Mkutano Mkuu
Matunda Ambayo Yanadumu
Mkutano mkuu wa Aprili 2024


Matunda Ambayo Yanadumu

Kwa Roho Mtakatifu kufunga ibada zetu ni muhimu kama tunataka kuwa na baraka zilizoahidiwa kwa ajili ya milele yote.

Nikiwa mvulana mdogo, nilipenda matunda ya pichi. Hadi leo, wazo la kung’ata tunda tamu, lililoiva la pichi na ladha yake tamu huloanisha kinywa changu. Yakiwa yamekomaa kikamilifu pichi zinachumwa, zinadumu kwa siku mbili hadi nne kabla ya kuharibika. Nina kumbukumbu nzuri sana za kuungana na mama yangu na ndugu zangu jikoni kwetu tulipokuwa tukizihifadhi pichi zilizovunwa kwa ajili ya majira ya baridi yanayokuja kwa kuzifungia katika chupa. Kama tukizihifadhi kwa usahihi, tunda hili tamu linaweza kudumu kwa miaka kadhaa, siyo tu kwa siku mbili hadi nne. Kama zimeandalliwa kwa usahihi na kupashwa joto, tunda hili linahifadhika hadi kizibo kinapovunjika.

Kristo ametuelekeza sisi “nendeni na mkazae matunda, … na matunda yenu yapate kukaa.”1 Lakini hakuwa akizungumza kuhusu pichi. Yeye alikuwa akizungumzia kuhusu baraka za Mungu kwa watoto Wake. Kama tukifanya na kushika maagano na Mungu, baraka zinazohusiana na maagano yetu zinaweza kuendelea kupita maisha haya na kufungwa juu yetu, au kuhifadhiwa, milele, na kuwa tunda ambalo litadumu milele yote.

Roho Mtakatifu, katika nafasi Yake tukufu kama Roho Mtakatifu wa Ahadi, atafunga kila ibada juu ya wale walio waaminifu kwenye maagano yao ili zipate kuwa hai baada ya maisha ya duniani.2a Kwa Roho Mtakatifu kufunga ibada zetu ni muhimu kama tunataka kuwa na baraka zilizoahidiwa kwa ajili ya milele yote, kuwa tunda linalodumu.

Hili ni muhimu zaidi kama tunataka kuinuliwa.3 Kama ambavyo Rais Nelson amefundisha, tunapaswa “kuanza na mwisho akilini. … Hakika, kwa kila mmoja, “mwisho” ambao tungependa zaidi kuupata ni kuishi milele pamoja na familia zetu katika hali ya kuinuliwa ambayo tutakuwa katika uwepo wa Mungu, Baba yetu wa Mbinguni, na Mwanawe Yesu Kristo.”4. Rais Nelson pia amesema: “Ndoa ya selestia ni sehemu muhimu ya maandalizi ya uzima wa milele. Inahitaji mtu kuoa au kuolewa na mtu sahihi, katika mahali sahihi, kwa mamlaka sahihi na kutii agano hilo takatifu kwa uaminifu. Ndipo mtu anaweza kuwa na uhakika wa kuinuliwa katika ufalme wa selestia wa Mungu.”5

Ni zipi baraka za kuinuliwa? Zinajumuisha kukaa katika uwepo wa Mungu pamoja kama mume na mke milele, tukirithi “enzi, falme, ukuu, na nguvu, … na muendelezo wa vizazi millele na milele,”6 tukipokea vyote ambavyo Mungu Baba anavyo.7

Bwana alifunua kupitia Joseph Smith:

“Katika utukufu wa selestia kuna mbingu tatu au madaraja ya utukufu;

“Na ili kupata la juu zaidi, mwanadamu lazima aingie katika utaratibu huu wa ukuhani [ikimaanisha agano jipya na lisilo na mwisho la ndoa];

“Na kama hakufanya hivyo, hawezi kulipata.

