2019
Amini katika Ukombozi wa Mwokozi
Aprili 2019


Amini katika Ukombozi wa Mwokozi

Kutoka kwenye hotuba ya mkutano wa ibada, “Nguvu ya Ukombozi,” iliyotolewa katika Chuo Kikuu cha Brigham Young mnamo Januari 15, 2008.

Upatanisho na Ufufuko wa Mwokozi unampa Yeye nguvu ya kutuimarisha katika majaribu yetu au kutukomboa kutokana nayo.

Picha
image of the Savior with arms outstretched

UTONDOTI KUTOKA KATIKA KWA MADHUMUNI HAYA, NA YONGSUNG KIM, KWA HISANI YA HAVEN LIGHT

Kwa wale kati yetu ambao tumepoteza wapendwa wetu, njia mbele inaweza kuwa yenye huzuni na upweke—hata zaidi kwa wale wasio na ufahamu na ushuhuda wa Upatanisho na Ufufuko wa Mwokozi Yesu Kristo. Kumbuka wanafunzi Wake wawili wenye shaka wakiwa njiani kwenda Emau. Bwana aliyefufuka alisogea karibu nao na kuwauliza kwa nini walikuwa na huzuni. Luka anatupatia jibu:

“Wakamwambia, Mambo ya Yesu wa Nazareti, aliyekuwa mtu nabii, mwenye uwezo katika kutenda na kunena mbele za Mungu na watu wote:

“Tena jinsi wakuu wa makuhani na wakubwa wetu walivyomtia katika hukumu ya kufa, wakamsulibisha.

“Nasi tulikuwa tukitumaini ya kuwa yeye ndiye atakayewakomboa Israeli” (Luka 24:19–21).

Tunapata faraja kutoka kwenye ufahamu na ushuhuda wetu kwamba Alikuwa Yeye aliyeikomboa Israeli. Alikuwa Yeye ambaye “[alikata] kamba za kifo” (Mosia 15:23). Alikuwa Yeye aliyekuwa “limbuko lao waliolala” (1 Wakorintho 15:20). Alikuwa Yeye aliyefanya maagano ya hekaluni yawezekane ambayo yanatuunganisha milele na wale “tuliowapenda tangu mwanzo, na tuliowapoteza muda mfupi!”1

Katika msimu huu wa Pasaka, ningependa kushiriki sehemu ya ujumbe wa mkutano wa ibada nilioutoa miaka kadhaa iliyopita kuhusu nguvu ya Mwokozi ya ukombozi. Umeniimarisha nilipouandaa na kuutoa. Ninaomba kwamba utawaimarisha ninyi pale mnapousoma.

Maisha hufika kikomo mapema kwa baadhi na hatimaye kwetu sote. Kila mmoja wetu atajaribiwa kwa kukabiliwa na kifo cha mtu tunayempenda.

Siku moja nilikutana na mwanaume ambaye nilikuwa sijamwona toka mke wake alipofariki. Ilikuwa ni nafasi kukutana katika hali ya mapumziko ya kupendeza. Alikuwa akitabasamu aliponikaribia. Nikikumbuka kifo cha mke wake, nilitoa salamu yangu ya kawaida kwa umakini: “Unaendeleaje?”

Tabasamu lilipotea, macho yake yakawa na majimaji, na akasema kwa utulivu, kwa ari kubwa, “naendelea vizuri. Lakini ni vigumu sana.”

Ni vigumu sana, kama wengi wenu mlivyojifunza na sisi sote tutakavyojua wakati mwingine. Sehemu ngumu ya jaribu hilo ni kujua nini cha kufanya kwenye huzuni, upweke, na kupoteza ambako tunaweza kuhisi kana kwamba sehemu yetu imeondolewa. Huzuni unaweza kuendelea kama maumivu ya muda mrefu. Na kwa baadhi, kunaweza kuweko hisia za hasira na kukosekana kwa haki.

