2020
Ananiweka Tena Pamoja
Oktoba 2020


Ananiweka Tena Pamoja

Rafiki yangu alisikia kwamba nilikuwa mgonjwa na alituma fumbo la kutengenezwa nyumbani lililotengenezwa mahususi kwa ajili yangu.

Picha
puzzle of a name

Kielelezo na Joshua Dennis

Daima nilijifikiria kama mtu mwenye afya njema. Hivyo nilishtuka nilipoamka asubuhi moja nikijisikia kama kifua changu kimeminywa kwa nguvu kikiwa karibu kupasuka. Nilikimbizwa hospitali, lakini baada ya masaa kadhaa ya vipimo, madaktari hawakuweza kuona tatizo. Walinirudisha nyumbani, ingawa nilikuwa bado nina maumivu makali sana. Ndivyo ilivyoanza shida ya miezi saba ya miadi ya kuonana na daktari, kukaa hospitalini, na maumivu makali ambayo sijawahi kuyahisi katika maisha yangu.

Nilianza kufadhaika. Ilinibidi kuacha masomo yangu ya chuo na kurudi kuishi na wazazi wangu. Sikuweza kutoka na marafiki zangu. Niliumia sana kutofanya vitu nilivyozoea. Nilihisi kwamba kila kitu nilichojali—matamanio yangu, uhusiano wangu, talanta zangu—vilikuwa vimekatika, na sasa vipande vya utu wangu wa zamani vilionekana kutowezekana kuunganika tena pamoja. Na nilianza kujiuliza: Je, Baba wa Mbinguni amewezaje kuruhusu jambo hili linitokee? Je, Hakunipenda?

Baada ya miadi nyingine ya kukatisha tamaa na daktari, nilichotaka kufanya ni kujiviringisha kama mpira na kulia. Lakini wakati nilipofika nyumbani, niliona kitu cha kushangaza kwenye kibaraza: boksi bovu bovu la viatu lililoviringwa kwa utepe na kuandikwa jina langu.

Barua juu ya boksi ilifichua kuwa kifurushi kilikuja kutoka kwa mmoja wa marafiki zangu. Alikuwa amesikia kwamba nilikuwa mgonjwa na alitaka kunifariji. Nilipofungua boksi la viatu, nikagundua lina vipande vidogo vidogo vya sponji. Ilikuwa ni fumbo la kutengenezwa nyumbani lililotengenezwa mahususi kwa ajili yangu.

Nikiwa naliunganisha fumbo pamoja, nilianza kulia. Fumbo lilitengeneza jina langu, likizungukwa na ujumbe mzuri wa upendo na wa kutia moyo. Nilihisi kuwa vipande vya utu wangu mwenyewe vilivyovunjika sasa vilikuwa vinarudishwa pamoja wakati nikiunganisha zawadi ya rafiki yangu.

Muda mfupi baadaye, nilianza kutumia dawa iliyopunguza dalili zangu na kuwasaidia madaktari kufanya ubainifu wa ugonjwa. Nilikuwa na hali ya nadra lakini inayoweza kutibika, na kwa dawa sahihi, ningeweza kurudi kwenye maisha ya kawaida.

Hata wakati mwili wangu ukiwa unapona, nilijua kuwa sitakisahau kile nilichojifunza. Kwa sababu ya zawadi nzuri ya rafiki yangu, nilijua kuwa nilipendwa na kwamba Baba wa Mbinguni hakunisahau. Baada ya miezi ya kuhisi kuvunjika, nikiwa na shukurani kwa ukarimu wa rafiki na upendo wa Baba yangu wa Mbinguni, nikawa mzima tena.