2016
Usipige Risasi
April 2016


Sauti za Watakatifu wa Siku za Mwisho

Nafasi ya Pili

Jina limefichwa

Picha
police officer on a bridge

Bob na mimi tuliketi kwenye gari letu la polisi, tukisubiri ishara ya harakati barabarani. Tulikuwa tumeanza uchunguzi wetu masaa mawili yaliyopita baada ya kuliona gari ambalo lilikuwa limetajwa katika tahadhari ya redio ya polisi.

“Wizi wa uporaji unaendelea,” tahadhari ilikuwa imesema. “Wanaume wawili, wote wana silaha. Walikuwa punde tu wameonekana kwenye gari la rangi ya machungwa. Mashahidi wanasema wanaume hao ni wakatili na wako tayari kupiga risasi.

Mfululizo wa wizi wa kutumia silaha ulikuwa umefanyika katika eneo hilo, lakini licha ya juhudi zetu bora, wezi hao walikuwa wametutoroka mara kwa mara. Fikira hizi zilipotea akilini mwangu punde tu nilipoona maumbo mawili yakitoka kwenye nyumba moja kwenye barabara hii iliyojaa giza na kuingia kwenye gari la rangi ya machungwa. Walikuwa sasa wanaelekea upande wetu.

“Nikiomba kikosi cha usaidizi,” Nilisema. “Washukiwa wanaelekea kaskazini kutoka eneo tulioko.

Kikosi chetu cha usaidizi, wapelelezi wawili wenye nguo za kiraia katika gari lisilo na alama, walienda mbele ya gari lile huku Bob na mimi tukifuata. Baada ya gari zetu tatu kuingia kwenye daraja, kikosi chetu cha usaidizi kilisimama ghafla kufunga daraja mbele ya gari la rangi ya machungwa na sisi tukasimama nyuma yake, tukiwaweka kati washukiwa wetu. Haraka sana, gari lilisimama na maumbo yote mawili yakatoweka machoni petu.

“Tokeni kwenye gari na mikono yenu juu ya vichwa vyenu!” Niliamuru baada ya kutoka nje ya gari langu. Hakuna aliyejibu.

Imara na tayari kupiga risasi, niliamuru tena, “Tokeni kwenye gari na mikono yenu juu ya vichwa vyenu. Fanya sasa hivi!”

Ghafla dereva aliinuka na kugeuka upande wangu. Niliweza kuona kitu ambacho kilichochovywa kwenye nikeli kikitoa nuru ghafla mikononi mwake.

Mafunzo yangu ya kipolisi na maarifa ya kawaida yaliamuru nipige risasi ili kuokoa maisha yangu. Lakini juu ya wasiwasi ya wakati huo, nilisikia sauti. Ilikuwa tulivu lakini yenye mamlaka na nguvu: “Usipige Risasi!”

Nilitarajia kupigwa risasi wakati wowote, lakini nilisubiri mtu kutoka ndani ya gari apige risasi ya kwanza. Badala yake, dereva aliinua mikono yake, akainua juu ya kichwa chake kitu kilichoonekana kama bastola, na kushusha mikono yake kwenye mapaja yake.

“Simama tuli!” Nilisema huku nikisongea gari kwa kasi. “Usisoge!”

Kipindi hicho kilionekana kama kipindi cha televisheni—hadi nilipogundua kwamba wale magaidi sugu ndani ya gari kwa kweli walikuwa wasichana wawili waliojawa na hofu. Nilichodhania kuwa bastola ilikuwa ni kifungo cha mkanda wa kiti.

Wasichana wale, punde tulikuja kujua kwamba, walikuwa wameazima lile gari toka kwa wapenzi wao. Hawakujua walikuwa wanaume wa aina gani.

“Nilidhani umekufa, Cal!” Bob aliniambia baadaye. “Nilikuwa karibu kupiga risasi. Sijui ni kwa nini sikufanya hivyo.”

Wale wapelelezi wawili katika lile gari lililokuwa halina alama walisema maneno hayo hayo pia, ingawaje hakuna aliyesikia sauti ile isipokuwa mimi. Ninajua kuwa ni nguvu za mbinguni pekee ndizo ambazo zingeweza kuwaokoa wasichana wale kutokana na kifo na maafisa wanne wa polisi kutokana na kufanya kosa la maafa hayo. Tukio hili lilinipa ufahamu hakika kuwa Baba yetu wa Mbinguni anaweza kuingilia kati na atafanya hivyo kwa manufaa yetu.