Mkutano Mkuu
Mtumaini Bwana
Mkutano mkuu wa Aprili 2024


Mtumaini Bwana

Uhusiano wetu na Mungu utakua tu hadi kwenye kiwango ambacho tuko radhi kuweka tumaini letu Kwake.

Katika familia yetu, kuna nyakati tunacheza mchezo tunaouita “Zoezi la Kuanguka Kinyume.” Yawezekana mmeucheza pia. Watu wawili wanasimama hatua chache kutoka kila mmoja, mmoja akimgeuzia mgongo mwingine. Kwa ishara kutoka kwa mtu wa nyuma, mtu wa mbele anaanguka kinyume kwenye mikono iliyo tayari ya rafiki zao.

Tumaini ni msingi wa uhusiano wote. Swali la kwanza kwenye uhusiano wowote ni je “Ninaweza kumtumaini mtu mwingine?” Uhusiano unaanzishwa pale tu watu wanapokuwa radhi kuweka tumaini kwa kila mmoja. Unakuwa si uhusiano ikiwa mtu mmoja anatumaini kikamilifu lakini yule mwingine hafanyi hivyo.

Kila mmoja wetu ni mwana au binti wa kiroho wa Baba yetu wa Mbinguni mwenye upendo.1 Lakini wakati asili ya kiroho inatoa msingi, yenyewe peke yake haijengi uhusiano wa maana na Mungu. Uhusiano unaweza kujengwa pale tu tunapochagua kuweka tumaini Kwake.

Baba wa Mbinguni anatamani kujenga uhusiano wa karibu, binafsi kwa kila mmoja wa watoto Wake wa kiroho.2 Yesu alionyesha hamu hiyo wakati Yeye alisali, “Ili wote wawe kitu kimoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako, ili nao waweze kuwa kitu kimoja na sisi.”3 Uhusiano Mungu anao utafuta na kila mtoto wa kiroho ni ule wa karibu sana na binafsi kiasi kwamba ataweza kushiriki vyote alivyonavyo na vyote Yeye alivyo.4 Aina hiyo ya uhusiano wa kina, endelevu unaweza kukuzwa pale tu tunapojenga juu ya tumaini kamili na timilifu.

Kwa sehemu Yake, Baba wa Mbinguni amefanya kazi kuanzia mwanzo kutoa tumaini Lake lote katika uwezekano wa kiungu wa kila mmoja wa watoto Wake. Tumaini lipo kwenye mpango alio uwasilisha kwa ajili ya ukuaji na maendeleo yetu kabla ya kuja kwetu duniani. Angetufundisha sheria za milele, angeumba dunia, kutupatia miili, kutupatia zawadi ya kufanya chaguzi sisi wenyewe, na kuturuhusu tujifunze na kukua kwa kufanya chaguzi zetu. Yeye anatutaka sisi tuchague kufuata sheria Zake na kurudi kufurahia uzima wa milele pamoja Naye na Mwanawe.

Akijua kwamba si mara zote tutafanya chaguzi nzuri, Yeye pia aliandaa njia kwa ajili yetu kujiokoa kutokana na matokeo ya chaguzi mbaya. Alimtoa Mwokozi kwetu—Mwanaye, Yesu Kristo—ili kulipia adhabu ya dhambi zetu na kutufanya safi tena kwa sharti la toba.5 Yeye anatualika tutumie zawadi ya thamani ya toba kila mara.6

Kila mzazi anajua jinsi ilivyo ngumu kumtumaini mtoto vya kutosha kumuacha afanye chaguzi zake mwenyewe, hususani wakati mzazi anapojua mtoto ana uwezekano wa kufanya makosa na hatimaye kuteseka kama matokeo. Bado Baba wa Mbinguni anaturuhusu sisi tutafanya chaguzi ambazo zitatusaidia tufikie uwezekano wetu wa kiungu! Kama Mzee Dale G. Renlund alivyofundisha, “lengo [Lake] si kuwafanya watoto Wake watende kile kilicho chema; ni kuwafanya watoto Wake wachague kutenda kile kilicho chema na hatimaye wawe kama Yeye.”7.

