Mkutano Mkuu
Ushuhuda Juu ya Yesu
Mkutano mkuu wa Aprili 2024


Ushuhuda Juu ya Yesu

Mwaliko wangu ni kutenda sasa ili kupata nafasi yako kama mtu ambaye ni jasiri katika ushuhuda wa Yesu.

Mnamo mwaka 1832, Joseph Smith na Sidney Rigdon walipokea ono kubwa kuhusu hatima ya milele ya watoto wa Mungu. Ufunuo huu ulizungumzia falme tatu za mbinguni. Rais Dallin H. Oaks alizungumza kuhusu “falme hizi za utukufu” Oktoba iliyopita,1 akibainisha kwamba, “kupitia ushindi na utukufu wa Mwanakondoo,”2 wote lakini watu wachache hatimaye watakombolewa katika moja ya falme hizi, “kulingana na hamu zilizoonyeshwa kupitia chaguzi zao.”3 Mpango wa Mungu wa ukombozi unajumuisha fursa kwa ulimwengu wote kwa watoto Wake wote, wakati wowote na popote walipo duniani.

Wakati utukufu hata mdogo zaidi kati ya falme hizi tatu, telestia, “unapita ufahamu wote,”4 tumaini la Baba yetu ni kwamba tutachagua—na, kupitia neema ya Mwanawe tustahili—utukufu wa juu na mkuu zaidi wa falme hizi, selestia, ambapo tunaweza kufurahia uzima wa milele kama “warithi pamoja na Kristo.”5 Rais Russell M. Nelson alitusihi “kufikiria selestia,” kufanya ufalme wa selestia lengo letu la milele na kisha kwa “umakini kufikiria wapi kila moja ya chaguzi [zetu] wakati wa maisha haya ya duniani [zitatuweka] katika ulimwengu ujao.”6

Wale walio katika ufalme wa selestia ni “wale waliopokea ushuhuda wa Yesu, … ambao ni watu wenye haki waliokamilishwa kupitia Yesu mpatanishi wa agano jipya.”7 Wakazi wa pili, au wa ufalme wa terestria, wanaelezewa kuwa wazuri kimsingi, ikiwa ni pamoja na “watu wenye kuheshimiwa duniani, ambao walipofushwa kwa ujanja wa wanadamu.” Tabia yao kuu ya kuwazuia ni kwamba “hawana ujasiri katika ushuhuda wa Yesu.”8 Kwa upande mwingine, wale waliopo chini, ufalme wa telestia ni wale ambao “hawakuipokea injili, wala ushuhuda wa Yesu.”9

Kumbuka kwamba sifa bainishi za wakazi wa kila ufalme ni jinsi wanavyohusiana na “ushuhuda wa Yesu,” kuanzia (1) kujitolea kwa moyo wote (2) kutokuwa jasiri (3) kukataliwa moja kwa moja. Katika uitikiaji wa kila mtu huja mustakabali wake wa milele.

I.

Ushuhuda wa Yesu ni nini?

Ni ushuhuda wa Roho Mtakatifu kwamba Yeye ni Mwana mtakatifu wa Mungu, Masiya na Mkombozi. Ni ushuhuda wa Yohana kwamba Yesu alikuwa mwanzoni na Mungu, kwamba Yeye ni Muumba wa mbingu na dunia, na kwamba “ndani yake kulikuwa na injili, na injili ilikuwa uzima, na uzima ulikuwa nuru ya wanadamu.”11 Ni “ushuhuda wa Mitume na Manabii, kwamba Yeye alikufa, akazikwa, na akafufuka siku ya tatu, na kupaa mbinguni.”11 Ni ufahamu kwamba “hakuna jina lingine ambalo kwalo huleta wokovu.”12 Ni “ushuhuda, wa mwisho wa yote,” uliotolewa na Nabii Joseph Smith “kwamba anaishi! … Kwamba Yeye ni Mwana wa Pekee wa Baba—kwamba kwa yeye, na kwa njia yake, na kutoka kwake, dunia zipo na ziliumbwa, na waliomo ni wana na mabinti wa Mungu.”13

II.

