Mkutano Mkuu
Uongofu Ndiyo Lengo Letu
Mkutano mkuu wa Aprili 2022


Uongofu Ndiyo Lengo Letu

Hakuna mbadala wa muda unaotumia katika maandiko, kumsikia Roho Mtakatifu akizungumza moja kwa moja na wewe.

Kwa zaidi ya miaka mitatu sasa, tumekuwa katika safari pamoja kama waumini wa Kanisa la Bwana. Ilikuwa Oktoba 2018 wakati Urais wa Kwanza na Akidi ya Mitume Kumi na Wawili walipotualika tujifunze kuhusu Yesu Kristo kwa kusoma maandiko kwa mtindo mpya na wa kutia moyo, kwa nyenzo ya Njoo, Unifuate kama mwongozo wetu.

Katika safari yoyote, ni vyema kutulia mara kwa mara ili kutathmini maendeleo yetu na kuhakikisha kuwa bado tunasonga mbele kuelekea lengo letu.

Uongofu Ndiyo Lengo Letu

Zingatia kauli hii ya kina kutoka kwenye utangulizi wa Njoo, Unifuate:

“Dhumuni la kujifunza na kufundisha injili ni kuongeza uongofu wetu kwa Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo.

“… Aina ya kujifunza injili inayoimarisha imani yetu na kuongoza kwenye muujiza wa uongofu haitokei yote kwa wakati mmoja. Inakwenda zaidi ya darasani mpaka ndani ya mioyo yetu na majumbani mwetu. Inahitaji jitihada endelevu, za kila siku ili kuelewa na kuishi injili. Kujifunza injili ambako kunapelekea uongofu wa kweli kunahitaji ushawishi wa Roho Mtakatifu.”1

Huo ndiyo muujiza tunaotafuta—wakati mtu mmoja anapokuwa na uzoefu katika maandiko,2 na uzoefu huo unabarikiwa na ushawishi wa Roho Mtakatifu. Matukio kama haya ni mawe ya thamani ya msingi kwa uongofu wetu kwa Mwokozi. Na kama vile Rais Russell M. Nelson alivyotukumbusha hivi karibuni, misingi ya kiroho lazima iimarishwe kila mara.3 Uongofu wa kudumu ni mchakato wa maisha yote.4 Uongofu ndiyo lengo letu.

Ili kuwa na ufanisi zaidi, uzoefu wako wa maandiko lazima uwe wako mwenyewe.5 Kusoma au kusikia kuhusu uzoefu na utambuzi wa mtu mwingine kunaweza kusaidia, lakini hiyo haitaleta nguvu sawa ya uongofu. Hakuna mbadala wa muda unaotumia katika maandiko, kumsikia Roho Mtakatifu akizungumza moja kwa moja na wewe.

Roho Mtakatifu Ananifundisha Nini?

Kila wiki ninapofungua mwongozo wangu wa Njoo, Unifuate mimi huandika swali hili juu ya ukurasa: “Roho Mtakatifu ananifundisha nini wiki hii ninaposoma sura hizi?”

Ninapojifunza maandiko, ninatafakari swali hilo tena na tena. Na bila kukosa, hisia za kiroho zinakuja, na ninaziandika katika mwongozo wangu.

Sasa, ninajuaje wakati Roho Mtakatifu anaponifundisha? Vyema, kwa kawaida hutokea kwa njia ndogo ndogo na rahisi. Wakati mwingine kifungu cha maandiko kitaonekana kuruka nje ya ukurasa kuja kwenye umakini wangu. Wakati mwingine, ninahisi kama akili yangu imeangaziwa ufahamu mpana wa kanuni ya injili. Pia ninahisi ushawishi wa Roho Mtakatifu wakati mke wangu, Anne Marie, na mimi tunapozungumza kuhusu kile tunachosoma. Mtazamo wake daima humwalika Roho.