Mwokozi anafahamu Huzuni Wetu

Upatanisho na Ufufuko wa Mwokozi unampa Yeye nguvu za kutukomboa katika jaribu kama hilo. Kupitia uzoefu Wake, Yeye anaweza kujua huzuni wetu wote. Angeweza kuujua kwa msukumo wa Roho, lakini badala yake Yeye alichagua kuujua kwa kuupitia Yeye mwenyewe. Haya ndiyo maneno:

“Na tazama, atazaliwa na Mariamu, huko Yerusalemu ambayo ni nchi ya babu zetu, yeye akiwa bikira, chombo cha thamani na kilichochaguliwa, ambaye atawezeshwa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu kupata mimba, na kumzaa mwana, ndio, hata Mwana wa Mungu.

“Na atakwenda, na kuteseka maumivu na masumbuko na majaribio ya kila aina; na hii kwamba neno litimizwe ambalo linasema atabeba maumivu na magonjwa ya watu wake.

“Na atajichukulia kifo, ili afungue kamba za kifo ambazo zinafunga watu wake; na atajichukulia unyonge wao, ili moyo wake ujae rehema, kulingana na mwili, ili ajue kulingana na mwili jinsi ya kuwasaidia watu wake kulingana na unyonge wao” (Alma 7:10–12).

Picha
Jesus Christ praying

UTONDOTI KUTOKA KWA SALA YA BWANA, NA YONGSUNG KIM, KWA HISANI YA HAVEN LIGHT

Watu wema wanaokuzunguka watajaribu kuelewa huzuni wako wakati wa kifo cha mpendwa wako. Wanaweza kuhisi huzuni wao wenyewe. Mwokozi haelewi tu huzuni bali pia anahisi huzuni wako binafsi ambao wewe pekee unahisi. Na anakujua kikamilifu. Anajua moyo wako.

Mwalike Roho Mtakatifu

Mwokozi anaweza kujua yapi kati ya mambo mengi unayoweza kufanya ambayo yatakuwa bora kwako unapomwalika Roho Mtakatifu kukufariji na kukubariki. Yeye atajua wapi ni pazuri kwako kuanzia. Wakati mwingine itakuwa ni kuomba. Wakati mwingine itakuwa kwenda kumfariji mtu mwingine. Ninafahamu kuhusu mjane aliyekuwa na ugonjwa wa kudhoofisha aliyepata msukumo wa kiungu wa kumtembelea mjane mwingine. Sikuwepo pale, lakini nina hakika kwamba Bwana alimpa msukumo mfuasi mwaminifu kumfikia mwingine na hivyo aliweza kuwasaidia wote.

Kuna njia nyingi Mwokozi anaweza kuwasaidia wale wanaohuzunika, kila moja ikiwa yenye kufaa kwao. Lakini unaweza kuwa na uhakika kwamba Yeye anaweza na atafanya katika njia ambayo ni bora sana kwa wale wanaohuzunika na wale wanaowazunguka. Kitu kimoja kisichobadilika pale Mungu anapowakomboa watu kutokana na huzuni ni kwamba wanahisi unyenyekevu kama wa watoto mbele Zake. Mfano mkuu wa nguvu ya unyenyekevu wa uaminifu huja kutoka kwenye maisha ya Ayubu (ona Ayubu 1:20–21). Kisichobadilika kingine, ambacho Ayubu pia alikuwa nacho, ni imani ya kudumu katika nguvu ya Ufufuo ya Mwokozi (ona Ayubu 19:26).

Sote tutafufuka, ikijumuisha wapendwa wako waliokufa. Kuunganika huku tena pamoja nao hakutakuwa kwa muda mfupi bali kwa miili ambayo haitakufa kamwe wala kuwa dhaifu.

Wakati Mwokozi alipowatokea Mitume Wake baada ya Ufufuko, Yeye hakuwaondolea tu hofu katika huzuni yao bali pia sisi sote ambao tungeweza kuhuzunika. Aliwaondolea hofu wao na sisi kwa njia hii:

“Amani iwe kwenu. …

“Tazameni mikono yangu na miguu yangu, ya kuwa ni mimi mwenyewe: nishikenishikeni, mwone; kwa kuwa roho haina mwili na mifupa, kama mnavyoniona mimi kuwa nayo” (Luka 24:36, 39).

