2016
Unabii na Ufunuo Binafsi
April 2016


Ujumbe wa Urais wa Kwanza

Unabii na Ufunuo Binafsi

Picha
youth and children first presidency message sidebars
Picha
family watching general conference

Kanisa la Yesu Kristo la kweli limerejeshwa na liko duniani hivi leo. Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho daima limekuwa likiongozwa na manabii na mitume walio hai, ambao hupokea mwongozo siku zote kutoka mbinguni.

Mfumo huo mtakatifu pia ulikuwa wa kweli siku za kale. Tunajifunza katika Biblia: “Hakika Bwana Mungu hatafanya neno lo lote, bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake” (Amosi 3:7).

Mungu amezungumza tena katika siku zetu, kupitia Nabii Joseph Smith. Alifunua kupitia Nabii Joseph Smith Injili ya Yesu Kristo katika utimilifu wake. Alirejesha ukuhani wake mtakatifu na funguo na haki zote, nguvu, na kazi za nguvu takatifu za ukuhani.

Katika siku zetu, manabii na mitume walio hai wanayo mamlaka ya kuzungumza, kufundisha, na kuongoza kwa mamlaka kutoka kwa Mungu Baba na Bwana Yesu Kristo. Mwokozi alimwambia Nabii, “Kile ambacho Mimi Bwana nimesema, nimekisema, na wala sijutii, na ingawa mbingu na dunia zitapita, neno langu halitapita kamwe, bali litatimia, iwe kwa sauti yangu mwenyewe au kwa sauti ya watumishi wangu, yote ni sawa” (M&M 1:38).

Katika mkutano mkuu mara mbili kwa mwaka, tunabarikiwa na nafasi ya kusikiliza neno la Bwana yetu kutoka watumishi Wake. Hii ni fadhila kuu sana. Lakini thamani ya fursa hiyo hutegemea kama tunapokea maneno yao chini ya ushawishi wa yule Roho ambaye alitolewa kwa watumishi wale (ona M&M 50:19–22). Kama vile ambavyo wao wanapokea mwongozo kutoka Mbinguni, na sisi lazima iwe vivyo hivyo. Na hivyo huhitajika kutoka kwetu juhudi za kiroho sawa sawa na hizo.

“Fanya Maandalizi”

Miaka kadhaa iliyopita mmoja wa washiriki wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili aliniomba nisome hotuba ambayo alikuwa akitayarisha kwa ajili ya mkutano mkuu. Nilikuwa mshiriki mdogo wa akidi. Ilikuwa heshima kubwa kwangu kwa sababu ya imani yake kwangu kuwa ningeweza kumsaidia kutafuta maneno ambayo Bwana angemtaka azungumze. Aliniambia huku akitabasamu, “Oh, hii ni rasimu ya 22 ya hotuba.”

Nilikumbuka ushauri wa mpendwa na mkarimu Rais Harold B. Lee (1899–1973) aliokuwa amenipa mapema kwa msisitizo mkubwa: “Hal, ukitaka kupokea ufunuo, fanya maandalizi.”

Nilisoma, nilitafakari, na kusali kuhusu ile rasimu ya 22. Niliisoma vyema kadiri iwezekanavyo chini ya ushawishi wa Roho Mtakatifu. Na wakati yule mshiriki wa ile akidi alipotoa hotuba yake, nilikuwa nimetimiza maandalizi yangu. Sina uhakika kama nilisaidia, lakini ninajua kwamba nilibadilika wakati niliposikiliza hotuba hiyo ikitolewa. Ujumbe ulionijia ni zaidi ya yale maneno ambayo nilikuwa nimeyasoma na yale aliyokuwa akiongea. Maneno hayo yalikuwa na maana kubwa zaidi kuliko yale niliyokuwa nimesoma kwenye rasimu. Na ujumbe ulionekana ulikusudiwa kwa ajili yangu, maalum kwa mahitaji yangu.

Watumishi wa Mungu hufunga na kusali ili wapokee ujumbe ambao Yeye anao ili wao wawape wale wanaohitaji ufunuo na maongozi. Kile ambacho nilijifunza kutoka tukio hilo, na matukio mengine mengi kama hayo, ni kuwa ili kupata manufaa makuu yanayoweza kupatikana kutokana na kuwasikiliza manabii na mitume walio hai, ni lazima tulipe gharama sisi wenyewe ya kupokea ufunuo.

Bwana anampenda kila mtu ambaye anaweza kusikiliza ujumbe Wake, na anajua mioyo na mazingira ya kila mmoja wetu. Anajua ni marekebisho gani, kuhamasisha gani, na ukweli upi wa injili utakuwa bora zaidi kumsaidia kila mmoja kuchagua njia yake katika safari hii ya kuelekea uzima wa milele.

Sisi ambao husikiliza na kutazama ujumbe wa mkutano mkuu mara nyingine hufikiria baadaye, “Ni kipi naweza kukumbuka vizuri sana? Matumaini ya Bwana kwa kila mmoja wetu ni kwamba jibu letu litakuwa: “Sitaweza kamwe kusahau wakati ambapo niliisikia sauti ya Roho akilini mwangu na moyoni ikiniambia kile ambacho ningeweza kufanya kumridhisha Baba yangu wa Mbinguni.”

Tunaweza kupata ule ufunuo binafsi wakati tunapowasikiliza manabii na mitume na tunapojitahidi kwa imani kuupokea, kama vile Rais Lee alivyosema tunaweza. Ninajua kuwa hayo ni kweli kutokana na tukio hili na kulingana na ushuhuda wa Roho.