Mkutano Mkuu
Uadilifu: Sifa Kama ya Kristo
Mkutano mkuu wa Aprili 2024


Uadilifu: Sifa Kama ya Kristo

Kuishi maisha ya uadilifu kunahitaji sisi kuwa wakweli kwa Mungu, kwa kila mmoja wetu na kwenye utambulisho wetu wa kiungu.

Katika masaa ya mwisho ya huduma ya Mwokozi, alienda kwenye Mlima wa Mizeituni kwenye bustani iliyoitwa Gethsemane na aliwaalika wanafunzi Wake kusubiri.1 Akiwa peke yake, Alimwomba Baba Yake, “Ikiwa ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki.”2 Akiwa katika maumivu makali, mateso Yake yalimfanya Yeye, “hata Mungu, mkuu kuliko wote, kutetemeka kwa sababu ya maumivu, na kutoka damu kwenye kila kinyweleo, … na kutamani nisinywe kikombe kichungu, na kusita.”3 Hata hivyo katika wakati huu wa kukata tamaa, Mwokozi hakusita “lakini akachukua na kukamilisha maandalizi [Yake] kwa watoto wa wanadamu.”4

Kama Mzaliwa wa Pekee wa Baba, Yesu Kristo alikuwa na uwezo juu ya kifo, maumivu na mateso lakini hakusita. Alitimiza agano alilofanya na Baba Yake na, kwa kufanya hivyo, alionyesha sifa ya Kristo inayozidi kuwa muhimu katika ulimwengu ambamo tunaishi—sifa ya uadilifu. Alibakia kuwa mkweli kwa Mungu, kwa kila mmoja wetu na kwenye utambulisho wake wa kiungu.

Uadilifu

Yesu Kristo ni Mfano wetu. Kuishi maisha ya uadilifu kunahitaji sisi kuwa wakweli kwa Mungu, kwa kila mmoja wetu na kwenye utambulisho wetu wa kiungu. Uadilifu hutiririka kutoka kwenye amri kuu ya kwanza ya kumpenda Mungu. Kwa sababu unampenda Mungu, wewe ni mkweli Kwake nyakati zote. Unaelewa kuna jema na baya na kwamba kuna ukweli kamili—ukweli wa Mungu. Uadilifu humaanisha hatushushi viwango vyetu au tabia ili kuwapendeza watu au kukubalika kwa wengine.5 “Unatenda mema” na “matokeo badaye.”6 Marekebisho ya hivi karibuni kwenye Hubiri Injili Yangu mwongozo wa umisionari imeongeza uadilifu kama sifa ya Kristo.7

Miaka kadhaa iliyopita, Mzee Uchtdorf alipewa jukumu la kuanzisha kigingi chetu. Wakati wa mahojiano yetu, aliniuliza swali ambalo sijalisahau: “Je, kuna kitu chochote katika maisha yako ambacho, kama kikiletwa kwa umma, kitakuwa aibu kwako au kwa Kanisa?” Nikiwa na mshangao, akili yangu ilikimbia haraka juu ya maisha yangu yote, nikijaribu kukumbuka nyakati ambazo nilikuwa nimekosea na kujiuliza, “kama wengine wangejua kila kitu nilichokuwa nimefanya, wangefikiria nini kuhusu mimi au Kanisa?”

Kwa wakati huo, nilifikiri Mzee Uchtdorf alikuwa akiuliza tu juu ya ustahiki, lakini nimekuja kuelewa lilikuwa ni swali kuhusu uadilifu. Je, nilikuwa mkweli kwa kile nilichokishuhudia? Je, ulimwengu ungeweza kuona uwiano kati ya maneno na matendo yangu? Je, wengine wangemwona Mungu kwa njia ya mwenendo wangu?

Rais Spencer W. Kimbal alifundisha, “Uadilifu” ni “utayari na uwezo wetu wa kuishi kwa imani na ahadi zetu.”8

Wakweli kwa Mungu

Maisha ya uadilifu yanatutaka sisi kwanza na zaidi ya yote kuwa wakweli kwa Mungu.

Kutokea utotoni mwetu, tulijifunza hadithi ya Danieli katika pango la simba. Danieli wakati wote alikuwa mkweli kwa Mungu. Wenzake wenye wivu “walitafuta fursa dhidi yake”9 na wakaweka amri ya watu kusali kwa miungu yao pekee. Danieli alijua amri hiyo lakini akaenda nyumbani—na “madirisha yake yakiwa wazi”10—alipiga magoti na kuomba mara tatu kwa siku kwa Mungu wa Israeli. Matokeo yake, Daniel alitupwa kwenye pango la simba. Asubuhi yake, mfalme aligundua Mungu wa Danieli alikuwa amemwokoa na akatoa amri mpya kwamba wote wanapaswa “kutetemeka na kuogopa mbele ya Mungu wa Danieli: kwa maana yeye ndiye Mungu aliye hai.”11

Mfalme alikuja kumjua Mungu kupitia uadilifu wa Danieli. Wengine humwona Mungu kupitia—maneno na matendo yetu. Kama Danieli, kuwa mkweli kwa Mungu kutazidi kutuweka sisi mbali na ulimwengu.

