Mkutano Mkuu
Penda, Shiriki, Alika
Mkutano mkuu wa Aprili 2022


Penda, Shiriki, Alika

Tunapopenda, kushiriki, na kualika, tunashiriki katika ile kazi kuu na tukufu ambayo huuandaa ulimwengu kwa ajili ya kurudi kwa Masiya wake.

Waza pamoja nami, kwa dakika, umesimama juu ya mlima katika Galilaya, ukishuhudia maajabu na utukufu wa Mwokozi aliyefufuka akiwatembelea wanafunzi Wake. Ni msukumo wa kushangaza jinsi gani kufikiria wewe binafsi kusikia maneno haya, ambayo Yeye alishiriki nao, maagizo Yake ya dhati “enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu.”1 Kwa kweli, maneno haya yangewezesha, kutia msukumo, na kuleta ari kwa kila mmoja wetu, kama yalivyoleta kwa Mitume Wake. Naam, walijitotolea maisha yao yote kufanya hilo pekee.

Cha kuvutia, sio tu Mitume ambao waliyaweka maneno ya Yesu moyoni. Waumini wa Kanisa la mwanzo, kuanzia wapya hadi wa muda mrefu, walishiriki katika agizo kuu la Mwokozi, kushiriki habari njema ya injili kwa wale waliokutana nao na kuwajua. Azimio la kushiriki ushuhuda wao wa Yesu Kristo lilisaidia Kanisa Lake lililoanzishwa upya kukua kwa mapana.2

Sisi pia, kama wafuasi wa Kristo, tunaalikwa kufuata agizo Lake leo, kama vile tulikuwepo pale juu ya mlima ule katika Galilaya wakati Yeye alipotangaza mara ya kwanza. Agizo hili lilianza tena mnamo 1830, wakati Joseph Smith alipomwekea mikono Samuel kaka yake kama mmisionari wa mwanzo wa Kanisa la Yesu Kristo.3 Tangu wakati huo, zaidi ya wamisionari milioni 1.5 wamesafiri kote ulimwenguni kuyafundisha mataifa yote na kuwabatiza wale waliokubali habari njema za injili iliyorejeshwa.

Haya ndiyo mafundisho yetu. Tamanio letu kuu.

Kuanzia watoto wetu wadogo hadi wazee miongoni mwetu, tunatamani wakati ambapo tunaweza kufuata mwito wa Mwokozi na kushiriki injili pamoja na mataifa ya ulimwengu. Nina hakika ninyi wavulana na wasichana mlihisi changamoto ya kuwezesha kama hiyo kutoka kwa nabii wetu jana alipokuwa anawaalika kujiandaa kwa ajili ya huduma ya umisionari kama Mwokozi alivyofanya pamoja na Mitume Wake.

Kama vile wanariadha wa mbio fupi kwenye vigingi vya kuanzia, tunangojea kwa matarajio ya mwaliko rasmi, uliokamilishwa kwa saini ya nabii, kuashiria kuanza kwa mbio! Tamanio hili ni adilifu na lina mwongozo, hata hivyo, acha tufikirie swali: kwa nini sisi sote tusianze sasa?

Mngeweza kuuliza, “Ni kwa jinsi gani ninaweza kuwa mmisionari bila beji?” Au tunajiambia wenyewe, “Wamisionari wanawekewa mikono kufanya kazi hii. Ningependa kusaidia lakini pengine baadaye wakati maisha yametulia kidogo.”

Akina kaka na akina dada, ni rahisi sana kuliko hivyo! Kwa shukrani, agizo kuu la Mwokozi linaweza kukamilishwa kupitia kanuni rahisi, zinazoeleweka kwa urahisi zinazofunzwa kwa kila mmoja wetu tangu utotoni: penda, shiriki, na alika.

Penda

Kitu cha kwanza tunachoweza kufanya ni kupenda kama Kristo alivyopenda.

Mioyo yetu ina huzuni kwa sababu ya kuteseka na misukusuko ya kibinadamu ambayo tunaiona kote ulimwenguni wakati wa nyakati hizi za ghasia. Hata hivyo, tunaweza pia kupata mwongozo wa faraja tele na ubinadamu ambao umeonyeshwa na watu kila mahali kupitia juhudi zao za kuwafikia waliotelekezwa—wale waliofurushwa kutoka nyumbani kwao, waliotenganishwa na familia zao au kupata aina zingine za huzuni na dhiki.

Hivi karibuni, vyanzo vya habari viliripoti jinsi kundi la akina mama wa Poland, kutokana na kuwajali familia zinazotoroka, waliacha magari ya kubebea watoto kwenye stesheni ya gari moshi katika mstari ulionyooka, tayari na yakiwangojea wanawake na watoto wakimbizi ambao wangeyahitaji wakivuka mpaka kushuka kutoka kwenye gari moshi. Hakika, Baba yetu wa Mbinguni hutabasamu juu ya vitendo vya kujitoa vya hisani kama hivi, kwani tunapobeba mzigo wa mmoja na mwingine, “tunatimiza sheria ya Kristo.”4

Wakati wowote tunapoonyesha upendo kama wa Kristo kwa jirani yetu, tunahubiri injili—hata kama hatusemi hata neno moja.

