2016
Nyakati za Wamisionari Wakubwa
April 2016


Nyakati za Wamisionari Wakubwa

Mojawapo ya njia bora za wamisionari wakubwa kuweza kujitengenezea kumbukumbu nzuri sana ni kupitia kuhudumu misheni kwa pamoja.

Picha
senior missionary couple

Wakati marafiki zetu walio na umri wa miaka 60 au 70 husahau kitu, mara nyingi kwa utani sisi huita kupitiwa huku wakati wa wakuu. Lakini ningependa kujadili aina tofauti ya wakati wa wakubwa—ni wakati wa kupendeza mno kiasi cha kuwa kumbukumbu yake itakuwa ya milele. Ni ule wakati ambao wanandoa wamisionari wakubwa hugundua kwamba sasa wanafanya hasa kile ambacho Bwana angependa wafanye. Wakati wa kukumbukwa kama huu wanatambua kuwa:

  • Wanayo matukio ya miaka mingi ya kusimuliana, na vipaji, ujuzi, na uelewa wa injili ambao wanaweza kutumia kuwabariki wengine.

  • Mfano wao ni baraka kwa watoto wao na watoto wa watoto wao.

  • Wanapohudumu wanaunda urafiki wa kudumu.

  • Ndoa yao inakua na kuimarika kila siku.

  • Huduma katika jina Lake ni tamu.

Nyakati Zinazokuja

Marafiki zangu wana ndoa wakubwa, nyakati kama hizi zinapaswa kutengenezwa na wengi wenu. Fikiria simulizi iliyotolewa na Mzee Jeffrey R. Holland wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili kuhusu kile ambacho wanandoa wakubwa waliokuwa wakihudumu kule Chile walichoweza kufanya. Mzazi wa mmoja wa mzee kijana alikuwa ameaga dunia. Rais wa misheni alikuwa mbali sana kiasi cha kutoweza kumfikia yule mmisionari kwa haraka.

Lakini kulikuwa na wanandoa wamisionari wazuri sana [waliokomaa] waliokuwa wakihudumu katika eneo lile, Mzee Holland anasema. Walikuja na wakaketi na yule mmisionari na kumhudumia kwa upole na kumfariji hadi wakati rais wa misheni alipoweza kumfikia yeye mwenyewe. Tulikuwa na wamisionari vijana mashuhuri sana katika misheni zetu, lakini hakuna mmisionari ambaye angeweza kumhudumia yule mzee jinsi ambavyo wanandoa wale waliweza kufanya.1

Ujuzi wao kwa wakati ule ulikuwa tu kumfariji katika wakati wa haja. Hawakuwa na wasiwasi kuhusu lugha ya kuongea zaidi ya kuongea lugha ya upendo kama wa Kristo. Hawakuwa na wasiwasi kuhusu kukosa kuwepo wakati wa siku ya kuzaliwa ya mjukuu wao au kubarikiwa kwa mtoto, hata kama shughuli hizo ni muhimu kiasi gani. Walikuwa na haja ya kuwa mahali ambapo Bwana angeweza kuwatumia ili kubariki maisha ya mmoja wa watoto Wake. Na kwa sababu walikuwa tayari, Yeye aliweza kuwapa nafasi ya kumwakilisha.

Ni Nadra Huduma Kuwa Rahisi

Ukweli ni kwamba, hakuna mmisionari mkubwa ambaye anaona urahisi kutoka nyumbani. Si Joseph Smith, Brigham Young, John Taylor, au Wilford Woodruff. Walikuwa na watoto na wajukuu pia, na walipenda familia zao kama sisi tunavyofanya. Lakini pia walimpenda Bwana na wakataka kumtumikia. Siku moja tutaweza kukutana na hawa watu maarufu ambao walisaidia katika kuanzisha kipindi hiki cha injili. Tutakapofanya hivyo, tutakuwa na furaha kwamba hatukujificha kivulini wakati tulipopaswa kuhudumu.

Wengine wanaweza kupendelea kuhudumu wakiwa wangali wanaishi nyumbani. Baada ya ugonjwa wa kiharusi kumwacha Aase Schumacher Nelson (hamna uhusiano) akiwa amezuiliwa kwenye kiti mwendo, alikuwa na hofu kuwa hamu ya maisha yake yote ya kwenda kuhudumu misheni na mumewe Don haingetimizwa. Kisha jirani akazungumza nao kuhusu misheni yake ya huduma ya Kanisa katika ghala la askofu. Wakiwa wametiwa moyo, walizungumza na msimamizi katika kituo hicho, wakajaza fomu zao za mapendekezo, na waliitwa kuhudumu siku mbili katika wiki katika ghala karibu na nyumbani kwao.

Ni rahisi kukaa tu na kufikiria, O, sihitajiki po pote, Aase Nelson anasema. Lakini sasa ninajisikia kwamba ninahitajika. Na hiyo imekuwa ushuhuda kwangu.

Kwa Hakika Unahitajika

Ikiwa umejaribiwa kufikiria kuwa hauhitajiki, wacha nikuhakikishie kuwa unahitajika. Hakuna rais wa misheni Kanisani ambaye hangependa kuwa na wanandoa wamisionari zaidi wakihudumu katika misheni yake. Wakubwa huimarisha wazee vijana na kina dada wamisionari. Wao hutoa msaada unaowezesha wengine kuhudumu vyema katika majukumu yao. Na unaweza kufikiria umuhimu wa haya kwa kiongozi ambaye amekuwa tu muumini kwa miaka michache kuwa na uwezo wa kufikia muumini wa Kanisa mwenye tajriba ya hali ya juu? Wanandoa wakubwa mara nyingi huwa ni jibu halisi kwa maombi ya maaskofu na marais wa matawi.

Tunawahimiza marais wa misheni kuwatafuta wanandoa ili kutimiza mahitaji katika misheni zao. Maaskofu wanapaswa kuwatafuta wanandoa wanaoweza kuhudumu. LDS.org inaorodhesha kurasa nyingi mno za nafasi za wanandoa wakubwa. Lakini zaidi ya hayo, wanandoa wenyewe wanapaswa kupiga magoti na kumwomba Baba wa Mbinguni ikiwa wakati ni sahihi kwao kwenda kuhudumu misheni pamoja. Kati ya sifa zote, hamu ya kuhudumu inaweza kuwa ya muhimu zaidi (ona M&M 4:3).

Huku nikisifu sana kazi ya wamisionari wakubwa, ninatambua kwamba kuna wengi ambao wangependa kuhudumu lakini hawawezi kufanya hivyo. Vizuizi vinavyotokana na umri au afya mbaya vinastahili tathmini ya kweli, vile vile mahitaji muhimu ya wanafamilia. Wakati ambapo una hamu sana lakini vizuizi vya aina hii vipo, wengine waweza kuwa mikono yako na miguu, na wewe unaweza kutoa fedha zinazohitajika.

Wanandoa wakubwa, bila kujali nyinyi ni kina nani au mahali mliopo, tafadhalini ombeni kuhusu nafasi hii ya kutengeneza nyakati nzuri za wamisionari wakubwa pamoja. Baba wa Mbinguni atakusaidia ujue unachoweza kufanya.

Muhtasari

  1. Jeffrey R. Holland katika Joseph Walker, “Elder Jeffrey Holland: LDS Church Desperately Needs More Senior Missionaries,” Deseret News, Sept. 14, 2011, 3.