2016
Ukuhani Nanga Imara
April 2016


Fasihi za Injili

Ukuhani: Nanga Imara

Makala haya yalitayarishwa na Mzee L. Tom Perry mnamo Mei 28, 2015, siku mbili tu kabla ya kuaga dunia, yalikuwa yashirikishwe kwa mwenye ukuhani vijana.

Picha
Aaronic Priesthood members passing the sacrament

Nguvu kubwa katika maisha yangu imekuwa ukuhani wa Mungu. Ninaamini utakuwa nanga imara pia kwenu ninyi vijana wa kiume. Lakini ili upate kuwa na nguvu katika maisha yenu, unahitaji kuuelewa na kuutumia.

Uzoefu wa awali na Ukuhani

Nimekulia katika mazingira mazuri huko Logan, Utah. Sikuwa na hofu ya kukosa chakula au nyumba wala elimu. Lakini pengine kwa sababu maisha yalikuwa rahisi, nilihitaji kitu cha kushikilia ambacho ningekitegemea kama nanga.

Kwangu mimi nanga hiyo ilikuwa ni ukuhani wa Mungu. Nilikuwa katika hali isiyo ya kawaida wakati nikikua. Baba yangu aliitwa kuwa askofu wakati nilipokuwa na umri wa mwaka mmoja, na aliendelea kuwa askofu wangu kwa miaka 19. Mwongozo wa ki-baba na wa kiroho ulikuwa msaada mkubwa sana kwangu.

Nadhani hii ndiyo sababu hasa kwa nini nilitarajia kupokea Ukuhani wa Haruni siku ya mwaka wa 12 wa kuzaliwa kwangu. Ninakumbuka siku hiyo maalumu niliisikia mikono ya baba yangu juu ya kichwa changu akinitawaza. Baada ya hapo, niliendelea kupitia ofisi zote za Ukuhani wa Haruni na kupokea miito niliyoipenda sana.

Kupitisha sakramenti ilikuwa kitu maalum sana kwangu. Ungeweza kuona watu wakiweka ahadi wenyewe ya kumtii Bwana na kushika amri zake wakati wakipokea ishara za mwili Wake na damu Yake.

Kukua katika Uelewa wa Ukuhani

Kadiri muda ulivyokuwa ukisonga, nilihitimu kutoka sekondari, na kisha baada ya mwaka mmoja chuoni, niliitwa kwenda misheni. Nilifurahia kila dakika ya misheni na niliwapenda wenzi wangu. Hususani mmoja ambaye alikuwa nguvu yangu. Nilijifunza mengi kutoka kwake wakati tukitimiza majukumu yetu.

Kwa sababu nchi ilikuwa vitani, niliporejea kutoka misheni nilijiunga na Jeshi la Marini la Marekani. Vita vilipomalizika, nilirejea chuoni, nikaoa, na kuanza familia. Uhamaji wa mara kwa mara kikazi ulinipeleka sehemu nyingi za Amerika, sehemu ambazo nilijifunza mengi nikitumikia katika miito mingi ya ukuhani. Hatimaye nikatua Boston, Massachusetts, ambako nilitumikia kama rais wa kigingi. Ilikuwa kutokea hapo ndipo nilipoitwa kuwa msaidizi wa Wale Kumi na Wawili na halafu, baada ya miezi 17, kwenye Akidi ya Mitume Kumi na Wawili.

Mambo Niliyojifunza kama Mtume

Nimejifunza nini kama mshiriki wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili?

Nimejifunza kuwa kuna mwongozo, nanga, na ulinzi katika ukuhani.

Ukuhani daima umekuwepo. Kabla Adamu hajaja duniani, alikuwa na ukuhani. Kadiri uzao wa Adamu ulivyokuwa ukisambaa pamoja na ukuhani, ilionekana kuwa ni muhimu kuweka utaratibu wa namna ya kutawala ukuhani. Bwana alifanya hivyo kwa kumwita Ibrahimu kuwa kiongozi wa wenye ukuhani katika familia yake. Utaratibu huu uliendelea chini ya Isaka na Yakobo, ambaye jina lake baadae likabadilishwa kuwa Israeli.

Karne kadhaa baadae, wana wa Israeli walijikuta wenyewe utumwani. Bwana alimtuma Musa kuwakomboa, lakini alipofanya hivyo, walijithibitisha wenyewe hawakuwa tayari kama watu kwa Ukuhani wa Melkizedeki. Hivyo wakabakiziwa Ukuhani wa Haruni hadi wakati wa Mwokozi.

Ninaona ni kitu cha kufurahisha sana kile ambacho Mwokozi alikifanya kwanza alipokuwa anaanza huduma Yake. Alianzisha Ukuhani wa Melkizedeki. Akawaita Mitume kumi na wawili na akawafundisha sheria na taratibu za ukuhani. Alimwita Petro kuwa Mtume kiongozi, akianzisha safu ya mamlaka katika Kanisa Lake. Katika siku ile na siku hii, ni Yesu Kristo ndiye anayemteua Mtume kiongozi Wake ili kuwa kiongozi juu ya Kanisa, na ni Mwokozi ndiye anayemwelekeza yeye katika kazi zake za ukuhani.

Hivyo ukuhani una safu ya moja kwa moja kutoka kwa Bwana na Mwokozi wetu kupitia kwa Mtume kiongozi hadi kwa Mitume wengine na kuendelea kwa makuhani wengine katika Kanisa. Funguo za mamlaka zimetolewa kwa Mitume, na ilimradi funguo hizo ziko duniani, tutaongozwa na Bwana Mwenyewe. Mwongozo huu wa kiungu hutulinda na kututhibitishia kwamba Kanisa halitapotoka mbali na ukweli. Litabaki imara kwa sababu haliongozwi na kiumbe ye yote wa duniani. Linaongozwa na Bwana.

Jifunzeni Mafundisho ya Ukuhani

Ushauri mkubwa kabisa ninaowapa ninyi vijana wa kiume ni kujifunza mafundisho ya ukuhani, eleweni nguvu mliyonayo katika kutumia ukuhani wenu, na jifunzeni namna, inavyoweza kubariki maisha yenu na maisha ya wengine.

Ninakuahidini kama mtajifunza mafundisho ya ukuhani na kutimiza kazi zenu za ukuhani, ukuhani utakuwa nanga imara ambayo itawaweka salama kiroho na kuwaleteeni furaha tele. Kuweni akidi ya kweli ya ukuhani. Wasaidieni marafiki zenu na waleteni katika akidi zenu. Jengeni udugu katika akidi yenu ambayo itakuwa msingi imara kwa maisha yenu.