Mkutano Mkuu
Mambo Yote kwa Faida Yetu
Mkutano mkuu wa Aprili 2024


Mambo Yote kwa Faida Yetu

Kwa muda na milele, dhumuni la Uumbaji na asili ya Mungu Mwenyewe ni kuvileta vitu vyote pamoja kwa faida yetu.

Leo ni Aprili 6, kumbukizi ya Yesu Kristo kurejesha Kanisa Lake la siku za mwisho—na kama sehemu ya msimu wa Pasaka kwa shangwe tunashuhudia maisha makamilifu ya Yesu Kristo, dhabihu ya kulipia dhambi na utukufu wa Ufufuko Wake.

Hadithi ya Kichina inaanza kwa mwana wa mtu anapata farasi mzuri.

“Ni bahati iliyoje,” majirani wanasema.

“Tutaona,” anasema yule mtu.

Kisha yule mwana anaanguka kutoka juu ya farasi na kupata majeraha ya kudumu.

“Bahati mbaya iliyoje,” majirani wanasema.

“Tutaona,” anasema yule mtu.

Usajili wa lazima jeshini unatokea na yule mwana aliyejeruhiwa anaachwa.

“Ni bahati iliyoje,” majirani wanasema.

“Tutaona,” anasema yule mtu.

Ulimwengu huu kigeugeu mara nyingi unahisi kutupwa na tufani, kutokuwa na uhakika, wakati mwingine bahati nzuri, na—mara nyingi—bahati mbaya. Bado, katika ulimwengu huu wa dhiki,1 “tunajua kwamba mambo yote yatafanyika pamoja kwa faida yao wanaompenda Mungu.”2 Ndiyo, tunapotembea wima na kukumbuka maagano yetu, “mambo yote yatafanyika pamoja kwa faida yenu.”3

Mambo yote kwa faida yetu.

Ni ahadi ya ajabu iliyoje! Hakikisho la faraja kutoka kwa Mungu mwenyewe! Katika njia ya kimuujiza, dhumuni la Uumbaji na asili ya Mungu Baba yetu na Mwanawe, Yesu Kristo, ni kujua mwanzo na mwisho;4 ili kuleta vyote ambavyo ni kwa faida yetu; na kuokoa na kuinua tunapokuwa tumetakaswa na watakatifu kupitia neema na Upatanisho wa Yesu Kristo.

Upatanisho wa Yesu Kristo unaweza kutuokoa na kutukomboa kutokana na dhambi. Lakini Yesu Kristo pia kwa upendo anaelewa kila maumivu yetu, mateso, magonjwa,5 huzuni, utengano. Kwa muda na milele ushindi Wake juu ya mauti na jahanamu unaweza kufanya mambo yote kuwa sawa.6 Yeye anasaidia kuponya waliovunjika na walioshushiwa hadhi, kuwapatanisha wenye hasira na walio tengana, kuwafariji walio wapweke na waliotengwa, kuwatia moyo wasio na hakika na wakosefu na kutoa miujiza inayoweza kufanywa na Mungu pekee.

Tunaimba haleluya na kupaza sauti hosana! Tunaimba kwa uwezo wa milele na wema usio na kikomo, katika mpango wa furaha wa Mungu, mambo yote yatafanyika pamoja kwa faida yetu. Tunaweza kuyakabili maisha kwa kujiamini na siyo kwa woga.

Tukiachwa peke yetu yawezekana tusijue faida yetu wenyewe. Wakati “ninapojichagua mwenyewe,” pia ninajichagulia mwenyewe vikwazo, madhaifu, mapungufu. Hatimaye, ili kufanya mema mengi ni lazima sisi tuwe wema.7 Kwa kuwa hakuna aokoaye ila Mungu,8 tunatafuta ukamilifu katika Yesu Kristo.9 Tunakuwa waaminifu tuwezavyo, bora zaidi tunapoachana na mwanaume au mwanamke wa asili na kuwa mtoto mdogo mbele za Mungu.