Bwana anaweza kutupatia msukumo wa kiungu kuifikia nguvu ya ukombozi kutoka kwenye huzuni katika njia ambayo inatufaa zaidi. Tunaweza kuchagua kuwahudumia wengine kwa ajili ya Bwana. Tunaweza kushuhudia juu ya Mwokozi, juu ya injili Yake, juu ya urejesho wa Kanisa Lake, na juu ya Ufufuo Wake. Tunaweza kutii amri Zake.

Yote kati ya chaguzi hizo humwalika Roho Mtakatifu. Ni Roho Mtakatifu anayeweza kutufariji katika njia inayokidhi hitaji letu. Na kwa msukumo wa Roho, tunaweza kuwa na ushuhuda wa Ufufuo na uoni wa wazi wa muunganiko mtakatifu mbeleni. Nilihisi faraja hiyo pale nilipoangalia chini kwenye jiwe la kaburi la mtu niliyemfahamu—mtu ninayefahamu kwamba ninaweza hapo baadaye kumkumbatia katika mikono yangu. Kujua hilo, siyo tu nilikombolewa kutoka kwenye huzuni bali pia kujazwa na tumaini la furaha.

Kama mtu yule mdogo angeishi kuwa mkubwa, angehitaji ukombozi katika aina nyingine ya majaribu. Angejaribiwa kubaki mwaminifu kwa Mungu kupitia changamoto za kimwili na kiroho ambazo huja kwa kila mtu. Japokuwa mwili ni uumbaji unaovutia, kuufanya uweze kutenda ni changamoto ambayo hutujaribu sote. Kila mtu lazima ahangaike kupitia ugonjwa na matokeo ya kuzeeka.

“Kuwa Mnyenyekevu”

Nguvu ya ukombozi kutokana na majaribu yetu ipo. Inafanya kazi kwa njia sawa kama ukombozi kutoka kwenye jaribu katika kukabiliana na kifo cha mpendwa wetu. Kama ukombozi ulivyo si mara zote kuwa uhai wa wapendwa wetu utalindwa, ukombozi wa kutoka majaribu mengine si kuwa utayaondoa. Bwana anaweza asitoe unafuu mpaka tuonyeshe imani kwenye kufanya chaguzi ambazo zitaleta nguvu ya Upatanisho kufanya kazi katika maisha yetu. Yeye haitaji hilo kwa sababu hajali bali kwa sababu ya upendo kwetu.

Mwongozo wa kupokea nguvu ya Bwana ya ukombozi kutokana na upinzani katika maisha ulitolewa kwa Thomas B. Marsh, wakati huo akiwa Rais wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili. Alikuwa katika majaribu magumu, na Bwana alijua angepata mengi zaidi. Hapa ni ushauri kwake ambao ninauchukua kwa ajili yangu na ninautoa kwenu: “Jinyenyekeze; na Bwana Mungu wako atakuongoza kwa mkono, na kukupa jibu la sala zako” (Mafundisho na Maagano 112:10).

Picha
Christ with lamb

UTONDOTI KUTOKA KWA MWANAKONDOO ALIYEPOTEA, NA YONGSUNG KIM, KWA HISANI YA HAVEN LIGHT

Mwokozi daima anataka kutuongoza kwenye ukombozi kupitia sisi kuwa wenye haki zaidi. Hilo linahitaji toba. Na hilo linachukua unyenyekevu. Hivyo njia ya ukombozi daima inahitaji unyenyekevu ili kwamba Bwana aweze kutuongoza kwa mkono pale ambapo Yeye anataka kutupeleka kupitia matatizo yetu na kwenye utakaso.

