2019
Kufanya Kuhudumu kuwe kwa Shangwe
Aprili 2019


Kanuni za Kuhudumu

Kufanya Kuhudumu kuwe Shangwe

Kuhudumu kwa upendo huleta shangwe kwa wote mtoaji na mpokeaji.

Picha
Jesus with the leper

MKOMA ALIYESEMA ASANTE, NA JOHN STEEL

Wakati mwingine utafutaji wetu wa furaha katika maisha haya unaweza kuonekana kama kukimbia juu ya kifaa cha mazoezi ya kukimbia. Tunakimbia na kukimbia na bado tunahisi kama hatukufika kokote. Kwa baadhi, wazo la kuwahudumia wengine kiurahisi huonekana nyongeza zaidi ya mambo ya kufanya.

Lakini Baba yetu wa Mbinguni anataka tupate uzoefu wa shangwe na ametuambia “wanadamu wapo, ili wapate shangwe” (2 Nefi 2:25). Na Mwokozi alifundisha kwamba kuwahudumia wengine ni sehemu muhimu ya jinsi tunavyoleta shangwe katika maisha yetu na katika maisha ya wengine.

Shangwe Ni Nini?

Shangwe imetolewa maana kama “hisia ya kuridhika kwa hali ya juu na furaha.”1 Manabii wa siku za mwisho wametoa ufafanuzi juu ya wapi shangwe inatoka na jinsi inavyopatikana. “Shangwe tunayohisi inahusiana kidogo sana na hali za maisha yetu na inahusiana kwa kila kitu na fokasi ya maisha yetu,” alisema Rais Russell M. Nelson. “… Shangwe huja kutoka kwa na kwa sababu ya [Yesu Kristo]. Yeye Ndiye kiini cha shangwe yote.”2

Kuhudumu kunaleta shangwe

Wakati Lehi alipokula tunda la mti wa uzima, nafsi yake ilijawa na “shangwe tele” (1 Nefi 8:12). Tamanio lake la kwanza lilikuwa ni kushiriki tunda hili pamoja na wale aliowapenda.

Utayari wetu wa kuwahudumia wengine unaweza kuleta aina hii ya shangwe kwetu na kwao. Mwokozi aliwafundisha wafuasi Wake kwamba matunda tunayoleta wakati tumeunganishwa Naye husaidia kutuletea utimilifu wa shangwe (ona Yohana 15:1–11). Kufanya kazi Yake kwa kuhudumia na kutafuta kuwaleta wengine Kwake kunaweza kuwa uzoefu wenye shangwe (ona Luka 15:7; Alma 29:9; Mafundisho na Maagano 18:16; 50:22). Tunaweza kupata uzoefu wa shangwe hii hata mbele ya upinzani na maumivu (ona 2 Wakorintho 7:4; Wakolosai 1:11).

Mwokozi alituonyesha mfano mkamilifu kwamba moja ya kiini kikuu cha shangwe ya kweli katika maisha ya duniani hupatikana kupitia huduma. Tunapowahudumia kaka na dada zetu kama Mwokozi, kwa hisani na upendo katika mioyo yetu, tunaweza kupata uzoefu wa shangwe ambayo inaenda zaidi ya furaha tu.

“Tunapokumbatia [kuhudumu] kwa moyo wa utayari, tuta … karibia kuwa watu wa Sayuni na kuhisi shangwe isiyo kifani na wale ambao tumewasaidia katika njia ya ufuasi,” alifundisha Dada Jean B. Bingham, Rais Mkuu wa Muungano wa Usaidizi wa Akina Mama.3

Tunawezaje Kufanya Kuhudumu Kuwe Shangwe Zaidi?

Kuna njia nyingi za kuleta shangwe tele katika kuhudumu kwetu. Hapa kuna mawazo machache:

  1. Elewa lengo lako katika kuhudumu. Kuna sababu nyingi za kuhudumu. Hatimaye, juhudi zetu zinapaswa kuwa sambamba na malengo ya Mungu “kuleta kutokufa na uzima wa milele wa mwanadamu” (Musa 1:39). Tunapokubali mwaliko wa Rais Russell M. Nelson wa kuwasaidia wengine katika njia ya agano, tunaweza kupata shangwe katika kushiriki kwenye kazi ya Mungu.4 (Kwa mengi juu ya lengo la kuhudumu, ona “Kanuni za Kuhudumu: Lengo Litakalobadilisha Kuhudumu Kwetu,” katika Liahona ya Januari 2019.)

  2. Fanya kuhudumu kuwahusu watu siyo majukumu. Rais Thomas S. Monson mara nyingi alitukumbusha “Kamwe usiruhusu shida ya kutatuliwa kuwa muhimu zaidi ya mtu anayepaswa kupendwa.”5 Kuhudumu kunahusu kuwapenda watu, siyo kuhusu mambo ya kufanya. Tunapoongezeka kwenye kupenda kama Mwokozi alivyopenda, tutakuwa wenye kuchanua zaidi kwenye shangwe ambayo huja kutokana na kuwatumikia wengine.

  3. Fanya kuhudumu kuwe rahisi Rais M. Russell Ballard, Kaimu Rais wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, anatuambia: “mambo makuu huletwa kupitia vitu vidogo na rahisi. … Matendo yetu madogo na rahisi ya ukarimu na huduma yataongeza kwenye maisha yaliyojawa na upendo kwa Baba wa Mbinguni, kujitoa kwenye kazi ya Bwana Yesu Kristo, na hisia za amani na shangwe kila mara tunapomfikia kila mmoja.6

  4. Ondoa msongo kwenye kuhudumu. Siyo jukumu lako kutafuta wokovu wa mtu fulani. Hiyo ni kati ya mtu yule na Bwana. Jukumu letu ni kuwapenda na kuwasaidia kumgeukia Yesu Kristo, ambaye ni Mwokozi wao.

