Mkutano Mkuu
Kuuponya Ulimwengu
Mkutano mkuu wa Aprili 2022


Kuuponya Ulimwengu

Majeraha na tofauti vinaweza kutatuliwa na hata kuponywa wakati tunapomheshimu Mungu, Baba yetu sote na Yesu Kristo, Mwana Wake.

Akina kaka na akina dada, katika msimu huu mtukufu wa Pasaka, tumebarikiwa sana kukutana na kupokea ushauri na maelekezo kutoka kwa watumishi wa Mungu.

Mwongozo na mafundisho matakatifu kutoka kwa Baba yetu wa Mbinguni hutusaidia kufanya chaguzi katika nyakati hizi za hatari. Kama ilivyotabiriwa, “moto na tufani,” “vita, uvumi wa vita na mitetemeko mahali mbali mbali,” “na kila aina ya machukizo,”1 “tauni,”2 “njaa, na magonjwa”3 vinaangamiza familia, jamii na hata mataifa.

Kuna janga lingine linalouathiri ulimwengu: mashambulizi kwenye uhuru wako na wangu wa dini. Mtazamo huu unaokua unatafuta kuondoa dini na imani katika Mungu kutoka kwenye maeneo ya umma, mashuleni, viwango vya jamii na mijadala ya kiraia. Wapinzani wa uhuru wa dini wanatafuta kuweka vikwazo kwenye madhihirisho ya hisia za moyoni. Wanakosoa na hata kufanyia mzaha tamaduni za imani.

Tabia kama hiyo huwakandamiza watu, huondoa thamani kwenye kanuni binafsi, usawa, heshima, mambo ya kiroho na amani ya nafsi.

Uhuru wa dini ni nini?

Ni uhuru wa kuabudu katika mifumo yake yote: uhuru wa kukusanyika, uhuru wa kuzungumza, uhuru wa kutenda kwenye imani binafsi na uhuru kwa ajili ya wengine kufanya vivyo hivyo. Uhuru wa dini unamruhusu kila mmoja wetu kujiamulia wenyewe kile tunachoamini, jinsi tunavyoishi na kutenda kulingana na imani yetu na nini Mungu hutarajia juu yetu.

Juhudi za kuzuia uhuru wa dini si mpya. Kote katika historia, watu wanaoamini mafundisho ya dini wameteseka vikali mikononi mwa wengine. Waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho wamejumuishwa pia.

Tangu mwanzo wetu, wengi wamtafutao Mungu walivutwa kwenye Kanisa hili kwa sababu ya mafundisho yake ya injili takatifu, ikiwa ni pamoja na imani katika Yesu Kristo na Upatanisho Wake, toba, mpango wa furaha na Ujio wa Pili wa Bwana wetu.

Upinzani, mateso na vurugu vilimkabili nabii wetu wa kwanza wa siku za mwisho, Joseph Smith na wafuasi wake.

Katikati ya machafuko mnamo 1842, Joseph alichapisha kanuni za msingi 13 za Kanisa linalokua, ikiwa ni pamoja na hii: “Tunadai haki ya kumwabudu Mungu Mwenyezi kulingana na mwongozo wa dhamiri yetu sisi wenyewe, na tunawaruhusu watu wote haki hiyo, na waabudu namna, mahali, au chochote watakacho.”4

Kauli yake ni jumuishi, yenye kuweka huru na yenye heshima. Hicho ndicho kiini cha uhuru wa dini.

Nabii Joseph Smith pia alisema:

“Nina ujasiri kutangaza mbele ya Mbingu kwamba niko tayari kufa katika kutetea haki za Mpresibiteri, Mbaptisti, au mtu mwema wa dhehebu lingine lolote; ikiwa kanuni ile ile ambayo itakiuka haki za … Watakatifu itakiuka haki za Wakatoliki, au za dhehebu lingine lolote ambalo si maarufu na dhaifu kujitetea.

“Ni kupenda uhuru [ambako] kunaivutia nafsi yangu—uhuru wa kiraia na uhuru wa dini kwa jamii yote ya wanadamu.”5

Bado, waumini wa mwanzo wa Kanisa walishambuliwa na kufukuzwa maelfu ya maili, kutoka New York kwenda Ohio mpaka Missouri, ambapo gavana alitoa amri kwamba waumini wa Kanisa “lazima wachukuliwe kama maadui na lazima wauwawe au waondoshwe jimboni.”6 Walikimbilia Illinois, lakini mateso yaliendelea. Kundi la wahalifu lilimuua Nabii Joseph, wakidhani kwamba kumuua kungeharibu Kanisa na kuwatawanya waaminio. Bali waaminifu walibaki imara. Mrithi wa Joseph, Brigham Young, aliwaongoza maelfu kwenye safari ya kufurushwa maili 1,300 (km 2,100) magharibi mpaka kwenye ile ijulikanayo sasa kama Jimbo la Utah.7 Mababu zangu walikuwa miongoni mwa walowezi waanzilishi wa mwanzo.

