2016
Pesa za Baba wa Mbinguni
April 2016


Pesa za Baba wa Mbinguni

Mwandishi anaishi Carolina Kaskazini, Marekani.

“Shika Amri. Katika hili kuna usalama na amani” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 146).

Picha
pesos for Heavenly Father

Ana alitafuna kitafunwa chake cha mwisho cha tortilla. Kilikuwa laini na kitamu. Ana alizipenda tortilla za bibi yake. Zilikuwa sehemu bora ya kifungua kinywa.

Ana alimtazama bibi yake, Abuela, akiosha vyombo.

Ilikuwa ni kama asubuhi nyingine. Lakini kitu kimoja hakikuwa sawa.

Abuela kawaida huenda sokoni kununua chakula. Lakini sio leo. Leo hapakuwa na pesa za kununua chakula.

“Kesho tutakula nini?” Ana aliwaza.

Kisha Ana akakumbuka. Alijua mahali zilipokuwa pesa fulani! Jana usiku alimwona Abuela akiweka pesa fulani katika kitambaa kidogo cheupe.

“Abuela, ulisahau? Unazo pesa za kununua chakula.”

“Pesa zipi?” Abuela aliuliza.

Ana alikimbia kwenda kuleta pesa zile. Alichukua mfuko ule mdogo wa sarafu. Clink! Clink!

Abuela alitabasamu. “Hiyo ni zaka yetu, Ana. Hiyo ni pesa Yake.”

“Lakini tutakula nini kesho?” Ana aliuliza.

“Usijali,” Abuela alisema. “Nina imani kuwa Baba wa Mbinguni atatusaidia.”

Asubuhi iliyofuatia Abuela alimpa Ana tortilla ya mwisho. Halafu yeye akaketi chini kwenye kiti chake. Alishona maua mekundu kwenye vazi na huku akihadithia kuhusu wakati alipokuwa msichana mdogo. Hakuonekana kuwa na wasiwasi.

Kisha Ana akasikia mtu akibisha hodi. Alikimbia kwenda kufungua mlango.

“Mjomba Pedro!”

“Nilijisikia kuwa lazima niwatembelee nyinyi wawili,” Mjomba Pedro alisema. Aliweka mifuko mitatu juu ya meza. Moja ulikuwa na unga wa mahindi wa kutengeneza tortillas. Mwingine ulikuwa na nyama. Mwingine ulikuwa na mboga za majani mabichi kutoka sokoni.

“Loo, mwanangu mpendwa,” Abuela alisema. “Nataka nikutayarishie supu yangu ya kebabu bora kabisa!”

“Supu yako ni bora ulimwengu kote,” Mjomba Pedro alisema.

Ana alicheka na kupiga makofi.

Halafu akasita. Kulikuwa na kitu kimoja alichotaka kujua. “Abuela, ulijua kuwa Mjomba Pedro angelikuja leo? Hiyo ndiyo maana hukuwa na wasiwasi?”

“Hapana,” Abuela alisema. “Ninapolipa zaka, nina imani kuwa Baba wa Mbinguni atanibariki. Naye amefanya hivyo!”

Ana akamkumbatia Abuela. Alijiona yu msichana mwenye furaha zaidi katika Mexico. Yeye na Abuela walikuwa na imani katika Baba wa Mbinguni. Sasa alikuwa na hamu kubwa ya kula supu tamu ya Abuela!