Mkutano Mkuu
Yote Yatakuwa Sawa Kwa Sababu ya Maagano ya Hekaluni
Mkutano mkuu wa Aprili 2024


Yote Yatakuwa Sawa Kwa Sababu ya Maagano ya Hekaluni

Hakuna chochote kilicho muhimu kuliko kuyaheshimu maagano uliyofanya au utakayoyafanya hekaluni.

Wapendwa kaka zangu na dada zangu, kikao hiki cha mkutano mkuu kimekuwa, kwangu mimi, wakati mtakatifu. Ninashukuru kwa ajili ya jukumu la kuzungumza na mamilioni ya Watakatifu wa Siku za mwisho na marafiki zetu kote ulimwenguni. Ninawapenda, na ninajua Bwana anawapenda.

Zaidi ya miaka 50 iliyopita, nilikuwa na fursa ya kutumikia kama rais wa Chuo cha Ricks huko Rexburg, Idaho. Asubuhi ya Juni 5, 1976, mimi pamoja mke wangu, Kathy, tulisafiri kwa gari kutoka Rexburg hadi Hekalu la Idaho Falls huko Idaho kuhudhuria kuunganishwa kwa rafiki wa karibu. Bila shaka, kukiwa na wavulana wanne wadogo katika nyumba yetu wakati huo, safari yetu ya hekaluni ingeweza tu kutimizwa kwa msaada wa mlezi shupavu! Tuliwaacha watoto wetu wa thamani katika uangalizi wake na tukafanya safari ya dakika 30.

Uzoefu wetu hekaluni siku ile ulikuwa wa kupendeza, kama ambavyo daima umekuwa. Hata hivyo, baada ya hitimisho la uunganishaji hekaluni—na tulipokuwa tunajiandaa kurudi nyumbani—tuliwaona wafanyakazi wengi wa hekalu na wageni wakizungumza kwa wasiwasi katika ushoroba wa hekalu. Ndani ya dakika chache, mmoja wa wafanyakazi wa hekaluni alituambia kwamba Bwawa la Teton lililokuwa limejengwa karibuni huko mashariki ya Idaho lilikuwa limebomoka! Zaidi ya galoni bilioni 80 (mita za ujazo milioni 300) za maji zilikuwa zinatiririka kutoka kwenye bwawa hadi kwenye maili 300 za mraba (kilomita 775 za mraba) za mabonde ya jirani. Sehemu kubwa ya mji wa Rexburg ilikuwa imefunikwa na maji, na nyumba na magari kusombwa na mafuriko. Theluthi mbili za wakazi 9,000 ghafla walikuwa bila makazi.1

Kama vile unavyoweza kufikiria, mawazo yetu na wasiwasi uligeukia kwenye usalama wa watoto wetu wapendwa, mamia ya wanafunzi wa chuo na kitivo, na jamii tuliyoipenda. Tulikuwa umbali usiozidi maili 30 (kilomita 50) kutoka nyumbani, na bado katika siku hii, kitambo sana kabla ya simu na jumbe za arafa, hatukuwa na njia ya kuwasiliana na watoto wetu kwa haraka, wala hatungeweza kuendesha gari kutoka Idaho Falls hadi Rexburg, kwa vile barabara zote zilikuwa zimefungwa.

Njia pekee tuliyobakiwa nayo ilikuwa ni kulala usiku huo katika hoteli huko Idaho Falls. Mimi pamoja na Kathy tulipiga magoti katika chumba cha hoteli na kwa unyenyekevu kumsihi Baba wa Mbinguni kwa ajili ya usalama wa watoto wetu wapendwa na maelfu ya wengine walioathiriwa na hili janga. Ninakumbuka Kathy akitembea tembea kwenye ghorofa hadi saa za mapema asubuhi, akiwa na wasiwasi kuwahusu watoto wake. Licha ya wasiwasi wangu mwenyewe, niliweza kutuliza akili na kupata usingizi.

Haikuwa muda mrefu baadaye mwenza wangu kipenzi aliponiamsha na kusema, “Hal, unawezaje kulala wakati kama huu?”

Maneno haya kisha yalikuja dhahiri moyoni mwangu na akilini. Nilimwambia mke wangu: “Kathy, vyovyote itakavyokuwa, yote yatakuwa sawa kwa sababu ya hekalu. Tumefanya maagano na Mungu na kuunganishwa kama familia ya milele.”

