Misaada ya Kujifunza
Kutoka


Kutoka

Kitabu kilichoandikwa na Musa katika Agano la Kale ambacho kinaelezea kuondoka kwa Waisraeli kutoka Misri. Historia ya awali ya Israeli kama ilivyoandikwa katika kutoka inaweza kugawanywa katika sehemu tatu: (1) utumwa wa watu hawa kwa Misri, (2) kuondoka kwao kutoka Misri chini ya uongozi wa Musa, na (3) kujitolea kwao kwa dhati katika huduma ya Mungu katika maisha yao ya kidini na maisha yao ya kisiasa.

Sehemu ya kwanza, Kutoka 1:1–15:21, inafafanua ukandamizwaji wa Israeli katika Misri; historia ya awali na wito wa Musa; Kutoka na kuanzishwa kwa Pasaka; na msafara wa kwenda Bahari ya Shamu, angamizo la jeshi la Farao, na wimbo wa Musa wa ushindi.

Sehemu ya pili, Kutoka 15:22–18:27, inaelezea juu ya ukombozi wa Israeli na matukio ya safarini kutoka Bahari ya Shamu hadi Sinai, maji machungu ya Mara, kutolewa kwa kware na mana, kuishika Sabato, zawadi ya kimuujiza ya maji huko Refidimu, na pambano lao hapo na Waamaleki; kuwasili kwa Yethiro kambini na ushauri wake juu ya kuwatawala watu na matatizo yao ya kila siku.

Sehemu ya tatu, mlango wa 19–40, hujishughulisha na kujiweka wakfu kwa Israeli kwa huduma ya Mungu wakati wa matukio mazito katika Sinai. Bwana aliwatenga watu kama ufalme wa makuhani na taifa takatifu; Yeye akatoa Amri Kumi; na Akatoa mafundisho juu ya hema, samani zake, na kuabudu ndani yake. Hatimaye inafuata historia ya dhambi za watu hawa katika kuabudu ndama wa dhahabu, na mwishowe historia ya ujenzi wa hema na kutolewa kwa vifaa vyote vya huduma yake.