Kuwapenda wengine ni onyesho la ufasaha la amri kuu ya pili ya kumpenda jirani yetu;5 inaonyesha mchakato wa utakasaji wa Roho Mtakatifu ukifanya kazi ndani ya nafsi zetu. Kwa kuonyesha upendo wa Kristo kwa wengine, tunaweza kuwasababisha wale wanaoona matendo yetu mema “wamtukuze Baba [yetu] aliye mbinguni.”6

Tunafanya hivi bila kutajaria chochote kama malipo.

Tumaini letu, bila shaka, ni watakubali upendo wetu na ujumbe wetu, ingawa vile watakavyofanya haiko katika uthibiti wetu.

Kile tunachofanya na vile tulivyo viko ndani ya uwezo wetu.

Kupitia upendo kama wa Kristo kwa wengine, tunahubiri injili tukufu ya Kristo, yenye sifa za kubadili maisha, na tunashiriki kwa umuhimu katika kutimiza agizo Lake kuu.

Shiriki

Kitu cha pili tunachoweza kufanya ni kushiriki.

Wakati wa miezi ya mwanzoni ya janga la UVIKO-19, Kaka Wisan kutoka Thailand alihisi msukumo kushiriki hisia na uvuvio wake juu ya kile alichokuwa akijifunza katika kusoma kwake Kitabu cha Mormoni katika akaunti yake ya mitandao ya kijamii. Katika mojawapo ya posti zake binafsi hasa, alishiriki hadithi ya wamisionari wawili wa Kitabu cha Mormoni, Amuleki na Alma.

Kaka yake, Winai, ingawaje alijikita katika imani zake za kidini, aliguswa na posti hiyo na kujibu, akiuliza bila kutarajia, “Je, ninaweza kupata kitabu hicho kwa Kithai?”

Wisan kwa hekima alifanya mpango nakala ya Kitabu cha Mormoni kupelekwa na wamisionari wawili wasichana, ambao walianza kumfundisha kaka yake.

Wisan alijiunga katika masomo ya mtandaoni, ambapo alishirki hisia zake kuhusu Kitabu cha Mormoni. Winai alijifunza kusali na kusoma kwa roho ya kutafuta ukweli, kuukubali na kuukumbatia. Ndani ya miezi kadhaa Winai alibatizwa!

Wisan baadaye alisema, “Tuna jukumu la kuwa chombo katika mikono ya Mungu, na lazima daima tuwe tayari kwa ajili Yake kufanya kazi Yake katika njia Yake kupitia sisi.” Muujiza wa familia yao ulikuja kwa sababu Wisan alishiriki tu injili katika njia ya kawaida na ya asili.

Sisi sote tunashiriki vitu na wengine. Tunafanya hivi kila mara. Tunashiriki ni sinema na chakula gani tunapenda, vitu vya kufurahisha tunavyoona, mahali tunapotembelea, sanaa tunazopenda, nukuu zinazotupatia msukumo.

Ni kwa jinsi gani tungeongeza kwenye orodha ya vitu ambavyo tayari tunashiriki kile tunachopenda kuhusu injili ya Yesu Kristo?

Mzee Dieter F. Uchtdorf alifafanua: “Kama mtu anakuuliza kuhusu wikiendi yako, usisite kuongelea juu ya uzoefu wa kanisani. Eleza kuhusu watoto wadogo waliosimama mbele ya mkusanyiko na kuimba kwa shauku jinsi wanavyojaribu kuwa kama Yesu. Zungumza kuhusu kundi la vijana waliotumia muda wao kuwasaidia wazee kwenye nyumba za kupumzika ili kukusanya historia zao binafsi.”7

Kushiriki si kuhusu “kuuza” injili. Hauhitaji kuandika hotuba au kusahihisha mitazamo hasi ya mtu.

Linapokuja suala la kazi ya umisionari, Mungu hakuhitaji wewe kuwa hakimu Wake, Yeye anataka, hata hivyo, kwamba uwe mshiriki Wake.

Kwa kushiriki uzoefu wetu chanya katika injili na wengine, tutashiriki katika kutimiza agizo kuu la Mwokozi.

Alika

Kitu cha tatu unachoweza kufanya ni kualika.

Dada Mayra ni muongofu wa karibuni kutoka Ecuador. Shangwe yake katika injili ilipanda mara moja kufuatia ubatizo wake pale alipowaalika rafiki zake na wapendwa wake kupitia akaunti za mitandao ya kijamii. Wanafamilia na marafiki wengi ambao waliona posti zake walijibu kwa maswali. Mayra aliunganika nao, kila mara akiwaalika nyumbani kwake kukutana pamoja na wamisionari.

Wazazi wa Mayra, ndugu zake, shangazi yake, binamu zake wawili, na marafiki zake kadhaa walibatizwa kwa sababu kwa ujasiri aliwaalika “njoo na uone,” “njoo na utumikie,” na “njoo na uwe wa hapa.” Kupitia mialiko yake ya kawaida na ya asili, zaidi ya watu 20 walikubali mwaliko wake wa kubatizwa kuwa waumini wa Kanisa la Yesu Kristo. Hii ilitokea kwa sababu Dada Mayra aliwaalika tu wengine kupata uzoefu wa shangwe aliyohisi kama muumini wa Kanisa.

