2016
Tafsiri ya Maandiko: Kwa Lugha ya Moyo
April 2016


Tafsiri ya Maandiko: Kwa Lugha ya Moyo Wetu

Matukio yasiyo na hesabu yanaonyesha mkono wa Bwana katika kazi ya Kutafsiri maandiko yake.

Picha
scriptures and woman

Picha ya kurasa za Kitabu cha Mormoni katika Kijapani, Kireno, na Kijerumani na Laura Seitz, Deseret News

Tukio hili linajulikana kwa wale ambao wamehusika katika kutafsiri maandiko kutoka Kingereza hadi lugha nyingine. Inafanyika mara kwa mara:

Kijana Mwarmenia aliyekuwa na Kitabu cha Mormoni mkononi ambacho kilikuwa tu kimetafsiriwa karibuni katika lugha yake alimkaribia mshiriki mmoja wa timu ambaye alisaidia katika tafsiri … “Asante,” yeye anasema. “Nimekisoma Kitabu cha Mormoni katika Kingereza. Nimekisoma Kitabu cha Mormoni katika Kirusi. Nimekisoma katika Kiukreni. Lakini hadi nilipoweza kukisoma katika Kiarmenia, kwa kweli sikuwa nimekielewa. Nilipokisoma katika Kiarmenia, hatimaye kilileta maana. Ilikuwa kama kuja nyumbani.”

Kuja Nyumbani

Ikiwa injili ya Yesu Kristo ni nyumbani kwetu kiroho, basi ni vyema tu ikiwa itahisika starehe na kujulikana. Nyumbani tunapumzika. Tunajilisha. Tunazungumza na wale tuwapendao katika lugha tuliyofundishwa magotini mwa mama. Hii ndiyo lugha ya moyo wetu, na kwa vile moyo ndiyo kitu ambacho injili inafaa kufikia, kusoma maandiko katika lugha ya moyo wetu ni muhimu.

Mafundisho na Maagano kinapendekeza hivyo. Hapo Bwana anafunua kuwa kupitia funguo za ukuhani zinazoshikiliwa na Urais wa Kwanza, “mkono wa Bwana utakapofunuliwa katika uwezo kwa kuyashawishi mataifa … juu ya injili ya wokovu wao.

“Kwani itakuja kutokea katika siku ile, kwamba kila mtu atasikia utimilifu wa injili katika ulimi wake, na katika lugha yake mwenyewe, kupitia wale waliotawazwa kwa uwezo huu, kwa huduma ya Mfariji, aliyemwagwa juu yao kwa ajili ya ufunuo wa Yesu Kristo” (M&M 90:10–11).

Jim Jewell, ambaye alifanya kazi na timu ya tafsiri ya maandiko katika makao makuu ya Kanisa, anaeleza simulizi kuhusu jinsi maandiko yanaweza kuleta hisia za kuwa nyumbani wakati yanapokuwa yametafsiriwa katika lugha ya roho:

“Katika kutafsiri Kitabu cha Mormoni katika Sesotho, lugha ambayo inazungumzwa katika taifa la Afrika la Lesutu, tulihitaji mtu wa kutusaidia kutathmini kazi ya timu ya tafsiri. Msimamizi wa mradi huo, Larry Foley, alimpata mshiriki mmoja wa Kanisa kutoka Lesutu ambaye alikuwa mwanafunzi wa shahada ya pili katika Chuo Kikuu cha Utah State. Kule Lesutu, masomo yanaendeshwa katika Kiingereza, kwa hivyo mwanamke huyu na watoto wake walikuwa wamesoma katika Kiingereza kuanzia darasa la kwanza kuendelea, lakini walikuwa wakizungumza nyumbani kwao katika Sesotho.

