Mkutano Mkuu
Ita, Usianguke
Mkutano mkuu wa Aprili 2024


Ita, Usianguke

Kama tutamwita Mungu, ninashuhudia hatutanguka.

Leo ningependa kuanza kwa kushuhudia uhakika kamili ndani ya moyo wangu kwamba Mungu anasikia sala zetu na kuzijibu kwa njia binafsi kwa kila mtu.

Katika ulimwengu unaopitia nyakati za kutokuwa na uhakika, maumivu, kukata tamaa na kuvunjika moyo, tunaweza kuhisi kutegemea zaidi uwezo na mapendeleo binafsi, pamoja na maarifa na usalama unaotoka ulimwenguni. Hii inaweza kutufanya tuweke pembeni chanzo halisi cha msaada na usaidizi ambacho kinaweza kukabiliana na changamoto za maisha haya ya duniani.

Picha
Chumba cha Hospitali.

Nakumbuka tukio moja wakati nilipolazwa kwa sababu ya ugonjwa, na ilikuwa vigumu kwangu kulala. Nilipozima taa na chumba kikawa giza, niliona ishara iliyoakisi kwenye dari mbele yangu ambayo ilisema, “Ita, usianguke.” Kwa mshangao wangu, siku iliyofuata niliona ujumbe huo huo ukirudiwa katika sehemu kadhaa za chumba.

Picha
Ishara ya Ita, usianguke.

Kwa nini ujumbe ule ulikuwa muhimu sana? Nilipomuuliza muuguzi kuhusu hilo, alisema, “Ni kuzuia pigo ambalo linaweza kuongeza maumivu uliyo nayo tayari.”

Maisha haya, kwa asili yake, huleta uzoefu wa uchungu, baadhi ni urithi kwenye miili yetu, baadhi kutokana na udhaifu wetu au mateso, baadhi kutokana na jinsi wengine wanavyotumia haki yao ya kujiamulia, na baadhi kutokana na matumizi ya haki yetu ya kujiamulia.

Je, kuna ahadi yenye nguvu zaidi kuliko ile ambayo Mwokozi Mwenyewe aliitoa wakati alipotamka, “Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni nanyi mtaona; bisheni,” au iteni “nanyi mtafunguliwa”?1

Sala ni njia ya mawasiliano na Baba yetu wa Mbinguni ambayo inatuwezesha “kuita na tusianguke.” Hata hivyo, kuna hali ambazo tunaweza kudhani kwamba sala haijasikika kwa sababu hatupati jibu la haraka au jibu linalolingana na matarajio yetu.

Hili wakati mwingine husababisha wasiwasi, huzuni au kukata tamaa. Lakini kumbuka onyesho la Nefi la imani katika Bwana wakati aliposema, “Je, kwa nini hawezi kunishauri, kwamba nijenge merikebu?”2 Sasa, ninakuuliza wewe, Je, kwa nini Bwana asikushauri wewe, kwamba usianguke?

Kujiamini katika majibu ya Mungu kunamaanisha kukubali kwamba njia Zake sio njia zetu3 na kwamba “vitu vyote lazima vitokee katika wakati wake.”4

Uhakika wa kujua kwamba sisi ni watoto wa Baba wa Mbinguni mwenye upendo na mwenye huruma unapaswa kuwa motisha ya “kuita” katika sala ya kumcha Mungu kwa mtazamo wa “kusali daima, na bila kuchoka; … ili utendaji [wetu] uwe kwa ajili ya ustawi wa nafsi [zetu].”5 Fikiria hisia za Baba wa Mbinguni pale ambapo katika kila sala tunaomba katika jina la Mwanawe, Yesu Kristo. Ni nguvu na upole ulioje, naamini, unaonyeshwa wakati tunapofanya hivyo!

Maandiko yamejaa mifano ya wale ambao “walimwita Mungu ili wasianguke. Helamani na jeshi lake, wakati wakikabiliwa na mateso yao, walimwita Mungu, wakimimina roho zao katika sala. Walipokea hakikisho, amani, imani na tumaini, wakipata ujasiri na ushupavu hadi walipofikia lengo lao.6

Fikiria jinsi ambavyo Musa angeweza kumwita na kumlilia Mungu wakati alipojikuta katikati ya Bahari ya Shamu na Wamisri wakikaribia kuwashambulia, au Ibrahimu wakati wa kutii amri ya kumtoa dhabihu mwanawe Isaka.

Nina hakika kwamba kila mmoja wenu amekuwa na atakuwa na uzoefu ambapo kuita kutakuwa jibu la kutoanguka.

Miaka thelathini iliyopita, wakati mimi na mke wangu tulipokuwa tukijiandaa kwa ndoa yetu ya kisheria na ndoa yetu ya hekaluni, tulipokea simu ikitujulisha kwamba ndoa za kisheria zilifutwa kwa sababu ya mgomo. Tulipokea simu siku tatu kabla ya sherehe iliyopangwa. Baada ya majaribio kadhaa katika ofisi zingine na kutopata miadi yoyote, tulianza kuhisi kufadhaika na kuwa na shaka kwamba hatutoweza kuoana kama ilivyopangwa.