Zaidi ya ushuhuda huu ni swali, Tunafanya nini na huu ushuhuda?

Warithi wa ufalme wa selestia “wanapokea” ushuhuda wa Yesu katika ufahamu kamili kwa kubatizwa, kupokea Roho Mtakatifu na kushinda kwa imani.14 Kanuni na kweli za injili ya Yesu Kristo zinatawala vipaumbele na chaguzi zao. Ushuhuda juu ya Yesu unadhihirishwa katika vile walivyo na vile wanavyokuwa. Lengo lao ni hisani, “upendo msafi wa Kristo.”15 Fokasi yao ni kutafuta “kipimo cha kimo cha utimilifu wa Kristo.”16

Angalau baadhi ya wale ambao watapatikana katika ufalme wa terestria pia wanakubali ushuhuda wa Yesu, lakini wanatofautishwa na kile ambacho hawafanyi juu yake. Kutokuwa jasiri katika ushuhuda juu ya Mwokozi kunaashiria kiwango cha kutojali au ukawaida—kuwa “vuguvugu”17—kinyume na watu wa Amoni katika Kitabu cha Mormoni, kwa mfano, ambao walikuwa “wakitofautishwa kwa ari yao kwa Mungu.”18

Wakazi wa ufalme wa telestia ni wale ambao wanakataa ushuhuda wa Yesu pamoja na injili Yake, maagano Yake na manabii Wake. Wanaelezewa na Abinadi kama “kwa vile walienda kulingana na nia zao za tamaa na tamaa za kimwili; wakiwa wamekosa kumlingana Bwana waliponyoshewa mikono kwani walinyoshewa mikono ya rehema, na hawakukubali.”19

III.

Inamaanisha nini kuwa jasiri katika ushuhuda wa Yesu?

Kuna uwezekano kadhaa ambao unaweza kuzingatiwa katika kujibu swali hili. Nitataja chache. Kuwa jasiri katika ushuhuda wa Yesu hakika ni pamoja na kulea na kuimarisha ushuhuda huo. Wanafunzi wa kweli hawapuuzi mambo yanayoonekana kuwa madogo ambayo yanadumisha na kuimarisha ushuhuda wao wa Yesu, kama vile sala, kujifunza maandiko, utii wa Sabato na kushiriki sakramenti, kutubu, kutumikia na kuabudu katika nyumba ya Bwana. Rais Nelson anatukumbusha kwamba “kwa kasi ya kutisha, ushuhuda ambao haulishwi kila siku ‘na neno jema la Mungu’ [Moroni 6:4] unaweza kubomoka. Kwa hivyo, … tunahitaji uzoefu wa kila siku wa kumwabudu Bwana na kusoma injili Yake. Kisha aliongeza: “nakusihi umruhusu Mungu ashinde maishani mwako. Mpe sehemu nzuri ya wakati wako. Unapofanya hivyo, tambua kile kinachotokea kwenye kasi yako chanya ya kiroho.”20

Kuwa jasiri pia kunaashiria kuwa muwazi na wa watu wote kuhusu ushahidi wa mtu. Katika ubatizo, tunathibitisha utayari wetu wa “kusimama kama mashahidi wa Mungu nyakati zote na katika vitu vyote, na katika mahali popote tulipo, hata hadi kifo.”21 Hasa katika kipindi hiki cha Pasaka, sisi kwa furaha, hadharani, na kwa uwazi tunatangaza ushuhuda wetu juu ya Kristo aliyefufuka, aliye hai.

