2019
Mwaliko kwa ajili ya Ricardo
Aprili 2019


Mwaliko kwa ajili ya Ricardo

Martin Apolo Cordova

Paraná, Brazil

Picha
stack of invitations

Kielelezo na Katy Dockrill

Ninaposikia kuhusu shughuli ya Kanisa, daima huwa ninawaalika watu 10 ambao siyo waumini wa Kanisa kuhudhuria. Nimefanya hili kwa miaka mingi. Ninatengeneza mialiko na kuuweka kila mmoja ndani ya bahasha nyeupe na kumwomba Roho aniongoze. Kisha ninatoa mialiko. Mara chache wote 10 wanahudhuria, lakini hata kama mmoja tu anahudhuria, ninahisi nimefanikiwa.

Miaka kadhaa iliyopita, niliandaa mialiko kumi kwa ajili ya shughuli ya wanandoa. Nilitoa tisa kwa watu kazini na kubaki na moja. Sikujua nani wa kumpa. Dakika chache baadae, Ricardo, mwakilishi wa mauzo, alipita karibu na meza yangu. Nilihisi msukumo wa kumualika, japokuwa alikuwa amekataa mwaliko kutoka kwa mfanyakazi mwenza wa kuhudhuria tukio kanisani kwake. Sikudhani Ricardo angevutiwa.

Lakini Ricardo alipopita karibu na meza yangu tena akielekea nje, nilihisi msukumo tena. Hata hivyo, alitoka haraka kiasi kwamba sikupata nafsi ya kuzungumza naye. Nilisali kwamba Ricardo angerejea ikiwa nilipaswa kumpa mwaliko.

Baada ya kumaliza kusali, Ricardo alirudi kuniuliza swali. Baada ya hapo, nilisema, “Ricardo, kanisa langu lina shughuli kwa ajili ya wanandoa. Tunakwenda kushiriki uzoefu kuhusu jinsi ya kuishi kwa furaha kila siku. Baada ya hapo, kutakuwa na dansi. Nikikualika, utakuja?”

“Bila shaka!” Ricardo alisema, lakini jibu lake halikunishawishi.

“Angalau nilifanya sehemu yangu,” niliwaza.

Mke wangu pamoja nami tuliwasili kwenye shughuli mapema ili kuwakaribisha watu wakati wakiingia. Ghafla, nilimwona Ricardo na mke wake, Regina. Niliwatambulisha kwa mke wangu na kwa wengine waliokuwa wakihudhuria. Jioni ile yote, Ricardo na Regina walionekana walikuwa wakifurahia. Nilishangazwa waliposema wangekuja kanisani jumapili kujifunza zaidi.

Ricardo, Regina, na watoto wao wawili walijifunza zaidi. Hatimaye, walijiunga na Kanisa. Baadae, waliunganishwa hekaluni. Ricardo wakati fulani aliniambia kwamba yeye na mke wake walikuwa wakizungumza kuhusu talaka, lakini ndipo Bwana alimuongoza Ricardo ofisini kwangu.

Tangu wakati huo nilimwomba Mungu msamaha kwa kudhani kwamba Ricardo asingekubali mwaliko wangu. Nimejifunza kwamba ni muhimu kumualika kila mtu. Huwezi kujua nani atakubali.