2020
Mioyo Iliyochomwa na Majeraha ya Kina: Kuelewa Unyanyasaji katika Familia
Oktoba 2020


Mioyo Iliyochomwa na Majeraha ya Kina: Kuelewa Unyanyasaji katika Familia

Mifumo isiyo na afya inaweza kukua katika uhusiano wowote ule. Kuitambua kunaweza kufichua unyanyasaji au kuuzuia kabla ya kuanza.

Picha
upset woman and husband

Picha zinatumika kwa makusudi ya kielelezo pekee, sura na waigizaji

Hivi karibuni niliitwa na baba aliyevunjika moyo. Binti yake Jenna (majina yamebadilishwa) alikuwa mbali chuoni akiwa na uhusiano mpya, na ulikuwa ukienda haraka. Mpenzi wake, Jake, alikuwa akiharakisha kufunga ndoa na kuwekea ukomo mawasiliano ya Jenna na wazazi wake. Jenna aliwaomba msamaha, akielezea kuwa ni mapenzi mazito ya Jake na hamu ya kutumia muda kama wanandoa.

Familia ya Jenna ilifadhaika wakati ilipogundua kwamba Jake alikuwa na mke wa zamani na mtoto ambao hakumweleza Jenna. Walimwita yule mke wa zamani, ambaye alisema Jake alikuwa na hasira mbaya na alikuwa mwenye wivu. Jake alipogundua alikasirika. Alisema wazazi wa Jenna walikuwa “wanamdhibiti” na alikumbushia wakati ambapo hawakukubali utani wa kashfa alioufanya kuhusu uwezo wa kufikiri wa Jenna. Jake kwa kejeli alisisitiza kwamba Jenna afanye maamuzi yake mwenyewe kwa kuzuia mawasiliano nao. Wazazi wa Jenna walikata tamaa wakati simu na ujumbe wao sasa havikuwa vikijibiwa.

Kila mtu anataka familia yenye furaha, lakini hata wakati watu wanapojaribu kuishi injili, uhusiano unaweza kuwa mbaya. Baadhi ya changamoto ni matokeo ya kutokuelewana na misuguano ya kawaida kwenye familia. Walakini, katika nyumba zenye afya, watu huombana radhi kwa tabia mbaya na kuziba mipasuko, wakati katika hali zisizo na afya, kuna mifumo inayoendelea ya ukatili au uonevu ambao unakuwa unyanyasaji.

Unyanyasaji wa Nyumbani na Injili

“Mmevunja mioyo ya wake zenu wapole, na kuvunja tumaini la watoto wenu” (Yakobo 2:35).

Unyanyasaji unajumuisha vitendo vilivyokusudiwa kuumiza au kudhibiti. Unajumuisha mlolongo wa tabia ambazo zinaweza kujumuisha kupuuza, kudanganya, ukosoaji wa maneno, na vurugu za kimwili au za kijinsia.2 Kwa bahati mbaya, tabia ya unyanyasaji ni ya kawaida, na baadhi ya wasomi wanakadiria kuwa karibu robo ya watoto ulimwenguni wameonewa vibaya kimwili, kijinsia au kihisia.2 Watu wazima pia wana viwango vya juu vya unyanyasaji, na takriban 1 kati ya wanawake 4 na 1 kati ya wanaume 10 wanapitia vurugu za kimwili kutoka kwa mwenzi.

Unyanyasaji unaweza kutokea katika uhusiano wowote, na wote mwanamume na mwanamke wanaweza kuwa wakosaji. Walakini, wanaume wana uwezekano mkubwa wa kudhibiti na kufanya vurugu kali za kimwili na kijinsia, na wanawake wana uwezekano mkubwa wa kutishwa, kutawaliwa, au kuumizwa vibaya na mwenzi wake.3

