Mkutano Mkuu
Kwa Maana Jinsi Hii Mungu Alitupenda Sisi
Mkutano mkuu wa Aprili 2022


Kwa Maana Jinsi hii Mungu Alitupenda Sisi

Mungu alitupenda sisi hata akamtuma Mwanaye wa Pekee — siyo kutuhukumu, bali kutuokoa.

“Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanaye wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele” (Yohana 3:16). Mara ya kwanza nilipoiona aya hii, sikuwa kanisani au katika jioni ya familia nyumbani. Nilikuwa naangalia tukio la mchezo kwenye runinga. Bila kujali kituo nilichokuwa nikiangalia, na bila kujali ni mchezo gani ulikuwa ukionyeshwa, angalau kulikuwa na mtu mmoja aliyeshikilia bango ambalo lililosomeka “Yohana 3:16.”

Nimekuja vile vile kuipenda aya ya 17: “Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye.”

Mungu alimtuma Yesu Kristo, Mwanaye wa Pekee katika mwili, ili autoe uhai Wake kwa ajili ya kila mmoja wetu. Hili alilifanya kwa sababu Yeye anatupenda sisi na alisanifu mpango kwa ajili ya sisi kurudi nyumbani kwake Yeye.

Lakini hili sio blanketi, la kudaka wote, mpango fulani wa kupata- na- kukosa. Ni wa binafsi, uliowekwa na Baba wa Mbinguni mwenye upendo, anayeijua mioyo yetu, majina yetu, na kile anachotaka sisi tufanye. Kwa nini tunaamini hivyo? Kwa sababu tunafundishwa hilo katika maandiko matakatifu:

Musa mara kwa mara alimsikia Baba wa Mbinguni akizungumza maneno “Musa mwanangu” (ona Musa 1:6; ona pia mstari wa 7, 40). Ibrahimu alijifunza kuwa yeye alikuwa mtoto wa Mungu, aliyeteuliwa kwa ajili ya misheni yake hata kabla ya kuzaliwa (ona Ibrahimu 3:12, 23). Kwa mkono wa Mungu, Esta aliwekwa katika nafasi yenye ushawishi ili awaokoe watu wake (ona Esta 4). Na Mungu alimwamini msichana, mjakazi, kushuhudia juu ya nabii aliye hai ili Naamani aweze kuponywa (ona 2 Wafalme 5:1–15).

Mahususi ninampenda yule mtu mwema, mfupi wa kimo, aliyepanda mti ili amwone Yesu. Mwokozi alijua kuwa alikuwa juu ya ule mti, alisimama, akaangalia juu kwenye matawi, na akasema maneno haya: “Zakayo, … leo imenipasa kushinda nyumbani mwako” (Luka 19:5). Na hatuwezi kumsahau yule mvulana wa umri wa miaka 14 aliyeenda kwenye kijisitu cha miti na akajifunza jinsi mpango ulivyo binafsi hasa: “[Joseph,] Huyu ni Mwanangu Mpendwa. Msikilize Yeye!” (Historia ya—Joseph Smith 1:17).

Akina kaka na akina dada, sisi ndio fokasi ya mpango wa Baba wa Mbinguni na ndio sababu ya misheni ya Mwokozi wetu. Kila mmoja wetu, binafsi, ni kazi Yao na utukufu Wao.

Kwangu mimi, hakuna kitabu cha maandiko kinachofafanua hili kwa uwazi zaidi kuliko ilivyokuwa katika kujfunza kwangu Agano la Kale. Mlango baada ya mlango tunagundua mifano ya jinsi Baba wa Mbinguni na Yehova kwa ukaribu wanavyojihusisha na maisha yetu.

Hivi karibuni tumekuwa tukijifunza kuhusu Yusufu, mwana kipenzi wa Yakobo. Tangu ujana wake alipendwa sana na Bwana, lakini bado alipitia majaribu makubwa kwenye mikono ya kaka zake. Wiki mbili zilizopita, wengi wetu tuliguswa na jinsi Yusufu alivyowasamahe kaka zake. Katika Njoo, Unifuate tunasoma: “Katika njia nyingi, maisha ya Yusufu yanarandana na yale ya Yesu Kristo. Ingawa dhambi zetu zilimsababishia Yeye mateso makuu, Mwokozi anatupatia msamaha, akitukomboa sisi sote kutokana na maangamizi makubwa kuliko njaa. Iwe sisi tunahitaji kupokea msamaha au kuutoa—mahali fulani sisi sote tunahitaji kufanya vyote—mfano wa Yusufu unatuelekeza sisi kwa Mwokozi, aliye chanzo cha kweli cha uponyaji na usuluhishi.”1

Somo ninalolipenda katika hadithi hiyo linatoka kwa kaka yake Yusufu aitwaye Yuda, ambaye alicheza sehemu katika mpango binafsi wa Mungu kwa Yusufu. Yusufu aliposalitiwa na kaka zake, Yuda aliwashawishi wasiutoe uhai wa Yusufu bali wamuuze utumwani (ona Mwanzo 37:26–27).