Tangu siku hizo za mateso makali, Kanisa la Bwana limekua kwa uimara kufikia takriban waumini milioni 17, zaidi ya nusu wakiishi nje ya Marekani.8

Mnamo Aprili 2020 Kanisa letu lilisherehekea kumbukizi ya miaka 200 ya Urejesho wa injili kwa tangazo kwa ulimwengu, lililoandaliwa na Urais wetu wa Kwanza na Akidi ya Mitume Kumi na Wawili. Linaanza, “Kwa dhati tunatangaza kwamba Mungu anawapenda watoto wake katika kila taifa la ulimwengu.”9

Nabii wetu mpendwa, Rais Russell M. Nelson alielezea zaidi:

“Tunaamini katika uhuru, ukarimu, na usawa kwa watoto wote wa Mungu.

“Sisi sote ni kaka na dada, kila mmoja mtoto wa Baba wa Mbinguni mwenye upendo. Mwana Wake, Bwana Yesu Kristo, anawaalika wote kuja Kwake, ‘weusi na weupe, wafungwa na walio huru, waume kwa wake.’(2 Nefi 26:33).”10

Fikiria pamoja nami njia nne ambazo jamii na watu binafsi wananufaika kutokana na uhuru wa dini.

Kwanza. Uhuru wa dini unaheshimu amri kuu ya kwanza na ya pili, ukimuweka Mungu kama kiini cha maisha yetu. Tunasoma kwenye Mathayo:

“Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote.”11

“Na ya pili yafanana nayo, Mpende jirani yako kama nafsi yako.”12

Iwe ni kanisani, kwenye sinagogi, msikitini au kwenye nyumba yenye paa la madebe, wafuasi wa Kristo na waaminio wengine wenye mawazo sawa na hayo, wanaweza kuelezea msimamo kwa Mungu kwa kumwabudu Yeye na utayari wa kuwahudumia watoto Wake.

Yesu Kristo ni mfano mkamilifu wa upendo na huduma hiyo. Wakati wa huduma Yake, aliwajali masikini,13 aliwaponya wagonjwa14 na vipofu.15 Aliwalisha wenye njaa,16 aliifungua mikono yake kwa watoto wadogo,17 na aliwasamehe wale waliomkosea, hata waliomsulubisha.18

Maandiko yanaeleza kwamba Yesu “akazunguka huko na huko akitenda kazi njema.”19 Nasi lazima tufanye hivyo.

Pili. Uhuru wa dini unachochea madhihirisho ya imani, tumaini na amani.

Kama kanisa, tunaungana na dini zingine kuwalinda watu wa imani zote na maoni na haki yao ya kuzungumza imani zao. Hii haina maana kwamba tunakubali imani zao, wala wao wakubali yetu, bali tunayo mengi yanayofanana kuliko tuliyonayo na wale wanaotamani kutunyamazisha.

Hivi karibuni nililiwakilisha Kanisa kwenye mkutano wa mwaka wa imani mbalimbali wa G20 huko Italia. Nilitiwa moyo, hata kuimarishwa, nilipokutana na viongozi wa serikali na dini kutoka ulimwenguni kote. Nilitambua majeraha na tofauti vinaweza kutatuliwa na hata kuponywa wakati tunapomheshimu Mungu, Baba yetu sote na Yesu Kristo, Mwana Wake. Mponyaji Mkuu wa wote ni Bwana na Mkombozi wetu, Yesu Kristo.

Nilipata wasaa mzuri pale nilipofunga hotuba yangu. Wazungumzaji saba waliotangulia hawakufunga katika njia yoyote ya tamaduni ya imani au katika jina la Mungu. Nilipozungumza, niliwaza, “je niseme tu asanteni na kuketi, au nifunge ‘katika jina la Yesu Kristo’?” Nilikumbuka mimi nilikuwa nani, na nilijua Bwana angenitaka mimi niseme jina Lake ili kuhitimisha ujumbe wangu. Hivyo nilifanya hivyo. Nikitazama nyuma, ilikuwa fursa yangu kuelezea imani yangu na nilipata uhuru wa dini wa kutoa ushahidi wangu wa jina Lake takatifu.

Tatu. Dini inawasukuma watu kuwasaidia wengine.