“Alikubali kushughulikia tafsiri hiyo. Tathmini ya sura ambazo tulimtumia kwa kweli ilikuwa na usaidizi. Mara kwa mara tuliwasilisha maswali maalum kuhusu msamiati na muundo wa lugha ambapo alitoa majibu yenye manufaa. Hata hivyo, tulibaini kuwa alikuwa ameangazia akitumia rangi ya manjano aya nyingi sana ambazo hazikuwa na uhusiano na maswali yetu. Tulipomwuliza kuhusu aya alizokuwa amezisisitizia, alisema: ‘O, aya hizo ni zile ambazo ziligusa moyo wangu sana ambazo sikuwa nimewahi kuzielewa kikamilifu katika Kiingereza. Niliziangazia ili niweze kuzishiriki na watoto wangu.’”

Mfano wa Tafsiri ya Maandiko

Kutafsiri kwa Biblia kuna historia ndefu sana ya kuvutia, kuanzia na tafsiri ya sehemu kadhaa za Agano la Kale kutoka Kiebrania hadi Kigiriki. Baadaye, Biblia kutafsiriwa kutoka Kigiriki hadi Kilatini, na kutoka Kilatini, Kiebrania, na Kigiriki hadi Kiingereza na lugha zingine nyingi mno.1 Kutokana na hayo, Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho halitafsiri Biblia kwa lugha tofauti lakini hukubali matoleo ambayo yashakubaliwa kama yenye kuaminika na Wakristo wanaozungumza lugha hizo.2

Picha
men at work translating

Kazi nyingi ya tafsiri ya kimaandiko ambayo Kanisa hufanya, hivyo basi, ni ya Kitabu cha Mormoni (kikiwa cha kwanza kutafsiriwa), Mafundisho na Maagano, na Lulu ya Thamani Kuu. Lugha ambayo vitabu hivi hutafsiriwa ni kutoka Kiingereza, lugha ambayo Nabii Joseph Smith alivifunua, lugha ya moyo wake. Mchakato ambao hutumika katika kutafsiri maandiko hadi kwa lugha ambazo si Kiingereza yafaa kujulikana na wanafunzi wa historia ya Kanisa. Ni karibu tu sawa na mchakato ambao Nabii alitumia katika kutafsiri Kitabu cha Mormoni hadi kwa Kiingereza.

Joseph Smith alikuwa mnyenyekevu, mvulana asiyesoma sana wa mashambani. Lakini alikuwa na tabia na uwezo ambao Bwana alihitaji kwa ile kazi ambayo ilihitajika kufanywa. Kwa kweli, Joseph na familia yake waliandaliwa na kuwekwa mahali palipo stahili ili kufanya kazi hii.3

Joseph pia alipewa usaidizi—kutoka mbinguni na kutoka kwa binadamu—katika kutafsiri kumbukumbu hizi za wanefi. Malaika Moroni alimtembelea Joseph kila mwaka kwa miaka minne kabla ya kumruhusu kuichukua kumbukumbu hiyo. Hatujui kila kitu ambacho Moroni alimfundisha Nabii, lakini ziara zake inaonekana zilimuandaa kiroho na kiakili kwa kazi iliyokuwa mbele.4

Bwana pia alitayarisha “vikalimani” mbele ya muda kama njia ya kutafsiri lugha ambayo ilikuwa imepotea. Vilivyoelezwa kama mawe mawili masafi yaliyofungwa katika fremu za chuma, hizi na kifaa kama hicho kinachoitwa jiwe la muonaji vilimsaidia Nabii kutafsiri kumbukumbu hiyo ya Wanefi hadi kwa Kiingereza. Nabii hakuzungumza kwa undani kuhusu mchakato huo: alisema tu kwamba alitafsiri Kitabu cha Mormoni “kwa kipawa na uwezo wa Mungu.”5

Kama nyongeza kwa usaidizi wa mbinguni aliopewa, Joseph Smith alikuwa na usaidizi wa binadamu kupitia waandishi ambao walitoa nakala iliyoandikwa ambayo wengine mwishowe walitayarisha, wakapiga chapa, wakalipia gharama, na kusambaza ulimwenguni.

Si kama utayarishaji na usaidizi ambao Joseph alipata katika kazi yake ya kutafsiri, wale waliopewa jukumu la kutafsiri maandiko kwa wakati huu wanatayarishwa na Bwana na kupewa usaidizi katika kazi yao—kutoka mbinguni na kutoka kwa binadamu.