Kwa matumaini na imani katika Mungu, majaribu na mateso yanaweza kuwekwa wakfu kwa faida yetu. Yusufu, aliuzwa utumwani Misri, baadaye aliiokoa familia yake na watu wengine. Kufungwa kwa nabii Joseph Smith katika jela ya Liberty kulimfundisha “mambo haya yote yatakupa wewe uzoefu, na yatakuwa kwa faida yako.”10 Tukiwa na imani, majaribu na dhabihu ambazo kamwe hatutovichagua vinaweza kutubariki sisi na wengine katika njia ambazo hatujawahi kufikiria.11

Tunaongeza imani na matumaini katika Bwana kwamba mambo yote yatafanyika pamoja kwa faida yetu tunapopata mtazamo wa milele;12 tunapoelewa majaribu yetu yanaweza kuwa “lakini kwa muda mfupi”;13 tukitambua mateso yanaweza kuwekwa wakfu kwa faida yetu;14 tukitambua ajali, kifo kisichotarajiwa, maradhi yanayodhoofisha na magonjwa ni sehemu ya maisha ya duniani; na kumtumaini Baba yetu mpendwa wa Mbinguni kwamba hatupi majaribu ili kutuadhibu au kutuhukumu. Asingempa jiwe mtu aliyeomba mkate au nyoka kwa mtu aliyeomba samaki.15

Wakati majaribu yanapokuja, mara nyingi kitu tunachotaka zaidi ni mtu kutusikiliza na kuwa pamoja nasi.16 Kwa wakati huo, maoni ya jumla yanaweza yasiwe na msaada, hata kama yamenuia kutoa faraja. Wakati mwingine tunatamani mtu ambaye atahuzunika, kuumia na kulia pamoja nasi; atakayeruhusu tuelezee maumivu, kukatishwa tamaa, hata hasira, na kukubaliana nasi kwamba kuna mambo hatuyajui.

Tunapomtumainia Mungu na upendo Wake kwetu, hata masikitiko yetu makubwa zaidi mwishowe yanaweza kuwa, kwa faida yetu.

Nakumbuka siku niliyopokea taarifa ya ajali mbaya ya gari ambayo iliwahusisha watu niwapendao. Kwa nyakati kama hizo, katika uchungu na imani, tunaweza tu kusema pamoja na Ayubu, “Bwana alitoa, na Bwana ametwaa; jina la Bwana lihimidiwe.”17

Kote katika Kanisa la ulimwenguni, vigingi na wilaya vipatavyo 3,500 na kata na matawi yapatayo 30,000 yanatoa kimbilio na usalama.18 Lakini ndani ya vigingi na kata zetu, familia na watu binafsi wengi walio waaminifu wanakabiliana na changamoto ngumu, hata wakati wakijua kwamba (pasipo kujua jinsi gani) mambo hayo yatafanyika kwa faida yao.

Huko Huddersfield, Uingereza, Kaka Samuel Bridgstock alifanyiwa vipimo na kugundulika akiwa katika hatua ya nne ya saratani muda mfupi kabla ya kuitwa kuwa rais mpya wa kigingi. Kutokana na uchunguzi huo, alimwuliza mke wake, Anna, kwa nini angeenda kuhojiwa.

“Kwa sababu,” Dada Bridgstock alisema, “unaenda kuitwa kama rais wa kigingi.”

Picha
Familia ya Bridgstock.

Mwanzoni alipewa mwaka mmoja au miwili ya kuishi, Rais Bridgstock (ambaye leo yuko hapa) yuko katika mwaka wake wa nne wa huduma. Ana siku nzuri na mbaya. Kigingi chake kinakusanyika kwa imani iliyoongezeka, huduma na wema. Siyo rahisi, lakini mke wake na familia wanaishi kwa imani, shukrani na huzuni inayoeleweka wakitumaini kutakuwa na shangwe ya milele kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo wenye kurejesha.19

Tunapokuwa watulivu, wa wazi na wanyenyekevu, tunaweza kuhisi uzuri, kusudi, na utulivu wa kuwa wa agano ambao Bwana anatoa. Katika nyakati takatifu, Yeye anaweza kutuachia tuone uhalisia mpana wa umilele ambao maisha yetu ya kila siku ni sehemu yake, ambapo mambo madogo na rahisi hufanya kazi pamoja kwa faida ya watoaji na wapokeaji.

Rebeka, binti wa rais wangu wa kwanza wa misioni, alishiriki jinsi Bwana alivyojibu sala yake kwa ajili ya faraja kwa fursa asiyotarajia ya kujibu sala ya mtu mwingine.

Picha
Rebeka alimpa mwanamke mashine ya oksijeni ya marehemu mama yake.

