usalama wa zizi.

Watu wa Alma wangejua kwamba wachungaji husimama kwenye mlango mwembamba wa zizi ili wakati kondoo wanapoingia wanahesabiwa6 na vidonda na maradhi yao yanaonekana na kushughulikiwa mmoja mmoja. Usalama na afya ya kondoo hutengemea utayari wao wa kuja katika zizi na kubaki katika zizi.

Miongoni mwetu yawezekana kuwa na baadhi yetu ambao wanahisi wako kando ya kundi, pengine wanafikiria hawahitajiki sana au hawana thamani kubwa au wao si wa zizi hilo. Na, kama katika zizi la kondoo, katika zizi la Mungu sisi wakati mwingine tunakanyagana vidole na tunahitaji kutubu au kusamehe.

Lakini Mchungaji Mwema7—mchungaji wetu wa kweli—ni mwema daima. Ndani ya zizi la Mungu, tunapata uzoefu wa uangalizi Wake na malezi Yake na tunabarikiwa kuhisi upendo Wake wenye kukomboa. Yeye alisema, “Nimekuchora katika vitanga vya mikono yangu; kuta zako ziko mbele zangu daima.”8 Mwokozi wetu amechora katika vitanga vya mikono yake dhambi zetu, maumivu yetu, masumbuko yetu,9 na yote yasiyo haki katika maisha.10 Wote wanakaribishwa kupokea baraka hizi, kama “wanatamani kuja”11 na kuchagua kuwa katika zizi. Kipawa cha haki ya kujiamulia siyo haki tu ya kuchagua; ni fursa ya kuchagua kilicho sahihi. Na kuta za zizi sio kizuizi bali ni chanzo cha usalama wa kiroho.

Yesu alifundisha kwamba kuna “kundi moja, na mchungaji mmoja.”12 Yeye alisema:

“Aingiaye mlangoni ni mchungaji wa kondoo. …

“Na kondoo humsikia sauti yake … ,

“… na wale kondoo humfuata, kwa maana waijua sauti yake.“13

Yesu kisha akatangaza, “Mimi ndimi mlango; mtu akiingia kwa mimi, ataokoka,”14 akifundisha wazi kwamba kuna njia moja tu kuingia katika zizi la Mungu na njia moja tu ya kuokolewa. Ni kwa na kupitia Yesu Kristo.15

Baraka Huja kwa Wale walio katika Zizi la Mungu

Tunajifunza jinsi ya kuja katika zizi kutokana na neno la Mungu, ambalo ni mafundisho yanayofundishwa na Yesu Kristo na manabii Wake.16 Tunapofuata mafundisho ya Kristo na kuja ndani ya zizi kupitia imani katika Yesu Kristo, toba, ubatizo na uthibitisho, na uaminifu endelevu,17 Alma aliahidi baraka nne mahususi, za kibinafsi. Wewe unaweza (1) “kukombolewa na Mungu,” (2) “kuhesabiwa pamoja na wale wa ufufuko wa kwanza,” (3) “kuwa na uzima wa milele,” na (4) Bwana “atamimina kwa wingi Roho yake juu yako.”18

Baada ya Alma kufundisha kuhusu baraka hizi, watu walipiga makofi ya furaha. Hapa ni kwa nini:

Kwanza: Kukomboa humaanisha kulipa deni au wajibu au kufanya huru kutokana na kitu kinachokusumbua au kuumiza.19 Hakuna kiasi cha uboreshaji binafsi wa sehemu yetu kinachoweza kututakasa kutokana na dhambi tulizofanya au kuponya vidonda tunavyougua bila Upatanisho wa Yesu Kristo. Yeye ni Mkombozi wetu.20

Pili: Kwa sababu ya Ufufuko wa Kristo, watu wote watafufuliwa.21 Baada ya roho zetu kutengana na miili yetu yenye kufa, sisi bila shaka tutatazamia ule wakati sisi tutakapoweza tena kuwa na mwili uliofufuka ili kuwakumbatia wale tunaowapenda. Tunatazamia kwa hamu kuwa miongoni mwa wale wa Ufufuko wa Kwanza.