Unyanyasaji unaumiza roho ya mkosaji na mwathirika na ni kinyume na mafundisho ya Mwokozi. Manabii wa sasa wameeleza kwamba wale “wanao wanyanyasa wenza au watoto … siku moja watawajibika mbele za Mungu.”4 Wanyanyasaji mara nyingi hupuuza au kuinyonya kanuni za injili. Kwa mfano, niliwashauri wenzi ambapo mume alijikita kwenye maswala ya kihisia na kuchezea kamari akiba yao, lakini badala ya kuomba msamaha, alimshinikiza mkewe asamehe na akasisitiza kuwa mkewe angekuwa na “dhambi kubwa zaidi” ikiwa mke hatamsamehe. Alipuuza maumivu ya mke na kudai kuwa yeye alikuwa sahihi kwa Mungu vinginevyo asingekuwa mfanyakazi wa hekaluni. Wakati mkewe alipoongea na viongozi wa Kanisa, yeye alificha usaliti wake na kukuza wasiwasi wa mke, akisema mkewe alikuwa mwenye huzuni. Mume alikuwa akikataa “kanuni za… heshima, upendo, [na] huruma”5 na akimtendea vibaya mkewe. Juhudi zake za kuishi kanuni za injili hazikuweza kurekebisha matatizo aliyokuwa akiyatengeneza.Kila mmoja wetu anaweza kujiingiza kwenye tabia mbaya. Kuna sifa fulani zinazojulikana kwa kila aina ya unyanyasaji, na kadiri uwavyo mkali zaidi na mara kwa mara, ndivyo kupungua kwa afya ya uhusiano kutakavyokuwa. Hapa kuna mifumo mitano ya kawaida ya unyanyasaji ambayo inaweza kukusaidia kutambua tabia mbaya kwako mwenyewe na kwa wengine.

Picha
sad little girl

1. Ukatili

Kwa ndimi zao wametumia udanganyifu; sumu ya manyoya iko chini ya midomo yao:… midomo [ yao] imejaa laana na uchungu” (Warumi 3:13–14).

mwanamume mmoja alikuja kuniona kwa ajili ya tiba dhidi ya matakwa ya mke wake, ambaye alimdhihaki kwa “kuhitaji msaada.” Kanisani alikuwa mcheshi na mcha Mungu, lakini nyumbani kwake alikuwa mkali kama mjeledi. Alikosoa mapato yake na kuita kazi yake ya ualimu kama “kazi ya msichana.” Alimwambia mwanawe, “Natumai hautakuwa mwoga kama baba yako,” na alitumia kila siku kwenye simu kuzungumza na mama yake, ambapo waliwadhalilisha waume zao. Watu wakosoaji wanahisi wana haki ya kusababisha uchungu na “kupenda kuwaona wengine wakiteseka” (Mafundisho na Maagano 121:13). Wanafamilia hawa huvunja amri za Yesu za “msihukumu” na “msilaumu” (Luka 6:37) pale wanapodhalilisha wanapoonyesha karaha au kuita majina.

2. Udanganyifu

“Wewe unaongozwa na roho wa uwongo, na umeweka mbali Roho wa Mungu” (Alma 30:42).

Udanganyifu hueneza unyanyasaji pale wakosaji wanapopunguza ukubwa wa vitendo vyao, kulaumu wengine, na kuchezesha maneno. waathiriwa hawa waliokanganywa, kama mmoja wa washiriki wa utafiti wangu alivyoelezea: “[Mume wangu angeweza] kupandwa na mhemko halafu akafanya jambo la kuomba msamaha kisha akasema, ‘Kweli ni kosa lako hata hivyo’ … angeendelea tena na tena na hadi nami nikaanza kuamini hivyo.”6 Kukataa huku kwa ukweli wa mwingine huitwa kuwasha gesi, na huwaacha waathiriwa wakiwa na mkanganyiko na kukosa usalama juu ya kumbukumbu na maoni yao. Kama aina zingine za udanganyifu, kuwasha gesi hutumiwa kudhibiti mazungumzo na kuweka mbele uwongo.

Wale wanao wanyanyasa wengine ni hodari wa kupinga kukubali kwamba ni wenye kuumiza na mara nyingi watadai kuwa wao ndio waathiriwa. Wakati Jenna alipoelezea wasiwasi kuhusu ukosoaji wa Jake kwa wazazi wake, Jake alikasirika na kusisitiza kwamba Jenna alikuwa “akimtukana.” Jake alikuwa ni miongoni mwa “wale wanaolia kwamba uvunjaji wa sheria umetendeka … na wao wenyewe ni wana wa uasi” (Mafundisho na Maagano 121:17). Siyo tu alikuza hadithi yake ya uwongo bali pia alichukia ukweli.7

Picha
man with head in hands

3. Visingizio

“Kukiri makosa yako na ule ubaya ambao umetenda” (Alma 39:13).