Nabii na Pasaka ya Wayahudi

Mwaka huu tunajifunza Agano la Kale—maandiko matakatifu ambayo hujaza roho zetu kwa nuru. Ninaposoma Agano la Kale, ninahisi kama ninatumia muda pamoja na viongozi ninaowaamini: Adamu, Hawa, Henoko, Nuhu, Ibrahimu, na wengine wengi.

Wiki hii, katika kujifunza Kutoka sura ya 7–13, tunajifunza jinsi Bwana alivyowaweka huru wana wa Israeli kutoka karne nyingi za utumwa huko Misri. Tunasoma kuhusu mapigo tisa—madhihirisho tisa yenye kushangaza ya nguvu za Mungu—ambayo Farao aliyashuhudia bila kulainisha moyo wake.

Kisha Bwana akamwambia nabii Wake, Musa, kuhusu pigo la kumi—na jinsi ambavyo kila familia katika Israeli ingejitayarisha kwa hilo. Kama sehemu ya ibada ambayo wangeiita Pasaka, Waisraeli walipaswa kutoa dhabihu ya mwana-kondoo dume asiye na dosari. Kisha walipaswa kutia alama kwenye miimo ya milango ya nyumba zao kwa damu ya mwana-kondoo. Bwana aliahidi kwamba nyumba zote ambazo zilitiwa alama ya damu zingelindwa kutokana na tauni mbaya ambayo ilikuwa karibu kuja.

Maandiko yanasema, “Na wana wa Israeli … wakafanya kama Bwana …alivyomwamuru Musa” (Kutoka 12:28). Kuna kitu chenye nguvu sana katika kauli hiyo rahisi ya utii.

Kwa sababu wana wa Israeli walifuata ushauri wa Musa na kutenda kwa imani, waliokolewa dhidi ya tauni na, baada ya muda, wakawekwa huru kutoka utumwa wao.

Kwa hivyo, Roho Mtakatifu alinifundisha nini katika sura hizi wiki hii?

Haya ni mawazo machache ambayo yamekaa akilini mwangu:

  • Bwana anafanya kazi kupitia nabii Wake kuwalinda na kuwaokoa watu Wake.

  • Imani na unyenyekevu wa kumfuata nabii vilitangulia muujiza wa ulinzi na ukombozi.

  • Damu kwenye miimo ya mlango ilikuwa ishara ya nje ya imani ya ndani katika Yesu Kristo, Mwana-Kondoo wa Mungu.

Nabii na Ahadi za Bwana

Ninavutiwa na ulinganifu kati ya jinsi Bwana alivyowabariki watu Wake katika tukio hili la Agano la Kale na jinsi anavyowabariki watu Wake leo.

Wakati nabii wa Bwana aliye hai, Rais Nelson, alipotutambulisha kwenye Njoo, Unifuate kama njia ya kujifunza maandiko, alitualika kubadilisha nyumba zetu kuwa mahali patakatifu pa imani na vituo vya kujifunza injili.

Kisha aliahidi baraka nne maalum:

  1. Siku zako za Sabato zitakuwa za furaha,

  2. Watoto wako watafurahia kujifunza na kuishi mafundisho ya Mwokozi,

  3. Ushawishi wa adui katika maisha yako na katika nyumba yako utapungua, na

  4. Mabadiliko haya katika familia yako yatakuwa makubwa na ya kudumu.6

Sasa, hatuna maingizo yoyote ya shajara kutoka kwa wale walioshuhudia Pasaka pamoja na Musa huko Misri. Hata hivyo, tuna ushuhuda mwingi kutoka kwa Watakatifu ambao, kwa imani sawa na hiyo, wanafuata ushauri wa Rais Nelson leo na kupokea baraka zilizoahidiwa.

