2016
Kutambua Mambo Bandia ya Shetani.
April 2016


Kutambua Mambo Bandia ya Shetani

Mwandishi anaishi Utah, Marekani.

Tunapokabiliwa na mambo ya udanganyifu wa kiroho, Kitabu cha Mormoni kinaweza kutusaidia kuamua kilicho cha kweli na kile ambacho sicho.

Picha
woman with money

Nilikuwa nikiweka noti za dola za Kimarekani ndani ya pochi yangu nikiwa katika duka la vyakula, wakati jicho langu lilivutiwa noti moja. Nilidhani rangi ya kijani kibichi ilikuwa nyepesi kidogo kuliko zingine, kwa hivyo niliichunguza kwa karibu. Halafu nikagundua ile picha ya Rais George Washington ilionekana kuwa duni. Hata karatasi yake ilionekana kuwa mbovu. Ilikuwa bandia! Karani aliibadilisha na noti ya dola halisi kisha akampa meneja wa duka ile noti bandia.

Nimefikiri sana kuhusu ile noti ya dola bandia kutoka siku hiyo. Niliwaza ni kwa muda gani ilikuwa imetumika na ni watu wangapi ilikuwa imewapumbaza kwa miaka mingi. Kwa kweli, kama sikuwa mwangalifu, pia nami ningekuwa nimepumbazwa. Lakini kwa kuilinganisha na ile halisi na kuzingatia tofauti zake badala ya kufanana kwake, niliweza kutambua kuwa ilikuwa bandia.

Kitabu cha Mormoni kimejaa mifano ya watu wenye kubuni mambo bandia ya kiroho, ambao walifuata mbinu za Shetani za udanganyifu na kuhadaa wengine kwa manufaa yao. Kwa kuchunguza hila na mbinu zao, tunaanza kugundua makosa yao kwa njia sawa na ile ambayo jicho lenye uzoefu linaanza kugundua tofauti kati ya fedha halisi na bandia. Tunavyozidi kufundisha jicho letu kutambua tofauti, ndivyo tutakavyokuwa tumejitayarisha vyema kufichua mambo bandia leo na kupinga uongo wake.

Kufanya Upelelezi kuhusu Mambo Bandia ya Shetani

Shetani anatafuta kutupotosha kwa njia ya aina yake ya vitu bandia vya kiroho, na ikiwa hatutakuwa waangalifu, tutapumbazwa. Rais Joseph F. Smith, (1838–1918) alionya: “Shetani ni mwigaji hodari, na kadiri ukweli wa injili halisi unavyotolewa kwa wingi ambao unazidi kuongezeka ulimwenguni, vivyo hivyo naye anasambaza sarafu bandia ya mafundisho ya uongo. Jihadhari na sarafu yake bandia, haitakununulia chochote ila tu masikitiko, huzuni na kifo cha kiroho.”1

Kinga bora tuliyonayo dhidi ya kupumbazwa na mambo bandia ya Shetani ni kuzijua vizuri kadiri tuwezavyo kweli hizi za injili. Tukijua ukweli kwa kina zaidi, ndivyo itakavyokuwa rahisi kutambua tofauti wakati Shetani anapowasilisha vitu vyake bandia mbele yetu. Kwa hivyo anapofanya hivyo, tunachohitaji kuchunguza ni tofauti na wala siyo kwa yale yanayofanana nayo, kama vile nilivyofanya kwa noti zangu za dola, kwa sababu hapo ndipo uongo utafichuliwa kila mara.

Rais Ezra Taft Benson (1899–1994) alifundisha: “Kitabu cha Mormoni huwaanika wazi maadui wa Kristo. … Mungu, kwa uelewa wake wa mambo kabla hayajawa ndipo akakiunda Kitabu cha Mormoni ili tupate kuweza kuona makosa na kujua jinsi ya kupambana na elimu ya uongo, kisiasa, kidini na falsafa za fikra za wakati wetu.”2

Leo tuko vitani dhidi ya Shetani. Sisi, kama jeshi lolote, tunahitaji kujua kile ambacho adui anafanya. Kujua wakati na mahali ambapo adui atafanya mashambulizi, kwa mfano, yaweza kuwa taarifa ya thamani kubwa. Hiyo ndiyo sababu istilahi ya kutafuta habari kama hii inaitwa “kufanya upelelezi.” Kumfahamu adui yetu ni kuwa mwerevu kuliko adui yetu huyo. Kitabu cha Mormoni kinaweza kutusaidia “kufanya upelelezi” kuhusu mbinu bandia za Shetani.