Licha ya tumaini la Mungu kwetu, uhusiano wetu na Yeye utakua tu hadi kwenye kiwango ambacho tuko radhi kuweka tumaini Kwake. Changamoto ni kwamba tunaishi kwenye ulimwengu ulioanguka na sote tumepata uzoefu wa tumaini kusalitiwa kama matokeo ya kukosa uaminifu, hila, shurutisho kutoka kwa wengine, au hali zinginezo. Tunaposalitiwa mara moja, tunaweza kushindwa kutumaini tena. Uzoefu huu wa tumaini hasi kwa wanadamu wasio wakamilifu unaweza kuathiri uwezo wetu na utayari wetu wa kumtumaini Baba wa Mbinguni aliye mkamilifu.

Miaka kadhaa iliyopita, marafiki zangu wawili, Leonid na Valentina, walionyesha hamu ya kuwa waumini wa Kanisa. Leonid alipoanza kujifunza injili, alipata wakati mgumu kusali. Mapema katika maisha yake, Leonid aliteseka kutokana na ulaghai na kudhibitiwa na watu waliomzidi cheo na alikuwa amejenga ukosefu wa tumaini kwa wenye mamlaka. Uzoefu huu uliathiri uwezo wake wa kuufungua moyo wake na kuonyesha hisia zake kwa Baba wa Mbinguni. Baada ya muda na kujifunza, Leonid alipata uelewa mzuri wa sifa ya Mungu na alipata uzoefu wa kuhisi upendo wa Mungu. Hatimaye, sala ikawa njia ya asili kwake ya kuonyesha shukrani na upendo aliokuwa akiuhisi kwa Mungu. Ongezeko la tumaini katika Mungu lilimwongoza yeye na Valentina kuingia kwenye maagano ili kuimarisha uhusiano wao na Mungu na mmoja na mwingine.

Ikiwa ukosefu wa tumaini wa siku za nyuma unakuzuia kumtumaini Mungu, tafadhali fuata mfano wa Leonid. Kwa subira jifunze zaidi kumhusu Baba wa Mbinguni, tabia Yake, sifa Zake na malengo Yake. Tafuta na uandike uzoefu unapohisi upendo na nguvu Zake katika maisha yako. Nabii wetu aliye hai, Rais Russell M. Nelson, amefundisha kwamba kadiri tunavyojifunza zaidi kumhusu Mungu, ndivyo itakavyokuwa rahisi kwetu kumtumaini Yeye.8

Wakati mwinginee njia nzuri zaidi ya kujifunza kumtumaini Mungu ni kwa kumtumaini tu. Kama vile “Zoezi la Kuanguka Kinyume,” wakati mwingine tunahitaji tu kuwa tayari kuanguka nyuma na kumuacha Yeye atudake. Maisha ya duniani ni mtihani. Changamoto zinazotunyoosha kupita uwezo wetu binafsi huja kila mara. Wakati maarifa na uelewa wetu vinapokuwa havitoshi, kiasili tunatafuta nyenzo za kutusaidia. Katika dunia yenye mrundikano wa taarifa, hakuna upungufu wa vyanzo vinavyotangaza masuluhisho yao kwa changamoto zetu. Hata hivyo, ushauri rahisi, wa muda mrefu katika Mithali unatupatia ushauri bora zaidi: “Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote.”9 Tunaonyesha tumaini letu katika Mungu kwa kumgeukia Yeye kwanza wakati tunapokabiliwa na changamoto za maisha.

Baada ya mimi kumaliza shule ya sheria huko Utah, familia yetu ilikabiliwa na uamuzi muhimu wa wapi tungefanya kazi na kujenga nyumba yetu. Baada ya kushauriana mmoja na mwingine na Bwana, tulihisi kuongozwa kuhamisha familia yetu hadi mashariki ya Marekani, mbali na wazazi na ndugu zetu. Mwanzoni, mambo yalienda vizuri, na tulihisi uthibitisho katika uamuzi wetu. Lakini kisha mambo yalibadilika. Kulikuwa na punguzo la wafanyakazi kwenye kampuni ya wanasheria, na nilikabiliwa na uwezekano wa kukosa ajira au bima wakati ambapo binti yetu Dora alizaliwa na changamoto kubwa ya kiafya na mahitaji maalumu ya muda mrefu. Wakati tukipambana na changamoto hizi, nilipatiwa wito wa kutumika ambao ungehitaji muda na kujitolea kwa hali ya juu.

Kamwe sikuwahi kukabiliwa na changamoto kama hii na nilizidiwa. Nilianza kutilia shaka uamuzi ambo tulikuwa tumefanya na uthibitisho ulioambatana nao. Tulipaswa kumtumaini Bwana, na mambo yalipaswa kufanikiwa. Nilikuwa nimeanguka kinyume, na ilikuwa inaonekana kwamba hakuna mtu wa kunidaka.