Usiku mmoja, Rebekah, akihuzunika kwa kufiwa na mama yake, alipata ono la wazi kwenda kununua mafuta kwa ajili ya gari lake. Alipofika kituo cha kuuza mafuta, akamkuta mwanamke mzee akipumua kwa shida na tanki kubwa la oksijeni. Baadaye, Rebeka akampa mwanamke yule mashine ya oksijeni ya kubebeka ya mama yake. Dada huyu kwa shukrani alisema, “Wewe umenirudishia uhuru wangu.” Mambo hufanyika pamoja kwa faida tunapohudumu kama ambavyo Yesu Kristo angefanya.

Baba aliyepangiwa pamoja na mwanawe wa umri wa mwalimu kama watumishi wenza alielezea, “Utumishi ni wakati tunapokuwa si tu majirani wenye kuleta biskuti kwa marafiki wenye kuaminika, bali waitikiaji wa kwanza wa kiroho.” Kuwa wa sehemu ya agano katika Yesu Kristo kunafariji, huunganisha, huweka wakfu.

Hata katika majanga, maandalizi ya kiroho yanaweza kutukumbusha Baba yetu wa Mbinguni alijua wakati tulipohisi kuwa hatarini zaidi na peke yetu. Kwa mfano, familia ambayo mtoto wao alikimbizwa hospitali na baadaye hupata faraja kwa kukumbuka Roho Mtakatifu amenong’ona mapema kabla ya nini cha kutarajia.

Wakati mwingine uhalisia mpana wa umilele ambao Bwana hutuacha tuuhisi unajumuisha familia zilizo upande wa pili wa pazia. Dada mmoja alipata faraja katika uongofu kwenye injili ya urejesho ya Yesu Kristo. Lakini bado matukio mawili yameathiri sana maisha yake—kuona ajali ya boti na kwa uchungu kumpoteza mama yake, ambaye alijiua.

Picha
Dada huyu alishinda hofu zake na kubatizwa.

Bado dada huyu alishinda hofu yake ya maji na kubatizwa kwa kuzamishwa. Na juu ya kile kilichokuja kuwa siku ya furaha sana, alishuhudia mtu mmoja, akisimama kwa niaba ya mama yake, aliyefariki akiwa anabatizwa hekaluni. “Ubatizo wa hekaluni ulimponya mama yangu na kuniweka mimi huru,” dada huyu alisema. “Ilikuwa mara ya kwanza kwangu kuhisi amani tangu mama yangu afariki.

Muziki wetu mtakatifu unatoa mwangwi wa hakikisho Lake kwamba mambo yote yatafanyika pamoja kwa faida yetu.

Tulia, nafsi yangu: Mungu Wako anatenda

Kuongoza siku zijazo, kama siku zilizopita.

Tumaini lako, ujasiri na usitingishike;

Yote sasa ya ajabu yatakuwa angavu mwishowe.20

Njooni enyi Watakatifu;

Kwa moyo tembea.

Safari yaweza kuwa ngumu,

Neema yatosha. …

Na tukifa kabla ya kufika,

Hakika! Yote ni sawa”21

Kitabu cha Mormoni ni ushahidi tunaoweza kuubeba mkononi mwetu kwamba Yesu ndiye Kristo na Mungu anatimiza ahadi Zake. Kikiwa kimeandikwa na manabii waliovuviwa ambao waliiona siku yetu, Kitabu cha Mormoni kinaanza na tamthiliya ya kawaida—familia ikishughulika na tofauti kubwa. Lakini, tunapojifunza na kutafakari 1 Nefi 1 hadi Moroni 10, tunavutiwa na Yesu Kristo na ushuhuda imara kwamba kile kilichotokea huko na kipindi hicho kinaweza kutubariki sisi hapa na sasa.