Kazi ya Ufunuaji

Picha
local reviewers reading

Inayolowesha mchakato huu mgumu wa kutafsiri ni nguvu ya kiroho ambayo inaweza kuelezwa bora kama “ufunuo kupitia baraza.” Watu hao wawili au watatu wanaochaguliwa kama wafasiri hujiunga pamoja na wengine katika kufanya kazi hiyo. Wana wasimamizi kutoka makao makuu ya Kanisa, wahakiki wa eneo, kamusi ya marejeo,6 miongozo ya tafsiri, programu za tarakilishi, na usaidizi wa viongozi wa Kanisa unaotamba hadi kwa Urais wa Kwanza. (Ona chati inayoambatana nayo) Wakati ambapo Urais wa Kwanza unatoa idhini ya mwisho ya tafsiri, kazi hiyo kisha inatayarishwa, inapigwa chapa, na kusambazwa. Ikiwa imetayarishwa katika muundo wa digitali, pia inawekwa katika LDS.org na katika Gospel Library app.

Juhudi za ushirikiano huu zilikuwa za umakinifu na zenye maongozi. Inahusisha kuwa mwangalifu sana kwa ubora wa yaliyomo na ubora wa umbo la muundo ambao umetumika kuyawasilisha. Tafsiri hufanyiwa mapitio katika viwango vingi, hasa katika kiwango cha kidini ambapo idhini ya Bwana inatafutwa. Ni wakati tu idhini hiyo inapotolewa ndipo tafsiri inaweza kusonga mbele. Huku ikiwa si kwa ufunuo sawa na ile njia Nabii Joseph Smith alitafsiri Kitabu cha Mormoni, mchakato huu ni wazi kuwa unaongozwa na Bwana—kwa karama zake na kwa nguvu zake.

Hii haimaanishi kuwa tafsiri huwa kamilifu wakati inapokamilika mara ya kwanza. Mara nyingi, muda na mapitio zaidi na wale wanaosoma maandiko hupendekeza uboreshaji katika sarufi na msamiati au wanapata makosa ya utayarishaji au tahajia. Ni nadra, mabadiliko yafanyike katika kueleza mafundisho. Wakati haya yanapofanyika, yanafanyika chini ya uongozi wa urais wa Kwanza.

Bwana Huandaa

Bwana huruzuku kazi hii ya kutafsiri kwa njia zingine pia. Kawaida huwa kunaripotiwa na timu ya tafsiri katika makao makuu ya Kanisa kuwa wakati mahitaji yanapotokeza, Bwana huandaa.

Kama mojawapo ya mifano mingi, mfasiri alihitajika kwa ajili ya kutafsiri na kurekodi raslimali za Kanisa katika Mam (inatamkwa “mum,” ukoo wa lugha na Wamaya, inayozungumzwa Gwatemala). Miongoni mwa wamisionari wa kwanza walioitwa Gwatemala kulikuwa na mzee ambaye Babu yake alizungumza Mam. Mmisionari alikuwa amelelewa mjini na alizungumza tu Kihispania. Lakini kila usiku babu yake angemjia katika ndoto na kumfundisha lugha ya Mam. Huyu mzee alikuja kuwa mfasiri wa pekee wa Mam Kanisani.

Mara nyingi, kazi ya kutafsiri hufanyika kwa kujitolea binafsi. Kutegemea na hali za kifedha, baadhi ya wafasiri hutoa msaada wa huduma na wengine hulipwa ili waweze kuwa na wakati wa kutenga kwa minajili ya kufanya tafsiri.

Mwanaume ambaye alikuja kuwa mmoja wa wafasiri wa Urdu aliongolewa kwa Kanisa kule Pakistani alipokuwa akifanya kazi kama mwalimu. Kwa sababu ya kuongoka kwake, alipoteza kazi yake; akapoteza nyumba yake, ambayo ilikuwa imetolewa na shule ambayo alikuwa akifundisha; na akapoteza masomo kwa watoto wake. Msimamizi mmoja wa tafsiri wa Kanisa alimwendea kuhusu kuhudumu kama mfasiri na kumpa malipo wastani. Baada ya kufanya kazi kama mfasiri kwa miezi kadhaa, bwana huyo alimtembelea msimamizi huyo na kwa woga kuuliza ikiwa msimamizi angeweza kumnunulia kalamu mpya ya wino. Ile ambayo alikuwa akitumia ilikuwa imeisha wino. Hapo tu ndipo msimamizi aligundua na kurekebisha makosa ya maandishi yaliyosababisha mfasiri kupokea tu kiwango kidogo cha malipo ambayo alistahili kupewa.