Wakati dini inapopewa nafasi na uhuru wa kustawi, waaminio hufanya matendo rahisi na wakati mwingine ya kishujaa ya huduma. Kirai cha kale cha Kiyahudi “tikkun olam,” ikimaanisha “kuurekebisha au kuuponya ulimwengu,” kinaakisiwa leo katika juhudi za wengi. Tumeungana na Misaada ya Kikatoliki ijulikanayo kama Caritas International, Msaada wa Kiislamu na kila idadi ya Wayahudi, Hindu, Budha, Sikh na taasisi za Kikristo kama vile Jeshi la Wokovu na Taasisi ya Kikristo ya Kitaifa. Kwa pamoja tunawahudumia mamilioni wenye uhitaji, hivi karibuni kwa kuwasaidia wakimbizi wa vita kwa mahema, magodoro ya kulalia na msaada wa chakula,20 na kutoa chanjo, ikijumuisha polio21na UVIKO.22 Orodha ya yale yanayofanywa ni ndefu, na ndivyo ilivyo kwa mahitaji.

Bila shaka, watu wa imani, wakifanya kazi pamoja, wanaweza kufanya ushiriki wenye maana. Wakati huohuo, huduma ya mtu mmoja mmoja mara nyingi haitangazwi lakini hubadili maisha kimya kimya.

Ninafikiria mfano katika Luka wakati Yesu Kristo alipomfikia mjane wa Naini. Yesu, akisindikizwa na kundi la wafuasi, alikuja kwenye maandamano ya mazishi ya mwana wa mjane. Bila kijana wake, mjane alikuwa akikabiliwa na uharibifu kihisia, kiroho na hata kiuchumi. Yesu, akiwa ameona uso wake uliojaa machozi, alisema, “Usilie.”23 Kisha akaligusa jeneza lililobeba mwili, na maandamano yakasimama.

“Kijana,” Aliamuru, “nakuambia, Inuka.

“Yule maiti akaketi, na akaanza kusema. Na [Yesu] akampa mama yake.”24

Kumfufua mfu ni muujiza, lakini kila tendo la ukarimu na kujali kwa mtu fulani anayehangaika ni njia ya agano ambayo kwayo kila mmoja wetu anaweza “[kwenda] huko na huko akitenda kazi njema” akijua “Mungu [yu] pamoja [nasi].”25

Na nne. Uhuru wa dini unafanya kazi kama nguvu ya kuunganisha na kuleta pamoja kwa ajili ya kuchagiza desturi na maadili.

Katika Agano Jipya tunasoma juu ya wengi wakiondoka kwa Yesu Kristo, wakilalamika juu ya injili Yake, “Neno hili ni gumu; ni nani awezaye kulisikia?”26

Kilio hicho bado kinasikika leo kutoka kwa wale wanaotafuta kufukuza dini kutoka kwenye mazungumzo na ushawishi. Ikiwa dini haipo pale kusaidia kubadili tabia na kuingilia nyakati ngumu, nani atafanya hivyo? Nani atafundisha uaminifu, shukrani, msamaha na uvumilivu? Nani atadhihirisha hisani, huruma na ukarimu kwa waliosahaulika na waliotwezwa? Nani atawakumbatia wale ambao wako tofauti na bado wakistahili, kama vile walivyo watoto wote wa Mungu? Nani watafungua mikono yao kwa walio katika uhitaji na kutotafuta malipo? Nani ataheshimisha amani na utiifu kwa sheria zilizo kuu zaidi ya mitindo ya siku? Nani ataitikia ombi la Mwokozi la “Enenda zako, nawe ukafanye vivyo hivyo”?27

Tutafanya hivyo! Ndiyo, akina kaka na akina dada, tutafanya hivyo.

Ninawaalika muunge mkono kusudi la uhuru wa dini. Ni kielelezo cha kanuni iliyotolewa na Mungu ya haki ya kujiamulia.

Uhuru wa dini huleta usawa kwenye filosofia zinazoshindana. Uzuri wa dini, mfiko wake na matendo ya kila siku ya upendo yanayochochewa na dini yanaongezeka pale tu tunapolinda uhuru wa kujieleza na kutendea kazi imani za msingi.

Ninatoa ushahidi kwamba Rais Russell M. Nelson ni nabii wa Mungu aliye hai. Ninashuhudia kwamba Yesu Kristo anaongoza na kuelekeza Kanisa hili. Alitoa dhabihu kwa ajili ya dhambi zetu, alisulubiwa msalabani na alifufuka siku ya tatu.28 kwa sababu Yake, tunaweza kuishi tena milele yote; na wale wenye tamanio hilo wanaweza kuwa na Baba yetu wa Mbinguni. Ukweli huu ninautangaza kwa ulimwengu wote. Nina shukrani kwa uhuru wa kuweza kufanya hivyo. Katika Jina la Yesu Kristo, amina.