2019
Kujihisi Mpya
Aprili 2019


Kujihisi Mpya

Mwandishi anaishi Texas, Marekani.

Estonia

Picha
Feeling New

“Nina jambo la kustaajabisha!” Ema (Mama) alisema wakati alipomchukua Rasmus kutoka shule. Walitembea pamoja kwenye mitaa yenye majengo yenye rangi nzuri yaliyo kwenye mstari.

Rosolje kwa ajili ya chakula cha usiku?” Rasmus alibashiri kwa matumaini. Walikuwa wameila wiki iliyopita kwenye mwaka wake wa saba wa kuzaliwa. Lakini mara zote angeweza kula kachumbari nyingi ya kiazi sukari na mbatata pamoja na samaki wa maji chumvi aliyetengenezwa kwa achali!

Ema alitikisa kichwa kwa tabasamu. “Nilikutana na wasichana wawili kwenye basi asubuhi ya leo. Wamisionari. Wanakuja kutembelea usiku huu kuzungumza kuhusu Kanisa lao.

Rasmus alitazama juu kwa udadisi. Hakuwahi kukutana na wamisionari kabla.

Alikuwa chumbani kwake akicheza na kigari chake wakati wamisionari walipokuja. “Tere! Tere! Habari!” walimsalimia Ema pale walipoelekea ndani. Walivua buti zao nzito na kuvaa malapa ya ndani ambayo Ema alitunza kwa ajili ya wageni. Ema aliwaongoza kwenye kochi la rangi ya machungwa. Lakini Rasmus alibaki nyuma mlangoni.

Mwanamke mrefu alimuona na kutabasamu. Beji yake nyeusi ilisema Õde Craig (Dada Craig). “Mama yako alituambia ulikuwa na siku ya kuzaliwa,” alisema. “Tumekuletea kitu.” Alitoa kadi ndogo. Rasmus aliingalia kwa karibu.

Ilikuwa picha ya mwanaume. Alikuwa amevaa joho jeupe, na mikono yake imenyooshwa.

“Unajua huyo ni nani?” Õde Craig aliuliza.

Rasmus hakujua jina la mwanaume yule. Hakuwahi kuona picha hii awali. Lakini mwanaume yule alionekana mkarimu na mwenye nguvu. “Nadhani ni mfalme!” Ramus alisema.

Wamisionari wote wawili walitabasamu. “Ndiyo, Yeye ni mfalme! Yeye ni Mfalme wa Wafalme! Jina lake ni Yesu Kristo.” Õde Craig alitoa kitabu chenye jalada la samawati. “Na hiki ni kitabu kinachofundisha kuhusu Yeye, Mormoni Raamat. Kitabu cha Mormoni.”

Yeye na Ema walianza kusoma Kitabu cha Mormoni kila siku kabla hajaenda shule. Wakati wa shule, Rasmus na darasa lake walifanya matembezi ya kufurahia asili na kulala usingizi kidogo. Baada ya shule, yeye na Ema mara nyingi walikutana na wamisionari. Walizungumza na wamisionari kuhusu kile walichosoma kwenye Kitabu cha Mormoni. Wakati mwingine Ema alitupatia kila mtu chakula kringel, mkate wa kusokota wa mdalasini. Mwisho wa wiki yeye na Ema waliendesha baiskeli au kuwa na mandari ufukoni. Wakati mwingine walifanya matembezi marefu msituni au pembeni mwa mto walioupenda sana.

Kwenye moja ya matembezi hayo ya msituni, Ema alimwambia kwamba alitaka kubatizwa. Rasmus alitabasamu. Wamisionari walikuwa wamuomba Ema kuomba kuhusu ikiwa abatizwe au la. Ilionekana kama vile alikuwa amepata jibu lake!

“Na ninajua wapi nitabatizwa,” alisema kwa tabasamu. “Unaweza kubahatisha?”

Rasmus aliwaza kuhusu somo la wamisionari kuhusu ubatizo. Walikuwa wameonyesha picha ikimwonyesha Yesu Kristo pamoja na Yohana Mbatizaji ndani ya mto. …

“Mto!” alitamka ghafla kwa mshangao. “Mto wetu tunaoupenda sana.”

Wiki moja baadaye, Rasmus alisimama kwenye ukingo wa mto pamoja na wamisionari na baadhi ya watu wengine kutoka kanisani. Ema alikuwa tayari kubatizwa. Alikwenda chini kabisa ya maji, kama vile Yesu alivyofanya. Alipotoka juu, alikuwa akitabasamu. Rasmus alitaka kukumbuka wakati huu siku zote—maji yenye rangi ya samawati, maua meupe ya kondeni ndani ya nyasi za kijani, na tabasamu la mama yake.

“Kubatizwa kuna hisia gani?” aliuliza baadae, wakati kila mmoja alipokuwa akila biskuti wamisionari walizoleta.

“Ya kupendeza,” alimwambia. “Nilitaka kubaki ndani ya maji siku zote. Najihisi Mpya kabisa!” Alimkumbatia kwa nguvu.

“Kwa ajili ya siku yangu ya kuzaliwa itakayofuata, ninataka kubatizwa, kama vile wewe na Yesu,” alimwambia. “Nataka kuwa mpya pia!” ●