Jambo moja la kuwa jasiri katika ushuhuda juu ya Yesu ni kuwasikiliza wajumbe Wake. Mungu hatulazimishi kuingia katika njia bora, njia ya agano, lakini Yeye anawaagiza manabii Wake kutufanya tufahamu kikamilifu matokeo ya chaguzi zetu. Na sio tu waumini wa Kanisa Lake. Kupitia manabii na mitume Wake, Yeye kwa upendo anausihi ulimwengu wote kutii ukweli ambao utawafanya wawe huru,22 akiwaokoa na masumbuko yasiyo lazima, na kuwaletea furaha ya kudumu.

Kuwa jasiri katika ushuhuda juu ya Yesu kunamaanisha kuwatia moyo wengine, kwa neno na mfano, kuwa jasiri, hasa wale wa familia zetu wenyewe. Mzee Neal A. Maxwell aliwahi kuhutubia “waumini muhimu ‘waheshimiwa’ [wa Kanisa] ambao wanapitia kitu juu juu badala ya kuzamisha kwa kina ufuasi wao na ambao wanajishughulisha kwa kawaida badala ya ‘kujishughulisha kwa shauku’ [Mafundisho na Maagano 76:75; 58:27]. “23 Akibainisha kwamba wote wako huru kuchagua, Mzee Maxwell aliomboleza: “Kwa bahati mbaya, hata hivyo, wakati wengine wanachagua uvivu, wanachagua sio tu kwa ajili yao wenyewe, bali kwa ajili ya kizazi kijacho na kijacho. Upotofu mdogo kwa wazazi unaweza kuzalisha mkengeuko mkubwa kwa watoto wao! Vizazi vya awali katika familia vinaweza kuwa vimeonyesha kujitolea kwa dhati, wakati baadhi katika kizazi cha sasa wakionyesha upotofu. Cha kusikitisha, baadaye, wengine wanaweza kuchagua uasi, kadiri mmomonyoko unavozidi kuchukua mkondo wake.”24

Miaka kadhaa iliyopita, Mzee John H. Groberg alisimulia hadithi ya familia changa iliyokuwa ikiishi katika tawi dogo huko Hawaii mwanzoni mwa miaka ya 1900. Walikuwa waumini wa Kanisa kwa karibu miaka miwili wakati mmoja wa binti zao alipougua ugonjwa ambao haukutambuliwa na kulazwa hospitalini. Kanisani Jumapili iliyofuata, baba na mwanawe waliandaa sakramenti kama walivyofanya wiki nyingi, lakini baba kijana alipopiga magoti kubariki mkate, rais wa tawi, ghafla alitambua ni nani aliyekuwa kwenye meza ya sakramenti, akasimama juu na kusema, “Acha. Huwezi kugusa sakramenti. Binti yako ana ugonjwa usiojulikana. Ondoka mara moja wakati huo mtu mwingine aandae mkate mpya wa sakramenti. Hatuwezi kuwa nawe hapa. Nenda.” Baba huyo aliyeshangaa alimtazama rais wa tawi na kisha mkusanyiko na, akiwa na wasiwasi mwingi na aibu kutoka kwa wote, akaiita familia yake, na wakatoka kimya kimya nje ya kanisa.

Hakuna neno lililosemwa, kwa majonzi, familia ilitembea kando ya njia kuelekea kwenye nyumba yao ndogo. Huko walikaa katika duara, na baba akasema, “Tafadhali kaeni kimya mpaka nitakapokuwa tayari kusema.” Mwanae yule mdogo wa kiume alijiuliza wangefanya nini ili kulipiza kisasi kwa aibu waliyokuwa wameipata: je, wangeua nguruwe wa rais wa tawi, au kuchoma moto nyumba yake au kujiunga na kanisa lingine? Dakika tano, kumi, kumi na tano, ishirini na tano zilipita kwa ukimya.