Tatu: Uzima wa milele humaanisha kuishi pamoja na Mungu na kama Yeye anavyoishi. Ni “kikuu katika vipawa vyote vya Mungu”22 na shangwe yao itakuwa tele milele.23 Ni kusudi na lengo la msingi la maisha yetu.

Nne: Wenzi wa mshiriki wa Uungu, Roho Mtakatifu, hutoa mwongozo unaohitajika sana na faraja wakati wa maisha ya duniani.24

Fikiria baadhi ya sababu za kutokuwa na furaha: taabu huja kutokana na dhambi,25 huzuni na upweke kutokana na kifo cha mpendwa, na hofu kutokana na kukosekana kwa uhakika wa kile kinachotokea tunapokufa. Lakini tunapoingia katika zizi la Mungu na kuyashika maagano yetu na Yeye, tunahisi amani ya kujua na kutumaini kwamba Kristo atatukomboa sisi kutokana na dhambi zetu, kwamba kutenganishwa kwa mwili wetu na roho kutaisha upesi sana, na kwamba tutaishi na Mungu milele katika namna ya utukufu sana.

Kumtumainia Kristo na Kutenda kwa Imani

Akina kaka na akina dada, maandiko yamejaa mifano ya ukuu wa nguvu za Mwokozi na huruma Yake yenye rehema na neema. Wakati wa huduma yake duniani, baraka Zake za uponyaji ziliwajia wale walio mtumainia Yeye na kutenda kwa imani. Kwa mfano, mtu asiyejiweza katika bwawa la Betheseda alitembea wakati, kwa imani yeye alifuata amri ya Mwokozi ya “simama, jitwike godoro lako, uende.”26 Wale waliokuwa wagonjwa au waliosumbuka kwa aina yo yote katika nchi ya Neema waliponywa wakati “kwa hiari” wao “walisonga mbele.”27

Vile vile, ili kupokea baraka hizi za ajabu zilizoahidiwa kwa wale ambao wanakuja ndani ya zizi la Mungu hutuhitaji sisi kufanya hivyo tu—tunahitaji kuchagua kuja. Alma Mdogo alifundisha, “Na sasa ninawaambia kwamba mchungaji mwema anawaita; na ikiwa mtaisikiliza sauti yake atawaleta katika zizi lake.”28

Miaka kadhaa iliyopita rafiki yangu mpendwa alifariki dunia kutokana na saratani. Wakati mke wake, Sharon, alipoandika kwa mara ya kwanza kuhusu uchunguzi wake wa ugonjwa, alisema: “Sisi Tulichagua Imani. Imani katika Mwokozi wetu, Yesu Kristo. Imani katika mpango wa Baba yetu wa Mbinguni, na imani kwamba Yeye anajua mahitaji yetu na anatimiza ahadi Zake.”29

Nimekutana na Watakatifu wa Siku za Mwisho wengi kama Sharon ambao wanahisi amani ya ndani ya kuwa salama ndani ya zizi la Mungu, hasa wakati majaribu, upinzani, au dhiki inapokuja.30 Wao wamechagua kuwa na imani katika Yesu Kristo na kumfuata nabii Wake. Nabii wetu mpendwa, Rais Russell M. Nelson amefundisha, “Kila kitu kizuri maishani—kila baraka inayowezekana ya umuhimu wa milele—huanza na imani.”31

Njoo Kikamilifu kwenye Zizi la Mungu

Babu wa babu wa babu yangu James Sawyer Holman alikuja Utah mwaka 1847, lakini yeye hakuwa miongoni mwa wale waliowasili mwezi Julai pamoja na Brigham Young. Alikuja baadaye mwaka huo na, kulingana kumbukumbu za familia, alikuwa na jukumu la kuwaleta kondoo. Hakufika Bonde la Salt Lake mpaka Oktoba, lakini yeye na kondoo walifika.32

Kuzungumza kiistairi, baadhi yetu bado tuko kwenye nyanda za tambarare. Si kila mtu anawasili katika kundi la kwanza. Marafiki zangu wapendwa, tafadhali endeleeni na safari—na wasaidieni wengine—kuja kikamilifu katika zizi la Mungu. Baraka za injili ya Yesu Kristo hazina kipimo kwa sababu ni za milele.

