Mkutano Mkuu
Kutawazwa Kutumikia kabla ya Maisha Haya
Mkutano mkuu wa Aprili 2024


Kutawazwa Kutumikia kabla ya Maisha Haya

Baba yetu wa Mbinguni anatamani kufunua kwako utawazo wako wa kabla ya maisha haya, na atafanya hivyo kadiri unavyotafuta kujifunza na kufuata mapenzi Yake.

Jioni hii, ninazungumza na vijana wa Kanisa, kizazi chipukizi cha wavulana na wasichana ambao ndio wabeba bendera kwa ajili ya kizazi kijacho.

Mnamo Oktoba 2013, nabii wetu mpendwa, Rais Russell M. Nelson alitangaza: “Baba yako wa Mbinguni amekujua wewe kwa muda mrefu sana. Wewe, kama mwana au binti Yake, ulichaguliwa na Yeye kuja duniani katika muda huu mahususi, kuwa kiongozi katika kazi Yake kuu duniani.”1

Miaka miwili iliyopita, Rais Nelson aliendelea:

“Leo, ninahakikisha kwa dhati kwamba Bwana ameamuru kila mvulana anayestahili, na mwenye uwezo ajiandae kwa ajili ya na kutumikia misioni. Kwa wavulana Watakatifu wa Siku za Mwisho, huduma ya kimisionari ni jukumu la kikuhani. Ninyi wavulana mmeletwa katika muda huu wakati kusanyiko lililoahidiwa la Israeli linafanyika. …

“Kwenu ninyi akina dada wenye uwezo, misioni pia ni kitu chenye nguvu, lakini ni fursa isiyo ya lazima, kwenu. … Sali kujua kama Bwana angetaka utumikie misioni, na Roho Mtakatifu atakujibu katika moyo wako na akilini mwako.”2

Marejeo ya nabii wetu kuhusu Bwana kuwatunza vijana kwa ajili ya siku yetu katika kuikusanya Israeli na mwaliko wake wa kusali ili kujua Bwana angependa ufanye nini, kwa sehemu, hurejelea maisha uliyoishi na baraka ulizozipokea kutoka kwa Mungu kabla hujazaliwa hapa duniani.3 Sote tuliozaliwa kwenye dunia hii kwanza tuliishi na Baba yetu wa Mbinguni kama watoto Wake wa kiroho.4 Bwana alitangaza kwa Musa, “Kwa maana Mimi, Bwana Mungu, niliviumba vitu vyote … kiroho, kabla ya kuwekwa kikawaida juu ya uso wa dunia.”5

Alipowaumba kiroho, Aliwapenda kama wana na binti Zake na kuweka ndani ya kila mmoja wenu asili takatifu na kudra ya milele.6

Wakati wa maisha yako kabla ya duniani, “ulikuza utambulisho wako na kuongeza uwezo wako wa kiroho.”7 Mlibarikiwa kwa kipawa cha haki ya kujiamulia, uwezo wa kufanya chaguzi kwa ajili yenu binafsi, na mlifanya maamuzi muhimu, kama vile uamuzi wa kufuata mpango wa furaha wa Baba wa Mbinguni, ambao ni “kupokea mwili na kupata uzoefu wa duniani ili kukua … na hatimaye kutambua kudra [zenu] takatifu kama warithi wa uzima wa milele.”8 Uamuzi huu uliathiri maisha yenu kipindi hicho, cha maisha kabla ya kuja duniani, na huendelea kuathiri maisha yenu sasa.9 Kama mtoto wa Mungu uliyeishi kabla ya kuja duniani, “uliongezeka kiakili na ulijifunza kupenda ukweli.”10

