2020
Kutambua Unyanyasaji wa Kihisia
Oktoba 2020


Kidijitali Pekee

Kutambua Unyanyasaji wa Kihisia

“Mume wangu si mnyanyasaji. Ananifokea na kuniita majina, lakini huo si unyanyasaji, sivyo?”

Tunajua kuwa “Bwana analaani tabia mbaya ya unyanyasaji katika hali yoyote ile.”1 Na aina kadhaa za unyanyasaji, kama vile unyanyasaji wa kimwili, ni rahisi kuuona, lakini unyanyasaji wa kihisia unaweza kuwa vigumu kuuona. Uharibifu unaweza kusababisha mkanganyiko, hofu, aibu, kutokuwa na tumaini, na hisia za kutokuwa na thamani.

Unyanyasaji wa kihisia ni jaribio la mtu mmoja kuondoa haki ya kujiamulia ya mtu mwingine na kupata udhibiti juu yao kwa maneno au tabia ambazo hutawala hisia au chaguzi. Unyanyasaji wa kihisia unaweza kutokea katika uhusiano wa aina yoyote: kati ya wenza wa ndoa, kati ya wazazi na watoto, katika urafiki, katika mahusiano ya miadi, au kati ya wafanyakazi wenza.

Baadhi ya Mifano ya Unyanyasaji wa Kijinsia Ni Ipi?

Kujua dalili za unyanyasaji wa kihisia kunaweza kukusaidia kujikinga wewe na wapendwa wako. Baadhi ya tabia za unyanyasaji ni pamoja na:

  • Kukuita majina au kukurejelea kwa njia za kudhoofisha.

  • Kukuaibisha hadharani.

  • Kukosoa na kushusha thamani mafanikio yako na kile unachofanya.

  • Kukulaumu wewe kwa matendo yao na kutokuwajibika.

  • Kukufanya uhisi kuwa na hatia ili ufanye jambo kwa ajili yao kwa sababu walifanya jambo kwa ajili yako.

  • Kukutenga kutoka kwa wengine na kudhibiti jinsi unavyotumia muda wako.

  • Kutoa vitisho ikiwa hutafanya kwa njia fulani au kufanya vitu fulani.

  • Kuzuia mapenzi mpaka uwafanyie mambo fulani.

  • Kukutawala kiroho kwa kutumia imani za kidini ili kukudhibiti.

Ninawezaje Kutambua Unyanyasaji wa Kihisia?

Ni muhimu pia kuwa na ufahamu wa tabia za unyanyasaji na dalili zako za ndani za tahadhari. Ifuatayo ni baadhi ya mitindo ya mawazo na maamuzi ya kawaida ambayo yanaweza kukuweka katika uhusiano wa unyanyasaji wa kihisia:

  1. Kusamehe tabia ya mnyanyasaji wako:

  2. Kuhalalisha tabia ya mnyanyasaji: “Yeye kwa kawaida asingefanya hivi—yuko chini ya shinikizo kubwa hivi sasa.”

  3. Kupunguza tabia: “Haikuwa kubwa sana.”

  4. Kujilaumu mwenyewe kwa tabia zao: “Laiti ningekuwa na chakula cha jioni tayari kwa wakati, asingekasirika na kunifokea.”

  5. Kupuuza kutokuwa huru kihisia. Kwa kuanza, kama wewe ni muathiriwa wa unyanyasaji wa kihisia, unaweza kutaka kumuepuka mkosaji kwa sababu unahisi kutokuwa huru au vibaya kwako mwenyewe pale wanapokuwa karibu. Ili kulinda uhusiano, unaweza kupuuza hisia hizi za kutokuwa huru. Kadiri ya muda, kutokuwa huru huko kunaweza kutoweka kama matokeo ya kujiweka kwenye tabia yao.