“Anaweza kuingia katika mwingine, lakini huo ndiyo mwisho wa ufalme wake; hawezi kuongezeka.”8

Tunajifunza hapa kwamba mtu anaweza kuwa katika ufalme wa selestia, au kukaa katika uwepo wa Mungu, na akawa peke yake. Lakini kuinuliwa katika lile daraja la juu zaidi la ufalme wa selestia, mtu lazima aingie katika ndoa kwa mamlaka sahihi na kisha awe mkweli kwenye maagano yaliyofanywa katika ndoa hiyo. Tunapokuwa waaminifu kwenye maagano haya, Roho Mtakatifu wa Ahadi anaweza kufunga agano letu la ndoa.9 Baraka ya jinsi hii ndiyo inakuwa tunda ambalo linadumu.

Nini kinahitajika ili kushika kwa uaminifu agano jipya na lisilo na mwisho la ndoa?

Rais Russell M. Nelson amefundisha kwamba kuna aina mbili za vifungo tunapoingia ndani ya hili agano la ndoa ya milele: kifungo cha mlalo kati ya mume na mke, na kifungo cha wima pamoja na Mungu.10 Ili baraka za kuinuliwa ziweze kufungwa juu yetu na kudumu baada ya maisha haya, lazima tuwe wakweli kwenye vifungo vyote viwili vya mlalo na wima vya agano.

Ili kushika kifungo mlalo na mwenza wako, Mungu ametushauri “mpende mke [wako] au [mume] kwa moyo [wako] wote … ambatana naye na sio mwingine.”11 Kwa wote waliooa au kuolewa, kuambatana naye na sio mwingine inamaanisha mnashauriana pamoja kwa upendo, mnapendana na kujaliana ninyi kwa ninyi, mnaweka vipaumbele vya muda na mwenza wako juu ya mapendeleo binafsi, na mnamlingana Mungu ili awasaidie mshinde mapungufu yenu.12 Pia inamaanisha hakuna uhusiano wa kihisia au uhusiano wa kujamiiana wa aina yoyote nje ya ndoa yenu, ikijumuisha kumzoea mtu kimapenzi, au kuweka miadi, na hakuna ponografia, vitu ambavyo huzalisha tamaa.13

Ili kushika kifungo mlalo katika agano, kila mtu lazima atamani kuwa katika ndoa. Rais Dallin H. Oaks hivi karibuni alifundisha: “Pia tunajua kwamba Yeye [Mungu] hatamlazimisha mtu yeyote kuingia katika uhusiano wa kuunganishwa tofauti na mapenzi ya mtu huyo. Baraka za uhusiano wa kuunganishwa zimehakikishwa kwa wote wanaotii maagano yao lakini kamwe si kwa kulazimisha uhusiano wa kuunganishwa kwa mtu mwingine ambaye hastahili au hayuko tayari..”14

Kifungo cha wima ambacho Rais Nelson amekiongelea ni kipi? Kifungo cha wima ni kile tunachofanya na Mungu.

Ili kushika kifungo cha wima na Mungu, tunakuwa wakweli kwenye maagano ya hekaluni ambayo tumeyafanya kuhusiana na sheria za utii, dhabihu, injili, usafi wa kimwili na wakfu. Pia tunaagana na Mungu kumpokea mwenzi wetu wa milele na kuwa wenza na wazazi waadilifu. Tunapotii kifungo cha wima, tunafuzu kwa ajili ya baraka za kuwa sehemu ya familia ya Mungu kupitia agano la Ibrahimu, ikijumuisha baraka za uzao, injili na ukuhani.15. Baraka hizi pia ni matunda ambayo yanadumu.

Wakati tunapotumaini kwamba wale wote wanaoingia ndani ya agano jipya na lisilo na mwisho la ndoa wanabaki wakweli na kuwa na baraka kufungwa juu yao kwa milele yote, wakati mwingine ubora huo huonekana kutofikika. Kote katika huduma yangu nimekutana na waumini wanaofanya na kushika maagano lakini wenza wao hawafanyi hivyo. Wapo pia wale walio waseja, hawajawahi kupata fursa ya kuoa au kuolewa hapa duniani. Na wapo wale ambao siyo waaminifu katika maagano yao ya ndoa. Je, ni nini kinachotokea kwa watu katika kila hali hizi?