Ninayo shukrani kuu kuwa muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Ninatoa ushahidi juu ya upendo wa Baba yetu wa Mbinguni na Mkombozi wetu, Yesu Kristo, na juu ya amani ambayo huja kutoka Kwao tu—amani ya ndani na baraka zinazopatikana katika zizi la Mungu. Katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Kama Waindonesia wengi wa kizazi chake, Kaka Samad ana jina moja tu. Mke wake, Sri Katoningsih, na watoto wao wanatumia Samad kama jina lao la ukoo.

  2. Kaka na Dada Samad wanaripoti kwamba angalau watu 44 katika familia yao kuu sasa ni waumini wa Kanisa. Wengine wengi pia wanafurahia baraka za injili kwa sababu ya mfano na huduma yao.

  3. Mosia 2:41.

  4. Ona Mafundisho na Maagano 59:23.

  5. Mosia 18:8.

  6. Ona Moroni 6:4.

  7. Ona Yohana 10:14; ona pia Gerrit W. Gong, “Mchungaji Mwema, Mwanakondo wa Mungu,” Liahona, Mei 2019, 97.

  8. Isaya 49:16.

  9. Ona Alma 7:11–13.

  10. Ona Dale G. Renlund, “Ya Kukasirisha Yasiyo Haki,” Liahona, Mei 2021, 41-44.

  11. Mosia 18:8.

  12. Yohana 10:16.

  13. Yohana 10:2-4.

  14. Yohana 10:9.

  15. Ona 2 Nefi 31:21; Helamani 5:9.

  16. Ona Henry B. Eyring, “The Power of Teaching Doctrine,” Liahona, Julai 1999, 85. Tunapotafuta kuja kwa Kristo, ni lazima tuje kulingana na maneno ya Kristo, “kwani kuna Mungu mmoja na Mchungaji mmoja duniani kote” (ona 1 Nefi 13:40–41).

  17. Mafundisho ya Kristo, kiurahisi yanasema, ni kwamba watu wote kila mahali lazima wafanye imani katika Yesu Kristo na Upatanisho Wake, watubu, wabatizwe, wapokeee Roho Mtakatifu, na kuvumilia hadi mwisho, au kama Mwokozi alivyofundisha katika 3 Nefi 11:38, “hamtarithi ufalme wa Mungu kwa vyo vyote.”

  18. Mosia 18:9, 10.

  19. Ona Merriam-Webster.com Dictionary, “redeem”; ona pia D. Todd Christofferson, “Ukombozi,” Liahona, Mei 2013, 109.

  20. Ona Alma 11:40.

  21. Ona 2 Nefi 2:8; 9:12.

  22. Mafundisho na Maagano 14:7.

  23. Ona 2 Nefi 9:18.

  24. Ona 1 Nefi 4:6; Moroni 8:26.

  25. Ona Mosia 3:24–25; Moroni 41:10.

  26. Yohana 5:8.

  27. 3 Nefi 17:9.

  28. Alma 5:60 Katika Musa 7:53, Masiya pia alisema, “Yeyote aingiaye langoni na kupanda kwa njia ya Mimi kamwe hataanguka.”

  29. Sharon Jones, “Diagnosis,” wechoosefaith.blogspot.com, Mar. 18, 2012.

  30. Hubiri Injili Yangu huelezea “kuvumilia hadi mwisho” kama ifuatavyo: “Kubaki mkweli kwa amri za Mungu na kuwa mkweli kwa ibada za endaumenti na kuunganishwa hekaluni licha ya majaribu, upinzani, na dhiki katika maisha yetu yote. Hii inapendekeza kwamba tutapitia majaribu, upinzani, na dhiki katika maisha yetu yote.

  31. Russell M. Nelson, “Kristo Amefufuka; Imani Kwake Itahamisha Milima,” Liahona, Mei 2021, 102.

  32. Ona wasifu mfupi wa James Sawyer Holman na Naomi Roxina LeBaron Holman na mjukuu wao Grace H. Sainsbury katika possession of the speaker (Charles C. Rich diary, Sept. 28, 1847, Church History Library, Salt Lake City; Journal History of The Church of Jesus Christ of Latter-day Saints, June 21, 1847, 49, Church History Library). Holman alikuwa nahodha katika mwaka wa 1847 wa kundi la Charles C. Rich.