  6. Kutumia imani za kidini kuhalalisha hali. Hii ni ya kawaida sana katika jamii yetu, ikiwa ni pamoja na hata washiriki wa Kanisa. Mtu anayenyanyaswa anaweza kufikiria kitu kama hiki: “Bwana alituamuru tusamehe. Ninafanya dhambi ikiwa sitasamehe.” Kusamehe ni amri. Lakini, kama Mzee Jeffrey R. Holland alivyofundisha kuhusu Mwokozi, “Yeye hakusema kwamba, ‘Hauruhusiwi kuhisi uchungu wa kweli au huzuni halisi kutokana na uzoefu wa kukasirisha uliowahi kuupata kwenye mkono wa mwingine.’ Wala Yeye hakusema, ‘Ili kusamehe kikamilifu, unapaswa kuingia tena kwenye uhusiano wa kudhuru au kurejea tena hali ya unyanyasaji, ya kuangamiza.’”2

  7. Kupuuza mahitaji yako mwenyewe. Unakidhi mahitaji ya wengine kwa gharama ya kujitunza mwenyewe. Kwa mfano, kuteseka maumivu ya kihisia ili kuzuia kuumiza hisia za mtu au kutoa pesa kwa rafiki, hata wakati hauwezi kufanya hivyo.

  8. Kuhisi kutokuwa na thamani. Unyanyasaji wa kihisia unaweza kuzuia hisia zako za kuwa na thamani. Walakini wewe bado ni mwana au binti wa Mungu na una asili ya Kiungu na takdiri. Thamani yako, ambayo ni kubwa, haibadiliki (ona Mafundisho na Maagano 18:10).

Naweza Kufanya Nini Ikiwa Ninanyanyaswa Kihisia?

Wakati mwingine uhusiano wa unyanyasaji wa kihisia unaweza kuwa wa kuharibu sana kiasi kwamba kuondoka kwenye uhusiano kunaweza kuwa muhimu. Hata hivyo, kuondoka si chaguo pekee katika kila hali. Badiliko linawezekana, na uhusiano unaweza kuwa wenye afya kwa kufanyiwa kazi na mara nyingi kwa msaada wa mtaalamu. Ikiwa unaamini unaweza kuwa upo katika uhusiano wa unyanyasaji wa kihisia, yafuatayo yanaweza kusaidia:

  1. Tafuta msaada na usaidizi kutoka kwa mtu anayeaminika ambaye pamoja naye unaweza kushiriki uzoefu wako, kama vile rafiki, kiongozi wa Kanisa, au mtaalamu katika shirika la jamii. Mtu huyu anaweza kutoa msaada wa kihisia na mtazamo chanya wa wewe ni nani na anaweza kutumia wakati mzuri na wewe mbali na unyanyasaji. (Ona abuse.ChurchofJesusChrist.org. Bonyeza “In Crisis” kwa ajili ya orodha ya misaada.)

  2. Weka na tunza mipaka na mtu anayeonyesha tabia ya unyanyasaji kwa kubaini tabia ambayo ni ya unyanyasaji na kuweka mipaka ya mwingiliano wenu unaoendelea. Unaweza kusema, “Ninahisi kudharauliwa na wewe hivi sasa. Nataka kuzungumza na wewe, lakini sitafanya hivyo mpaka unichukulie kwa heshima na ukarimu.”

  3. Pata msaada kutoka kwa mshauri wa kitaalamu anayejua juu ya unyanyasaji wa kihisia na athari zake. Wakati mwingine wakosaji hawajui kuwa wananyanyasa. Wanaweza kujifunza kubadilika ikiwa wako tayari kutafuta msaada. Ikiwa uhusiano hautaendelea, kutafuta msaada wa wataalamu, pamoja na msaada wa Bwana, vitakusaidia kupona.

  4. Pata taarifa na rasilimali zaidi za usaidizi kwenye abuse.ChurchofJesusChrist.org.

Licha ya hali yako, jua kwamba kuna watu ambao wanakupenda na wanataka kukusaidia. Na kwa kumgeukia Baba yako wa Mbinguni, Mwokozi, na Roho Mtakatifu, tumaini na uponyaji vinawezekana.

Muhtasari

  1. Barua ya Urais wa Kwanza, “Kujibu Unyanyasaji,” Julai 28, 2008.

  2. Jeffrey R. Holland, “Huduma ya Upatanisho,” Ensign au Liahona, Nov. 2018, 79.