Mkutano Mkuu
Mvaeni Bwana Yesu Kristo
Mkutano mkuu wa Aprili 2024


Mvaeni Bwana Yesu Kristo

Kupitia kuheshimu maagano yetu, tunamwezesha Mungu kumimina baraka nyingi zilizoahidiwa zinazohusiana na maagano hayo.

Kadiri watoto wangu wadogo wawili walivyokuwa wakikua, niligundua vitabu ambavyo vilikuwa vya kuburudisha na kuhusisha lakini pia vilivyotumia ishara katika hadithi zake. Tuliposoma pamoja wakati wa jioni, nilipendelea kuwasaidia watoto wangu waelewe ishara mwandishi alizokuwa akitumia kufundisha kanuni kuu, hata kanuni za injili.

Nilijua hili lilikuwa likieleweka wakati siku moja kijana wangu wa kiume alipokuwa kwenye umri wake wa kuuanza ujana. Alikuwa ameanza kitabu kipya na alitaka tu kufurahia hadithi, lakini akili yake ilizidi kujaribu kutafuta maana kuu katika kila kitu alichokisoma. Alikasirishwa, lakini mimi nilitabasamu kwa ndani.

Yesu alifundisha kupitia hadithi na ishara1—mbegu ya haradali kufundisha nguvu ya imani,2 kondoo aliyepotea kufundisha thamani ya nafsi,3 mwana mpotevu kufundisha sifa ya Mungu.4 Mifano yake ilikuwa ishara ambazo kwazo angeweza kufundisha masomo makuu kwa wale waliokuwa na “masikio ya kusikia.”5 Lakini wale wasiotafuta maana kuu hawangeelewa,6 kama vile ambavyo wale waliosoma vitabu vilevile nilivyowasomea watoto wangu kamwe hawakufahamu kulikuwa na maana kuu na mengi zaidi ya kupata kwenye hadithi hizo.

Wakati Mungu Baba alipomtoa Mwana Wake wa Pekee kama dhabihu kwa ajili yetu, Yesu Kristo Mwenyewe alikuwa ishara muhimu zaidi ya upendo hai wa Baba yetu wa Mbinguni kwa kila mmoja wetu.7 Yesu Kristo alikuwa Mwana-kondoo wa Mungu.8

Tunayo fursa na baraka ya kualikwa kwenye uhusiano wa agano na Mungu, ambapo maisha yetu wenyewe yanaweza kuwa ishara ya agano hilo. Maagano hutengeneza aina ya uhusiano ambao humruhusu Mungu kutufinyanga na kutubadilisha kulingana na muda na kutuinua tuwe zaidi kama Mwokozi, akituvuta karibu zaidi Kwake na kwa Baba yetu9 na hatimaye kutuandaa tuingie kwenye uwepo Wao.

Kila mtu hapa duniani ni mwana au binti wa kipekee wa Mungu.10 Tunapochagua kuwa sehemu ya agano, inachochea na kukuza uhusiano wetu na Yeye. Rais Russell M. Nelson amefundisha kwamba tunapochagua kufanya maagano na Mungu, uhusiano wetu na Yeye unaweza kuwa wa karibu zaidi kuliko ilivyokuwa kabla ya agano letu, na inamwezesha Yeye kutubariki kwa kipimo cha ziada cha rehema na upendo Wake, upendo wa agano unaojulikana kama hesed katika lugha ya Kiebrania.11 Njia ya agano ni kuhusu uhusiano wetu na Mungu—uhusiano wetu wa hesed pamoja Naye.12

Baba yetu anataka uhusiano wa kina na wana na mabinti Zake wote,13 lakini ni chaguo letu. Tunapochagua kusonga karibu Naye kupitia uhusiano wa agano, inamruhusu Yeye asonge karibu nasi14 na kutubariki zaidi na zaidi.