Vidole vya baba vilivyojikunja vilianza kulegea, na machozi kumlengalenga. Mama alianza kulia, na mara kila mmoja wa watoto alikuwa akilia kimya kimya. Baba alimgeukia mkewe na kusema, “Ninakupenda” na kisha akarudia maneno hayo kwa kila mmoja wa watoto wao. “Ninawapenda wote na ninahitaji tuwe pamoja, milele, kama familia. Na njia pekee inayowezekana ni kwa sisi sote kuwa waumini wazuri wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho na kuunganishwa kwa ukuhani mtakatifu katika hekalu. Hili sio kanisa la rais wa tawi. Hili ni Kanisa la Yesu Kristo. Hatutamruhusu mtu yeyote au madhara yoyote au aibu au kiburi kutuzuia kuwa pamoja milele. Jumapili ijayo tutakwenda tena kanisani. Tutakaa peke yetu hadi ugonjwa wa binti yetu utakapojulikana, lakini tutakwenda tena.”

Walikwenda tena, binti yao akapona, na familia iliunganishwa katika Hekalu la Laie Hawaii lilipokamilika. Leo, zaidi ya roho 100 zinamwita baba yao, babu, na babu yao aliyebarikiwa kwa sababu aliyaweka macho yake kwenye umilele.25

Jambo moja la mwisho la kuwa jasiri katika ushuhuda juu ya Yesu ambalo nitalitaja ni ufuatiliaji wetu binafsi wa utakatifu binafsi. Yesu ni Mkombozi wetu muhimu,26 na Yeye anatusihi, “Tubuni nyinyi nyote katika sehemu zote za dunia, na mje kwangu na mbatizwe katika jina langu kwamba muweze kutakaswa kwa kupokea Roho Mtakatifu, ili msimame mbele yangu bila mawaa katika siku ya mwisho.”27

Nabii Mormoni anaelezea kundi moja la Watakatifu ambao walivumilia kwa njia hii licha ya “kupitia mateso mengi”28:

“Walakini walifunga na kuomba kila wakati, na wakapokea nguvu kwa wingi katika unyenyekevu wao, na wakawa imara zaidi na imara katika imani kwa Kristo, hadi nafsi zao zikajazwa na shangwe na faraja, ndiyo, hata kwenye kusafishwa na utakaso wa mioyo yao, utakaso ambao huja kwa sababu ya wao kumtolea Mungu mioyo yao.”29 Ni badiliko hili kuu la moyo—kukabidhi mioyo yetu kwa Mungu na kuzaliwa upya kiroho kupitia neema ya Mwokozi—ndiko tunatafuta.30

Mwaliko wangu ni kutenda sasa ili kupata nafasi yako kama mtu ambaye ni jasiri katika ushuhuda wa Yesu. Kama toba inavyohitajika, “msiahirishe siku ya toba yenu,”31 isije “katika saa msiyodhani wakati wa majira ya joto yamepita, na mavuno yamekwisha, na nafsi zenu hazijaokolewa.”32 Kuwa na bidii katika kushika maagano yako na Mungu. Usikubali “kukwazwa [kwa] ukali wa neno.”33 “Kumbuka kubaki na jina la [Kristo] likiwa limeandikwa mioyoni mwenu, … kwamba [muweze] kusikia na kujua sauti ambayo itawaita, na pia, lile jina ambalo atawaita.”34 Na hatimaye, “amueni vitu hivi mioyoni mwenu, kwamba mtatenda vitu hivi ambavyo [Yesu] atawafundisha, na kuwaamuru ninyi.”35

Baba yetu anataka watoto Wake wote ambao watataka kufurahia uzima wa milele pamoja Naye katika ufalme Wake wa selestia. Yesu aliteseka, alikufa na akafufuka ili kufanya hilo liwezekane. Yeye “amepaa mbinguni, na ameketi mkono wa kulia wa Mungu, kudai kutoka kwa Baba haki zake za huruma ambazo anazo juu ya watoto wa watu.”36 Ninaomba kwamba sote tubarikiwe kwa ushuhuda wa kina wa Bwana Yesu Kristo, tufurahi na kuwa jasiri katika ushuhuda huo, na kufurahia matunda ya neema Yake katika maisha yetu daima. Katika jina la Yesu Kristo, amina.