Mkutano Mkuu
Fanya Kilicho Muhimu Zaidi
Mkutano mkuu wa Aprili 2022


Fanya Kilicho Muhimu Zaidi

Tunapofokasi maisha yetu kwa Yesu Kristo tutabarikiwa kwa nguvu ya kiroho, kuridhika, na shangwe.

Si muda mrefu uliopita, rafiki mpendwa alipata msukumo wa kumtembelea mwanamke katika kata yake. Alipuuzia uvuvio huo kwa sababu hakuwa akimfahamu yeye vyema—haikuleta maana. Lakini kwa sababu wazo liliendelea kumjia, aliamua kutendea kazi uvuvio huo. Kwa sababu tayari alikuwa akihisi wasiwasi kuhusu matembezi yaliyokaribia, aliamua kwamba kupeleka kitu kwa dada huyo kungepunguza wasiwasi wake. Hakika asingeenda mikono mitupu! Kwa hiyo alinunua kopo la aiskrimu, na aliondoka kuanza kile alichokuwa akihofia kingekuwa matembezi ya kutia waswasi.

Aligonga mlango wa mwanamke huyo, na punde dada alifungua. Rafiki yangu alimpa aiskrimu iliyo katika mfuko wa karatasi ya hudhurungi, na mazungumzo yalianza. Haikuchukua muda mrefu kwa rafiki yangu kutambua kwa nini matembezi hayo yalihitajika. Walipokuwa wameketi pamoja kwenye baraza la mbele, yule mwanamke alisimulia changamoto nyingi alizokuwa akikabiliana nazo. Baada ya saa ya mazungumzo katika hali ya hewa ya joto, rafiki yangu aliona aiskrimu ikiyeyuka kupenya mfuko wa karatasi ya hudhurungi.

Alisema, “Nasikitika sana kwamba aiskrimu yako imeyeyuka!”

Mwanamke kwa upole alijibu, “Ni SAWA! Nina shida ya kung’ata sukari!”

Katika ndoto, Bwana alimwambia nabii Lehi, “Umebarikiwa ewe Lehi, kwa sababu ya vitu ambavyo umetenda.”1

Kuwa mfuasi wa Yesu Kristo kunahusisha zaidi tu ya kutumaini au kuamini. Kunahitaji juhudi, kusonga, na kuweka msimamo. Kunahitaji kwamba tufanye kitu fulani, kuwa “watendaji wa neno, na siyo wasikilizaji tu.”2

Katika suala la aiskrimu iliyoyeyuka, ni nini kilikuwa muhimu zaidi? Aiskrimu? Au kwamba rafiki yangu alifanya kitu?

Nilikuwa na uzoefu mzuri na msichana mpendwa ambaye aliuliza swali la dhati sana: “Dada Craven, ni kwa jinsi gani unajua kwamba kitu chochote kuhusu Kanisa ni kweli? Kwa sababu mimi sihisi chochote.”

Kabla ya kurukia jibu, kwanza nilimuuliza maswali kadhaa. “Niambie kuhusu kujifunza maandiko kwako.”

Alijibu, “Sisomi maandiko.”

Nikauliza, “Je, pamoja na familia yako? Je, mnajifunza Njoo, Unifuate pamoja?”

Alisema, “Hapana.”

Nikamuuliza kuhusu sala zake: “Unahisi nini unaposali?”

Akajibu: “Sisali.”

Jibu langu kwake lilikuwa rahisi: “Kama unataka kujua chochote, itabidi ufanye kitu.”

Je, hiyo si kweli katika chochote tunachotaka kujifunza au kujua? Nilimwalika rafiki yangu mpya kuanza kufanyia kitu injili ya Yesu Kristo: kusali, kujifunza, kuwatumikia wengine, na kumtumaini Bwana. Uongofu hautakuja kama hatufanyi chochote. Unakuja kupitia nguvu ya Roho Mtakatifu kwa makusudi tunapofanya juhudi ya dhati kujua kwa kuomba, kutafuta, na kubisha. Unakuja kwa kufanya.3

Katika Mafundisho na Maagano, Bwana mara kwa mara anasema, “Si muhimu.”4 Inanifanya nitafakari kwamba kama vitu fulani si muhimu, au ni muhimu kidogo, lazima kuna vitu ambavyo ni muhimu zaidi. Katika juhudi zetu za kufanya kitu au kufanya chochote, tungeweza kujiuliza wenyewe, “Ni nini kilicho muhimu zaidi?”