Siku moja, maneno “Usiulize kwa nini; uliza ni kipi ninataka ujifunze” yalikuja kwa uwazi kwenye akili yangu na moyo wangu. Sasa nilikuwa nimekanganyikiwa hata zaidi. Katika wakati ule wa mkanganyiko wangu kuhusu uamuzi wangu wa mwanzo, Mungu alikuwa akinialika nimtumaini Yeye hata zaidi. Nikikumbuka nyuma, huu ulikuwa ni wakati muhimu sana katika maisha yangu—ulikuwa wakati nilipotambua kwamba njia bora ya kujifunza kutumaini katika Mungu ilikuwa kumtumaini Yeye tu. Katika wiki zilizofuata, nilitazama kwa mshangao Bwana alipofungua mpango Wake wa ajabu wa kubariki familia yangu.

Walimu na makocha wazuri wanajua kwamba ukuaji kiakili na nguvu ya kimwili vinaweza kutokea tu wakati akili na misuli inatanuliwa. Vivyo hivyo, Mungu anatualika tukue kwa kutumaini ufundishaji Wake wa kiroho kupitia uzoefu unaotanua nafsi. Kwa hiyo, tunaweza kuwa na uhakika kwamba licha ya tumaini lolote ambalo tumelionesha huko nyuma, uzoefu mwingine wa kutanua tumaini bado upo mbele. Mungu anafokasi kwenye ukuaji na maendeleo yetu. Yeye ni Mwalimu Mkuu, kocha mkamilifu ambaye daima anatunyoosha ili kutusaidia tutambue zaidi uwezekano wetu wa kiungu. Hiyo mara zote itajumuisha mwaliko wa baadaye wa kuongeza kiwango cha kumtumaini Yeye.

Kitabu cha Mormoni kinafundisha mpangilio ambao Mungu anautumia kutunyoosha ili kujenga uhusiano imara na sisi. Katika Njoo, Unifuate, hivi karibuni tumejifunza kuhusu jinsi tumaini la Nefi kwa Mungu lilivyojaribiwa wakati yeye na kaka zake walipoamriwa warejee Yerusalemu kuchukua mabamba ya shaba. Baada ya jaribio lao la mwanzo kushindwa, kaka zake walikata tamaa na walikuwa tayari kurejea bila hayo mabamba. Lakini Nefi aliamua kuweka tumaini lake kamili kwa Bwana na alifanikiwa katika kuyapata mabamba.10 Uzoefu huo yawezekana uliimarisha ujasiri wa Nefi kwa Mungu wakati upinde wake ulipovunjika na familia ilikuwa ikikabiliwa na njaa nyikani. Tena, Nefi alichagua kumtumaini Mungu, na familia iliokolewa.11 Uzoefu huu wenye mafanikio ulimpa Nefi ujasiri imara kwa Mungu kwa ajili ya kazi kubwa yenye kukuza tumaini ya kujenga merikebu.12

Kupitia uzoefu huu, Nefi aliimarisha uhusiano wake na Mungu kwa kumtumaini Yeye daima na kwa uthabiti. Mungu anatumia mpangilio huo huo kwetu. Yeye anatoa mialiko ili kuimarisha na kukuza imani yetu Kwake.13 Kila wakati tunapokubali au kutendea kazi mwaliko, tumaini letu kwa Mungu hukua. Ikiwa tutapuuzia au kuukataa mwaliko, maendeleo yetu yanasimama mpaka tutakapokuwa tayari kutendea kazi mwaliko mpya.

Habari njema ni kwamba bila kujali tumaini tulilochagua au ambalo hatukuchagua kuliweka kwa Mungu kipindi cha nyuma, tunaweza kuchagua kumtumaini Mungu leo na kila siku kuanzia sasa na kuendelea. Ninaahidi kwamba kila wakati tunapotenda, Mungu atakuwa hapo kutushika, na uhusiano wetu wa kutumaini utakua imara zaidi na zaidi mpaka siku ile tutakuwa wamoja na Yeye na Mwanawe. Kisha tunaweza kutangaza kama Nefi, “Ewe Bwana, nimekuamini, na nitakuamini milele.”14 Katika jina la Yesu Kristo, amina.