Majaribu yanaweza kuzaa uchungu au kuvunjika moyo. Unyenyekevu mimi na wewe tunaohitaji kwa ajili ya Bwana kutuongoza kwa mkono huja kutokana na imani. Huja kutokana na imani kwamba Mungu kweli anaishi, kwamba Yeye anatupenda, na kwamba kile Yeye anachohitaji—kigumu kadri kitakavyokuwa—kitakuwa daima bora kwetu.

Mwokozi alituonyesha unyenyekevu huo. Mmesoma jinsi Alivyoomba katika Bustani ya Gethsemane wakati alipoteseka kwa jaribu kwa niaba yetu kupita uwezo wetu wa kufikiri au kuvumilia, au hata kwangu kuelezea. Mnakumbuka ombi Lake: “Baba, ikiwa ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki: walakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke” (Luka 22:42).

Alimfahamu na kumwamini Baba Yake wa Mbinguni, Elohimu mkuu. Alifahamu kwamba Baba Yake alikuwa na nguvu zote na ukarimu usio na mwisho. Mwana Mpendwa aliomba kwa maneno ya unyenyekevu—kama yale ya mtoto mdogo—kwa nguvu ya ukombozi kumsaidia.

Chukua Ujasiri na Faraja

Baba hakumkomboa Mwana kwa kuondoa jaribu. Kwa ajili yetu Hakufanya hivyo, bali alimruhusu Mwokozi kumaliza kazi aliyokuja kutimiza. Bado daima tunaweza kuchukua ujasiri na faraja kutokana na kufahamu usaidizi ambao Baba alitoa:

“Malaika kutoka mbinguni akamtokea akamtia nguvu.

“Naye kwa vile alivyokuwa katika dhiki akazidi sana kuomba: hari yake ikawa kama matone ya damu yakidondoka nchini.

“Alipoondoka katika kuomba kwake, akawajia wanafunzi wake, akawakuta wamelala usingizi kwa huzuni,

“Akawaambia, Mbona mmelala usingizi? Ondokeni, mkaombe, msije mkaingia majaribuni” (Luka 22:43–46).

Mwokozi aliomba kwa ajili ya ukombozi. Kile Alichopewa hakikuwa kukimbia kutoka kwenye jaribu bali faraja ya kutosha kulishinda kwa shangwe.

Amri Yake kwa wanafunzi Wake, ambao wao wenyewe walikuwa wakijaribiwa, ni mwongozo kwetu. Tunaweza kuamua kuufuata. Tunaweza kuamua kunyanyuka na kuomba kwa imani na unyenyekevu mkubwa. Na tunaweza kufuata amri iliyoongezwa katika kitabu cha Marko: “Ondokeni, Twendeni zetu” (Marko 14:42).

Kutoka kwenye hili, una ushauri wa kushinda majaribu ya kimwili na kiroho ya maisha. Utahitaji msaada wa Mungu baada ya kufanya yote unayoweza wewe mwenyewe. Hivyo ondoka na uende, lakini pata msaada Wake mapema kadiri uwezavyo, siyo kusubiri hali ya hatari ili kuomba ukombozi.

Ninawapa ushahidi wangu wa dhati kwamba Mungu Baba anaishi na anatupenda. Ninajua hilo. Mpango Wake wa furaha ni mkamilifu, na ni mpango wa furaha. Yesu Kristo alifufuka, kama sisi tutakavyofufuka. Aliteseka ili kwamba Yeye aweze kutusaidia katika majaribu yetu yote. Alilipa deni kwa ajili ya dhambi zetu zote na za Watoto wote wa Baba wa Mbinguni ili kwamba tungeweza kukombolewa kutokana na kifo na dhambi.

Ninajua kwamba katika Kanisa la Yesu Kristo, Roho Mtakatifu anaweza kuja kutufariji na kutusafisha pale tunapomfuata Bwana. Hebu na mpokee faraja Yake na usaidizi katika wakati wenu wa uhitaji, kupitia majaribu yote na taabu za maisha yenu.

Muhtasari

  1. “Lead, Kindly Light,” Nyimbo za Kanisa, no. 97.