Mungu anaweka masharti na ahadi za maagano tunayofanya.15 Tunapochagua kuingia kwenye uhusiano huo, tunashuhudia Kwake, kupitia matendo ya kiishara ya kila agano, kwamba tuko radhi kutii masharti aliyoyaweka.16 Kupitia kuheshimu maagano yetu, tunamruhusu Mungu kumimina wingi wa baraka zilizoahidiwa zinazohusiana na maagano hayo,17 ikijumuisha ongezeko la nguvu za kubadilika na kuwa zaidi kama Mwokozi wetu. Yesu Kristo ni kiini cha maagano yote tuyafanyayo, na baraka za maagano huwezeshwa kwa sababu ya dhabihu Yake ya kulipia dhambi.18

Ubatizo kwa kuzamishwa ni ishara ya lango ambalo kupitia kwalo tunaingia kwenye uhusiano wa agano na Mungu. Kuzamishwa na kuinuliwa tena ni ishara ya kifo na Ufufuko wa Mwokozi kwenye maisha mapya.19 Wakati sisi tunapobatizwa, sisi kwa ishara tunakufa na kuzaliwa upya kwenye familia ya Kristo na kuonesha tuko radhi kujichukulia juu yetu jina Lake.20 Sisi wenyewe tunawakilisha ishara hiyo ya agano. Katika Agano Jipya tunasoma, “Maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo.”21 Kwa ubatizo wetu tunamvaa Kristo kwa ishara.

Ibada ya sakramenti pia inatuelekeza kwa Mwokozi. Mkate na maji ni ishara ya mwili na damu ya Kristo iliyomwagwa kwa ajili yetu.22 Zawadi ya Upatanisho Wake hutolewa kwetu kwa ishara kila wiki wakati mwenye ukuhani, akimwakilisha Mwokozi Mwenyewe, anapotupatia mkate na maji. Tunapofanya tendo la kula na kunywa nembo za mwili na damu Yake, Kristo kwa ishara anakuwa sehemu yetu.23 Tunamvaa tena Kristo pale tunapofanya upya agano kila wiki.24

Tunapofanya maagano na Mungu ndani ya nyumba ya Bwana, tunaongeza kina cha uhusiano wetu na Yeye.25 Kila kitu tunachokifanya ndani ya hekalu kinatuelekeza kwenye mpango wa Baba yetu kwa ajili yetu, ambao kiini chake ni Mwokozi na dhabihu Yake ya kulipia dhambi.26 Bwana atatufundisha mstari juu ya mstari27 kupitia ishara za ibada na maagano pale tunapoifungua mioyo yetu na kwa sala kutafuta kuelewa maana kuu.

Kama sehemu ya endaumenti ya hekaluni, sisi tunaidhinishwa kuvaa gamenti ya ukuhani mtakatifu. Ni ahadi takatifu na fursa takatifu.

Katika tamaduni nyingi za kidini, mavazi maalumu ya nje huvaliwa kama ishara ya imani ya mtu na msimamo kwa Mungu,28 na mavazi ya ibada mara nyingi huvaliwa na wale wanaoongoza shughuli za ibada. Mavazi hayo matakatifu yanabeba maana kuu kwa wale wanaoyavaa. Tunasoma katika maandiko kwamba nyakati za kale, mavazi matakatifu ya ibada yalivaliwa pia sambamba na sherehe za hekaluni.29

Kama waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku Za Mwisho, wale kati yetu tuliochagua kufanya maagano na Mungu ndani ya nyumba ya Bwana tunavaa nguo za nje za ibada wakati wa ibada ya hekaluni, ishara ya mavazi yaliyovaliwa katika ibada za hekaluni za hapo kale. Tunavaa pia gamenti ya ukuhani mtakatifu, wakati wa kuabudu na kwenye maisha yetu ya kila siku.30

Gamenti ya ukuhani mtakatifu ni ishara kuu na pia inaelekeza kwa Mwokozi. Adamu na Hawa walipokula tunda na ikabidi waondoke kutoka Bustani ya Edeni, walipewa mavazi ya ngozi kwa ajili ya kujisitiri.31 Yawezekana kwamba mnyama alitolewa dhabihu ili kutengeneza mavazi hayo ya ngozi—ishara ya dhabihu ya Mwokozi kwa ajili yetu. Kaphar ni neno la msingi la Kiebrania la dhabihu, na moja ya maana yake ni “kufunika.”32 Gamenti yetu ya hekaluni hutukumbusha kwamba Mwokozi na baraka za Upatanisho Wake hutufunika maisha yetu yote. Tunapovaa gamenti ya ukuhani mtakatifu kila siku, ishara hiyo ya kupendeza inakuwa sehemu yetu.