Mtu mnyenyekevu hujisikia majuto kwa kuumiza wengine na kutubu na hufanya vizuri zaidi. Mtu ambaye ni mnyanyasaji anapinga wito wa dhamiri kwa udhuru. Kama mmoja wa washiriki wa utafiti wangu alivyokumbuka, “Ningejisikia vibaya juu ya unyanyasaji huo wa kimwili, na kisha baadaye ningefikiria isingetokea kama tu angekuwa amefunga mdomo wake.” “Huzuni yake haikuwa ya toba”(Mormoni 2:13) lakini badala yake alisukumwa kando na hasira kali na lawama.

Katika kutoa tiba, niliwahi kumwambia mke kuwa sikuwahi kumshuhudia akionyesha huzuni ya kimungu kwa miaka ya kumkosoa mumewe. Jibu lake halikuwa majuto bali kununa: “Vizuri, hapa kuna jambo lingine ambalo silifanyi” Watu wanyanyasaji hukataa uwajibikaji na ni wenye hamaki na wanaojitetea. Wao hukasirishwa kwa urahisi na vitu vidogo.

4. Kiburi

“Kwa unyenyekevu kila mtu amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake” (Wafilipi 2:3).

Kiburi ni pamoja na kujiona mwenye haki na ubinafsi. Mwanamume mmoja aliwapiga mkewe na watoto wake kila wakati alipofikiria walikuwa “hawamuheshimu.” Ikiwa maoni yao hayaendani na yake, walikuwa “wakimdharau” yeye au “hawakuwa watiifu.” Kiburi kina ushindani na huzingatia wadhifa na kushinda. Kwa upande mwingine, familia yenye afya inashirikiana, pale ambapo kuna usawa wa haki, na washiriki “kila kila mmoja anamtendea mwingine haki” (4 Nefi 1:2). Wanandoa wanapaswa kuwa wabia walio sawa,8 ambapo kila mmoja ana kauli na maoni yote yanathaminiwa.

5. Dhibiti

“Wakati … tunapotumia udhibiti au utawala au ulazimishaji juu ya nafsi za wanadamu, … mbingu hujitoa zenyewe” (Mafundisho na Maagano 121:37).

Ingawa tunathamini haki ya kujiamulia, inashangaza ni mara ngapi washiriki wa familia huambiana jinsi ya kufikiria, kuhisi, na kutenda. Baadhi hata wanadhibiti kupitia kuogofya, aibu, kuondoa upendo, au vitisho. Mume mmoja alikuwa na matarajio magumu ya kwamba mke wake anapaswa kuandaa kifungua kinywa kila siku kwa wakati fulani, kutimiza maombi fulani ya kimahaba, na kumsikiliza kuhusu “wasiwasi” wake, ambao kwa kawaida ulihusisha jinsi gani mke angejiboresha. Alifuatilia matumizi yake na alikasirika ikiwa hakujibu haraka ujumbe wake.

Mama mwingine alielezea kukatishwa tamaa mara nyingi kwa binti yake wa miaka kumi na kitu wakati wowote msichana huyo alipoonyesha huzuni au hakufanya kulingana na viwango vya mama. Ikiwa matarajio hayakufikiwa, au ikiwa mumewe alionyesha wasiwasi, yeye aliwanyamazia kimya wote.

Picha
holding hands

Matumaini na Uponyaji

“Nimesikia maombi yako, na nimeona machozi yako: tazama, nitakuponya” (2 Wafalme 20:5).

Ingawa unyanyasaji unavunja moyo, mabadiliko daima yanawezekana. Waathiriwa wanaweza kuzifikia nyenzo za kiroho na za kitaalam na kutafuta nguvu ya Upatanisho wa Mwokozi ili kuponya majeraha yao. Ili kupata msaada, nenda abuse.ChurchofJesusChrist.org

Wale ambao wamekuwa wanyanyasaji lazima watubu na kuomba msaada. Hii inahitaji kwenda “chini kwenye unyenyekevu” (3 Nefi 12:2) na kukubali uwajibikaji kamili kwa ajili ya tabia zao. Mabadiliko yanachukua zaidi ya ahadi za muda mfupi na juhudi za juu juu. Uchungu wa toba ya kina ni wa kuumiza moyo , na wengine hawatakubali kufanya hivyo, kitu ambacho kinawaacha wathiriwa kwenye maamuzi magumu juu ya jinsi ya kujilinda.9