Mimi na mchumba wangu “tuliita,” tukizimimina roho zetu kwa Mungu katika sala. Hatimaye, mtu mmoja alituambia kuhusu ofisi katika mji mdogo nje kidogo ya jiji ambapo mtu aliyemjua alikuwa meya. Bila kusita, tulienda kumtembelea na kumuuliza ikiwa inawezekana kutufungisha ndoa. Kwa furaha yetu, alikubali. Katibu wake alisisitiza kwamba tulipaswa kupata cheti katika mji huo na kutoa nyaraka zote kabla ya mchana siku iliyofuata.

Siku iliyofuata, tulihamia kwenye mji mdogo na kwenda kituo cha polisi kuomba hati inayohitajika. Kwa mshangao wetu, afisa huyo alisema kwamba hangetupatia, kwa sababu wanandoa wengi vijana walikuwa wakikimbia kutoka kwa familia zao ili kuoana kwa siri katika mji huo, ambapo kwa kweli haikuwa lengo letu. Kwa mara nyingine tena, hofu na huzuni vilitushika.

Nakumbuka jinsi nilivyomwita kimya kimya Baba yangu wa Mbinguni ili nisianguke. Nilipokea msukumo wa wazi akilini mwangu, ukirudiarudia kusema, “Kibali cha hekaluni, kibali cha hekaluni.” Kwa haraka, nilichukua kibali changu cha hekaluni na kumkabidhi afisa, mchumba wangu akibaki na mshangao.

Ni mshangao gani tuliokuwa nao tulipomsikia afisa akisema, “Kwa nini hukuniambia kwamba wewe unatoka Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho? Ninalijua kanisa lenu vizuri.” Mara moja akaanza kuandaa nyaraka. Tulishangaa zaidi wakati afisa huyo alipoondoka kituoni bila kusema chochote.

Dakika 50 zilipita, na hakurudi. Ilikuwa tayari saa 5:55 asubuhi, na tulikuwa na muda hadi saa sita mchana tu wa kuwasilisha nyaraka hizo. Ghafla alionekana akiwa na mbwa mdogo mzuri na kutuambia ilikuwa zawadi ya harusi na akatupatia pamoja na hati.

Tulikimbia kuelekea ofisi ya meya tukiwa na hati yetu na mbwa wetu mpya. Kisha tukaona gari la serikali likija mbele yetu. Nilisimama mbele yake. Gari lilisimama, na tukamwona katibu ndani. Alipotuona, alisema, “Samahani; niliwaambia saa sita. Lazima niende kwenye kazi nyingine.”

Nilijinyenyekeza mwenyewe kwa kukaa kimya, “nikiita” kwa moyo wangu wote kwa Baba yangu wa Mbinguni, nikiomba msaada tena ili “nisianguke.” Ghafla, muujiza ukatokea. Katibu alituambia, “Mna mbwa mzuri sana. Ninaweza kupata wapi kama huyo kwa ajili ya mwanangu?”

“Huyu ni kwa ajili yako” tulimjibu mara moja.

Katibu alitutazama kwa mshangao na kusema, “Sawa, twendeni ofisini na tufanye mipango.”

Siku mbili baadaye, mimi na Carol tulioana kisheria, kama ilivyopangwa, na kisha tukaunganishwa katika Hekalu la Lima Peru.

Bila shaka, tunahitaji kukumbuka kwamba “kuita” ni suala la imani na matendo—imani kutambua kwamba tuna Baba wa Mbinguni ambaye anajibu sala zetu kulingana na hekima Yake isiyo na mwisho, na kisha, hatua inayoendana na kile tulichoomba. Kusali—kuita—inaweza kuwa ishara ya tumaini letu. Lakini kuchukua hatua baada ya kusali ni ishara kwamba imani yetu ni ya kweli, imani ambayo inajaribiwa wakati wa maumivu, hofu au kukata tamaa.

Ninapendekeza mfikirie yafuatayo:

  1. Daima fikiria juu ya Bwana kama chaguo lako la kwanza la msaada.

  2. Ita, usianguke. Mgeukie Mungu katika sala ya dhati.

  3. Baada ya kusali, fanya yote uwezayo ili kupata baraka ulizoziomba.

  4. Jinyenyekeze ili kukubali jibu katika muda Wake na njia Zake.

  5. Usiache! Endelea kusonga mbele kwenye njia ya agano wakati unasubiri jibu.

Labda kuna mtu sasa hivi ambaye, kwa sababu ya hali, anahisi kama anakaribia kuanguka na angependa “kuita” kama alivyofanya Joseph Smith wakati alipopaza sauti, “Ewe Mungu, uko wapi? … Ni kwa muda gani mkono wako utazuiliwa?”7

Hata katika hali kama hizi, sali kwa “kasi ya kiroho,” kama Rais Russell M. Nelson alivyofundisha,8 kwa sababu sala yako inasikika daima!

Kumbuka huu wimbo wa dini:

Ulipoamka leo,

Je, uliomba?

Katika jina la Kristo,

Kusihi upendeleo

Ili kulindwa?

Jinsi sala hufariji!

Nuru huongezeka.

Punde ukiwa gizani,

Kumbuka sala.9

Tunaposali, tunaweza kuhisi kumbatio la Baba yetu wa Mbinguni, ambaye alimtuma Mwanawe wa Pekee ili kupunguza mizigo yetu, kwa sababu ikiwa “tunamwita Mungu,” ninashuhudia hatutaanguka. Katika jina la Yesu Kristo, amina.