Mkutano Mkuu
Kujiamini Kimaagano kupitia Yesu Kristo
Mkutano mkuu wa Aprili 2024


Kujiamini Kimaagano kupitia Yesu Kristo

Tunapoingia nyumba ya Bwana, tunaanza safari takatifu ya kujifunza kuwa wanafunzi wa juu na watakatifu zaidi wa Kristo.

Akina Kaka na Dada wapendwa, ninaomba kwamba tupate kufanywa upya kiroho kwa jumbe zenye mwongozo kutoka kwa viongozi wetu mwishoni mwa wiki hii na kufurahia katika kile ninachokiita “kujiamini kimaagano kupitia Yesu Kristo.” Kujiamini huku ni hakikisho tulivu lakini uhakika wa kupokea baraka ambazo Mungu anaahidi kwa wale wanaoshika maagano yao na inahitajika sana katikati ya hali zenye changamoto za siku yetu.

Ujenzi wa hizi nyumba mpya za Bwana kote ulimwenguni, chini ya uongozi wa Rais Russell M. Nelson, umesababisha shangwe kuu miongoni mwa waumini wa Kanisa na kutumika kama ishara muhimu ya upanuzi wa ufalme wa Mungu.

Nikitafakari uzoefu wangu wa kustaajabisha kwenye uwekaji wakfu wa Hekalu la Feather River California mwezi wa Oktoba iliyopita, nilijiuliza kama wakati mwingine tunapotea katika msisimko wa kuwa na mahekalu mapya katika majiji yetu na jumuiya na kupuuza dhumuni takatifu la maagano matakatifu yanayofanywa katika hekalu.

Maneno yaliyoandikwa kwenye sehemu ya mbele ya kila hekalu ni kauli makini: “Utakatifu kwa Bwana.”1 Maneno haya yenye mwongozo wa kiungu ni dalili ya wazi ya mwaliko kwamba tunapoingia nyumba ya Bwana, tunaanza safari takatifu ya kujifunza kuwa wanafunzi wa juu na watakatifu zaidi wa Kristo. Tunapofanya maagano katika utakatifu mbele za Mungu na kuahidi kwa dhati kumfuata Mwokozi, tunapokea nguvu ya kubadili mioyo yetu, kufanywa upya roho zetu na kuimarisha kwa kina uhusiano wetu na Yeye Jitihada kama hii inaleta utakaso wa nafsi zetu na kuunda kifungo kitakatifu pamoja na Mungu na Yesu Kristo, ambao wameahidi kwamba tunaweza kurithi zawadi ya uzima wa milele.2 Matokeo ya safari hii takatifu ni kwamba tunapata kujiamini kwa hali ya juu na takatifu zaidi kwa ajili ya maisha ya kila siku ndani ya maagano yetu yaliyofanywa kupitia Yesu Kristo.

Kujiamini kwa jinsi hii ndio kilele cha muunganiko wetu wa kiungu na Mungu na kunaweza kutusaidia sisi kuongeza kujitolea kwetu kwa dhati na shukrani kwa Yesu Kristo na dhabihu Yake ya kulipia dhambi. Kunaimarisha uwezo wetu wa kuwapenda na kuwahudumia wengine, na kutaimarisha nafsi zetu ili kuishi katika ulimwengu usio mtakatifu ambao unaogezeka giza na kukatisha tamaa. Kunatupa nguvu sisi kushinda mbegu za mashaka na kukata tamaa, hofu na kufadhaika, huzuni na kukosa matumaini ambako adui wa ukweli wote anajaribu kuuzamisha ndani ya mioyo yetu hasa wakati maisha ni magumu au hali zinapokuwa ngumu. Aya moja ya kibiblia hutoa ushauri muhimu kwa kila mmoja wetu tunapokumbana na upepo mkali wa changamoto za ulimwengu wa leo: “Basi msitupe ujasiri wenu.”3

Wapendwa kaka na dada zangu, wale wanaopata ujasiri halisi katika maagano waliyofanya katika nyumba ya Bwana kupitia Yesu Kristo wanamiliki mojawapo ya nguvu zenye uwezo zaidi tunazoweza kufikia katika maisha haya.

Kama ambavyo tumejifunza katika Kitabu cha Mormoni katika Njoo, Unifuate mwaka huu, tumeshuhudia jinsi ambavyo Nefi kwa uzuri kabisa alivyoonyesha uwezo wa aina hii ya kujiamini kupitia uaminifu wake alipokabiliwa na vikwazo na changamoto kama vile kupata mabamba kama alivyoamriwa na Bwana. Nefi, licha ya kuwa mwenye huzuni kupita kiasi kwa sababu ya uwoga na ukosefu wa imani wa Lamani na Lemueli alibaki mwenye kujiamini kwamba Bwana angewaletea yale mabamba. Yeye alisema kwa kaka zake: “Kadiri Bwana aishivyo, na tuishivyo sisi, hatutarudi kwa baba yetu nyikani mpaka tukamilishe kile kitu ambacho Bwana alituamrisha sisi.”4 Kwa sababu ya kujiamini kwa Nefi katika ahadi za Bwana, aliweza kukamilisha kile ambacho aliamriwa kukifanya.5 Baadaye, katika ono lake, Nefi aliona ushawishi wa kujiamini wa aina hii, aliandika “Mimi, Nefi, niliona nguvu ya Mwanakondoo wa Mungu, ambayo imeshuka juu ya watakatifu wa kanisa la Mwanakondoo, na juu ya watu wa agano wa Bwana, … na walikuwa wamevikwa haki pamoja na nguvu ya Mungu katika utukufu mkuu.”6