Picha
Jesus with children

KRISTO NA WATOTO KATIKA KITABU CHA MORMONI. NA DEL PARSON

Usicheleweshe Shangwe ya Kuhudumu

Wakati mwingine watu wanasita kuomba msaada unaohitajika, hivyo kutoa huduma yetu kunaweza kuwa hasa kile walichohitaji. Lakini kujilazimisha kwa watu siyo jibu, vilevile. Kuomba ruhusa kabla ya kuhudumu ni wazo zuri.

Mzee Dieter F. Uchtdorf wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili alisimulia kuhusu mama mseja aliyepata tetekuwanga—na kisha watoto wake kuugua pia. Nyumba ambayo kwa kawaida ilikuwa safi ikawa na mparaganyiko na chafu. Vyombo na nguo chafu zikawa nyingi.

Katika wakati ambapo alihisi kuzidiwa kabisa, akina dada wa Muungano wa Usaidizi wa Akina Mama walibisha kwenye mlango wake. Hawakusema, “Tujulishe kama tunaweza kusaidia.” Walipoiona hali, waliharakisha kwenye kutenda.

“Walisafisha nyumba, wakaleta mwangaza na uwazi nyumbani, na wakamwita rafiki alete chakula kilichohitajika sana. Wakati hatimaye walipomaliza kazi yao na kusema kwaheri, walimwacha mama yule kijana akiwa analia—machozi ya shukrani na upendo.”7

Wote watoaji na wapokeaji walihisi mwako wa shangwe.

Kuza Shangwe katika Maisha Yako

Kadiri zaidi tunavyokuza shangwe, amani, na kuridhika katika maisha yetu, ndivyo zaidi tutaweza kushiriki na wengine pale tunapohudumu. Shangwe huja kupitia Roho Mtakatifu (ona Wagalatia 5:22 na Mafundisho na Maagano 11:13). Ni kitu ambacho tunaweza kukiomba (ona Mafundisho na Maagano 136:29) na kukialika katika maisha yetu. Hapa kuna mawazo machache kwa ajili ya kukuza shangwe katika maisha yetu wenyewe:

  1. Hesabu baraka zako. Unapotathmini maisha yako, andika katika shajara yako mambo ambayo Mungu amekubariki nayo.8 Gundua mazuri yanayokuzunguka kote.9 Kuwa makini kwenye kile kinachoweza kuwa kinakuzuia kuhisi shangwe na andika njia za kukitatua au kuvielewa vizuri zaidi. Wakati wa msimu huu wa Pasaka, tenga muda wa kutafuta muunganiko mkubwa zaidi na Mwokozi (ona Mafundisho na Maagano 101:36).

  2. Fanyia mazoezi kujali. Shangwe inaweza kukupata kiurahisi zaidi katika nyakati tulivu za tafakuri.10 Sikiliza kwa makini kile kinachokuletea shangwe (ona 1 Mambo ya Nyakati 16:15). Kukaa mbali na vyombo vya habari wakati mwingine kunaweza kuwa muhimu ili kufanyia mazoezi kujali.11

  3. Epuka kujilinganisha. Imesemwa kwamba ulinganishaji ni mwizi wa shangwe. Paulo alionya kwamba wale “wanaojipima nafsi zao na nafsi zao, na wakijilinganisha nafsi zao na nafsi zao, hawana akili” (2 Wakorintho 10:12).

  4. Tafuta ufunuo binafsi. Mwokozi alifundisha: “Ikiwa utaomba, nawe utapokea ufunuo juu ya ufunuo, maarifa juu ya maarifa, ili uweze kujua siri na mambo ya amani—yale ambayo huleta shangwe, yale ambayo huleta uzima wa milele” (Mafundisho na Maagano 42:61).

Mwaliko wa Kutenda

Ni kwa jinsi gani unaweza kuongeza shangwe unayopata katika maisha yako kupitia kuhudumu?

Muhtasari

  1. “Shangwe,” en.oxforddictionaries.com

  2. Russell M. Nelson, “Shangwe na Kunusurika Kiroho,” Liahona, Nov. 2016, 82.

  3. Jean B. Bingham, “Kuhudumu Kama Mwokozi Anavyofanya,” Liahona, Mei 2018,106.

  4. Ona Russell M. Nelson, “Tunaposonga Mbele Pamoja,” Liahona, Aprili 2018, 4–7.

  5. Thomas S. Monson, “Kupata Shangwe katika Safari,” Liahona, Nov. 2008, 86.

  6. M. Russell Ballard, “Kupata Shangwe kupitia Huduma ya Upendo,” Liahona, Mei 2011, 49.

  7. Dieter F. Uchtdorf, “Kuishi Injili kwa Shangwe,” Liahona, Nov. 2014,120–123.

  8. Ona Henry B. Eyring, “Ee Kumbuka, Kumbuka,” Liahona, Nov. 2007, 67.

  9. Jean B. Bingham, “Kwamba Shangwe Yenu Iwe Timilifu,” Liahona, Nov. 2017, 87.

  10. Ona Dieter F. Uchtdorf, “Kwa Vitu Vyenye Umuhimu Zaidi,” Liahona, Nov. 2010, 21.

  11. Ona Gary E. Stevenson, “Kupatwa Kiroho,” Liahona, Nov. 2017, 46.