Picha
Dada Mayra na wale aliowaalika kupata shangwe ya injili.

Kuna mamia ya mialiko tunayoweza kuitoa kwa wengine. Tunaweza kuwaalika wengine “kuja na kuona” ibada ya sakramenti, shughuli ya kata, video ya mtandaoni ambayo inaelezea injili ya Yesu Kristo. “Njoo na uone” unaweza kuwa mwaliko wa kusoma Kitabu cha Mormoni au kutembelea hekalu jipya wakati wa ufunguzi wake kabla ya kuwekwa wakfu. Wakati mwingine mwaliko ni kitu tunachotoa kutoka ndani—mwaliko kwetu wenyewe, ukitupatia ufahamu na ono la fursa zinazotuzunguka, za kushughulikia.

Katika kizazi chetu cha dijitali, waumini kila mara wanashiriki jumbe kupitia mitandao ya kijamii. Kuna mamia, kama si maelfu, ya mambo ya kuinua unayoweza kuona yanastahili kuyashiriki. Maudhui haya yanatoa mialiko ya “njoo na uone,” “njoo na utumikie,” na “njoo na uwe wa hapa.”

Tunapowaalika wengine wajifunze zaidi kuhusu injili ya Yesu Kristo, tunashiriki katika mwito wa Mwokozi wa kushiriki kwenye kazi ya agizo Lake.

Hitimisho

Akina kaka na dada zangu wapendwa, tumezungumza leo juu ya mambo matatu tu—mambo rahisi—ambayo kila mtu anaweza kufanya. Mambo wewe unayoweza kufanya! Pengine wewe tayari unayafanya—hata bila kutambua kikamilifu kwamba unafanya hivyo!

Ninawaalika mfikirie jinsi mnavyoweza kupenda, kushiriki, na kualika. Mnapofanya hivyo, mnaweza kuhisi kiwango cha shangwe mkijua kwamba mnafuata maneno ya Mwokozi wetu mpendwa.

Kile ninachowahimiza ninyi kufanya si programu mpya. Mmesikia kanuni hizi hapo awali. Hili si “jambo kubwa sana linalofuata” ambalo Kanisa linawaomba mfanye. Mambo haya matatu ni nyongeza tu ya vile tulivyo tayari kama wafuasi wa Yesu Kristo.

Hakuna beji au barua inayohitajika.

Hakuna wito rasmi unaohitajika.

Mambo haya matatu yanapokuwa sehemu asilia ya sisi ni kina nani na jinsi tunavyoishi, yatakuwa onyesho la upendo halisi, usiolazimishwa.

Kama wale wanafunzi wa Kristo ambao walikusanyika pamoja kujifunza kutoka Kwake huko Galilaya miaka 2,000 iliyopita, sisi pia tunaweza kukumbatia agizo la Mwokozi na kwenda kote ulimwenguni kuhubiri injili.

Tunapopenda, kushiriki, na kualika, tunashiriki katika ile kazi kuu na tukufu ambayo huuandaa ulimwengu kwa ajili ya kurudi kwa Masiya wake.

Kwamba tuweze kukubali wito wa Mwokozi na kujitahidi kushiriki katika agizo Lake kuu ndiyo sala yangu katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Mathayo 28:19

  2. Ni nini kilikuwa kiini cha ukuaji wa Kanisa la mwanzo? Mwana historia mmoja anapendekeza: “Kitu cha kwanza ambacho kingeweza kushawishi uchunguzi wa kina kuhusu asili ya imani kingekuwa uchangamani wa moja kwa moja na waaminio wengine. … Kuishi na kufanya kazi bega kwa bega na wale waliomfuata Yesu, kushuhudia tabia zao kwa karibu sana, na kusikiliza wakati wakizungumza kuhusu injili katikati ya shughuli zao za kawaida za kila siku kulipaswa kukabiliwa kwa ushahidi wa maisha yaliyobadilishwa. Kwa namna hii, nguvu ya kuvuta ya imani ya Ukristo lazima kila mara imekuwa si kama tamko la umma la wawakilishi wake mashuhuri kabisa kama ilivyo katika ushuhuda tulivu wa waabuduo wa kawaida wa Yesu wakishuhudia ukweli wa ahadi yao kwa uadilifu wao, uthabiti, na uwazi kwa wengine” (Ivor J. Davidson, The Birth of the Church: From Jesus to Constantine, A.D. 30–312 [2005], 108–9).

  3. Ona Lucy Mack Smith, History, 1845, page 169, josephsmithpapers.org.

  4. Wagalatia 6:2.

  5. Ona Mathayo 22:39.

  6. Mathayo 5:16.

  7. Dieter F. Uchtdorf, “Kazi ya Umisonari: Shiriki Yaliyo Moyoni Mwako,” Liahona, Mei 2019, 17.