Mkutano Mkuu
Upinzani Katika Mambo Yote
Mkutano mkuu wa Aprili 2024


Upinzani Katika Mambo Yote

Ili kuweza kutumia haki yetu ya kujiamulia, tunahitaji kuwa na chaguzi zinazokinzana.

Hivi karibuni, nikiwa naendesha gari katika jiji tusilolijua, kwa bahati mbaya nilikosea barabara, hii ilituingiza mimi na mke wangu kwenye barabara ya mwendo kasi kwa maili nyingi bila kuweza kugeuza tena. Tulipokea mwaliko mzuri wa kutembelea nyumbani kwa rafiki na tulihofia kwamba sasa tungefika kwa kuchelewa sana kuliko tulivyotarajia.

Tukiwa kwenye barabara hii ya mwendo kasi na tukifikiria cha kufanya bila mafanikio, nilijilaumu kwa kutokuweka umakini kwenye mfumo wa kuniongoza. Uzoefu huu ulinifanya nifikirie jinsi wakati mwingine katika maisha yetu unavyofanya maamuzi mabaya na jinsi inavyobidi kuishi na madhara yake kwa unyenyekevu na kwa ustahimilivu mpaka tubadilishe mwenendo wetu tena.

Maisha yamejaa ufanyaji wa chaguzi. Baba yetu wa Mbinguni alitupatia kipawa cha kiungu cha haki ya kujiamulia ili kwamba tujifunze kutokana na chaguzi zetu—zile zilizo sahihi na pia mbaya. Tunasahihisha chaguzi zetu mbaya pale tunapotubu. Hapa ndipo ukuaji hutokea. Mpango wa Baba wa Mbinguni kwa ajili yetu sote ni kuhusu kujifunza, kukua na kusonga kuelekea uzima wa milele.

Tangu mimi na mke wangu tulipofundishwa na wamisionari na kujiunga na Kanisa miaka mingi iliyopita, daima nimevutiwa kwa mafundisho yasiyo na kifani ambayo Lehi alimpa mwana wake Yakobo katika Kitabu cha Mormoni. Alimfundisha kwamba “Bwana Mungu amemruhusu mwanadamu kujitendea mwenyewe”1 na kwamba “lazima, kuwe na upinzani katika vitu vyote.”2 Ili kuweza kutumia haki yetu ya kujiamulia, tunahitaji kuwa na chaguzi zinazokinzana. Kwa kufanya hivyo, Kitabu cha Mormoni pia hutukumbusha kwamba “tumeshauriwa kikamilifu”3 na kwamba “Roho ya Kristo”4 imetolewa kwa kila mmoja wetu “ili kujua jema na baya.”5

Katika maisha, mara kwa mara tunakabiliana na chaguzi nyingi muhimu. Kwa mfano:

  • Kuchagua kama tutafuata amri za Mungu au la.

  • Kuchagua kuwa na imani na kutambua pale miujiza inapotokea au kwa shauku kusubiri kitu kutokea kabla ya kuchagua kuamini.

  • Kuchagua kukuza tumaini katika Mungu au kwa hofu kutarajia changamoto nyingine katika siku inayofuatia.

Kama vile nilipokosea njia katika barabara ile, mateso yatokanayo na madhara ya maamuzi yetu mabovu, mara nyingi yanaweza kuwa ya maumivu kwa sababu sisi ndio wa kulaumiwa. Hata hivyo, tunaweza daima kuchagua kupokea faraja kupitia mchakato wa kiungu wa toba, kufanya mambo maovu kuwa mema tena, na kwa kufanya hivyo kujifunza baadhi ya masomo ya kubadilisha maisha.

Wakati mwingine tunaweza kupitia upinzani na majaribu kutokana na vitu nje ya uwezo wetu, kama vile:

  • Nyakati za afya na vipindi vya ugonjwa.

  • Nyakati za amani na nyakati za vita.

  • Nyakati za mchana na usiku na nyakati za joto na baridi.

  • Nyakati za kazi zikifuatiwa na nyakati za mapumziko.

Ingawa kwa kawaida hatuwezi kuchagua hali hizi kwa sababu hutokea tu ghafla, bado tuko huru kuchagua jinsi ya kutenda kwenye hali hizi. Tunaweza kufanya hivyo kwa mtazamo chanya au hasi. Tunaweza kujifunza kutokana na uzoefu huu na kuomba msaada wa Bwana au tunaweza kudhani kwamba tuko peke yetu katika jaribu hili na kwamba tunateseka peke yetu. Tunaweza “kubadilisha hali yetu” kwenye uelekeo mpya au tunaweza kuamua kutobadili chochote. Katika giza la usiku tunaweza kugeukia taa zetu. Katika baridi ya msimu wa baridi, tunapaswa kuchagua kuvaa mavazi ya joto. Katika msimu wa ugonjwa, tunaweza kutafuta msaada wa matibabu na wa kiroho. Tunachagua jinsi ya kutenda kwenye hali hizi.

Rekebisha, jifunze, tafuta, na chagua yote haya ni vitenzi vya matendo. Kumbuka kwamba sisi ni watendaji na sio vitu. Na kamwe tusisahau kwamba Yesu aliahidi “atabeba maumivu na magonjwa ya watu wake … ili … atusaidie,” au atuinue pale tunapomgeukia Yeye.6 Tunaweza kuchagua kujenga msingi wetu juu ya mwamba ambao ni Yesu Kristo ili kwamba wakati pepo kali zijapo “hazitakuwa na nguvu juu [yetu].”7 Yeye ameahidi kwamba Yeyote ajaye [Kwake], huyo atampokea; na wamebarikiwa wale wajao [Kwake].”8

Sasa, kuna kanuni moja ya ziada ambayo ni muhimu hasa. Lehi alisema kwamba, “lazima … kuwe na upinzani katika vitu vyote.”9 Hii humaanisha kwamba vitu pinzani havikai mbalimbali. Vinaweza hata kukamilishana. Hatungeweza kutambua shangwe kama hatujapitia huzuni kwa kiwango fulani. Kuhisi njaa wakati mwingine hutusaidia kuwa na shukrani wakati tuna cha kutosha kula tena. Hatungeweza kutambua ukweli kama hatujaona uongo hapa na pale.