Hotuba Ya Kujipendekeza Ni Bandia

Zaidi ya nusu ya wahusika katika mambo bandia katika Kitabu cha Mormoni wanatumia hotuba za kujipendekeza na haiba kutimiza malengo yao. Kwa mfano, Sheremu “alikuwa na ufahamu kamili wa lugha ya watu wale; kwa sababu hiyo, aliweza kutumia maneno mengi ya kujipendekeza, na alikuwa na uwezo mkubwa wa kuzungumza, kulingana na nguvu ya ibilisi” (Yakobo 7:4). Makuhani waovu wa mfalme Nuhu walinena “maneno ya hovyo na ya kujipendekeza” (Mosia 11:7), na hivyo basi kuwafanya watu kujiingiza katika ibada za sanamu na uovu mwingine. Korihori alipata matokeo kama hayo katika siku zake, “akipotosha mioyo ya wengi” (Alma 30:18). Amalikia na Gadiantoni wote wawili walitumia uhodari wao wa kutumia maneno ya kujipendekeza ili kujenga jeshi la wafuasi waovu (ona Alma 46:10; Helamani 2:4).

Hii siyo kwa bahati mbaya. Udanganyifu ni kina kifupi, unafiki, tupu, na umetiwa chumvi. Nefi alionya kuhusu wale “watakaofundisha kwa namna hii, mafundisho ya uwongo na yasiyofaa na ya kipumbavu, na watajifurisha mioyoni mwao, na watajitahidi kumficha Bwana ushauri wao; na matendo yao yatakuwa gizani” (2 Nefi 28:9).

Maneno ya kujipendekeza mara nyingi hutumika kulaghai; kwa kawaida huwa na azimio la chini chini au ajenda iliyofichika. Udanganyifu unahusu mtindo zaidi kuliko kiini, na inavutia ubatili na kiburi cha mwanadamu wa asili ndani yetu. Manabii wa Mungu, hata hivyo, wanatueleza ukweli rahisi lakini muhimu ambao tunahitaji kuusikia.

Kujipendekeza ni lugha ambayo Shetani huongea. Rais James E. Faust (1920–2007), Mshauri wa Pili katika Urais wa Kwanza, alielezea: “[Shetani] sauti yake mara nyingi huonekana ikiwa na busara na ujumbe wake ni rahisi sana kuuhalalisha. Ni ya kusihi, sauti ya kuvutia yenye toni nyororo. Siyo katili na wala haina mfarakano. Hakuna mtu ambaye angesikiliza sauti ya Shetani ikiwa ingesikika kama ya ukatili au dhalifu.”3

Picha
whispering

Wakati ambapo ulimwengu unatupatia dhana, falsafa, au maoni ambayo yanaonekana kutufurahisha tu katika upuuzi wetu au kiburi chetu au mbona hii inaonekana kuwa rahisi hivi kiasi cha kutoaminika, hilo linapaswa kuwa onyo kwetu mara moja. Zichukulie dhana hizo kama bandia. Zilinganishe dhidi ya ukweli unaofundishwa na manabii wa Bwana. Tafuta tofauti, siyo kufanana kwake, na dhana zilizo bandia zitakuwa dhahiri.

Nehori—Mdanganyifu Maarufu!

Nehori alitumia waziwazi mtindo wa udanganyifu wa Shetani. Wacha tumchunguze kama jambo la utafiti wa mtu mdanganyifu wa kiroho. Nehori, ambaye mafundisho yake yanaonekana kukubali dhana ya mkombozi, alikuwa maarufu na mhubiri mwenye haiba kubwa miongoni mwa Wanefi. Nehori aliweza kuwa na wafuasi wengi kwa kufundisha kwamba “wanadamu wote wataokolewa katika siku ya mwisho” na “watapokea uzima wa milele” (Alma 1:4).