Kama Bwana kupitia nabii Wake aliye hai anavyoleta nyumba zaidi za Bwana karibu katika maeneo zaidi, baraka za hekaluni hufanya mambo pamoja kwa faida yetu. Tunakuja kwa agano na ibada kwa Mungu Baba yetu na Yesu Kristo na kupata mtazamo wa milele hapa duniani. Ikifanyika moja baada ya nyingine, jina baada ya jina, tunawapatia wanafamilia—mababu—ibada okozi na baraka za maagano katika mpangilio wa Bwana wa waokozi juu ya mlima Sayuni.22

Kadiri mahekalu yanavyokuja karibu na sisi katika maeneo mengi, dhabihu ya hekaluni tunayoweza kutoa ni kutafuta utakatifu katika nyumba ya Bwana mara nyingi zaidi. Kwa miaka mingi, tumeweka akiba, tumepanga na kutoa dhabihu ya kuja hekaluni. Sasa, kadiri hali inavyoruhusu, tafadhali njoo hata mara nyingi zaidi kwa Bwana katika nyumba Yake takatifu. Ruhusu kuabudu na kuhudumu hekaluni mara kwa mara kubariki, kulinde na kukushawishi wewe na familia yako—familia uliyo nayo na familia utakayokuwa nayo na utakayotaka iwe siku moja.

Picha
Bibi nje ya hekalu

Pia, ikiwa hali yako inaruhusu, tafadhali zingatia baraka ya kumiliki nguo zako za hekaluni.23 Bibi mmoja kutoka familia moja alisema kati ya kitu chochote ulimwenguni, alichokihitaji sana kilikuwa ni nguo zake za hekaluni. Mjukuu wake alisema, “Bibi alininong’oneza, ‘nitahudumu katika nguo zangu za hekaluni, na baada ya mimi kufa, nitazikwa nazo.’” Na wakati muda ulipofika, ilikuwa hivyo.

Kama Rais Russell M. Nelson anavyofundisha, “Kila kitu tunachoamini na kila ahadi ambayo Mungu ameifanya kwa watu Wake wa agano hufanyika hekaluni.”24

Kwa muda na milele, dhumuni la Uumbaji na asili ya Mungu Mwenyewe ni kuvileta vitu vyote pamoja kwa faida yetu.

Hili ndilo dhumuni la milele la Bwana. Ndio mtazamo Wake wa milele. Ndio ahadi Yake ya milele.

Wakati maisha yamejaa vitu vingi, na kusudi haliko wazi, wakati unapotaka kuishi vyema lakini haujui jinsi ya kufanya, njoo kwa Mungu Baba yetu na Yesu Kristo. Amini Wanaishi, na wanataka mambo yote kwa faida yako Ninashuhudia kwamba Wao wanataka hivyo, pasipo ukomo na milele, katika jina takatifu na tukufu la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Ona Yohana 16:33.

  2. Warumi 8:28.

  3. Mafundisho na Maagano 90:24. Kishazi maarufu cha “Yote mema” mara nyingi humaanisha mambo yako SAWA na katika utaratibu, pasipo kumaanisha kwa ukweli yako kwa faida yetu.

  4. Ona Musa 1:3.

  5. Ona Alma 7:11.

  6. Ona 2 Nefi 9:10–12. Mungu anaheshimu maadili ya haki ya kujiamulia, wakati mwingine akiruhusu hata matendo yasiyo ya haki ya watu wengine kutuathiri sisi. Lakini tunapokuwa tayari kufanya yote tunayoweza, neema ya Yesu Kristo na nguvu Yake yenye kuwezesha na dhabihu Yake ya kulipia dhambi vinaweza kutuosha, kutuponya na kutuunganisha, kutupatanisha na sisi wenyewe na kila mmoja, pande zote mbili za pazia.

  7. Ona Moroni 7:6, 10–12. Profesa Terry Warner anaandika kwa uangalifu juu ya mada hii.

  8. Ona Warumi 3:10; Moroni 10:25.

  9. Ona Moroni 10:32.

  10. Ona Mafundisho na Maagano 122:4, 7.

  11. Tunajifunza kwa uzoefu ambao tusingeweza kuuchagua. Wakati mwingine kubebeana mizigo kwa msaada wa Bwana kunaweza kuongeza uwezo wetu wa kubeba mizigo hiyo; Mosia 24:10–15 inafafanua ahadi ya Bwana ya “kuwatembelea watu wangu katika mateso yao na kuwaimarisha ili waweze kuibeba mizigo yao.” Alma 33:23 inafundisha kwamba “mizigo yetu ipate kuwa miepesi, kupitia shangwe ya Mwanawe.” Mosia 18:8 inatukumbusha kwamba tunakuwa “tayari kubebeana mizigo,” … “iwe miepesi.”