Nimeona mwenyewe kwa macho yangu ahadi za upendo za Bwana na nguvu zinazotiririka ndani ya maisha ya watoto wa Mungu, zikiwaimarisha kukabiliana na hali za maisha. Siku nyingine mke wangu alikuja nyumbani baada ya kuabudu kwake hekaluni na kuniambia jinsi alivyoguswa kwa kina na kile alichokipitia huko. Alipokuwa anaingia nyumba ya Bwana, aliwaona mwanaume mmoja amekaa katika kitimwendo akitembea pole pole sana na mwanamke akitembea kwa shida sana kwa kutumia fimbo, wote wawili kwa ujasiri wakija kuabudu. Kadiri mke wangu alipotembea katika eneo la ibada za mwanzo, alimwona dada mmoja mrembo ambaye alikuwa hana mkono mmoja—na akiwa na nusu tu ya mkono mwingine—kwa uzuri kabisa na kiselestia akitekeleza kazi yoyote aliyopewa.

Mimi na mke wangu na tulipokuwa tukizungumza kuhusu tukio hilo, tulihitimisha kwamba ni ujasiri ulio safi na wenye kugusa moyo tu katika ahadi za milele ambazo Mungu hutoa kupitia maagano matakatifu yanayofanywa pamoja na Yeye katika nyumba Yake ungeweza kusababisha wanafunzi wale wazuri wa Kristo kuacha nyumba zao katika siku ile yenye baridi kali, licha ya hali zao binafsi za kimaisha.

Marafiki zangu wapendwa, kama kuna kitu kimoja tungeweza kumiliki—na kitu kimoja ambacho tungeweza kuwarithisha watoto na wajukuu zetu ambacho kingemsaidia kila mmoja katika mitihani na majaribu yanayokuja—ingekuwa kujiamini katika maagano yaliyofanywa kupitia Yesu Kristo. Kupata mali kama hiyo ya kiungu kutawasaidia wao kuishi kama Bwana alivyoahidi wafuasi Wake waaminifu: “Wafuasi wangu watasimama katika mahali pa takatifu, na wala hawataondoshwa.”7

Je, tunapataje kujiamini kama huku kupitia Yesu Kristo? Kunakuja kupitia unyenyekevu, kumweka Yesu Kristo kuwa kitovu cha maisha yetu, kuishi kwa kanuni za injili ya Yesu Kristo, kupokea ibada za wokovu na kuinuliwa, na kuheshimu maagano na Mungu katika nyumba Yake takatifu.

Katika maneno yake ya kufunga mkutano mkuu wa Oktoba 2019, mpendwa nabii wetu alitukumbusha kuhusu hatua muhimu katika kupata kujiamini kimaagano, akisema “Ustahiki binafsi wa kuingia nyumba ya Bwana unahitaji zaidi maandalizi ya kiroho ya mtu binafsi. … Ustahiki binafsi unahitaji uongofu wa jumla wa akili na moyo kuwa zaidi kama Bwana, kuwa raia mwaminifu, kuwa mfano mzuri na kuwa mtu mtakatifu.”8 Kwa hiyo, kama tunabadilisha maandalizi yetu ya kuingia hekaluni tutabadilisha uzoefu wetu hekaluni, ambao utabadilisha maisha yetu nje ya hekalu. “Ndipo kujiamini kwako kutakuwa imara katika uwepo wa Mungu; na mafundisho ya ukuhani yatatona tona juu ya nafsi yako kama umande utokao mbinguni.”9

Askofu ninayemjua anaelezea darasa la zamani zaidi katika Msingi kama siyo darasa la “Msingi” bali kama darasa la “maandalizi ya hekaluni.” Mwezi Januari askofu anakuwa na washiriki wa darasa na walimu wao kuja ofisini kwake, mahali ambapo wanaongelea kuhusu jinsi watakavyotumia mwaka mzima kujiandaa kuingia hekaluni. Askofu anautumia muda huo kupitia maswali husika ya kibali cha hekaluni, ambayo kisha yanajumuishwa katika masomo yao ya Msingi. Anawaalika watoto kuandaliwa ili watakapokuwa wanakuja katika ofisi ya askofu baada ya mwaka mmoja, wanajiamini, kujiamini kimaagano, wako tayari kupokea kibali cha hekaluni na kuingia nyumba ya Bwana. Mwaka huu yule askofu alikuwa na wasichana wanne wadogo ambao walikuwa na shauku kubwa, wamejiandaa, na wanajiamini kwenda hekaluni kwamba walimtaka askofu achapishe vibali vyao siku ya Mwaka Mpya saa 6:01 usiku.

