2016
Je Maelekezo Yanaleta Maana
April 2016


Tafakari

Je, Maelekezo Yanaleta Maana

Mwandishi, ambaye aliishi Colorado, Marekani, aliaga duniani mwaka jana.

Safari kwa baiskeli ilinishawishi juu ya haja ya kuangalia mara kwa mara ramani ya barabara ya maisha.

Picha
bike riding through France

Miaka kadhaa iliyopita nilienda safari ya baiskeli kule Ufaransa pamoja na dadangu, shemeji yangu, na binti yake. Kila asubuhi tulipewa kurasa tatu zilizokuwa na maelezo ya kina ambayo, ikiwa yangefuatwa sawasawa, yangetuongoza hadi mwisho wa safari ya siku hiyo. Tulipokuwa tukiendesha baiskeli kupitia mashamba ya mizabibu, maelekezo yangetuelekeza, “nenda futi 165 (50 m) Kaskazini, kisha geuka upande wa kushoto na uende futi 330 (100 m).” Mara nyingi, maelekezo yalitupa ishara na majina ya barabara.

Asubuhi moja tuliendesha baiskeli kwenye barabara ya kuvutia lakini punde tukagundua ya kwamba maelekezo yetu hayakuwa yanalingana na eneo hilo. Tukiwa tunapotea kwa haraka sana, tuliamua kurudi mahali ambapo tulijua kuwa tulikuwa kwenye barabara sahihi ili kuona ikiwa tungeweza kutatua ni wapi tungeenda.

Kwa uhakika, tulipofika pale, tuliona ishara ndogo ya barabarani, ilioonyeshwa kwenye maelekezo yetu, ambayo tulikosa kuiona. Punde tulikuwa njiani tena, tukilinganisha mwendo wetu na maelekezo, ambayo tena yalikuwa yanaleta maana kamilifu.

Tukio hilo lilikuwa kama sitiari ambayo ilijibu swali la kutatanisha nililokuwa nalo: Kwa nini, wakati ambapo mtu ameisha kuwa na ushuhuda kuhusu injili, anawezaje kupotea njia tena? Ilikuwa wazi kwangu kuwa tunapochukua hatua mbaya (dhambi) au kukosa kufuata amri za Mungu, maelekezo (neno la Mungu) hayaleti maana tena. Ramani, kama ilivyokuwa, hailingani na eneo tulilokuwemo. Ikiwa hatujapotea mbali sana, tunaweza kugundua kwamba makosa ni yetu na kuwa tunahitaji kurudi (kutubu) au kuahidi tena kuishi jinsi ambavyo Mungu ametuamuru mahali ambapo tulijua tulikuwa kwenye njia sahihi.

Mara nyingi sana wakati maelekezo hayalingani na mahali tulipo, tunakuwa na shaka kuhusu maelekezo. Badala ya kurudi nyuma, tunalaumu maelekezo na kisha kuyaacha kabisa. Hatimaye, tukiwa tumepoteza ono la mwisho wa safari yetu, tunapotea, tukizurura katika njia ambazo zinaweza kuonekana, kwa muda, za kuvutia mno lakini hazitatufikisha mahali ambapo tunahitaji kwenda.

Kila siku tunayo fursa ya kusoma maandiko. Na kila miezi sita, tuna mkutano mkuu wa Kanisa. Je, hizi sio nyakati ambazo tunaweza kuangalia ramani zetu za barabara na kuhakikisha kuwa tuko mahali ambapo tunahitaji kuwa? Wakati mmoja, nilipokuwa nikisikiliza mkutano, nilihisi kuwa, licha ya mapungufu tuliyonayo, tunaweza kujua tuko kwenye njia sahihi ikiwa maelekezo haya yanaleta maana kamilifu kwetu.

Jinsi ambavyo kufuata mwelekeo sahihi kutatufikisha mwisho wa safari zetu maishani, kusoma maandiko na kutii ushauri wa manabii walio hai huturuhusu sisi kuangalia njia yetu na kurekebisha pale inapohitajika ili, hatimaye, tuwasili nyumbani kwetu mbinguni.