Miaka mingi baadaye, Yuda na kaka zake walihitaji kumpeleka ndugu yao mdogo zaidi, Benyamini, huko Misri. Mwanzoni baba yao alipinga. Lakini Yuda alitoa ahadi kwa Yakobo—kwamba yeye angemrudisha Benyamini nyumbani.

Huko Misri, ahadi ya Yuda iliwekwa majaribuni. Kijana Benyamini kwa uwongo alishutumiwa kwa kosa la jinai. Yuda, akiwa mkweli kwa ahadi yake, alijitolea afungwe jela badala ya Benyamini. “Kwani,” yeye alisema, “nitawezaje kumwendea baba yangu, na huyu kijana hayuko pamoja nami?” (ona Mwanzo 44:33–34). Yuda alikusudia kutimiza ahadi yake na kumrudisha Benyamini akiwa salama. Je, umewahi kuhisi kuhusu wengine kama Yuda alivyohisi kwa Benyamini?

Je, hivi sivyo wazazi wanavyohisi kuhusu watoto wao? Jinsi wamisionari wanavyohisi kuhusu watu wanaowahudumia? Jinsi viongozi wa Msingi na wa vijana wanavyohisi kuhusu wale wanaowafundisha na kuwapenda?

Bila kujali wewe ni nani au hali yako ya sasa, kuna mtu anahisi hivyo kuhusu wewe. Mtu fulani anataka kurudi kwa Baba wa Mbinguni pamoja na wewe.

Ninawashukuru wale ambao hawakati tamaa juu yetu, ambao wanaendelea kumimina mioyo yao katika sala kwa ajili yetu, na ambao wanaendelea kutufundisha na kutusaidia ili tustahili kurudi nyumbani kwa Baba yetu huko Mbinguni.

Hivi karibuni rafiki yangu mpendwa alitumia siku 233 hospitalini kwa sababu ya UVIKO-19. Katika wakati huo, alitembelewa na marehemu baba yake ambaye aliomba ujumbe upelekwe kwa wajukuu zake. Hata kutoka upande wa pili wa pazia, babu huyu mwema alitamani kuwasaidia wajukuu zake kurudi nyumbani kwao mbinguni.

Kwa ongezeko kubwa, wafuasi ya Kristo wanawakumbuka akina “Benyamini” katika maisha yao. Kote ulimwenguni wamesikia wito wa baragumu ya nabii wa Mungu aliye hai, Rais Russell M. Nelson. Wavulana na wasichana wameingia katika kikosi cha askari vijana wa Bwana. Watu binafsi na familia wanajitolea katika roho ya kuhudumu—kuwapenda, kushiriki, na kuwaalika marafiki na majirani kuja kwa Kristo. Vijana na watu wazima wanakumbuka na wanajitahidi kushika maagano yao—wakiyajaza mahekalu ya Mungu, wakitafuta majina ya marehemu wa familia zao, na kupokea ibada kwa niaba yao.

Je, ni kwa nini mpango binafsi wa Baba wa Mbinguni kwa ajili yetu sisi unajumuisha kuwasaidia wengine kurejea Kwake? Kwa sababu hivyo ndivyo tunavyoweza kuwa kama Yesu Kristo. Hatimaye, hadithi ya Yuda na Benyamini inatufundisha kuhusu dhabihu ya Mwokozi kwa ajili yetu sisi. Kupitia Upatanisho Wake, Yeye aliutoa uhai Wake ili kutuleta sisi nyumbani. Maneno ya Yuda yanaelezea upendo wa Mwokozi: “Nitawezaje kumwendea baba yangu, na [wewe] hauko pamoja nami?” Kama wakusanyaji wa Israeli, haya yanaweza kuwa maneno yetu pia.