Baba yetu wa Mbingu anatujali sisi kama vile baba aliyesumbuka ambaye aliniita kuhusu binti yake. Upendo wa Mungu ni “mpana kama milele” (Musa 7:41), na Anaumia sana wakati watoto Wake wanapoumizana wao kwa wao. Katika mazungumzo ya upole na Henoko, Yeye analia. “Hao ndugu zako; ni kazi ya mikono yangu mwenyewe,… na nimewamuru, kwamba wapendane, … lakini tazama, hawana mapenzi, na wanaichukia damu yao wenyewe” (Musa 7:32–33). Kuna kilio mbinguni na duniani wakati miili na roho zinapojeruhiwa. Walakini, kwa unyenyekevu, nguvu ya Mungu, na msaada wa wataalamu wakati unapohitajika, inawezekana kuacha tabia yenye kuharibu na kujenga nyumba yenye heshima, usalama, na upendo.

Muhtasari

  1. Kwa maelezo zaidi kuhusu unyanyasaji wa kimwili, ona abuse.Churchof JesusChrist.org. Kwa maelezo zaidi kuhusu unyanyasaji wa kijinsia na shambulio, ona Benjamin M. Ogles, “Haki ya kujiamulia, Uwajibikaji, na Upatanisho wa Yesu Kristo: Application to Sexual Assault” (Brigham Young University devotional, Jan. 30, 2018), speeches.byu.edu; na Chieko N. Okazaki, “Healing from Sexual Abuse” (Brigham Young University conference, Okt. 23, 2002).

  2. Ona Maryam Ajilian Abbasi, Masumeh Saeidi, Gholamreza Khademi, Bibi Leila Hoseini, Zahra Emami Moghadam, “Child Maltreatment in the World: A Review Article,” International Journal of Pediatrics, vol. 3, no. 1 (2014), 353–65.

  3. Ona Hamby, S., “Mabishano ya hivi sasa: Je! Wanawake kweli wana vurugu kama wanaume? The ‘gender symmetry’ controversy,” katika Claire M. Renzetti, Jeffrey L. Edleson, na Raquel Kennedy Bergen, Sourcebook on Violence Against Women, 3rd ed. (2018), 78–82.

  4. “Familia: Tangazo kwa Ulimwengu,” Liahona, Mei 2017, 145; ona pia abuse.ChurchofJesusChrist.org.

  5. “Familia: Tangazo kwa Ulimwengu.”

  6. Jason B. Whiting, Megan Oka, na Stephen T. Fife, “Appraisal distortions and intimate partner violence: Gender, power, and interaction,” Journal of Marital and Family Therapy (2012), suppl: 1:113–49.

  7. Kwa ajili ya mifano mingine ya kimaandiko juu ya kuchukia ukweli, ona Yohana 3:19–21; Matendo 7:54; 2 Nefii 1:25–26; na 2 Nefi 4:13.

  8. Ona “Familia: Tangazo kwa Ulimwengu”; tazama pia H. Burke Peterson, “Unrighteous Dominiont,” Ensign, Julai 1989, 6–11, kwa habari zaidi juu ya mafundisho ya usawa na maswali ya kuzingatia kuhusu maagano ya uhisiano.

  9. Wale walio katika hali ya unyanyaswaji mara nyingi wanakabiliwa na chaguo juu ya jinsi ya kulinda usalama wao, au ule wa wengine, vile vile kama wao wanahitaji kuweka mipaka au kupunguza mwingiliano wao na wale wenye kuumiza. Rais James E. Faust (1920-2007) alijadili hali hii ngumu wakati mtu anapokuwa ametegewa katika “uhusiano wa muda mrefu na dhahiri ambao huharibu utu wa mtu kama mwanadamu” (“Stawisha Ndoa Yako,” Liahona, Aprili 2007, 3 ); ona pia “Msaada kwa waathiriwa” kwenye tovuti ya Kanisa ya kuzuia unyanyasaji kwa ajili ya habari zaidi na chaguzi.