Wakati ule, ilikuwa ni kama Roho wa Bwana akithibitisha katika mioyo yetu na akili zetu kile ambacho sote tayari tulikuwa tunajua ni cha kweli: ibada za kuunganishwa, zinazopatikana katika nyumba ya Bwana pekee na kufanywa kwa mamlaka ya ukuhani sahihi, zilikuwa zimetuunganisha sisi pamoja kama mume na mke, na watoto wetu walikuwa wameunganishwa nasi. Hakika hakukuwa na haja ya kuhofu, na tulikuwa na shukrani baadaye kujua kwamba wavulana wetu walikuwa salama.

Pengine kauli hii kutoka kwa Rais Thomas S. Monson inaelezea vyema kile mimi na Kathy tulichohisi katika usiku huo usiosahaulika. “Tunapohudhuria hekaluni, kunaweza kuja kwetu kipimo cha kiroho na hisia za amani. … Tutaelewa maana sahihi ya maneno ya Mwokozi pale aliposema: ‘Amani ninawaachieni, amani yangu nawapeni. … Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga [Yohana 14:27].’”2

Nimebarikiwa kuhisi amani hiyo kila wakati ninapoingia ndani ya hekalu takatifu. Ninaikumbuka siku yangu ya kwanza nilipoingia katika Hekalu la Salt Lake. Nilikuwa mvulana mdogo.

Nilitazama juu kwenye dari ndefu nyeupe ambayo ilifanya chumba kuwa na nuru kana kwamba kilikuwa wazi kuelekea mawinguni. Na katika wasaa ule, wazo likanijia akilini mwangu kwa maneno haya dhahiri: “Nimewahi kuwa mahali hapa angavu kabla.” Lakini kisha ghafla yakaja akilini mwangu, sio kwa sauti yangu, maneno haya: “Hapana, hujawahi kamwe kuwa mahali hapa. Unakumbuka wakati kabla ya kuzaliwa kwako. Ulikuwa mahali patakatifu kama hapa ambapo Bwana angeweza kuja.”

Akina Kaka na akina dada, ninashuhudia kwa unyenyekevu kwamba tunapohudhuria hekaluni, tunaweza kukumbushwa asili ya milele ya roho zetu, uhusiano wetu na Baba na Mwanawe mtakatifu, na tamanio letu la kurudi nyumbani kwetu mbinguni.

Katika hotuba za hivi karibuni za mkutano mkuu, Rais Russell M. Nelson amefundisha:

“Mahali salama zaidi pa kuwa kiroho ni kuishi ndani ya maagano yako ya hekaluni!”

Kila kitu tunachokiamini na kila ahadi ambayo Mungu ameifanya kwa watu Wake wa agano hufanyika hekaluni.”3

“Kila mtu anayefanya maagano … hekaluni—na kuyashika—ameongeza ufikiaji kwenye uweza wa Yesu Kristo.”4

Pia alifundisha kwamba “mara tu tunapofanya agano na Mungu, tunaondoka kwenye kuwa vuguvugu milele. Mungu hatatupilia mbali uhusiano Wake na wale ambao wameunda mfungamano kama huo na Yeye. Kwa hakika, wale wote ambao wamefanya agano na Mungu wana njia ya kupata aina maalumu ya upendo na rehema.”5

Chini ya uongozi wenye uvuvio wa Rais Nelson, Bwana ameharakisha, na ataendelea kuharakisha, ujenzi wa mahekalu kote ulimwenguni. Hii itawapa watoto wote wa Mungu fursa ya kupokea ibada za wokovu na kuinuliwa na kufanya na kushika maagano matakatifu. Kustahili kufanya maagano matakatifu siyo juhudi ya mara moja tu bali ni mpangilio wa maisha yote. Bwana amesema itachukua moyo wetu wote, uwezo, akili, na nguvu.6

Ushiriki wa kila mara katika ibada za hekaluni unaweza kujenga mpangilio wa msimamo kwa Bwana. Unaposhika maagano yako ya hekaluni na kuyakumbuka, unaalika wenza wa Roho Mtakatifu ili kukuimarisha na kukutakasa.

Unaweza kisha kuhisi hisia ya nuru na tumaini vikishuhudia kwamba ahadi ni za kweli. Utakuja kujua kwamba kila agano na Mungu ni nafasi ya kusogea karibu na Yeye, ambayo kisha italeta tamanio katika moyo wako la kushika maagano ya hekaluni.