Kabla ya kuzaliwa, Mungu alimchagua kila mmoja wenu kutimiza jukumu maalum katika maisha yenu ya hapa duniani.11 Kama ukibakia mwenye kustahili, baraka za agizo hilo la kabla ya kuja duniani zitakusaidia uwe na fursa za aina zote katika maisha haya, ikijumuisha fursa ya kutumikia Kanisani na kushiriki katika kazi muhimu sana inayofanyika duniani leo: kuikusanya Israeli.12 Ahadi na baraka hizo za kabla ya kuja duniani zinaitwa utawazo kabla ya maisha haya. “Mafundisho ya utawazo kabla ya maisha haya hutumika kwa waumini wote wa Kanisa.”13 Utawazo kabla ya maisha haya hakutoi hakikisho kuwa utapokea wito au wajibu fulani. Baraka hizi na fursa huja katika maisha haya kama matokeo ya matumizi yako ya haki ya kujiamulia kwa uadilifu, kama vile kutawazwa kwako kabla kulivyokuwa katika maisha kabla ya kuja duniani kama matokeo ya uadilifu.14 Utakapothibitisha kwamba unastahili na kusonga kwenye njia ya agano, utapokea fursa za kutumikia katika darasa lako la wasichana au akidi ya ukuhani. Utabarikiwa kutumikia katika hekalu, kuwa kaka au dada mhudumiaji na kutumikia misioni kama mwanafunzi wa Yesu Kristo.

Kwa nini ni muhimu kutafuta kujua na kuelewa utawazo wako wa kabla ya kuja duniani? Katika siku ambayo maswali huongezeka, wakati ambapo wengi hutafuta kujua utambulisho wao halisi, ukweli kwamba Mungu humjua na amembariki kila mmoja wetu binafsi kabla ya kuzaliwa kwenye dunia hii tukiwa na “tabia za msingi za … maisha kabla ya kuja duniani, maisha ya duniani, na utambulisho na lengo la milele” huleta amani na hakikisho akilini na mioyoni mwetu.15 Kujua wewe ni nani huanza na kuelewa baraka za utawazo wako zilizowekwa juu yako kabla ya kuzaliwa kwenye dunia hii. Baba yetu wa Mbinguni anatamani kufunua kwako utawazo wako wa kabla, na atafanya hivyo kadiri unavyotafuta kujifunza na kufuata mapenzi Yake.16

Ninapenda kusoma jumbe fupi za Rais Nelson za Instagram. Moja ya nilizozipenda ulikuwa wa Julai 20, 2022. Aliandika:

“Ninaamini kwamba kama Bwana angekuwa anazungumza na wewe moja kwa moja, kitu cha kwanza ambacho angehakikisha unakielewa ni utambulisho wako halisi. Marafiki zangu wapendwa, nyinyi kiuhalisia ni watoto wa kiroho wa Mungu. …

“… Usifanye makosa kuhusu hilo: Uwezekano wako ni wa kiungu. Kwa utafutaji wako kwa bidii, Mungu atakupatia taswira ndogo ndogo ya kile unachoweza kuwa.”17

Je, naweza kushiriki pamoja nanyi jinsi baba yangu wa duniani alivyonifundisha kugundua utambulisho wangu na mpango wa Mungu katika maisha yangu?

Jumamosi moja asubuhi nikiwa na miaka 13, nilikuwa nikifyeka nyasi kama sehemu ya majukumu yangu ya wiki. Nilipomaliza, nilisikia milango ikifunga nyuma ya nyumba yetu na niliona baba yangu akiniita niungane naye. Nilizunguka nyuma ya veranda ya nyuma, na alinialika nikae pamoja naye kwenye ngazi. Ilikuwa ni asubuhi nzuri. Bado nakumbuka akiwa ameketi karibu sana na mimi hadi mabega yetu yaligusana. Alianza kwa kuniambia kwamba ananipenda. Aliniuliza malengo yangu ni yapi katika maisha. Niliwaza, “hilo ni jambo rahisi.” Nilijua mambo mawili kwa uhakika: nilitaka kuwa mrefu na nilitaka kwenda kupiga kambi mara kwa mara. Nilikuwa nafsi ya kawaida tu. Alitabasamu, akatulia kwa muda, na kusema: “Steve, ningependa kushiriki kitu pamoja nawe ambacho ni muhimu sana kwangu. Nimeomba kwamba Baba yetu wa Mbinguni atasababisha kile ninachokisema sasa kisifutike akilini mwako na kwenye nafsi yako ili kwamba usikisahau daima.”

Baba yangu alivuta umakini wangu wote aliposema hivyo. Aligeuka na kuniangalia machoni na kusema, “Mwanangu, linda nyakati za faragha za maisha yako.” Kulikuwa na kimya kirefu akiruhusu maana kuzama ndani zaidi ya moyo wangu.