  1. Kama utabaki mwaminifu kwenye maagano uliyoyafanya wakati ulipopokea endaumenti, utapokea baraka binafsi zilizoahidiwa kwako katika endaumenti hiyo hata kama mwenza wako amevunja maagano hayo au amejitoa katika ndoa. Kama ulishaunganishwa na baadaye kupata talaka, na kama kuunganishwa kwako hakujafutwa, baraka binafsi za uunganishaji huo zitaendelea kuwepo kwa ajili yako kama utabaki mwaminifu.16

    Wakati mwingine, kutokana na hisia za usaliti na maumivu halisi, mwenza mwaminifu anaweza kutaka kufuta kuunganishwa kwake na mwenza asiye mwaminifu ili kuwa nao mbali iwezekanavyo, kote hapa duniani na milele. Kama una wasiwasi kwamba kwa namna fulani unaweza kuunganishwa na mwenza wa zamani ambaye hakutubu, kumbuka, haitatokea! Mungu hatahitaji mtu yeyote kubaki katika uhusiano wa kuunganishwa milele yote kinyume na mapenzi yake. Baba wa Mbinguni atahakikisha kwamba tunapokea kila baraka ambayo matamanio na chaguzi zetu zinaruhusu.17

    Hata hivyo, kama ufutaji wa kuunganishwa unahitajika, haki ya kujiamulia inaheshimika. Taratibu kadhaa zinaweza kufuatwa. Lakini hili halipaswi kufanywa kwa njia za kawaida! Urais wa kwanza unashikilia funguo za kufunga duniani na mbinguni. Pale kufutwa kwa uunganishaji kunapokuwa kumetolewa na Urais wa Kwanza, baraka zinazohusiana na uunganishaji huo zinakuwa hazina nguvu tena; zinakuwa zimefutwa kwa vifungo vyote, kifungo mlalo na wima. Ni muhimu kuelewa kwamba ili kupokea baraka za kuinuliwa, ni lazima tuonyeshe kwamba tuko tayari kuingia katika agano na kwa uaminifu kulishika agano hili jipya na la milele, ama katika maisha haya au yajayo.

  2. Kwa wale waumini wa Kanisa walio waseja, tafadhali kumbuka kwamba “katika njia na wakati wa Bwana mwenyewe, hakuna baraka itakayozuiliwa kwa Watakatifu Wake walio waaminifu. Bwana atamhukumu na kumlipa kila mtu kulingana na [matamanio] ya moyoni pamoja na matendo yake.”18

  3. Kama hujabaki mwaminifu kwenye maagano ya hekaluni, je, kuna tumaini? Ndiyo! Injili ya Yesu Kristo ni injili ya mtumaini. Tumaini hilo huja kupitia Yesu Kristo kwa toba ya dhati na kwa utiifu kufuata mafundisho ya Yesu Kristo. Nimeona watu wakifanya makosa makubwa sana, wakivunja maagano matakatifu. Katika utaratibu wa kawaida, ninaona wale ambao wanatubu kwa dhati, wanasamehewa na kurudi kwenye njia ya agano. Kama umevunja maagano yako ya hekaluni, ninakusihi umgeukie Yesu Kristo, shauriana na askofu wako, tubu, na ufungue nafsi yako kwenye nguvu madhubuti ya uponyaji inayopatikana kwa sababu ya Upatanisho wa Yesu Kristo

Akina Kaka na akina dada, Baba yetu wa Mbinguni mwenye upendo ametupatia maagano ili tupate kufikia yale yote aliyonayo. Baraka hizi takatifu kutoka kwa Mungu ni tamu zaidi kuliko tunda lolote la duniani. Zinaweza kuhifadhiwa kwa ajili yetu milele, na kuwa tunda ambalo linadumu, kadiri tuwavyo waaminifu kwenye maagano yetu.