Vinyume hivi ni kama pande mbili za sarafu moja. Pande zote mbili huwa zipo siku zote. Charles Dickens alitoa mfano wa wazo hili alipoandika kwamba “ilikuwa ni muda mzuri zaidi, ilikuwa ni muda mbaya zaidi.”10

Acha nitoe mfano kutoka kwenye maisha yetu wenyewe. Kuoana, kuunda familia na kuwa na watoto kumeleta kwetu nyakati za shangwe kuu tuliyowahi kuipitia katika maisha yetu lakini pia nyakati kuu za maumivu, uchungu na huzuni pale kitu kinapotokea kwa mmoja wetu. Shangwe isiyo na mwisho na furaha pamoja na watoto wetu ilifuatiwa pia na vipindi vilivyojirudia vya magonjwa, kulazwa hospitalini na kutolala usiku kulikojaa mkanganyiko, pia kupata ahueni kupitia sala na baraka za ukuhani. Uzoefu huu unaokinzana ulitufunza kwamba kamwe hatuko peke yetu katika nyakati za mateso na pia ulituonyesha jinsi gani tunaweza kuhimili kwa msaada wa Bwana. Uzoefu huu ulisaidia kutuchonga katika njia nzuri, na umekuwa ni wa kufaa siku zote. Je, hiki sio kile tulichokuja kukifanya hapa duniani?

Katika maandiko pia tunapata mifano ya kuvutia:

  • Lehi alimfundisha mwana wake Yakobo kwamba mateso aliyoteseka nyikani yalimsaidia kujua wema wa Mungu na kwamba “[Mungu] ataweka wakfu masumbuko [yake] kwa faida [yake].”11

  • Wakati wa mateso makali ya Joseph Smith huko Gereza la Liberty, Bwana alimwambia kwamba “mambo haya yote yatampa [yeye] uzoefu, na yatakuwa kwa faida [yake].”12

  • Hatimaye, dhabihu isiyo na mwisho ya Yesu kristo kwa dhati ilikuwa ni mfano mkuu wa maumivu na mateso ambayo hayajapata kuonekana, lakini pia yalileta baraka nzuri za Upatanisho Wake kwa watoto wote wa Mungu.

Palipo na mwangaza, vivuli lazima vitakuwepo. Mafuriko yanaweza kuleta uharibifu, lakini huleta maisha pia. Machozi ya huzuni mara nyingi hugeuka kuwa machozi ya ahueni na furaha. Hisia za huzuni pale mpendwa anapoondoka baadaye hujazwa kwa shangwe ya kukutana tena. Katika nyakati za vita na uharibifu, matendo mengi madogo ya wema na upendo pia hutokea kwa wale wenye “macho ya kuona na masikio ya kusikia.”13

Ulimwengu wetu leo mara nyingi umekuwa wa hofu na mashaka—hofu ya kile kitakachotokea kesho. Lakini Yesu ametufundisha kumwamini na “[kumtegemea] katika kila wazo; msitie shaka, msiogope.”14

Acha tufanye jitihada za mara kwa mara za dhati za kuona kila upande wa shilingi iliyotolewa kwetu. Ingawaje pande zote wakati mwingine zinaweza zisionekane kwetu moja kwa moja, tunaweza kujua na kutumaini kwamba pande hizo zitakuwepo.

Tunaweza kujihakikishia kwamba magumu yetu, huzuni, mateso na uchungu havitufafanui; bali, ni jinsi tunavyovishughulikia ndicho kitakachotusaidia kukua na kusonga karibu na Mungu. Ni mtazamo wetu na chaguzi zetu ndizo ambazo hutufafanua sisi zaidi kuliko changamoto zetu.

Ukiwa na afya, thamini na shukuru kwa hilo kila wakati. Ukiwa na ugonjwa, tafuta kwa subira kujifunza kutokana na hilo na fahamu kwamba hili linaweza kubadilika tena kulingana na mapenzi ya Munngu. Ukiwa katika huzuni, tumaini kwamba furaha i karibu; mara nyingi hatuwezi kuiona papo hapo. Kwa dhati hamisha fokasi yako na kuza mawazo yako kwenye mtazamo chanya wa changamoto, kwa sababu siku zote zipo! Kamwe usisahau kuwa mwenye shukrani. Chagua kuamini. Chagua kuwa na imani katika Yesu Kristo. Chagua daima kumtumaini Mungu. Chagua “kufikiria selestia,” kama Rais Russell M. Nelson alivyotufundisha HIVI karibuni!15

Acha tuutambue mpango mzuri wa Baba yetu wa Mbinguni kwa ajili yetu. Anatupenda na alimtuma Mwana Wake Mpendwa atusaidie katika mateso yetu na kutufungulia njia ya kurejea Kwake. Yesu Kristo yu hai na yupo muda wote, akitusubiri tuchague kumlingana Yeye ili tupokee msaada, nguvu na wokovu. Kwa mambo haya ninashuhudia katika jina la Yesu Kristo, amina.