Agano la kale limejazwa na miujiza na huruma nyororo ambazo ni sifa bainifu za mpango wa Baba wa Mbinguni. Katika 2 Wafalme, mlango wa 4, kifungu cha maneno “iliangukia juu ya siku” kimetumika mara tatu ili kunisisitizia kwamba matukio muhimu yanatokea kulingana na kalenda ya Mungu, na hakuna maelezo yaliyo madogo sana kwake Yeye.

Rafiki yangu mpya Paulo anashuhudia juu ya ukweli huu. Paulo alikulia katika nyumba ambayo wakati mwingine ilikuwa na unyanyasaji na daima isiyovumilia dini. Wakati akihudhuria shule kwenye kambi ya jeshi huko Ujerumani, aliwaona akina dada wawili ambao walionekana kuwa na nuru ya kiroho. Kuwauliza kwa nini wao walionekana kuwa tofauti kulileta jibu kwamba wao ni wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.

Muda mfupi baadaye Paulo alianza kukutana na wamisionari na alialikwa Kanisani. Jumapili iliyofuata, alipokuwa akishuka kwenye basi, aliwaona wanaume wawili waliovaa mashati meupe na tai. Aliwauliza kama wao walikuwa wazee wa Kanisa. Walimjibu ndiyo, hivyo Paulo akawafuata.

Wakati wa ibada, mhubiri aliwachagua watu waliokuwa mkutanoni na kuwakaribisha kushuhudia. Mwisho wa kila ushuhuda, mpiga ngoma alipiga ngoma na mkutano uliitikia, “Amina.”

Mhubiri alipomchagua Paulo, Paulo alisimama na kusema, “Ninajua Joseph Smith alikuwa nabii na Kitabu cha Mormoni ni cha kweli.” Hakukuwa na mlio wa ngoma au amina. Paulo mwishowe alitambua kwamba alikuwa ameenda mahali pasipo sahihi. Punde, Paulo aliipata njia yake ya kwenda mahali sahihi na alibatizwa.

Siku ya ubatizo wa Paulo, mgeni mmoja alimwambia, “Wewe uliokoa maisha yangu.” Wiki chache mwanzoni, mtu huyu aliamua kutafuta kanisa jingine na alihudhuria ibada ya ngoma na amina. Wakati yule mtu alipomsikia Paulo akitoa ushuhuda wake juu ya Joseph Smith na Kitabu cha Mormoni, alitambua kwamba Mungu alimjua, alitambua mahangaiko yake, na alikuwa na mpango kwa ajili yake. Kwa wote Paulo na yule mtu, hakika “iliwaangukia siku ile!”

Sisi pia tunajua kwamba Baba wa Mbinguni anao mpango binafsi wa furaha kwa ajili ya kila mmoja wetu. Kwa sababu Mungu alimtuma Mwanaye Mpendwa kwa ajili yetu, miujiza tunayoihitaji “itaangukia siku hiyo” muhimu hasa kwa ajili ya mpango Wake kutimizwa.

Ninashuhudia kwamba mwaka huu tunaweza kujifunza zaidi kuhusu mpango wa Mungu kwa ajili yetu katika Agano la Kale. Juzuu hiyo takatifu inafundisha kuhusu jukumu la manabii katika nyakati za mashaka na mkono wa Mungu katika ulimwengu ambao umekanganyikiwa na mara nyingi wenye mabishano. Pia ni kuhusu waumini wanyenyekevu ambao kwa uaminifu walitazamia kuja kwa Mwokozi wetu, kama vile ambavyo tunatazamia na kujitayarisha kwa ajili ya Ujio Wake wa Pili—ujio Wake uliotabiriwa zamani, wenye utukufu.

Hadi siku hiyo, yawezekana tusione kwa macho yetu ya asili usanifu wa Mungu kwenye vipengele vyote vya maisha yetu (ona Mafundisho na Maagano 58:3). Lakini tunaweza kukumbuka jibu la Nefi alipokuwa akikabiliwa na kitu ambacho hakukielewa: wakati alipokuwa hajui maana ya mambo yote, alijua kwamba Mungu anawapenda watoto Wake (ona 1 Nefi 11:17).

Huu ni ushahidi wangu katika siku hii nzuri ya asubuhi ya Sabato. Na tuuandike mioyoni mwetu na kuruhusu ujaze nafsi zetu kwa amani, tumaini, na shangwe ya milele: Kwa maana jinsi hii Mungu alitupenda sisi hata akamtoa Mwanaye wa Pekee—siyo kutuhukumu bali kutuokoa sisi. Katika Jina la Yesu Kristo, amina.