Ninashuhudia kwamba Mungu amerejesha mamlaka ya kufunga duniani na mbinguni. Mamlaka hayo yanapatikana katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Mamlaka hayo yanashikiliwa na Urais wa Kwanza na Akidi ya Mitume Kumi na Wawili na mamlaka hayo yanatumika chini ya maelekezo ya Rais Russell M. Nelson. Wale wanaoingia katika agano jipya na lisilo na mwisho la ndoa na kushika agano hilo wanaweza kukamilishwa na mwishowe kupokea utimilifu wa utukufu wa Baba, bila kujali hali zilizo nje ya udhibiti wao.19

Hizi baraka zilizoahidiwa zinazohusiana na maagano yetu zinaweza kufungwa juu yetu na Roho Mtakatifu wa Ahadi na kuwa matunda ambayo yanadumu milele na milele. Ninashuhudia hivyo katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Yohana 15:16.

  2. Ona Dale G. Renlund, “Kufikia Nguvu za Mungu kupitia Maagano,” Liahona, Mei 2023, 35–38; Mafundisho na Maagano 132:7.

  3. Ibada inafungwa wakati inapokuwa imefanywa kuwa hai kote mbinguni na duniani kwa sababu inafanywa na mtu aliye na mamlaka na kuthibitishwa na Roho Mtakatifu.

    “Tunapenda kudhani kwamba mamlaka ya kuunganisha yanatumika tu kwa aina fulani ya ibada za hekaluni, lakini mamlaka hayo ni muhimu katika kufanya ibada yoyote kuwa halali na yenye kuunganisha baada ya kifo. Nguvu ya kuunganisha huweka muhuri wa uhalali kwenye ubatizo wako, kwa mfano, ili kwamba ubatizo huo utambulike hapa na mbinguni. Hatimaye, ibada zote za ukuhani zinatekelezwa chini ya funguo za Rais wa Kanisa, na kama Rais Joseph Fielding Smith alivyoelezea: ‘Yeye [Rais wa Kanisa] ametupatia sisi mamlaka, ameweka nguvu za kuunganisha katika ukuhani wetu, kwa sababu yeye anashikilia funguo hizo’ [kama ilivyonukuliwa na Harold B. Lee, katika ripoti ya Mkutano Mkuu, Okt 1944, 75] ” (D. Todd Christofferson, “Nguvu ya Kuunganisha,” Liahona, Nov. 2023, 20).

    “Tendo linalotiwa muhuri na Roho Mtakatifu wa Ahadi ni lile linalothibitishwa na Roho Mtakatifu; na ndilo linaloidhinishwa na Bwana. … Hakuna anayeweza kumdanganya Roho Mtakatifu na kupita bila kugundulika. … Kanuni hizi pia zinatumika kwa kila ibada nyingine yoyote na utekelezaji katika Kanisa. Hivyo basi kama pande zote [katika ndoa] ni za ‘haki na kweli’ [Mafundisho na Maagano 76:53], kama wanastahili, muhuri wa kuthibitisha unawekwa juu ya ndoa yao ya hekaluni, kama hawastahili, hawahesabiwi haki na Roho na hivyo uthibitishaji wa Roho Mtakatifu huzuiliwa. Ustahiki unaofuata utafanya muhuri kuwa halali na ukosefu wa uadilifu utavunja muhuri wowote” (Bruce R. McConkie, “Holy Spirit of Promise),” katika Preparing for an Eternal Marriage Student Manual [2003], 136).

    Roho Mtakatifu wa Ahadi ni Roho Mtakatifu anayeweka muhuri wa kuidhinisha juu ya kila ibada, ubatizo, uthibitisho, kutawazwa, ndoa. Ahadi ni kwamba baraka zitapokelewa kupitia uaminifu. Kama mtu atavunja agano, iwe agano la ubatizo, kutawazwa, ndoa, au kitu kingine chochote, Roho huondoa muhuri wa kuidhinisha, na baraka hiyo haitapokelewa. Kila ibada hufungwa kwa ahadi ya baraka kulingana na uaminifu. Roho Mtakatifu anatoa ule muhuri wa idhini pale ambapo maagano yamevunjwa” (Joseph Fielding Smith, Doctrines of Salvation, comp. Bruce R. McConkie [1954], 1:45).

  4. Russell M. Nelson, Heart of the Matter: What 100 Years of Living Have Taught Me (2023), 15. Maagano yote lazima yaunganishwe na Roho Mtakatifu wa Ahadi ili kuwa na nguvu baada ya ufufuko wa wafu” (ona Mafundisho na Maagano 132:7).