  12. Nabii Isaya anazungumza juu ya Masiya: “Roho ya Bwana Mungu i juu yangu; kwa sababu Bwana amenitia mafuta niwahubiri wanyenyekevu habari njema; amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo, … kuwafariji wote waliao; kuwaagizia hao waliao katika Sayuni, wapewe taji ya maua badala ya majivu, mafuta ya furaha badala ya maombolezo, vazi la sifa badala ya roho nzito” (Isaya 61:1–3). Vile vile, mtunzi wa Zaburi anatoa mtazamo wa ahadi Zake: “Huenda kilio huja kukaa usiku, Lakini asubuhi huwa furaha.” (Zaburi 30:5) Hii inajumuisha ahadi tukufu kwa wenye haki juu ya Ufufuko wa Kwanza.

  13. Mafundisho na Maagano 122:4. Ukiamini majaribu yatakuwa kwa kile kijulikanacho katika umilele “kitambo kidogo” haimaanishi kushusha au kuyafanya yenye kujaribu kidogo au changamoto kwa maumivu makali au mateso tunayoweza kupitia siku baada ya siku katika maisha haya, usiku usiovumilika wa kukosa usingizi, au kutokuwa na uhakika wa kila siku mpya. Labda ahadi ya kuweza kuangalia nyuma na kuona mateso yetu ya duniani katika nuru ya huruma ya Mungu na mtazamo wa milele unaongeza baadhi ya mtazamo kwenye uelewa wetu wa kidunia na matumaini yetu ya kuvumilia kwa imani na matumaini katika Yeye hata mwisho. Pia, tunapokuwa na macho ya kuona, mara nyingi kuna kizuri sasa; hatuna lazima ya kusubiri kwa siku za baadaye kuona yaliyo mazuri.

  14. Ona 2 Nefi 2:2.

  15. Ona Mathayo 7:9–10. Kumruhusu Mungu ashinde katika maisha yetu sio tu kukubali chochote kinachokuja. Ni kikamilifu kuamini kwamba Baba wa Mbinguni na Mwokozi wetu Yesu Kristo, wanataka tu na daima wanataka kile kilicho bora kwa ajili yetu. Wakati misiba inaposhambulia, tunaweza kujiuliza kwa imani, siyo “Kwa nini mimi” bali “ninaweza kujifunza Nini?” Na tunaweza kulia na waliovunjika mioyo na roho iliyopondeka, tukijua, kwa wakati Wake na katika njia Yake baraka za fidia na fursa zitakuja.

  16. Tumeagana kuomboleza na wanaoomboleza na kuwafariji wale wanaohitaji faraja (ona Mosia 18:9).

  17. Ayubu 1:21.

  18. Ona Mafundisho na Maagano 115:6.

  19. Imani katika uso wa magumu ni kinyume cha maumivu yaliyopo na kukata tamaa ambayo Kitabu cha Mormoni inaelezea juu ya wale “wanao mlaani Mungu, na kutamani kufa,” lakini ambao “hata hivyo … wangepambana kwa upanga kwa ajili ya maisha yao” (Mormoni 2:14).

  20. “Be Still, My Soul,” Hymns, no. 124.

  21. “Njooni Enyi Watakatifu,” Wimbo, namba. 30. Fikiria pia:

    Ni Hekima na Upendo Mkubwa Kiasi Gani. …

    Usanifu mkuu wa ukombozi,

    Pale haki, upendo, na rehema hukutana

    Kwenye uwiano wa kiungu!

    “Ni Upendo Ulioje,” Nyimbo za Kanisa,, na. 108.

    Katikati ya kutokuwa na uhakika wa maisha, tunajua muundo mkuu wa ukombozi utaleta haki, upendo na huruma pamoja kwa faida yetu.

  22. Ona Obadia 1:21. Nabii Joseph Smith alifundisha: “Inawezekanaje wao [watakatifu wa siku za mwisho] kuwa waokozi juu ya Mlima Sayuni? Kwa kujenga mahekalu yao, kusimamisha visima vyao vya ubatizo, na kusonga mbele kupokea ibada zote … kwa niaba ya wazao wao wote waliofariki” (Teachings of Presidents of the Church: Joseph Smith [2007], 473).

  23. Waumini wanaohudhuria hekaluni kwa mara ya kwanza wanaweza kununua nguo za hekaluni kwa bei ya punguzo.

  24. Russell M. Nelson, “Hekalu na Msingi Wako wa Kiroho,” Liahona,, Nov. 2021, 94.