Mwokozi anatukumbusha, “Ulimwenguni mnayo dhiki: lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu.”12 Rais Russell M. Nelson alishauri “[Kuushinda ulimwengu] inamaanisha kushinda vishawishi vya kujali zaidi kuhusu mambo ya ulimwengu kuliko mambo ya Mungu. Inamaanisha kutumaini mafundisho ya Kristo zaidi kuliko falsafa za wanadamu.”13 Vivyo hivyo, lazima tuepuke jaribu la kutembea “kwenye njia [yetu] wenyewe, na kwa mfano wa mungu wetu wenyewe, ambaye ni mfano wa kitu cha duniani.”14

Msukumo kinzani wa ulimwengu huu ni sehemu muhimu ya mpango wa Mungu wa wokovu. Jinsi tunavyojibu kwenye msukumo huo ndicho kiini cha sisi ni nani—kipimo cha uadilifu wetu. Msukumo wa kidunia unaweza kuwa wa moja kwa moja kama kuharibu uaminifu katika ndoa au kama hila ya kuposti kwa kuficha utambulisho, maoni ya kukosoa mafundisho au desturi ya Kanisa. Kuwa na uadilifu katika chaguzi zetu ni kudhihirisha msimamo wa ndani wa kumfuata Mwokozi Yesu Kristo.

Wakweli kwa Wengine

Kama vile uadilifu unavyotiririka kutoka kwenye amri kuu ya kwanza ya kumpenda Mungu, kuwa mkweli kwa kila mtu hutiririka kutoka kwenye ya pili, kuwapenda majirani zetu kama sisi wenyewe. Maisha ya uadilifu sio maisha ya ukamilifu; ni maisha ambayo tunajitahidi kila siku kuwa wakweli kwa Mungu na ndani ya muktadha huo kuwa wakweli kwa wengine. Rais Oaks anatukumbusha, “Lakini ari yetu ya kutii amri hii ya pili lazima isitusababishe kusahau ya kwanza.”15

Dunia inazidi kupambana na uadilifu kwa kuweka kanuni za maadili au sheria za maadili zinazosimamia uhusiano kati ya watu na taasisi. Japo ni nzuri, sheria hizi kwa ujumla hazijikiti katika ukweli kamili na huwa zinabadilika kulingana na matakwa ya jamii. Sawa na swali lililoulizwa na Mzee Uchtdorf, baadhi ya mashirika yanawafundisha wafanyakazi kuzingatia maamuzi yao au mchakato wa kufanya maamuzi utaonekanaje kama yatachapishwa mtandaoni au kwenye ukurasa wa mbele wa gazeti maarufu. Kanisa linapotoka kusikojulikana na kutoka gizani,16 sisi, kama Danieli, lazima tuinuke juu ya matarajio ya kidunia na kuwa uso wa Mungu wa kweli na aliye hai wakati wote na katika sehemu zote.17

Kusema tuna uadilifu haitoshi ikiwa matendo yetu hayaendani na maneno yetu. Vivyo hivyo, wema wa Kikristo sio mbadala wa uadilifu. Kama watu wa agano, na kama viongozi katika Kanisa Lake, lazima tuepuke lawama na tuambatane na viwango ambavyo Bwana ameviweka.

Kutenda kwa uadilifu hujenga imani na tumaini na kuwahakikishia wengine kwamba tunatafuta kufanya mapenzi ya Bwana pekee. Katika mabaraza yetu, tunapinga ushawishi wa nje na kufuata mchakato wa Bwana uliofunuliwa, kutafuta ufahamu kutoka kwa kila mwanamke na mwanamume na kutenda kulingana na ushauri wa kiungu uliopokelewa.18

Fokasi yetu ni kwa Mwokozi, na tuko makini kuepuka vitendo ambavyo vinaweza kuonekana kama kutumikia maslahi yetu wenyewe, kunufaisha familia yetu au kumpendelea mtu kwa gharama ya mwingine. Tunajiweka pembeni ili kuepuka mtazamo wowote kwamba matendo yetu yanaweza kushawishiwa na heshima za wanadamu,19 kupokea sifa binafsi, kutafuta kupendwa zaidi, kunukuliwa au kuchapishwa.

Wakweli kwenye Utambulisho Wetu wa Kiungu

Hatimaye, maisha ya uadilifu yanatutaka sisi kuwa wakweli kwenye utambulisho wetu wa kiungu.

Tunajua baadhi ya watu ambao hawakuwa. Ninayemlenga hasa hapa ni mpinga-Kristo Korihori, ambaye aliipotosha mioyo ya wengi, akivutia “tamaa zao za kimwili.”20 Hata hivyo, katika nyakati za mwisho za maisha yake, alikiri, “Siku zote nilijua kwamba kuna Mungu.”21 Rais Henry B. Eyring alifundisha kwamba kudanganya “ni kinyume na asili ya roho zetu,”22 utambulisho wetu wa kiungu. Korihori alijidanganya mwenyewe, na kweli haikuwa ndani yake.23

Kwa upande mwingine, Nabii Joseph Smith kwa ujasiri alitangaza, “Nilijua hivyo, nami nilijua kwamba Mungu alijua, na sikuweza kukataa.”24

Hyrum kaka wa Joseph alipendwa na Bwana “kwa sababu ya uadilifu wa moyo wake.”25 Yeye na Joseph walibaki wakweli hadi mwisho—wakweli kwenye asili yao ya kiungu, nuru na maarifa waliyopokea, na wakweli kwa mtu waliyejua wanaweza kuwa.

Hitimisho

Na tujipatanishe wenyewe “kwa mapenzi ya Mungu”26 na tuendeleze sifa ya Kristo ya uadilifu. Na tumfuate Mfano wetu, Mwokozi wa ulimwengu, na si kusita bali tuishi maisha ambayo ni ya kweli kwa Mungu, kwa kila mmoja wetu na kwenye utambulisho wetu wa kiungu.

Kama Ayubu alivyosema, “Na nipimwe katika mizani iliyo sawa sawa, ili Mungu aujue uelekevu wangu.”27 Katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.