2019
Mwana Wetu ni Mwana wa Baba wa Mbinguni
Aprili 2019


Nyumba Zetu, Familia Zetu

Mwana Wetu ni Mwana wa Baba wa Mbinguni

Mwandishi anaishi Arizona, Marekani.

Maneno ambayo hayakuwa ya kwangu yaliingia akilini mwangu: “Unadhani unampenda kuliko ninavyompenda?”

Picha
mother and son

Picha ya mwandishi na mwanaye

Mwana wetu mpendwa mdogo, Hayden, alikuja kwenye ulimwengu huu akiwa wa bluu, hapumui, na akihangaika kwa ajili ya maisha. Halii. Hajongei.

Wakati madaktari na wauguzi walipoharakisha kuingia chumbani hospitalini, nilijua kuna kitu hakikuwa sawa kabisa. Mume wangu na baba yangu haraka walimpa Hayden baraka ya ukuhani, na Hyden alikimbizwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi. Punde aligundulika kuwa na tatizo lisilo la kawaida la moyo kutofanya kazi ipasavyo. Ndani ya siku chache alipitia upasuaji kadhaa wa moyo.

Kupitia nguvu ya muujiza ya baraka ya ukuhani, kufunga, na sala, Hayden alishinda yote na alinusurika. Tulikuwa na shangwe isiyo kifani kumleta mwana wetu nyumbani na kuanza maisha yetu mapya pamoja.

Hayden alileta shangwe isiyopimika kwenye maisha yetu. Tulimthamini na kumpenda mno. Lakini kadiri muda ulivyopita, nilianza kuwa na wasiwasi kwamba alikuwa haonyeshi maendeleo kama ilivyotarajiwa. Japokuwa wataalamu walituhakikishia kwamba hatimaye angekuwa sawa, wasiwasi wa kusumbua uliendelea pale nilipohangaika kumsaidia mwanangu.

Mimi na mume wangu tulijifunza yote tuliyoweza kuhusu ugonjwa wa Hayden. Tulifanya kila kitu tulichoagizwa na madaktari kufanya. Bado maendeleo hayakuja.

Nilichoka na kukata tamaa. Nilimsihi Baba wa Mbinguni kunisaidia kumpata mtu ambaye angeweza kumsaidia Hayden, lakini usaidizi haukuja. Hali ya Hayden ilizidi kuwa mbaya. Alianza kupata kifafa. Tulipata hofu. Tulidhani tulikuwa tunampoteza.

Usiku mmoja, nilichelewa kulala nikitafuta majibu. Nilimwandikia Hayden barua. Nilimwambia jinsi gani ninampenda na kwa kiasi gani nilikuwa nikijaribu kufanya maisha yake yawe rahisi. Niliahidi ningetumia siku zote zilizobaki za maisha yangu nikijaribu kumpatia msaada aliohitaji.

Kukata tamaa na kutokuwa na uhakika kwa muda vilinizidia. Nilipiga magoti na kumuuliza Baba yangu wa Mbinguni, “Kwa Nini?” Nilidhani alimtuma Hayden kwangu kwa sababu alijua sitakata tamaa kujaribu kumsaidia mwanangu. Hivyo kwa nini sikupata jibu lolote? Kwa nini kila daktari mpya na kila tiba mpya ilipelekea kikwazo kingine? Je, Baba wa Mbinguni alimpenda Hayden?

Sitasahau kamwe wakati ule. Hisia nyingi za upendo ghafla zilinifunika. Maneno ambayo hayakuwa ya kwangu yaliingia akilini mwangu: “Jerlyn, unadhani unampenda kuliko Ninavyompenda?”

Niliganda. Wakati uliganda. Machozi yalititirika usoni mwangu—siyo kwa kukata tamaa kama mwanzo, bali kwa tumaini, uelewa, na upendo.

Katika dakika ile moja, kila kitu kilibadilika. Moyo wangu ulilainika. Maswali yangu yalibadilika. Ninajua sasa kwamba Baba yangu wa Mbinguni anampenda Hayden kwa upendo mkamilifu. Hayden aliletwa hapa katika mwili ambao ulikidhi mahitaji yake na fursa zake kwa ajili ya ukuaji na kujifunza. Ana seti yake ya kipekee ya uwezo na changamoto kama vile kila mmoja wetu. Nimekuja kujua kwamba watoto wenye ulemavu ni wa thamani na watoto wapendwa wa Baba wa Mbinguni ambao wana kazi maalumu hapa katika dunia hii.

Mume wangu na mimi kwa uaminifu tunapokea majibu na baraka, lakini yanakuja katika wakati wa Bwana, siyo wakati wetu. Tumeongozwa kwenye vitabu sahihi, tiba sahihi, shule sahihi, na waalimu sahihi kumsaidia Hayden kufanikiwa katika maisha yake ya duniani. Tunajitahidi kutafuta njia ambayo Baba yetu wa Mbinguni ameitoa kwa Hayden badala ya njia tuliyotaka yeye apite. Tunafanya kila tunachoweza kumsaidia Hayden kufikia uwezekano wake mtakatifu na kuishi maisha ambayo Baba yake wa Mbinguni amemtengenezea. Uelewa wa mpango wa Baba wa Mbinguni umekuwa wazi zaidi sasa kiasi kwamba tunaelewa kuwa Hayden alikuwa Wake kabla Hayden hajawa wetu.