Kisha aliendelea: “Unajua, zile nyakati ambazo upo peke yako na hakuna mwingine anayejua unachokifanya? Zile nyakati unapodhani, ‘kila ninachokifanya sasa hakimuathiri mwingine yeyote, ila mimi tu’?”

Kisha akasema, “Zaidi ya wakati mwingine wowote katika maisha yako, kile unachofanya katika nyakati zako za faragha za maisha kitakuwa na matokeo makubwa ya jinsi unavyokabiliana na changamoto na maumivu utakayoyapitia; na kile unachofanya katika nyakati za faragha za maisha yako kitakuwa na matokeo makubwa ya jinsi unavyokabiliana na mafanikio na shangwe utakayoipata kuliko wakati wowote katika maisha yako.”

Baba yangu alipata tamanio la moyo wake. Mlio na toni ya sauti yake, na upendo niliouhisi katika maneno yake, yalibakia katika akili yangu na nafsi yangu siku hiyo.

Kwa miaka mingi nimejifunza kwamba muujiza mkuu wa siku hiyo katika ngazi za nyumba ya utoto wangu ulikuwa ni kwamba, katika nyakati za faragha za maisha yangu, ningeweza kwenda kwa Mungu katika sala ili kupokea ufunuo. Baba yangu alikuwa ananifundisha jinsi ambavyo ningejifunza baraka za mungu za utawazo wa kabla ya maisha haya. Katika nyakati hizo za faragha, nilijifunza kwamba Kitabu cha Mormoni ni neno la Mungu. Nilijifunza kwamba Mungu alikuwa amenitawaza kabla ili kutumikia misioni. Nilijifunza kwamba Mungu ananijua na anasikia na kujibu sala zangu. Nilijifunza kwamba Yesu ni Kristo, Mwokozi na Mkombozi wetu.

Ingawa tangu siku hiyo ya kukumbukwa nikiwa na baba yangu nimefanya makosa mengi, kujitahidi kulinda nyakati zangu za faragha za maisha kumebakia kuwa nanga katikati ya dhoruba za maisha na kunisaidia nitafute kimbilio salama na uponyaji, baraka za kuimarisha za upendo wa Mwokozi wetu na dhabihu ya upatanisho.

Akina kaka na dada zangu wadogo, mnapolinda nyakati zenu za faragha za maisha kwa burudani nzuri; kusikiliza muziki wa kuinua; kusoma maandiko; kuwa na sala za mara kwa mara, zenye maana, na kufanya jitihada kupokea na kutafakari baraka yako ya kipatriaki, utapokea ufunuo. Katika maneno ya Rais Nelson, macho yako “yatafunuliwa kwa upana kwenye ukweli kwamba maisha haya ni muda ambapo unaamua ni aina gani ya maisha wewe unataka kuishi milele.”18

Baba yetu wa Mbinguni atajibu sala zako, hasa sala zako zitolewazo wakati wa nyakati za faragha za maisha yako. Atafunua kwako vipaji na talanta zako ulizotawazwa nazo kabla ya maish ahaya, na utahisi upendo Wake ukikuzunguka, kama kwa dhati utauliza na kwa dhati kutaka kujua. Unapolinda nyakati za faragha za maisha yako, ushiriki wako katika ibada na maagano ya injili vitakuwa vya maana sana. Utajiunganisha na Mungu kikamilifu zaidi katika maagano uyafanyayo pamoja Naye, na utainuliwa uwe na tumaini kubwa, imani kubwa na uthibitisho katika ahadi Alizozifanya kwako. Je, unataka mpango wa Mungu kwako? Ninatoa ushahidi kwamba Yeye anataka ujue, na aliwapa msukumo wa kiungu manabii Wake ulimwenguni kumwalika kila mtu kusali na kupokea uzoefu huu wa kufumbua macho kwa ajili yetu wenyewe.19 Ninatoa ushahidi wa uhalisia na nguvu ya dhabibu ya upatanisho ya Mwokozi wetu ambayo inafanya iwezekane kuishi kuzifikia na kuzifurahia baraka zote za Mungu za utawazo wa kabla ya maisha haya, katika jina la Yesu Kristo, amina.