Lakini tu jinsi ambavyo Bwana alimbariki Joseph Smith kwa njia ambazo zilimwezesha kukamilisha kazi yake, Bwana huwabariki wafasiri wake. Kwa mfano, mfasiri wa maandiko ya Kilativia alikuwa mwanasheria ambaye alikuwa amesomea sheria kule Urusi, ambako alikuwa ameongolewa kwa injili ya urejesho. Kule Lativia, alikuwa anaanzisha biashara yake. Alikuwa pia anahudumu kama rais wa tawi. Alikuwa na shughuli nyingi mno, lakini Kanisa lilimhitaji pamoja na weledi wake wa Kingereza.

Aliomba muda apate kusali kuhusu ombi hilo kwa sababu kukubali kungekuwa na maana, jinsi alivyomwambia mwakilishi wa Kanisa, “kutaondoa chakula vinywani mwa watoto wake.” Baada ya kuomba, aliamua kukubali lakini akamwuliza Bwana ambariki na uwezo wa kufanya kilichokuwa kigumu, uangalifu wa kiroho, na kazi yenye kuchukua muda mwingi.

Alianza kwenda katika ofisi yake ya sheria saa moja mapema kila siku na kutumia saa hiyo moja kutafsiri Kitabu cha Mormoni. Alimaliza kwa wakati mzuri chini ya muda wa miaka mitano ambao mchakato huo kawaida huchukua. Kwa kweli, hii ilikuwa mojawapo wa tafsiri zilizofanywa haraka sana tangu wakati Joseph Smith alitafsiri Kitabu cha Mormoni katika muda wa takriban siku 60.

Matukio mengi sana yanaweza kutolewa ili kuonyesha mkono wa Bwana katika kazi ya kutafsiri maandiko Yake. Yote yanadhihirisha wazi kuwa hii ni kazi Yake na anajali sana kuihusu. Yeye huwatayarisha watu kufanya kazi Yake. Yeye hutayarisha vifaa wanavyohitaji kuharakisha kazi. Na Yeye anawapa maongozi na kuwabariki njiani.

Matokeo ni ulimwengu ulioimarishwa na neno la Mungu, na kupewa watoto wake katika lugha ya moyo.

Picha
family reading the scriptures

Muhtasari

  1. Ona mfululizo wa sehemu nane, “Namna Biblia Ilikuja Kuwa,” na Lenet H. Read ilichapishwa katika Ensign between Januari na Septemba 1982.

  2. Ona, kwa mfano, “Toleo la Kanisa la Biblia ya Kihispania Iliyochapishwa Sasa,” mormonnewsroom.org.

  3. Ona Matthew S. Holland, “Njia ya Kuelekea Palmyra,” Liahona, Juni 2015, 14–19.

  4. Ona Kent P. Jackson, “Ujumbe wa Moroni kwake Joseph Smith,” Ensign, Ago. 1990, 12–16.

  5. Joseph Smith, katika utangulizi wa Kitabu cha Mormoni. Kwa maelezo kamili kuhusu tafsiri ya Joseph Smith ya Kitabu cha Mormoni, ona Mada ya Injili, “Book of Mormon Translation,” topics.lds.org.

  6. Kamusi ya marejeo hufafanua kila neno katika maandiko ya Kiingereza ili wafasiri waweze kuelewa vyema maana ya maneno. Mara nyingi, maneno huwa na zaidi ya maana moja, kwa hivyo wafasiri lazima wategemee muktadha, msukumo, na ushirikiano kutafuta suluhu mwafaka. Mara kwa mara, maswali kuhusu maana hutatuliwa tu na Urais wa Kwanza.