  5. Russell M. Nelson, “Celestial Marriage,” Liahona, Nov. 2008, 94.

  6. Mafundisho na Maagano 132:19.

  7. Ona Mafundisho na Maagano 84:38.

  8. Mafundisho na Maagano 131:1–4.

  9. Ona Mafundisho na Maagano 132:19–20. “Makazi ya juu zaidi—kuinuliwa katika ufalme wa selestia—ndiyo fokasi ya Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.—” (Dallin H. Oaks, “Falme za Utukufu,” Liahona, Nov. 2023, 26).

  10. “Kama vile ambavyo ndoa na familia zinashiriki kifungo cha kipekee cha mlalo ambacho huleta upendo maalumu, hivyo ndivyo ulivyo uhusiano mpya unaundwa wakati tunapojifunga sisi wenyewe kwenye agano la wima na … Mungu” tunapoingia katika agano jipya na lisilo na mwisho la ndoa (Russell M. Nelson, Heart of the Matter, 41–42).

  11. Mafundisho na Maagano 42:22; ona pia Kitabu cha Maelezo ya Jumla: Kuhudumu katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, 38.6.16. Katika kujadili ndoa hapa, nimeongelea ndoa kulingana na sheria ya Mungu, ambayo inafafanua ndoa kama muungano wa kisheria kati ya mwanamume na mwanamke (ona “Familia: Tangazo kwa Ulimwengu,” Maktaba ya Injili).

  12. Ona “Familia: Tangazo kwa Ulimwengu,” Maktaba ya Injili.

  13. Ona Mafundisho na Maagano 42:22–24.

  14. Dallin H. Oaks, “Falme za Utukufu,” 29; msisitizo umeongezwa.

  15. Ona Mafundisho na Maagano 86:8–11; 113:8; Ibrahimu 2:9–11.

  16. Ona Kitabu cha Maelezo ya Jumla, 38.4.1.

    Wakati nikihudumu kama mmisionari huko Switzerland, mimi pamoja na mmisionari mwenzagu tulishiriki injili na wanandoa wazuri wenye umri wa miaka 60 wa Kiswisi. Tulipokuwa tunawafundisha wanandoa hawa kuhusu Kanisa lililorejeshwa la Yesu Kristo, mwanamke alionyesha kupendezwa katika yale tuliyoyafundisha. Katika wiki chache zilizofuata, alipata ushuhuda juu ya uhalisia kwamba Kanisa la Yesu Kristo limerejeshwa likiwa na mamlaka sahihi kutoka kwa Mungu na kwamba Yesu Kristo analielekeza Kanisa Lake kupitia manabii na mitume walio hai. Tulitazamia kuendelea kuwafundisha wanandoa hawa kuhusu mafundisho muhimu ya Urejesho, fursa ya ndoa ya milele. Cha kushangaza, hata hivyo, tulipokuwa tukiwafundisha wanandoa hawa kuhusu mafundisho ya ndoa ya milele, mwanamke yule wa Kiswisi alisema hakutaka kuwa na mume wake huyo kwa milele yote. Kwake yeye, mbinguni haikujumuisha kuwa na mume wake huyo, ambaye ameolewa naye kwa miaka 36. Dada huyu alibatizwa, lakini mume wake hakubatizwa. Kamwe hawakuunganishwa hekaluni.

    Kwa wengi, hata hivyo, mbingu haitakuwa mbingu pasipo kuwa na mtu ambaye wameoana. Kuwa pamoja na mwenza unayempenda milele hakika inasikika kama mbinguni. Kama Mzee Jeffrey R. Holland alivyoshiriki kuhusu mpendwa mke wake, Pat, mbinguni kusingelikuwa mbinguni pasipo yeye (ona “Scott Taylor: For Elder Holland, Heaven without His Wife and Children ‘Wouldn’t Be Heaven for Me,’” Church News, July 22, 2023).

  17. Ona Dallin H. Oaks, “Falme za Utukufu,” 26.

  18. Russell M. Nelson, “Ndoa ya Selestia,” 94.

  19. Ona Yohana 15:16.