Hapa kuna shuhuda chache kama hizo:

Mama mmoja wa familia changa alisema: “Tunazungumza kuhusu Kristo na kufurahi katika Kristo nyumbani mwetu. Kwangu mimi hiyo ndiyo baraka kuu—kwamba watoto wangu wanaweza kukua na mazungumzo haya ya injili nyumbani ambayo yanawaleta karibu na Mwokozi.”7

Kaka mmoja mkubwa aliita kujifunza kwake maandiko kupitia Njoo, Unifuate “njia iliyojaa nuru takatifu ambayo hutusaidia kuona mafundisho ya injili ambayo ni muhimu kwa ustawi wetu wa kiroho.”8

Mke kijana alielezea baraka katika ndoa yake: “Nimeweza kuujua moyo wa mume wangu kwa undani zaidi, na nimeweza kumfungulia zaidi moyo wangu pale tunapojifunza pamoja.”9

Mama wa familia kubwa aliona jinsi jitihada zake za kufundisha familia yake zilivyobadilika. Alisema: “Nikitazama nyuma, ilikuwa kana kwamba nilikuwa nikipiga piano nikiwa nimevaa glavu za theluji. Nilikuwa nikipiga mapigo ya muziki, lakini muziki haukuwa sawa kabisa. Sasa nimevua glavu, na wakati muziki wangu bado si mzuri, nasikia utofauti. Njoo, Unifuate imenipa maono, uwezo, fokasi na lengo.”10

Mume kijana alisema: “Vipaumbele vyangu muhimu zaidi nyumbani vimekuwa wazi zaidi tangu nifanye Njoo, Unifuate kuwa sehemu ya kawaida ya asubuhi zangu. Kusoma kunanielekeza kufikiria zaidi kuhusu mambo ambayo ni muhimu zaidi kwangu, kama vile hekalu, uhusiano wangu na mke wangu, na wito wangu. Ninashukuru kwamba nyumbani kwangu ni patakatifu ambapo Mungu hupewa kipaumbele kabla ya kitu kingine.”11

Dada mmoja alishiriki: “Matukio yangu ya kila siku kwenye Njoo, Unifuate si ya kustaajabisha sana, lakini baada ya muda ninaweza kuona jinsi ninavyobadilishwa kwa kujifunza maandiko kwa uthabiti na kwa fokasi. Usomaji wa namna hiyo unaninyenyekeza, kunifundisha, na kunibadilisha kidogo kidogo.”12

Mmisionari aliyerejea aliripoti: “Programu ya Njoo, Unifuate imenisogeza kwenye kiwango cha kujifunza maandiko sawa na kile ambacho nilikifikia kwenye misheni yangu, na nimeweza kutoka kwenye dhana ya kuweka alama ya vema kwenye usomaji wa maandiko hadi kwenye vipindi vya kutajirisha vya kutaka kumjua Mungu.”13

Kaka mmoja alisema: “Ninahisi Roho Mtakatifu akikaribishwa zaidi katika maisha yangu na kuhisi mwongozo wa ufunuo wa Mungu katika kufanya maamuzi. Nina mazungumzo ya kina zaidi kuhusu uzuri katika mafundisho rahisi ya Kristo na Upatanisho Wake.”14

Mtoto mwenye umri wa miaka saba alisema: “Ninabatizwa hivi karibuni, na Njoo, Unifuate inanitayarisha. Mimi na familia yangu tunazungumza kuhusu ubatizo, na sihisi woga kuhusu kubatizwa sasa. Njoo, Unifuate humsaidia Roho Mtakatifu kuja moyoni mwangu, na ninahisi vizuri ninaposoma maandiko.”15

Na hatimaye, kutoka kwa mama wa watoto kadhaa: “Tunapojifunza neno la Mungu, Ameisaidia familia yetu kutoka kwenye wasiwasi hadi kwenye nguvu; kutoka kwenye majaribu na changamoto hadi ukombozi; kutoka kwenye mabishano na ukosoaji hadi upendo na amani; na kutoka kwenye ushawishi wa adui hadi kwenye ushawishi wa Mungu.”16

Hawa pamoja na wafuasi wengine wengi waaminifu wa Kristo kiishara wameweka damu ya Mwana-Kondoo wa Mungu kwenye milango ya nyumba zao. Wanaonyesha msimamo wao wa ndani wa kumfuata Mwokozi. Imani yao hutangulia miujiza. Ni muujiza wa mtu mmoja mwenye uzoefu katika maandiko na uzoefu huo unabarikiwa kwa ushawishi wa Roho Mtakatifu.