Tumeahidiwa, “Kwa sababu ya agano letu na Mungu, Yeye kamwe hatachoka katika juhudi Zake za kutusaidia sisi, na kamwe sisi hatuwezi kuichosha subira Yake ya rehema kwetu.”7

Ni kupitia maagano ya kuunganishwa katika hekalu kwamba tunaweza kupokea hakikisho la miunganiko ya upendo ya familia ambayo itaendelea baada ya kifo na kudumu milele. Kuheshimu maagano ya ndoa na familia yaliyofanywa katika mahekalu ya Mungu kutatupatia ulinzi kutokana na uovu wa ubinafsi na kiburi.

Utunzaji thabiti wa akina kaka na akina dada kwa ajili ya mmoja na mwingine utakuja tu kwa juhudi thabiti za kuiongoza familia yako katika njia ya Bwana. Wape watoto fursa za kusali kwa ajili ya mmoja na mwingine. Tambua upesi vyanzo vya mizozo, na tambua vitendo vya huduma isiyo na ubinafsi, hasa kutoka kwa mmoja kwenda kwa mwingine. Wakati ndugu wanapoombeana na kuhudumiana, mioyo italainishwa na kugeukiana mmoja kwa mwingine na kwa wazazi wao.

Kwa sehemu, hicho ndicho kile kilichoelezwa na Malaki alipotoa unabii juu ya kuja kwa nabii Eliya: “Atapanda katika mioyo ya watoto ahadi zilizofanywa kwa baba, na mioyo ya watoto itawageukia baba zao. Kama haingekuwa hivyo, dunia yote ingeliharibiwa kabisa wakati wa kuja kwake.”8

Majaribu, changamoto, na machungu hakika yatakuja kwetu sote. Hakuna yeyote kati yetu aliye na kinga dhidi ya “miiba katika mwili.”9 Hata hivyo, tunapohudhuria hekaluni na kukumbuka maagano yetu, tunaweza kujiandaa kupokea maelekezo binafsi kutoka kwa Bwana.

Wakati mimi na Kathy tulipooana na kuunganishwa katika Hekalu la Logan Utah, wakati huo Mzee Spencer W. Kimball alifanya uunganishaji wetu. Katika maneno machache aliyoyazungumza, alitoa ushauri huu: “Hal na Kathy, muishi ili kwamba wakati wito utakapokuja, mnaweza kuondoka kwa urahisi.”

Mwanzoni, hatukuelewa kile ushauri huo ulichomaanisha kwetu, lakini tulifanya bidii tuwezavyo kuishi maisha yetu katika njia ambayo tungeweza kujiandaa kuondoka kumtumikia Bwana wakati wito utakapokuja. Baada ya kuwa tumeoana kwa takribani miaka 10, wito usiotarajiwa ulikuja kutoka kwa Kamishina wa Elimu ya Kanisa, Neal A. Maxwell.

Ushauri wa upendo uliotolewa na Rais Kimball hekaluni wa tuweze “kuondoka kwa urahisi” ulikuwa halisi. Kathy na mimi tulipokea wito wa kuacha kile kilichokuwa kinaonekana kama fursa nzuri ya familia huko California kwenda kutumikia katika jukumu na sehemu ambayo sikujua chochote kuihusu. Hata hivyo, Familia yetu ilikuwa tayari kuondoka kwa sababu nabii, ndani ya hekalu takatifu, mahali pa ufunuo, aliona tukio la siku za usoni ambalo kwalo sisi tulikuwa tumeandaliwa.

Wapendwa kaka zangu na dada zangu, ninatoa ushahidi kwamba hakuna chochote kilicho muhimu zaidi ya kuyaheshimu maagano uliyoyafanya au unayoweza kuyafanya hekaluni. Bila kujali uko wapi kwenye njia yako ya agano, ninakuhimiza ustahili na uwe mwenye kufaa kuhudhuria hekaluni. Hudhuria mara nyingi kadiri hali zinavyoruhusu. Fanya na shika maagano matakatifu na Mungu. Ninakuhakikishia ukweli sawa na ule nilioushiriki na Kathy katikati ya usiku ule karibia miongo mitano iliyopita katika chumba cha hoteli cha Idaho Falls: “Vyovyote itakavyokuwa, yote yatakuwa sawa kwa sababu ya hekalu.”

Ninawapeni ushahidi wangu wa hakika kwamba Yesu ndiye Kristo. Yu hai na analiongoza Kanisa Lake. Mahekalu ni nyumba za Bwana. Rais Russell M. Nelson ni nabii aliye hai wa Mungu ulimwenguni. Ninampenda, na ninampenda kila mmoja wenu. Katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.