Maandalizi siyo tu kwa wale waendao hekaluni kwa mara ya kwanza. Sisi sote tunapaswa tuwe daima wenye kujiandaa kwenda katika nyumba ya Bwana. Kigingi kimoja ninachokifahamu kimepitisha kauli mbiu isemayo “Kiini chake nyumbani, kuungwa mkono na Kanisa na kufungwa hekaluni. Kufungwa10 ni neno la kupendeza kwani humaanisha kufokasi kwenye uelekeo, lakini pia linamaanisha kufungwa au salimishwa kwa, kwa kuamua na kwa dhamiria, ya hakika. Hivyo kuwa mwenye kufungwa hekaluni kunatusalimisha sisi kwa Mwokozi, kunatupatia uelekeo sahihi na uthabiti wakati tukihakikisha tuna ujasiri wa agano kupitia Yesu Kristo. Kwa hiyo sisi sote tunapaswa kwa makusudi kuboresha kufungwa huko kwa kuweka miadi na Bwana katika nyumba Yake, iwe hekalu li karibu au mbali sana.11

Nabii wetu mpendwa, Rais Russell M. Nelson, alitukumbusha sisi kuhusu hii kanuni muhimu kwa kusema: “Hekalu ni kitovu cha kuimarisha imani yetu na uimara wa kiroho kwa sababu Mwokozi na mafundisho Yake ndiyo kiini hasa cha hekalu. Kila kitu kinachofundishwa ndani ya hekalu, kupitia maelekezo na kupitia Roho, huongeza uelewa wetu wa Yesu Kristo. Ibada Zake muhimu hutuunganisha Kwake kupitia maagano matakatifu ya ukuhani. Kisha, tunapotunza maagano yetu, Yeye hutubariki kwa nguvu Yake ya uponyaji, ya kuimarisha.” Na lo, ni kiasi gani tutahitaji nguvu Yake katika siku zijazo.”12

Bwana anatamani kwamba tuwe waliojiandaa kuelewa, kwa uwazi mkuu, jinsi sahihi ya kutenda tunapofanya maagano pamoja na Baba yetu wa Mbinguni katika jina Lake. Yeye anatutaka tuwe tumejiandaa kupata fursa zetu, ahadi na majukumu; tujiandae kupata umaizi wa kiroho na uamsho ambao tunauhitaji katika maisha haya. Ninajua kwamba Bwana anapoona hata cheche tu ya hamu au mngaro mdogo wa juhudi ya haki katika utayari wetu wa kuweka kitovu cha maisha yetu juu Yake na kwenye ibada na maagano tunayofanya katika nyumba Yake, Yeye atatubariki katika njia Yake kamilifu kwa miujiza na huruma nyororo tunayohitaji.

Nyumba ya Bwana ni mahali tunapoweza kubadilishwa katika njia ya juu na takatifu zaidi. Hivyo basi, tunapotoka nje ya hekalu, tumebadilishwa kwa matumaini yetu katika ahadi za yale maagano, tumevikwa silaha pamoja na nguvu kutoka juu, tunalichukua hekalu pamoja nasi ndani ya majumba yetu na maisha yetu. Ninakuhakikishieni kwamba kuwa na roho wa nyumba ya Bwana ndani yetu hutubadilisha, kabisa.

Tunajua pia kutoka hekaluni kwamba kama tunataka Roho wa Bwana asizuiliwe kuja katika maisha yetu, hatuwezi kuwa na lazima tusiwe na hisia zozote ambazo si njema kwa mtu yeyote. Kutoa nafasi mioyoni mwetu au akilini kwa ajili ya hisia mbaya zitazaa maneno na matendo yasiyo na huruma, iwe katika mitandao ya kijamii au katika nyumba zetu, yakisababisha Roho wa Bwana kujitoa mioyoni mwetu. Kwa hiyo, tafadhali msitupe kujiamini kwenu, bali afadhali, acheni kujiamini kwenu kuimarike.

Uendelevu na kasi ya ujenzi wa mahekalu itaendelea kutuchochea, kututia msukumo na kutubariki sisi. La muhimu zaidi, tunapofanya maandalizi yetu ya kuingia hekaluni, tutabadilisha uzoefu wetu hekaluni, ambao utabadili maisha yetu nje ya hekalu. Na mabadiliko haya yatujaze ujasiri katika maagano yetu matakatifu tuliyofanya na Mungu na Yesu Kristo. Mungu yu hai, Yesu Kristo ni Mwokozi wetu, na hili ni Kanisa lake lililorejeshwa duniani. Kwa unyenyekevu natamka kweli hizi katika jina takatifu la Mwokozi wetu, Yesu Kristo, amina.