Tunapojifunza maandiko, hakuna njaa ya kiroho katika nchi. Kama Nefi alivyosema, “Yeyote atakayesikiliza hilo neno la Mungu, na alizingatie hataangamia; wala majaribu na mishale ya moto ya adui kuwalemea na kuwapofusha ili kuwaelekeza kwenye maangamio” (1 Nefi 15:24).

Katika nyakati za kale, wana wa Israeli walipofuata mwongozo wa Bwana uliotolewa kupitia nabii Musa, walibarikiwa kwa ulinzi na uhuru. Leo, tunapofuata mwongozo wa Bwana uliotolewa kupitia nabii wetu aliye hai, Rais Nelson, tunabarikiwa vile vile kwa uongofu katika mioyo yetu na ulinzi katika nyumba zetu.

Ninashuhudia kwamba Yesu Kristo yu hai. Hili ni Kanisa Lake, lililorejeshwa duniani kupitia Nabii Joseph Smith. Rais Russell M. Nelson ni nabii wa Bwana leo. Ninampenda na kumuidhinisha. Katika Jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Agano la Kale 2022, vii.

  2. “Kila mmoja wetu anawajibika kwa ukuaji wetu binafsi wa kiroho” (Russell M. Nelson, “Hotuba za Ufunguzi,” Liahona,, Nov. 2018, 8).

  3. Ona Russell M. Nelson, “Hekalu na Msingi Wako wa Kiroho,” Liahona, Nov. 2021, 93–96.

  4. Hii ni sababu muhimu kwa nini Rais Nelson ametusihi “kutenga muda kwa ajili ya Bwana! Fanya msingi wako mwenyewe wa kiroho kuwa imara na unaoweza kuhimili majaribu ya kila wakati kwa kufanya mambo yale ambayo yanamruhusu Roho Mtakatifu kuwa pamoja nawe daima” (“Tenga Muda Kwa ajili ya Bwana,” Liahona, Nov. 2021, 120).

  5. “Bila kujali nini wengine wanaweza kusema au kufanya, hakuna hata mmoja anayeweza kamwe kuutoa ushahidi iliobebwa kwenye moyo na akili yako kuhusu nini ni kweli.” (Russell M. Nelson, “Ufunuo kwa ajili ya Kanisa, Ufunuo kwa ajili ya Maisha Yetu,” Liahona, May 2018, 95).

  6. Ona Russell M. Nelson, “Kuwa Mtakatifu wa Siku za Mwisho wa Mfano,” Liahona, Nov. 2018, 113–14. Rais Nelson alirudia mwaliko huu Aprili iliyopita: “Dhamira yako ya kufanya nyumba yako sehemu ya msingi takatifu ya imani haipaswi kamwe kukoma. Wakati imani na utukufu vinapopungua katika ulimwengu huu ulioanguka, hitaji lako la mahali patakatifu utaongezeka. Ninakusihi uendelee kufanya nyumba yako kuwa mahali patakatifu ‘na usiondoshwe’ [Mafundisho na Maagano 87:8; msisitizo umeongezwa] kutoka kwenye lengo hilo la msingi” (“Kile Tunachojifunza na Kamwe Hatutakisahau,” Liahona, Mei 2021, 79).

  7. Ulinganifu binafsi; ona pia 2 Nefi 25:26.

  8. Ulinganifu binafsi.

  9. Ulinganifu binafsi.

  10. Ulinganifu binafsi.

  11. Ulinganifu binafsi.

  12. Ulinganifu binafsi.

  13. Ulinganifu binafsi.

  14. Ulinganifu binafsi.

  15. Ulinganifu binafsi.

  16. Ulinganifu binafsi.