Tunaweza kuona ni kwa nini ujumbe wa Nehori unaweza kuvutia sana? Alikuwa akifundisha kuhusu Mungu ambaye si mkali na ni mtulivu—Mungu ambaye, kwa vile anampenda kila mtu, atamwokoa kila mtu, liwe liwalo. Kwa hivyo endelea kufanya lolote utakalo, kwa sababu yote ni mema. Ni falsafa ya kuvutia ambayo ilikumbatiwa sana na watu wa siku za Nehori (ona Alma 1:5) kama ilivyo kwa watu wengi siku hizi. Tikiti ya bure ya kuingia mbinguni inaonekana kuwa ni kitu ambacho watu wanataka.

Kwa hivyo kulikuwa na shida gani katika ujumbe wa Nehori? Sasa ngoja tuangalie hoja kuu za mjadala wake:

  • Mungu aliumba wanadamu wote—kweli.

  • Mungu anawapenda wanadamu wote—kweli.

  • Hatupaswi kumwogopa Mungu—kweli.

  • Tunapaswa kushangilia dhana ya wokovu—kweli.

Kufikia hapa, kuna kufanana kwingi kati ya mafunzo ya Nehori na ukweli wa injili. Lakini kumbuka—kama vile ilivyo kwa pesa bandia, tunahitajika kuangalia tofauti, sio kufanana. Kwa hivyo wacha tuangalie hoja ya mwisho ya Nehori:

  • Mungu atawapa wanadamu wote uzima wa milele—uongo!

Sasa hii ndiyo tofauti kubwa ambayo inatuelezea kuwa Nehori alikuwa mwenye udanganyifu wa kiroho. Wokovu kutokana na kifo cha kimwili ni hakika kwa wote, lakini wokovu kutokana na kifo cha kiroho inategemea hiari yetu ya kutubu. Ikiwa tutatubu, basi tunaweza kupokea uzima wa milele (ona Yakobo 6:11). Lakini hakuna cha bure.

Gidioni na Alma Walimtambua Mdanganyifu

Uovu wa Nehori ulifichuliwa siku ambayo alikutana na Gidioni, mwalimu mwenye haki katika Kanisa la Mungu. Gidioni alikuwa amekabiliana na Mfalme Nuhu miaka kadhaa hapo awali na hivyo basi alikuwa na uzoefu na wadanganyifu wa kiroho (ona Mosia 19:4–8). Nehori “akaanza kubishana na Gidioni kwa ukali, ili awapotoshe watu wa kanisa; lakini [Gidioni] alimpinga, na kumwonya kwa maneno ya Mungu” (Alma 1:7). Gidioni alimtambua Nehori kama Mdanganyifu. Mara alipofichuliwa, Nehori aliamua kutumia mbinu nyingine ya Shetani—mauaji. Lakini kifo cha Gidioni hakikuwa bure. Watu walimleta mdanganyifu Nehori kwa Alma ili ahukumiwe.

Alma alitambua kuwa Nehori hakuwa tu na hatia ya ukuhani wa uongo na mauaji lakini pia ikiwa ungeachwa kuendelea, ukuhani wa uongo miongoni mwa watu, “ungethibitisha maangamizo yao kabisa” (Alma 1:12). Kwa hivyo Nehori alihukumiwa kifo, na alikufa “kifo cha aibu” (Alma 1:15).

Gidioni na Alma ni mifano kwetu. Wakati tukiwa na Roho pamoja nasi, tutaona na kusikia “vile vitu vilivyo” (Yakobo 4:13). Tutatambua mipango na mbinu bandia za shetani “tukiwa na ufahamu kamili, kama mwangaza wa mchana ulivyo kwa giza la usiku” (Moroni 7:15).

Adui yetu wa “vitu bandia” ni mwerevu, lakini kama Gidioni na Alma, tunaweza kuwa werevu zaidi. Kama vile nilivyoanza kugundua taratibu tofauti kati ya jozi yangu ya noti za dola, tunaweza taratibu kufundisha macho yetu na vilevile akili na roho zetu kutambua tofauti kati ya ukweli na uongo. Tunapofanya hivyo, tutawatambua wenye vitu bandia na kupinga uongo wao.

Muhtasari

  1. Joseph F. Smith, Mafundisho ya Injili, to. la 5 (1939), 376.

  2. Teachings of Presidents of the Church: Brigham Young (1997), 280. Ezra Taft Benson (2014), 132.

  3. James E. Faust, “Nguvu Ambazo Zitatuokoa,” Liahona, Jan. 2007, 4.