2019
Koti Lililopotea
Aprili 2019


Koti Lililopotea

Mwandishi anaishi lowa, Marekani.

“Mimi, Bwana, nitamsamehe yule nitakaye kumsamehe, lakini ninyi mnatakiwa kuwasamehe watu wote” (Mafundisho na Maagano 64:10).

Picha
The Missing Coat

“Mama koti langu halipo!” Brad alisema. Ilikuwa ni muda wa kwenda nyumbani kutoka kanisani, lakini Brad hakuliona koti lake juu ya chanja.

“Una uhakika hapo ndipo ulipolitundika?” Mama aliuliza.

“Ndiyo. Lilikuwa hapo hapo.” Koti la Brad lilikuwa rangi iliyong’aa ya samawati na nyekundu. Ilikuwa ni vigumu kulikosa.

“Labda lilihamishwa. Acha tuangalie kuzunguka jengo,” Baba alisema.

Mama, Baba, na Brad walitawanyika kuangalia kwenye vyumba tofauti. Walitafuta kwenye kisanduku cha vitu vilivyopotea na kupatikana, ndani ya chumba cha ibada, ndani ya chumba cha Brad cha Shule ya Jumapili, ndani ya chumba cha msingi, na juu ya kila chanja ya koti. Walitafuta hadi maliwatoni, lakini hawakulipata koti.

“Labda mtu amelichukua kwa bahati mbaya. Nina uhakika watalirudisha wiki ijayo mara tu watakapogundua siyo la kwao,” Baba alisema.

“Kwa sasa, unaweza kuvaa koti lako la zamani,” Mama alisema.

Brad alichukia. Hakupenda koti lake la zamani. Lilikuwa jembamba, limepauka, na dogo sana kwake. Alipenda jinsi koti lake jipya la samawati na nyekundu lilivyomfanya aonekane kama shujaa mkubwa.

“Pengine mtu aliona koti langu lilivyo zuri na kuliiba,” Brad aliwaza. Hilo lingewezaje kutokea kanisani? Kila mmoja pale alipaswa kuwa mwaminifu. Brad asingeweza kumwacha mwizi yule apotee nalo. Alikuwa na mpango. Jumapili ijayo, angetazama kwa makini kuona nani alikuwa amevaa koti lake. Kisha angelikwapua kwa nyuma na kupiga kelele, “Simama, mwizi!” Wangejuta kwa nini walilichukua.

Brad alipata shida kuisubiri Jumapili ili kutimiza mpango wake. Lakini Jumapili iliyofuata ilikuwa na joto sana kwa watu kuvaa makoti, kadhalika na Jumapili iliyofuatia.

Jumapili baada ya hiyo, Brad aliwaangalia kwa mashaka wavulana katika darasa la msingi, akijiuliza nani aliiba koti lake. Je, ni yule mvulana mrefu? Au pengine alikuwa ni msichana. Alihisi kama hakuweza kumwamini yeyote. Brad hakupenda hisia ile.

Baada ya ibada Brad aliharakisha kuzunguka jengo, akitazama familia zikivaa makoti yao. Lakini hakuona koti lake popote. Aliangalia hata kwenye sanduku la vitu vilivyopotea na kupatikana … lakini hakukuwa na koti. Litakuwa wapi?

Njiani kurudi nyumbani, Brad alifikiria mpango mpya. Angesali. Alijua Baba wa Mbinguni angeweza kupata vitu vilivyopotea. Usiku ule Brad aliomba na kusema, “Baba wa Mbinguni, tafadhali niambie nani alichukua koti langu. Nalitaka.”

Brad alisubiria jina au sura ya mwizi kuja akilini. Lakini badala yake alianza kumfikiria rafiki yake Carl. Brad mara nyingi alikaa karibu na Carl katika darasa la Msingi. Walitaniana na kucheka pamoja mara nyingi. Lakini Carl hakuwepo kanisani kwa wiki kadhaa. Brad alimkosa.

Vipi kama Carl alikuwa amechukua koti lake? Pengine Carl aliogopa kuja kanisani sasa kwa sababu alidhani Brad asingekuwa rafiki yake tena. Brad alitaka Carl aje kanisani tena. Ikiwa Carl alikuwa amechukua koti lake, Brad aliamua, asingempigia kelele. Angemsamehe.

Brad alipanda kitandani, akijiskia vizuri.

Jumapili iliyofuata katika darasa la Msingi, Carl hakuwepo, lakini mvulana mgeni alikuwepo. Alikuwa amevalia tai yenye mistari myekundu na samawati.

“Tai nzuri,” Brad alisema, akiketi karibu na mvulana mgeni. “Inakufanya uonekane kama shujaa mkubwa.”

Mvulana alitabasamu.

Brad alitabasamu pia. Hakuwa akiwatafuta wezi tena. Alikuwa akitafuta marafiki.●