Katika Agano Jipya kitabu cha Warumi, tunasoma: “Usiku umeendelea sana, mchana umekaribia: basi na tuyavue matendo ya giza, na kuzivaa silaha za nuru. … Mvaeni Bwana Yesu Kristo.”33

Nina shukrani kubwa kwa fursa ya kuvaa gamenti ya ukuhani mtakatifu ili kunikumbusha kwamba Mwokozi na baraka za Dhabihu Yake isiyo na mwisho daima hunifunika katika maisha yangu yote ya duniani. Pia inanikumbusha kwamba kadiri ninavyotii maagano niliyoyafanya na Mungu ndani ya nyumba ya Bwana, kiishara ninamvaa Kristo, ambaye Yeye mwenyewe ni nguzo ya nuru. Yeye atanilinda kutokana na maovu,34 atanipa nguvu na ongezeko la uwezo,35 na kuwa nuru na mwongozo wangu36 kupita giza na magumu ya ulimwengu huu.

Kuna maana ya kina na kiishara nzuri sana katika garmenti ya ukuhani mtakatifu na uhusiano wake na Kristo. Ninaamini kwamba utayari wangu37 wa kuvaa gamenti takatifu unakuwa ishara yangu Kwake.38 Hii ni ishara yetu binafsi kwa Mungu na si ishara kwa wengine.39

Ninashukuru sana kwa ajili ya Mwokozi wangu, Yesu Kristo.40 Dhabihu Yake ya kulipia dhambi kwa ajili yetu ilikuwa ishara kuu zaidi ya upendo Wake usio na mwisho na wa Baba yetu wa Mbinguni kwa kila mmoja wetu,41 ukiwa na ishara ya kushikika ya upendo na dhabihu hiyo—alama kwenye mikono, miguu na ubavu wa Mwokozi—zikibakia hata baada ya ufufuko Wake.42

Kadiri ninavyoshika maagano na majukumu yangu kwa Mungu, ikijumuisha kuvaa gamenti ya ukuhani mtakatifu, maisha yangu yanaweza kuwa ishara binafsi ya upendo wangu na shukrani kuu kwa Mwokozi wangu, Yesu Kristo, na tamanio langu la kuwa Naye daima.

Ikiwa bado hujafanya hivyo, ninakualika uchague uhusiano wa kina na Mungu kwa kufanya Naye maagano ndani ya nyumba ya Bwana. Soma hotuba za nabii wetu (ikijumuisha mafundisho mazuri yaliyopo kwenye tanbihi za hotuba yake, ambazo hotuba nyingi za mkutano mkuu zinazo). Amesema akirudia rudia kuhusu maagano kwa miaka mingi na hasa tangu alipokuwa Rais wa Kanisa. Jifunze kutoka kwenye mafundisho kuhusu baraka nzuri na ongezeko la nguvu na uwezo ambao unaweza kuwa wako, kupitia kufanya na kushika maagano na Mungu.43

Kitabu cha Maelezo ya Jumla kinasema kwamba huitajiki kuwa na wito wa misheni au kuchumbiwa kwa ajili ya ndoa ndipo ufanye maagano.44 Mtu lazima awe na angalau miaka 18, na awe amemaliza shule ya sekondari au ya upili, na awe muumini wa Kanisa kwa angalau mwaka mmoja. Pia kuna viwango vya utakatifu binafsi vinavyohitajika.45 Ikiwa una tamanio la kukuza kwa kina uhusiano wako na Baba yako aliye Mbinguni na Yesu Kristo kwa kufanya maagano matakatifu katika nyumba ya Bwana, ninakualika uzungumze na askofu wako au rais wa tawi na umjulishe tamanio lako. Yeye atakusaidia ujue jinsi kujiandaa kupokea na kuheshimu maagano hayo.

Kupitia uhusiano wa agano na Mungu, maisha yetu wenyewe yanaweza kuwa ishara hai ya msimamo wetu na upendo wa kina kwa Baba yetu wa Mbinguni, hesed yetu kwa ajili Yake,46 na tamanio letu la kupiga hatua na hatimaye tuwe kama Mwokozi wetu, tukitayarishwa siku moja kuingia kwenye uwepo Wao. Ninashuhudia kwamba baraka kuu za uhusiano huo wa agano ni za thamani kuliko chochote. Katika jina la Yesu Kristo, amina.