Watangazaji kila mara wanatumia msemo kama “Muhimu” au “Lazima Kuwa Nacho” katika kutumainia kutushawishi tuamini bidhaa wanayouza ni muhimu kwa furaha yetu au ustawi wetu. Lakini je, kile wanachouza kweli ni cha muhimu? Je, ni lazima kweli tuwe nacho? Je, kweli ni muhimu?

Haya ni baadhi ya mawazo ya kuzingatia: Ni nini kilicho muhimu zaidi?

  • Kuna “likes” ngapi tunapata katika posti zetu za mitandao ya kijamii? Au tunapendwa na kuthaminiwa kiasi gani na Baba yetu wa Mbinguni?

  • Kuvaa mtindo mpya kabisa wa nguo? Au kuonyesha heshima kwa miili yetu kwa kuvaa kwa staha?

  • Kutafuta majibu kupitia utafutaji wa intaneti? Au kupokea majibu kutoka kwa Mungu kupitia Roho Mtakatifu?

  • Kutaka vingi zaidi? Au kuridhika na kile tulichopewa?

Rasi Russell M. Nelson anafundisha:

“Mkiwa na Roho Mtakatifu kama mwenzi wenu, mnaweza kuona vizuri kupitia utamaduni wa umaarufu ambao unavutia sana jamii yetu. Mnaweza kuwa werevu zaidi kushinda vizazi vilivyopita. …

“Weka kiwango kwa ajili ya ulimwengu wote!”5

Inahitaji juhudi kubaki umefokasi juu ya kile kilicho muhimu hasa kwa ajili ya furaha ya kudumu. Shetani hapendi kingine chochote zaidi ya sisi kupoteza thamani yetu ya milele, akituongoza kupoteza muda wa thamani, talanta, au nguvu ya kiroho katika vitu ambavyo si muhimu. Ninamwalika kila mmoja wetu kwa sala azingatie vitu hivyo ambavyo vinatuvuruga mawazo tusifanye kilicho muhimu zaidi.

Mwalimu wa mwana wetu mkubwa wa darasa la tatu alifundisha darasa lake “kuwa bosi wa akili yako.” Ilikuwa ukumbusho kwa wanafunzi wake wadogo kwamba wao ni wathibiti wa mawazo yao na kwa hiyo wangeweza kuthibiti kile wanachofanya. Mimi najikumbusha kuwa “bosi wa akili yangu” pale ninapojikuta nikielekea kwenye vitu visivyo muhimu zaidi.

Mwanafunzi wa shule ya upili hivi karibuni aliniambia kwamba imekuwa maarufu kwa vijana wa Kanisa kupuuza amri kwa mpango wa makusudi wa kutubu hapo baadaye. “Ni kitu kama beji ya heshima,” niliambiwa. Hakika Bwana ataendelea kuwasamehe wale ambao wanatubu kwa unyenyekevu “kwa kusudi halisi.”6 Lakini Upatanisho wenye rehema wa Mwokozi haupaswi kamwe kutumika kwa njia ya kejeli kama hiyo. Tunafahamu fumbo la kondoo mmoja aliyepotea. Bila shaka, mchungaji atawaacha wale kondoo 99 ili kumtafuta yule mmoja aliyepotea. Lakini unaweza kufikiria shangwe ambayo wale wanaochagua kuwa 99 huleta kwa Mchungaji Mwema? Wale ambao wanabaki pamoja na kusaidiana kila mmoja kuishi maagano yao? Je, unaweza kupata taswira ya vile ulimwengu, shuleni kwako au kazini kwako au nyumbani kwako kungekuwaje kama utiifu ungekuwa jambo maarufu la kufanya? Si kuhusu kufanya maisha kikamilifu—ni kuhusu kutafuta furaha wakati tukifanya kwa uwezo wetu wote kuishi maagano tuliyoyafanya na Bwana.

Katika ulimwengu unaoonyesha shaka zaidi kuhusu Mungu na mkanganyiko na mashinikizo vikiongezeka, huu ni wakati ambapo lazima tuwe karibu zaidi na nabii. Kwa vile yeye ni msemaji wa Bwana, tunaweza kutumaini kwamba kile anachotuhimiza, kutushauri, na kutusihi sisi tufanye ni mambo ambayo ni muhimu zaidi.

Ingawa inaweza isiwe rahisi, daima kuna njia ya kufanya kitu sahihi. Wakati nikizungumza na kundi la marafiki shuleni, msichana alihisi moyo wake ukivunjika wakati mjadala ulipogeuka kuwa ukosoaji wa viwango vya Kanisa. Aligundua asingeweza kubaki kimya—alipaswa kufanya jambo. Kwa heshima, alizungumza juu ya upendo wa Baba wa Mbinguni na jinsi ambavyo amri Alizoweka zinapaswa kuwabariki na kuwalinda watoto Wake. Ingekuwa rahisi zaidi kwake kutofanya lolote. Lakini ni nini kilicho muhimu zaidi? Kukubaliana na umati? Au kusimama dhahiri kama shahidi wa Mungu “nyakati zote na katika vitu vyote, na katika mahali popote”?7

Ikiwa Kanisa la Urejesho la Yesu Kristo litatoka gizani, sisi lazima tutoke gizani. Kama wanawake watunza maagano, lazima tuangaze nuru yetu ya injili kote ulimwenguni kwa kuchukua hatua na kuwa mifano bora. Tunafanya hili pamoja kama mabinti wa Mungu—jeshi la wanawake milioni 8.2 wa umri wa miaka 11 na zaidi, ambao kazi yao ni sawa. Tunaikusanya Israeli wakati tunaposhiriki katika kazi ya wokovu na kuinuliwa: tukijitahidi kuishi injili ya Yesu Kristo, kuwatunza wale walio na mahitaji, kuwaalika wote kuipokea injili na kuziunganisha familia milele.8 Injili ya Yesu Kristo ni injili ya matendo na injili ya furaha! Hebu tusipuuzie uwezo wetu wa kufanya mambo yale yaliyo muhimu zaidi. Urithi wetu wa kiungu hutupatia ujasiri na kujiamini kufanya na kuwa vyote ambavyo Baba yetu wa Mbinguni anajua tunaweza kuwa.

Dhima ya vijana kwa mwaka huu inatoka Mithali 3:3–6:

“Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe.

“Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako.”

Kipengele muhimu katika kumtumaini Bwana ni kusonga mbele, tukiamini Yeye atatuongoza hata wakati hatuna majibu yote.

Akina Dada, siyo tu kuhusu aiskrimu. Na siyo tu kuhusu kufanya zaidi. Ni kuhusu kufanya kilicho muhimu. Ni kutumia mafundisho ya Kristo katika maisha yetu pale tunapojitahidi kuwa zaidi kama Yeye.

Kadiri tunavyofanya zaidi kuwa imara katika njia ya agano, ndiyo zaidi imani yetu itakua. Na kadiri imani yetu inavyokua, ndivyo zaidi tutatamani kutubu. Na kadiri tunavyotubu, ndivyo zaidi tutaimarisha uhusiano wetu wa agano na Mungu. Uhusiano wa agano unatuvuta kwenye hekalu, kwa sababu kushika maagano ya hekaluni ndiyo jinsi tunavyovumilia hadi mwisho.

Tunapofokasi maisha yetu kwa Yesu Kristo, tutaongozwa kufanya kile kilicho muhimu sana. Na tutabarikiwa na nguvu za kiroho, kuridhika na shangwe! Katika Jina la Yesu Kristo, amina.